7

Click here to load reader

Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

Embed Size (px)

DESCRIPTION

Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uzinduzi wa uchunguzi wa saratani ya mlango wa uazi na matiti Morogoro

Citation preview

Page 1: Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI

WA UFUNGUZI WA HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI NA YA MATITI

MKOANI TABORA, TAREHE 7 JUNI, 2014

Mhe. Mama Salma Kikwete, Mlezi wa MEWATA;

Mhe. Kebwe Steven Kebwe (Mb.), Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa

Jamii;

Mhe Fatma Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora;

Wakuu wa Wilaya – Tabora, Nzega na Urambo;

Wabunge Wote wa Mkoa wa Tabora Mliopo;

Dkt. Serafina Mkuwa, Mwenyekiti wa MEWATA;

Wawakilishi wa Washirika Wetu wa Maendeleo;

Dkt. Joseph Komwihangiro, Mwakilishi wa Marie Stopes;

Madaktari Wote wa MEWATA na Watumishi wa Sekta ya Afya;

Mwakilishi wa Shirika la Marie Stopes na Wawakilishi wa Mashirika

Yasiyo ya Kiserikali Waliopo;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Shukrani na Pongezi

Niruhusuni nianze kwa kuwashukuru Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif

Rashid (aliyewakilishwa hapa leo na Naibu Waziri Mhe.Dkt. Stephen Kebwe) na

Mwenyekiti wa Chama cha Madakatari Wanawake Tanzania (MEWATA), Dkt.

Sarafina Mkuwa kwa kunialika kuja kuzindua huduma za uchunguzi wa saratani ya

mlango wa kizazi na saratani ya matiti Mkoani Tabora. Nawapongeza nyote kwa

maandalizi mazuri kwani ni ukweli usiopingika kuwa shughuli hii imefana

sana. Aidha, nawashukuru wenyeji wetu wa Mkoa wa Tabora wakiongozwa na Mkuu

wa Mkoa, Mheshimiwa Fatma Mwasa, kwa mapokezi mazuri mliyonipatia mimi, mke

wangu na wageni wenzetu. Sikutegemea kupata mapokezi tofauti na haya hapa

Tabora, kwani upendo wenu kwangu na ukarimu wenu tunaujua na unasifika na

wengi.

Page 2: Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

Madhumuni ya Ziara

Ndugu Wananchi;

Nimekubali kuja kujumuika nanyi katika uzinduzi huu, siku ya leo, ili kuongeza sauti

yangu na uzito kuhusu shughuli hii muhimu na adhimu inayofanywa na Madaktari

Wanawake hapa nchini. Ni ukweli ulio wazi kuwa MEWATA imesaidia kuokoa maisha

ya akinamama wengi nchini ambao, vinginevyo, wangepoteza uhai kwa saratani hizi

mbili zinazowapata wanawake. Hatuna budi kuvunja ukimya na kuungana na

Madaktari Wanawake kuzungumzia maradhi haya na kuelimishana ili wananchi,

wadau na Serikali kwa umoja wetu au mmoja mmoja, tuchukue hatua stahiki za

kukabiliana na maradhi haya.

Aidha, ni nafasi nzuri ya kutoa pongezi zangu kwa wanachama wa MEWATA kwa kazi

kubwa na nzuri waifanyayo na mafanikio yaliyopatikana. Sijui hali ya maradhi haya

ingekuwaje hapa nchini kama Madaktari Wanawake wasingeamua kufanya kazi hii

njema wanayoifanya. Kwa niaba ya wanawake na wanaume wote wa Tanzania

tafadhali pokeeni pongezi zetu za dhati. Endeleeni kufanya kazi hii njema na

Mwenyezi Mungu atawalipa kwa wema wenu na mioyo yenu ya huruma. Nawaahidi

kuendelea kuwaunga mkono kwa hali na mali na kwa kadri ya uwezo

utakavyoniruhusu.

Nimefurahi sana kwamba ndugu zetu wa MEWATA wameweza kufika hapa Tabora

siku ya leo. Mtakumbuka kuwa nilipokuja kwenye Sherehe za Siku ya Wanawake

Duniani tarehe 8 Machi, 2010, niliahidi kwamba nitawaomba MEWATA waje kufanya

uchunguzi wa saratani za mlango wa kizazi na matiti kwa akinamama. Hayawi hayawi

leo yamekuwa. Nawashukuru sana viongozi na wanachama wa MEWATA kwa kuja

kwenu. Mmenitoa kimasomaso. Wahenga walisema: “Ada ya Mja kunena,

muungwana na vitendo”. Ndugu zangu wa Tabora ahadi imetimia, kazi

kwenu. Jitokezeni kwa wingi kupima muokoe maisha yenu.

