5
HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA NANE YA KITAIFA YA SIKU YA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI, UKUMBI WA KARIMJEE - DAR ES SALAAM, TAREHE 10 DESEMBA 2015 Mhe. Said Meck Sadick Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; Mhe. Bahame Tom Nyanduga Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Mhe. George Masaju Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria; Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Ofisi ya Tanzania; Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi mbalimbali mliopo hapa; Viongozi mbalimbali wa Serikali; Wawakilishi wa Asasi za Kiraia; Wageni Waalikwa; Waandishi wa Habari; Ndugu Wananchi; Mabibi na Mabwana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukusanyika hapa leo ili kushiriki katika Maadhimisho haya ya Siku ya Haki za Binadamu ambayo husherehekewa Duniani kote Desemba 10 kila mwaka. Hii ni siku muhimu kwetu na kwa mataifa mengi duniani.

Hotuba Ya Haki Za Binadamu 10.12.2015 (Press)

Embed Size (px)

DESCRIPTION

HOTUBA YA HAKI ZA BINADAMU 10.12.2015 (PRESS)

Citation preview

Page 1: Hotuba Ya Haki Za Binadamu 10.12.2015 (Press)

HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA

MAADHIMISHO YA NANE YA KITAIFA YA SIKU YA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI, UKUMBI WA KARIMJEE - DAR ES SALAAM,

TAREHE 10 DESEMBA 2015

Mhe. Said Meck Sadick Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

Mhe. Bahame Tom Nyanduga Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;

Mhe. George Masaju Mwanasheria Mkuu wa Serikali;

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria;

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Ofisi ya Tanzania;

Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi mbalimbali mliopo hapa;

Viongozi mbalimbali wa Serikali;

Wawakilishi wa Asasi za Kiraia;

Wageni Waalikwa;

Waandishi wa Habari;

Ndugu Wananchi;

Mabibi na Mabwana.

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukusanyika hapa leo ili kushiriki katika Maadhimisho haya ya Siku ya Haki za Binadamu ambayo husherehekewa Duniani kote Desemba 10 kila mwaka. Hii ni siku muhimu kwetu na kwa mataifa mengi duniani.

Niwashukuru pia wale wote waliofanikisha maadhimisho haya kwa njia moja ama nyingine. Kipekee niwashukuru Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Ofisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania na Ofisi ya Umoja wa Nchi za Ulaya

Page 2: Hotuba Ya Haki Za Binadamu 10.12.2015 (Press)

Tanzania, asasi za kiraia, na wadau wengine wote kwa jitihada zao kubwa za kuratibu na hatimaye kufanikisha Maadhimisho haya. Hongereni Sana!

Aidha, niwashukuru wale wote walioshiriki katika maandamano, mmeonesha kuthamini Siku hii ya leo - Nawapongeza Sana!

Ndugu Wananchi;Mabibi na Mabwana;Leo t unaadhimisha Siku ya Haki za Binadamu tukikumbuka miaka 67 tangu Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu likubaliwe na kupitishwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1948. Azimio hilo limekuwa chimbuko la utetezi wa haki za binadamu ulimwenguni na heshima ya utu wa mwanadamu katika nchi zote ulimwenguni zinazotekeleza matakwa ya Azimio hilo. Mikataba mingi ya kikanda na kitaifa imeridhiwa na nchi nyingi ulimwenguni na misingi ya haki za binadamu iliyomo kwenye Azimio imeingizwa kwenye katiba za nchi nyingi, ikiwemo Tanzania.

Kitaifa tumekuwa tukiadhimisha siku hii kutokana na ukweli kuwa sisi Tanzania ni wanachama wa Umoja wa Mataifa ambako ndiko chimbuko la Haki za Binadamu, na kwamba kama Serikali, tunaamini na tunawajibika moja kwa moja kukuza, kulinda na kutekeleza haki hizo hapa nchini.

