16
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya Kitaifa 15 Agosti 2012

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

  • Upload
    others

  • View
    37

  • Download
    0

Embed Size (px)

Citation preview

Page 1: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

1

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania

Katiba Mpya na Mustakabali waWakulima wadogo Warsha ya Kitaifa

15 Agosti 2012

Page 2: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

2

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

1. Utangulizi

Warsha ya kitaifa ya MVIWATA ya kila mwaka ilifanyika tarehe 15 Agosti 2013 ambapo mada kuu ilikuwa ni “Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo”. Warsha hiyo iliandaliwa na kufanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa MVIWATA ambao wenyewe ulifanyika tarehe 16 Agosti 2012 katika Hoteli ya Glonency 88 iliyopo Morogoro.

Washiriki 236 (wanaume 143 na wanawake 93) walihudhuria warsha na Mkutano Mkuu wa MVIWATA, wakiwemo, wakulima wanachama wa MVIWATA, wawakilishi kutoka wizara na asasi za serikali, wawakilishi kutoka mashirika wenza, viongozi na timu ya menejimenti ya MVIWATA, wawakilishi wa vyombo vya habari na wanafunzi kutoka vyuo vikuu waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo.

Malengo ya warsha yalikuwa kama ifuatavyo: Kutafakari mchakato unaoendelea juu ya uundwaji na upatikanaji wa katiba mpya na

mustakabali wake katika kulinda maslahi na haki za wakulima wadogo Kutafakari ushiriki wa wakulima wadogo katika mchakato wa upatikanaji wa katiba

mpya ya Tanzania Kuandaa maoni ya wakulima wadogo kupitia MVIWATA na kuyawasilisha kwa tume

inayoratibu mchakato wa maoni ya katiba mpya.

Picha za washiriki wa warsha wakisikiliza mawasilisho. Kulia; Mgeni Rasmi, Ndugu Joseph Butiku, Mkurugenzi Mtrendaji wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa MVIWATA.

Mada za Warsha:Warsha hii ilikuwa na mada kuu mbili:i. Mchakato wa ukusanyaji maoni ya katiba mpya na nafasi ya wakulima wadogo:

Mada hii iliwasilishwa na Ndugu Deus Kibamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania.

ii. Masuala muhimu/mahususi yanayohusu wakulima wadogo katika katiba mpya: Mada hii iliwasilishwa na Ndugu Bashiru Ally, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mchakato wa warshaWarsha ilianza kwa utangulizi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Ndugu

Page 3: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

3

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

Stephen A. Ruvuga ambaye aliwakaribisha wajumbe wote, wageni waalikwa na kufuatiwa na utambulisho wa washiriki wote wa warsha.

Mkurugenzi Mtendaji alitoa maelezo ya awali juu ya malengo ya warsha na kutaja kuwa msingi wa mada ya warsha ambayo inatokana na maazimio ya Mkutano Mkuu wa 16 ambao ulilenga kuwawezesha wakulima kushiriki katika mchakato wa katiba mpya. Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu na kuwezesha mchakato huu na kuwakumbusha wakulima kuwa wao ni kundi kubwa hivyo lazima washiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata katiba mpya. Alisisitiza wakulima kutumia chombo chao cha MVIWATA na jukwaa la Mkutano Mkuu wa 17 katika kutoa maoni yao yatakayowasilishwa kwa tume ya kukusanya maoni yatakayotumika katika kuandaa katiba mpya.

Baada ya maelezo haya ya awali alikaribisha washiriki kutoka katika taasisi wadau na marafiki wa MVIWATA akiwemo Ndugu Esta Mbigo Kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Ndugu George Mboje kutoka ANSAF, Ndugu Joe Mzinga kutoka ESAFF na Ndugu George Onyango kutoka SCC ili waweze kutoa salaam kwa niaba ya wadau wote waliokuwa wamealikwa.