Hali ya Magonjwa ya Saratani ya Wanawake Nchini

Ndugu Wananchi,

Tanzania inatambulika kuwa ni moja ya nchi zenye kiwango kikubwa cha maradhi ya

saratani ya mlango wa kizazi hapa Afrika ya Mashariki. Inakadiriwa kuwa takriban

wanawake 56 katika kila wanawake 100,000 hupata saratani hii. Inakadiriwa pia kuwa

Page 3: Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

zaidi ya watu 35,000 wanapata saratani hii kila mwaka na zaidi ya watu 27,000

hupoteza maisha. Mwaka 2010 peke yake, wanawake wapatao 6,000 waligundulika

kuwa na saratani ya mlango wa kizazi na wanawake 4,000 kati yao walifariki dunia.

Wataalamu wanatuambia kuwa, saratani hii huwapata wanawake wa umri wa miaka

30 na 50. Aidha, wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI wako katika hatari zaidi

ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 50. Pamoja na tatizo hili, bado tunayo

changamoto ya saratani ya matiti ambayo ni ya pili kwa kusababisha vifo vya

wanawake wengi nchini. Hivyo basi, hapa nchini wanawake wako kwenye hatari

kubwa ya kufa kwa saratani kuliko wanaume kwa sababu saratani nyinginezo,

hazibagui ukiacha ile ya tezidume inayowapata wanaume pekee.

Hatua za Tahadhari za Kuzingatiwa

Bahati nzuri, saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti zinaweza kutibika

ikiwa zitagunduliwa mapema. Njia pekee ya kuweza kugundua mapema ni kupima

mara kwa mara. Wataalamu wanashauri kuwa ni vyema wanawake wenye umri wa

kati ya miaka 30 na 50 wakachunguza afya zao walau mara moja katika kila miaka

mitatu. Na, kwa wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanashauriwa

kuchunguzwa walau mara moja kwa mwaka.

Bahati mbaya sana, uzoefu umeonyesha kuwa wanawake wengi hufika hospitali wakati

ambapo ugonjwa umeshapea na kuenea sehemu nyingine za mwili. Wanakwenda

hospitali wakati maradhi yamefikia hatua isiyoweza kutibika na hivyo kupoteza

maisha. Hivyo basi, kupima na kugundulika mapema kwa saratani ni hatua muhimu

sana ya kuepusha vifo vinavyotokana na maradhi hayo. Bahati nzuri hivi karibuni

kumekuwepo na mwamko na mwitikio mzuri wa kujitokeza kwa wanawake wengi

kupima saratani ya matiti. Haya ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na

MEWATA. Juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa. Zinastahili kuungwa mkono.

Hatua Zinazochukuliwa na Serikali

Ndugu Wananchi;

Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na saratani ya mlango wa

kizazi. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha Programu inayoshughulikia

masuala ya Saratani za Uzazi katika Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto mwaka 2008.

Kupitia programu hii tuna Mpango Mkakati wa Kukinga na Kudhibiti Saratani ya

Page 4: Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

Mlango wa Kizazi (2011-2016). Mwongozo wa kutoa huduma umeandaliwa pamoja

na miongozo ya mafunzo kwa watoa huduma na ujumbe wa kuelimisha jamii kupitia

njia mbalimbali. Kupitia programu hii tumeweza kuanzisha vituo zaidi ya 130

vinavyotoa huduma ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi katika Mikoa 17

hapa nchini. Ukilinganisha na mwaka 2008 tulipokuwa na vituo vinne tu vilivyokuwa

vinatoa huduma hii ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na tiba ya

mabadiliko ya awali, haya ni maendeleo makubwa.

Ndugu Wananchi,

Kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Serikali imeendelea kushirikiana na

wadau mbalimbali wakiwemo MEWATA, Marie Stopes, WAMA na wengineo

kutekeleza mpango wa “Utepe wa Pinki na Utepe Mwekundu” yaani “Pink Ribbon Red

Ribbon”. Kupitia program hiyo, kampeni ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa

kizazi na matiti ilizinduliwa katika mkoa wa Mwanza mwezi Machi mwaka huu katika

kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Kupitia mpango huo, tumekabidhi mashine 16 za kutolea huduma za matibabu ya

mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi (Cryotherapy machine) kwa

mikoa ya Mwanza, Mara, Iringa, Njombe na Mbeya. Mipango inaendelea kwa mikoa

iliyosalia pamoja na Tabora kupatiwa mashine hizo kuendeleza juhudi za Serikali

kupanua upatikanaji wa huduma hizi katika mikoa yote nchini.