Kaulimbiu ya Kimataifa ya Siku hii ya Haki za Binadamu mwaka huu ni– “Haki Zetu, Uhuru Wetu Daima” (Our Rights, Our Freedoms Always) inaakisi hamu ambayo kila mmoja wetu aliyonayo popote pale alipo na wakati wowote ule ya kuona kuwa haki na uhuru wake kama binadamu unatambuliwa, unalindwa na kuheshimiwa wakati wote.

Natumaini wote tutatafakari kaulimbiu hii ya “Haki Zetu, Uhuru Wetu Daima” tukijikumbusha kuwa haki za binadamu siyo bidhaa ya anasa bali ni kitu muhimu katika maisha yetu sote, wanawake kwa wanaume, watoto, vijana wote, wasichana na wavulana, pamoja na wazee wanahitaji kufurahia uhuru wao na haki zao kuheshimiwa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inao wajibu wa kulinda na kukuza uhuru na haki hizi, kwa kuzingatia misingi iliyopo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ya Haki za Binadamu na sheria mbalimbali za nchi, katika jitihada zake za kutimiza wajibu huu muhimu, wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu.

Tanzania imeridhia mikataba mingi ya kimataifa inayohusu Haki za Binadamu. Baadhi ya mikataba hiyo ni pamoja na; Mkataba wa

2

Page 3: Hotuba Ya Haki Za Binadamu 10.12.2015 (Press)

Kimataifa wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi wa mwaka 1965; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni 1966; Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya Wanawake wa mwaka 1979; Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa mwaka 1981; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto 1989; Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Watoto wa mwaka 1990, Itifaki ya Afrika ya Haki za Wanawake, (Maputo Protocol) ya 2003, na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2008.

Ili kuhakikisha kuwa ulinzi wa haki za binadamu unaimarishwa, Serikali yetu imekwisha ingiza baadhi ya mikataba hii katika sheria zetu za nchi, ama kwa kuunda sheria mpya au kurekebisha zile zilizopo.

Isitoshe, Serikali imekuwa ikiandaa ripoti za utekelezaji wa Haki za Binadamu kwa mujibu wa mikataba tajwa ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwenye vyombo vya kimataifa kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa mapendekezo ya utekelezaji.

Ndugu Wananchi;Mabibi na Mabwana;Maadhimisho haya yanatoa fursa nzuri kwetu sote kujiuliza; tumefanya nini katika kipindi cha mwaka mzima uliopita, changamoto zinazokabili suala zima la haki za binadamu na tunatarajia kufanya nini siku za usoni. Tunafanya haya yote tukikumbuka kuwa utekelezaji wa haki za binadamu ni mchakato, hivyo siku zote ni lazima tuendelee kuboresha haki hizo hatua kwa hatua.

Sisi katika Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuziwezesha taasisi zinazosimamia utekelezaji wa sheria na kutoa haki ili kutimiza wajibu wake. Napenda kuwahakikishia kuwa haki na uhuru wa kila Mtanzania itaheshimiwa, itahifadhiwa na kulindwa.

Ndugu Wananchi;Mabibi na Mabwana;Pamoja na juhudi kubwa za Serikali kuboresha mazingira ya upatikanaji na utoaji wa Haki za Binadamu nchini, matukio ya ukiukaji wa haki hizo yameendelea kuongezeka. Taarifa za vyombo mbalimbali vya habari na ripoti za kitafiti, zimeonesha na kuthibitisha uwepo wa matukio kadhaa ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini. Baadhi ya matukio hayo ni kama yale ya mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, mauaji ya wanawake vikongwe, ghasia zinazohusiana na vurugu za makundi; Mahabusu kuwekwa rumande muda mrefu kabla ya kesi kusikilizwa, unyanyasaji dhidi ya wanawake, unyanyasaji wa watoto

3

Page 4: Hotuba Ya Haki Za Binadamu 10.12.2015 (Press)

ikiwemo ukeketaji, ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, mauaji kwa wanaozaliwa na ulemavu, utekaji nyara, ajira mbaya n.k.

Nawahakikishieni kuwa Serikali imejipanga vema kukabiliana na kutokomeza uovu huo bila kumwonea huruma mtu yeyote anayejihusisha na maovu hayo.