Baada ya salaam za wadau hao, Mkurugenzi alimkaribisha Mwenyekiti wa MVIWATA Ndugu Habibu Simbamkuti ili atoe nasaha zake na baada ya hapo aweze kumkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa warsha. Mwenyekiti aliwaeleza wajumbe kuwa ni bahati sana kumpata mgeni rasmi kama Ndugu Joseph Butiku ambaye kwa nafasi yake, kama mjumbe mteule wa Tume ya Katiba, itakuwa ni rahisi akishapokea ujumbe kutoka kwa wakulima na kuufanyia kazi. Mwenyekiti wa MVIWATA alisisitiza kuwa mada kuu inayojadiliwa ni katiba mpya na hili ni suala kubwa kwa wakulima kwani kuchezea katiba ni sawa na kuchezea maisha na ndiyo maana MVIWATA inataka katiba itakayoundwa ilinde maslahi ya mkulima mdogo. Baada ya hapo alimkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa warsha.

Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA akielezea malengo ya warsha

Mwenyekiti wa MVIWATA akimkaribisha mgeni rasmi

Page 4: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

4

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

2. Ufunguzi Rasmi wa Warsha

Mgeni Rasmi, Ndugu Joseph Butiku, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere na mjumbe wa Tume ya Kukusanya maoni ya katiba mpya alianza kuwapongeza viongozi wa MVIWATA, watendaji, wageni waalikwa kwa kushiriki katika kongamano hilo ambalo kwao ni fursa ya kujadili mustakabali wao. Mgeni rasmi alipongeza na kushukuru viongozi wa MVIWATA kwa kumualika kuwa mgeni rasmi; hata hivyo alisema kuwa kwa nafasi yake ya kama mjumbe wa Tume ya Katiba, hawezi kutoa maoni kama mwanaharakati bali atajaribu kutoa elimu juu ya sheria na miongozo juu ya uundwaji wa katiba mpya na kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.

Katika hotuba yake, mgeni rasmi aligusia mambo yafuatayo:i. Umuhimu wa elimu kuhusu Sheria juu ya Mabadiliko ya Katiba,ii. Maelezo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) iliyopo.iii. Katiba mpya na mustakabali wa maslahi na haki za wakulima wadogoiv. Maeneo machache ambayo tayari yalikuwa yamesemewa na wakulima wadogo katika

baadhi ya mikoa ya Tanzania ambapo tume imeshapita:

Katika hotuba yake, mgeni rasmi alianza na hadithi ifuatayo;”Nikiwa mdogo nilikuwa na rafiki ambaye alipenda sana asali. Jirani na nyumbani kwetu kulikuwa na mti wenye nyuki na asali. Siku moja tuliamua kwenda katika ule mti ambapo rafiki yangu alichukua mti na kuchovya katika mzinga ili kulamba asali; akachovya mara ya kwanza,akalamba; akachovya mara ya pili,akalamba; alipochovya mara ya tatu alitoka na nyuki ambao walimng’ata na kumjeruhi mpaka aliposaidiwa na watu. Hadithi hii naifananisha na mchakato wa uundaji wa katiba ambapo Tume imechokoza Watanzania ambao nao wametikia kutoa maoni na matakwa mengi ambayo itabidi tujadili vizuri namna ya kuyafanyia kazi.”

Katika simulizi hii Ndugu Butiku alikuwa akifananisha tukio hilo na zoezi la kuwasukuma, kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi watoe maoni yao ambapo kwa sasa hamasa imekuwa kubwa, mijadala imekuwa mingi na Tume haina budi kusikiliza kwa namna yoyote.

Page 5: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

5

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

i. Elimu kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya KatibaMgeni Rasmi alielezea kuwa taifa letu limeamua kuanzisha mchakato wa kuandika katiba ya nchi yetu kutokana na majadiliano ya muda mrefu kuhusu mapungufu yaliyomo katika katiba ya sasa ambayo yalitolewa na watu binafsi na makundi ya Watanzania wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa hasa vyama vya upinzani katika nyakati na mahali tofauti. Baadhi ya sababu za madai hayo ni kama zifuatazo: Watanzania wengi leo (wasomi, watu wenye uelewa na uzoefu tofauti) hawakushiriki

katika kuandaa Katiba zilizopita, na hata ile ya sasa ya mwaka 1977. Katiba ya sasa imebadilishwa mara nyingi sana (mara 14) na hivyo imejaa viraka, hata

hivyo wakati katiba za zamani zinabadilishwa wasomi walikuwa wachache sana. Katiba ya sasa haikidhi matakwa ya leo ya taifa ambayo ni mengi, na yanayohusu

makundi mengi mbalimbali. Matatizo ya sasa ya taifa yanatokana na mapungufu ya katiba. Mifano tatizo kuu la

kushuka kwa maadili, kukithiri kwa umaskini, uhalifu n.k.