Lengo letu katika kufanya hivyo ni kutaka kupunguza mzigo mkubwa unaoielemea

Hospitali yetu ya kuu kansa ya Ocean Road. Pia, tunataka kuwapunguzia wanawake

adha na gharama ya kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kwa ajili ya

uchunguzi. Tunatambua umuhimu wa huduma hizi kuwa karibu zaidi na walipo watu

ili ziwafikie wanawake wote bila kujali hali zao za kipato.

Ndugu Wananchi;

Katika jitihada za kutokomeza maradhi haya, Serikali, kupitia Mpango wa Taifa wa

Chanjo, imeanza kutoa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa Kizazi ya “Human

Papilloma Virus (HPV)”. Chanjo hii hutolewa kwa watoto wa kike wenye umri wa

miaka 9. Chanjo hii hukinga wasipate maambukizi ya virusi ambavyo husababisha

Saratani ya Mlango wa Kizazi. Wizara ya Afya tayari imezindua mpango huo wa utoaji

Page 5: Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

wa chanjo ya HPV kwa wasichana tarehe 29 Aprili, 2014 wakati wa Maadhimisho ya

Wiki ya Chanjo Duniani na mama Salma Kikwete. Mpango huo ulizinduliwa kwa

Halmashauri tano za Hai, Siha, Moshi Vijijini, Moshi Mjini na Rombo za Mkoa wa

Kilimanjaro, kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa azma ya kutoa chanjo hii nchi nzima

ifikapo mwaka 2016.

Shukrani kwa Wadau

Ndugu Wananchi;

Napenda kutoa pongezi na shukrani za pekee kwa MEWATA kwa kazi nzuri na kubwa

ya kukuza uelewa wa jamii na kuhamasisha uchunguzi wa saratani zinazowapata

wanawake. Ni dhahiri kwamba ili jambo hili lifanikiwe lazima liwe na mshika bango

wake. Bahati nzuri ndugu zetu wa MEWATA wamejitoa kimasomaso na wamefanya

kazi ya Serikali kuwa rahisi. MEWATA imekuwa inafanya kazi kwa karibu na Serikali

pamoja na wadau wengine katika kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya Saratani ya

Matiti na ya Mlango wa Kizazi. Kama nilivyokwisha kusema awali, juhudi hizo

zimewafikia wanawake wengi nchini na kuokoa maisha yao.

Aidha, napenda kuchukua fursa hii kutambua na kutoa shukrani maalum kwa Shirika

la Marie Stopes na wadau wote ambao wanashirikiana na Serikali katika kupambana

na tatizo hili kubwa la Saratani ya Mlango wa Kizazi. Vilevile, tunawashukuru wale

wote wanaotoa huduma ya afya ya uzazi na mtoto nchini. Napenda kwa mara nyingine

tena kuwahakikishia ushirikiano wa Serikali ya CCM ninayoiongoza kwenu. Ni,

dhamira yetu kupunguza na ikiwezekana hata kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na

Saratani ya Mlango wa Uzazi na Saratani ya Matiti ambazo kwa kweli zinaweza

kuzuilika.

Wito kwa Wananchi

Ndugu Wananchi;

Natoa wito kwa wanawake wa Tabora kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa

saratani hizi na wataalamu walioko hapa. Napenda kuwatoa hofu kuwa saratani ya

mlango wa kizazi na saratani ya matiti siyo magonjwa ya aibu au ya mkosi au uchawi

au laana na wala siyo magonjwa yasiyotibika. Magonjwa haya huweza kumpata

mwanamke ye yote, awe ameolewa au hajaolewa, awe amezaa au hajazaa, awe tajiri au

maskini. Madhali ni mwanamke anaweza kupata. Sharti lake la kupona ni

kugundulika mapema na kuanza tiba mapema. Kuchelewa kugundulika na kuchelewa

Page 6: Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

kuanza matibabu ndiko kunakosababisha vifo kutokana na maradhi haya. Waswahili

wana msemo usemao, mficha maradhi kifo humuumbua. Hivyo ndugu zangu kina

mama nashauri mfanye uchunguzi mapema, ili kama kuna tatizo muanze tiba

mapema.