Ndugu Wananchi;Mabibi na Mabwana;Mtakumbuka kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika Awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika mapema kwa uandikishaji wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba lililotupatia Katiba inayopendekezwa. Serikali itatekeleza wajibu wake kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2013, na iwapo Katiba inayopendekezwa itapitishwa hapo baadaye, itachangia sana ukuaji wa haki za binadamu nchini.

Hatua nyingine ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuzichukua ili kuboresha haki za wananchi nchini kadiri alivyofafanua hivi karibuni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi, umaskini, upungufu wa ajira, kuboresha elimu na afya.

Tutaendeleza mapambano dhidi ya ubadhirifu, wizi na ufujaji wa fedha za umma. Yote haya yatafanyika kwa kuzingatia sheria, na matamko ya haki za binadamu. Mathalani watuhumiwa kufikishwa kwenye vyombo vya haki ili sheria ichukue mkondo wake bila ya kumwonea mtu yeyote. Ikumbukwe kwamba ubadhirifu, wizi, rushwa na ufisadi umechangia katika kudumaza ukuaji wa uchumi na hivyo kuendeleza umasikini na kuwaacha wananchi walio wengi, kukosa haki za msingi za maisha. Hali hiyo haikubaliki, kwani ikiachiwa iendelee, itarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia Malengo ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu, (Sustainable Devevelopment Goals), Mpango ambao umezinduliwa na Umoja wa Mataifa Septemba 2015, unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 1 Januari, 2016 ukiwa na malengo kumi na saba (17). Mpango huu unachukua nafasi ya Mpango wa Maendeleo wa Millenia (Millenium Development Goals) baada ya kufikia tamati.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kupanua elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu na kuongeza ubora wa elimu inayotolewa. Serikali itahakikisha kuanzia Januari mwakani

4

Page 5: Hotuba Ya Haki Za Binadamu 10.12.2015 (Press)

elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure. Aidha, tutahakikisha wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati na pia haki za walimu zinaboreshwa kwa kiwango kinachostahili.

Kwa upande wa huduma za afya, pamoja na mambo mengine Serikali ya Awamu ya Tano inakusudia kuanzisha na kuimarisha huduma kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kwa kuongeza wataalamu, kutoa vifaa tiba bora na vya kisasa, kuongeza bajeti ya dawa, kuboresha mfumo wa upatikanaji wake na kuhamasisha wananchi wajiunge na mifuko ya bima ya afya.

Tunatambua afya haiwezi kuimarika iwapo wananchi hawapati maji safi na salama, hivyo Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020.

Ndugu wananchi, Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia Malengo ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu kwa kushirikiana na wadau wengine, zikiwemo taasisi za Serikali, taasisi zisizo za kiserikali na wananchi kwa ujumla.

Ndugu Wananchi;Ndugu Wageni Waalikwa;Mabibi na Mabwana;Nitumie fursa hii pia kuwaasa Watanzania wenzangu kuanzisha kampeni maalum za kukuza maadili mema katika ngazi mbalimbali zikiwemo zile za utumishi wa umma, taasisi za dini, taasisi za elimu na katika nyanja zote za maisha ya kila siku. Suala hili likifanyika vizuri, naamini sote kwa pamoja, tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa kulinda haki za binadamu, kwani bila maadili mema, itakuwa vigumu kuheshimu utu wa mwanadamu ambao ndio msingi mkuu wa haki za binadamu, na hivyo kutekeleza kaulimbiu ya Haki Zetu, Uhuru Wetu Daima.

Jukumu la kukuza, kulinda na kuheshimu haki za binadamu ndani ya jamii yetu, ni letu sote, mtu mmoja mmoja, familia au kaya, na Serikali kwa ujumla. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuhakikisha kuwa haki za binadamu na misingi ya utawala bora inazingatiwa hapa nchini.

Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima natamka kuwa Maadhimisho ya Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu, yamefunguliwa rasmi.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

5

Page 6: Hotuba Ya Haki Za Binadamu 10.12.2015 (Press)

6