Kutokana na madai hayo ya muda mrefu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, aliridhia hoja ya kuwepo mchakato wa mabadiliko ya katiba kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kujadili na kufikia muafaka wa aina na nchi wanayoitaka, na aina ya katiba itakayotumika kuongoza taifa na wananchi wake.

Alielezea kuwa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya hauendeshwi kienyeji; bali unaendeshwa kwa mujibu wa katiba ya sasa na sheria za nchi. Aliwafafanulia wajumbe kwamba ibara 98 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), vifungu (1) na (2) vinaruhusu kufanya mabadiliko ya masharti ya katiba.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura 83 (Toleo la mwaka 2012) imetungwa kwa kuzingatia hiyo ibara ya 98 ya Katiba iliyopo kwa mujibu wa vifungu (1) na (2) vya Katiba hiyo. Sheria hiyo ya mabadiliko ya katiba ndiyo iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa mujibu wa ibara ya 5 na 6. Vile vile sheria hiyo kupitia vifungu vyake imefafanua mambo yafuatayo: imetoa ufafanuzi katika utangulizi wa mambo ya msingi, ikiwa ni pamoja na maana ya

katiba katika mchakato huu; imetaja na kuorodhesha madhumuni ya sheria yenyewe imetaja hadidu za rejea za tume katika ibara ya 8, 9, 17 na katika Tangazo la Serikali

namba 110 la 2012. imeweka utaratibu wa utendaji wa tume ambao unawashirikisha wananchi katika

mchakato mzima. inataja awamu nne muhimu zinazowashirikisha wananchi katika mchakato wa

mabadiliko ya katiba kama ifuatavyo:

Awamu ya Kwanza: inahusu mikutano na mabaraza yanayoitishwa na Tume katika sehemu na nyakati mbalimbali kama Tume itakavyoamua: Utaratibu huu unawakutanisha wananchi na Tume ana kwa ana, na kutoa maoni yao mmoja mmoja siyo katika makundi, awamu hii itaendelea hadi mwishoni mwa Octoba, 2012.

Awamu ya Pili ya Mabaraza ya Katiba: Tume itaunda, katika muda maalum, mabaraza ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu ya katiba. Maoni

Page 6: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

6

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

yatatolewa juu ya rasimu ya katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi. Mabaraza haya ya katiba yanaundwa kutokana na makundi yafuatayo: asasi zisizo za kiserikali, wakulima, wafugaji, wavuvi, madhehebu ya dini, vyama vya ushirika, vyama vya siasa, taasisi za elimu ya juu, makundi yenye mahitaji maalum (wazee, walemavu, wanawake, vijana), vyama vya wafanyakazi

Awamu ya Tatu: Rasimu ya Katiba iliyojadiliwa katika mabaraza ya Katiba na kufanyiwa maboresho na Tume, itawasilishwa katika Bunge Maalum litakalokuwa na wabunge wafuatao baada ya kutangazwa na Rais katika Gazeti la Serikali: Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wajumbe wote wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, Wajumbe 166 watakaoteuliwa kutoka ( asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kisheria,

vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu, makundi yenye mahitaji maalum katika jamii, vyama vya wafanyakazi, jumuia ya wakulima, jumuia ya wafugaji, kikundi kingine chochote cha watu wenye malengo yanayofanana)

Awamu ya Nne: Uhalalishaji wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu. Utafanywa na wananchi wote wenye sifa za kupiga kura, watapiga kura ya maoni ya ndiyo au hapana ili kuhalalisha au kutohalalisha katiba inayopendekezwa. Katika awamu hii wananchi watapewa elimu na watahamasishwa. Tume na vyama vya siasa na vyama vya kijamii vinaweza kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya katiba inayopendekezwa. Siku 30 zimetengwa kwa shughuli hii kuanzia siku ya Rasimu ya Katiba kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.

ii. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).Maana ya Katiba: imefafanuliwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura 83 Toleo la 2012. Kwa lugha nyepesi tu; katiba ni sheria kuu, au sheria mama inayotokana na mazungumzo na kufikia muafaka wa watu katika makundi mbali mbali. Taifa au nchi inaweza kuwa na katiba yake iliyoandikwa au isiyoandikwa.