Napenda kutumia fursa hii, kuwaasa akina baba na walezi nao kusaidia katika juhudi

za kuzuia na kutibu magonjwa haya ya saratani ya wanawake. Mwanamke anayepata

magonjwa haya anahitaji matunzo na upendo siyo masimango na unyanyapaa.

Masimango na unyanyapaa huwafanya wanawake waogope kujitokeza kuchunguza

afya zao na kupatiwa tiba kwa kuogopa kubaguliwa au kuachwa. Magonjwa haya

yanatibika. Si kila mwanamke anayepata saratani hufariki dunia. Kinachotakiwa ni

baba na mama kushirikiana kumpeleka mama kufanyiwa uchunguzi na kupata tiba

iwapo atagundulika kuwa na maradhi. Saratani siyo ugonjwa wa zinaa, hivyo,

msiwanyanyapae akina mama bali muwalee na kuwatunza ili waweze kurejea katika

hali zao za kawaida. Akina baba muwe ndiyo nguzo ya mafanikio katika mapambano

dhidi ya saratani.

Na, kwa wanaume wenzangu, tujenge mazoea ya kupima afya zetu hususan kuhusu

saratani ya tezidume (prostate). Hii ni saratani inayoua wanaume wengi duniani na

hapa nchini. Lakini nayo kama zilivyo saratani za matiti na mlango wa kizazi

zinatibika kama zitagundulika mapema. Kila mkienda kupima afya pimeni afya ya

tezidume mjue mustakabali wenu.

Ndugu Wananchi;

Sote tukiungana pamoja tunaweza kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi na

saratani ya matiti. Nia ya kutokomeza maradhi haya tunayo, sababu ya kutokomeza

tunayo na uwezo wa kuyatokomeza tunao. Kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu zetu

pamoja. Mimi na mke wangu Mama Salma Kikwete tuko nanyi na tutaendelea kuwa

nanyi bega kwa bega katika vita hii sasa na hata baada ya kuacha Urais

mwakani. Inawezekana, timiza wajibu wako!

Ndugu Wananchi;

Kwa vile niko Tabora ni vyema nikatumia nafasi hii pia, kuyazungumzia baadhi ya

mambo niliyoyazungumzia au kuahidi kufanya safari zilizopita. Kwa upande wa

barabara, napenda kuwahakikishia kuwa barabara kuu zinazoendelea kujengwa hapa

Page 7: Hotuba Ya Mhe. Kikwete Tarehe 7-6-2014 Morogoro

Mkoani Tabora tutazimaliza. Subira yavuta heri. Barabara ya Urambo –Kaliua ujenzi

utaanza mwaka huu wa fedha na Chaya – Nyahua, mchakato wa kutafuta fedha

unaendelea ili nayo ujenzi wake uweze kuanza kabla ya mimi kumaliza kipindi changu

cha uongozi. Kuhusu kupata maji ya Ziwa Victoria, kwa Igunga, Nzega, Tabora,

Urambo na Sikonge hatua za awali zimeanza na kinachofuatia ni kutafuta fedha kwa

ajili ya mradi huo mkubwa. Tunakusudia kuiomba Serikali ya India ambayo ndiyo

iliyogharamia matayarisho ya mradi. Tuna matumaini ya kufanikiwa. Sote tuzidi

kuomba iwe hivyo.

Kwa upande wa tatizo la wakulima wa tumbaku kutokulipwa stahili zao na vyama vya

ushirika nimeelezwa na kulielewa. Kuna tuhuma za wizi na ubadhilifu. Nimemuagiza

Inspekta Jenerali wa Polisi atume watu wake wa upelelezi wa makosa ya Jinai waje

wafanye uchunguzi ili wahusika wakamatwe na kufikishwa Mahakamani na kupewa

adhabu zinazostahili. Ameniahidi kuwa keshokutwa Jumatatu watu hao

watakuja. Wapeni ushirikiano unaostahili ili tukomeshe uhalifu na dhuluma

zinazofanywa na Maofisa wa Vyama vya Ushirika na taasisi za fedha kwa muda mrefu

sasa.

Baada ya kusema hayo, naomba nitangaze sasa zoezi hili la uchunguzi wa Saratani ya

Mlango wa Kizazi na ya Matiti limefunguliwa rasmi.

Nawashukuruni sana.