Katiba yetu inazo Sura 10, Sura ya kwanza, yenye sehemu 3, ndiyo yenye mambo ya msingi ya Taifa kama ifuatavyo: eneo, mipaka na jina la taifa, misingi ya taifa (amani, uhuru, haki, udugu), malengo ya taifa, haki na wajibu muhimu,

Mgeni Rasmi alisema kuwa tume imebaini maeneo 13 muhimu yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, yanayoweza kutolewa maoni na wananchi. Mambo haya hayamfungi mwananchi asitolee maoni, kuongea jambo au mambo mengine yoyote yaliyomo moyoni au rohoni mwake. Mambo hayo ni kama ifuatavyo: utaifa, uzalendo, maadili na uwajibikaji haki na wajibu wa raia wajibu wa serikali dola, mamlaka yake na mgawanyo wa madaraka ardhi, maliasili na rasilimali za taifa, muungano wa Tanzania demokrasia, vyama vya siasa na uchaguzi, mfumo wa utawala uhusiano wa tanzania, Afrika na ulimwengu uwakilishi na mfumo wa kutunga sheria mfumo wa utoaji haki (mahakama zetu)

Page 7: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

7

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

mfumo wa utawala na vyombo vya utawala mamlaka na madaraka ya umma, kupitia serikali za mitaa ulinzi na usalama

Baada ya kuielezea, mgeni rasmi aligawa nakala za katiba alizokuwa amekuja nazo

iii. Katiba mpya na mustakabali wa maslahi na haki za wakulima wadogoMgeni rasmi alielezea kuwa Katiba yoyote ile inahusu watu; wananchi wote na mali au rasilimali zao na vitu vyovyote vile wanavyozalisha kwa kazi za akili, ujuzi na mikono yao. WAKULIMA WADOGO wa Tanzania ni sehemu kubwa ya Watanzania hivyo wanazo haki zao za msingi kama zilivyotajwa katika Sura ya Kwanza: haki ya usawa wa binadamu, usawa mbele ya sheria; haki ya kuishi, haki ya kufanya kazi, haki ya kupata ujira wa haki, haki ya kumiliki mali (Ibara 9 (i) inasema kwa msisitizo “kwamba matumizi ya utajiri wa taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha Umaskini, Ujinga na Maradhi.”).

Mustakabali wa maskini na haki za wakulima wadogo vinategemea, na vitatokana na mihimili yote ya dola, na hasa serikali inayotazamiwa kutekeleza kazi zake zote kwa kuzingatia misingi yote hiyo. alinukuu kwamba watuwengi wanasikika wakisema kwamba wakulima wadogo ni maskini, tena wanao ujinga mwingi unaowasabibishia washambuliwe na maradhi na washindwe au wachelewe kutumia rasililimali walizo nazo za taifa kuboresha maisha yao. Hata hivyo alisema kwamba ukweli ni kwamba wakulima siyo maskini kiasi hicho. Alisema kwamba tatizo lao la msingi ni ujinga; elimu ya ufahamu ya kutosha na ile ya utambuzi na ujuzi wa jinsi ya kutumia rasilimali zao kuboresha hali ya maisha yao. Ardhi ndiyo rasilimali ya msingi ya taifa lolote na watu wake. Maana nchi au taifa ni watu na maliasili zao zote hasa ardhi na maji. Alisisitiza kwamba wajibu wa wakulima wadogo ni kuhakikisha kwamba wanazitambua, kuzidai na kuzipigania haki zao kwa njia za amani na pia kutimiza wajibu wao. Aliwambia kwamba haki na wajibu wao ni mambo ya kikatiba na yote yamo katika Katiba yetu ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

iv. Baadhi ya maeneo machache ambayo tayari yalikuwa yamesemewa na wakulima wadogo katika baadhi ya mikoa ya TanzaniaNdugu Butiku alidokeza kwamba katika maeneo ambapo tume imekwishapita, baadhi ya maoni yaliyotolewa na wakulima ni kama ifuatavyo ; Katiba iwaangalie wakulima na wafugaji na ieleze jinsi na taratibu za kuwatengea na

kuwamilikisha ardhi Katiba ieleze vizuri taratibu za kutoa fidia kwa wakulima endapo mazao yao

yataharibiwa na wanyama pori Rasilimali (madini n.k.) inayopatikana sehemu fulani iwanufaishe wananchi wa

sehemu ile Wawekezaji wasiruhusiwe kumiliki ardhi kwa muda usiozidi miaka 10 -50 Ardhi isiuzwe kwa wageni, bali ikodishwe tu Kusiwe na ubinafsishaji wa rasilimali za umma Wakulima waliotimiza umri wa miaka 60 walipwe pensheni Katiba ielekeze taratibu za kutoa ruzuku kwa wakulima

Page 8: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

8

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

Ndg. Joseph Butiku akijibu Maswali ya washiriki

Baada ya hotuba ya Mgeni Rasmi, washiriki walipewa nafasi ya kuuliza maswali ambapo maswali mbalimbali yaliulizwa ikiwemo yafuatayo: Bunge maalum la katiba linateuliwa namna gani ni nini majukumu yake? Tanzania ni kubwa sana na ina vijiji vingi, tume itafanyaje kuwafikia wananchi wote? Katika baadhi ya maeneo hasa Zanzibar watoa maoni wamekuwa wakiwekwa kitimoto,

tume itafanyaje kuweka uhuru? Je baadhi ya taasisi kama MVIWATA zinaruhusiwa kutoa maoni ya pamoja? Ratiba ya mzunguko inachelewa kutoka kwa nini isiboreshwa?Mgeni Rasmi aliyajibu maswali kama ifuatavyo: Muundo wa bunge maalum la Katiba umeelezwa katika Sura ya 5 ya Sheria ya

Mabadiliko ya Katiba Ibara ya 21. Jukumu lake ni kujadili maoni ya wananchi na litavunjwa mara tu baada ya kupitisha katiba mpya.

Katika kukusanya maoni kuna miezi 18 imetengwa ambapo Tume itazunguka vijijini, lakini alikiri kwamba kulingana na ukubwa wa nchi yetu siyo rahisi kufika kila eneo.

Alisisitiza kuwa wakati wa kulalamika umekwisha, tutumie muda huu kutoa maoni na kila kitu kiongelewe bila wasiwasi na kwa uhuru wote, mtu atakayeweka pingamizi katika mchakato anaweza kushitakiwa kisheria.

Alieleza kwamba suala la kutoa vipeperushi kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi ni ruksa ila inatakiwa kupata kibali cha Tume. Pia aliwambia washiriki kwamba vyombo kama MVIWATA vinaweza kupeleka maoni yake mbele ya Tume kama maoni ya asasi au chama cha wakulima.

Akiongelea suala la kuchelewa kwa ratiba, Mgeni rasmi alisema kuwa mwanzoni kulikuwa na ucheleweshaji lakini kwa sasa wameboresha sana na wananchi watakuwa wakipata ratiba mapema sana.

Shukrani kutoka kwa Makamu Mwenyekiti -MVIWATABaada ya hotuba ya Mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa MVIWATA, Bi. Veronica

Page 9: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

9

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

Sophu alimshukuru mgeni rasmi kwa hutuba yake. Alisema kwamba hotuba hiyo ni kama darasa kwani mgeni rasmi alifundisha mchakato mzima wa uandaaji wa katiba mpya kwa kutoa mwongozo na vielelezo juu ya mchakato mzima. Alikiri kuwa kwake ni mara ya kwanza kuishika katiba na aliwaomba wakulima wenzake kufikisha elimu hiyo kwa wakulima wengine.

Uzinduzi wa Kitabu; Insha za Mapambano ya WanyongeKatika kuhitimisha ratiba yake kwa siku hiyo, mgeni rasmi alizindua kitabu kiitwacho Insha za Mapambano ya Wanyonge kilichoandikwa na Profesa Issa Shivji na kuhaririwa na Mwlimu Bashiru Ally. Kitabu hicho ni mkusanyiko wa makala mbalimbali kuhusiana na historia ya nchi yetu. Kitabu hicho kilikuwa tayari kimezinduliwa Dar es Salaam mwezi Aprili 2012 na huo ulikuwa uzinduzi maalum kwa ajili ya MVIWATA. Sababu kubwa ya kitabu hiki kuzinduliwa kwa mara ya pili na MVIWATA ni kwa kuwa mada moja wapo ndani ya Kitabu hiki inaongelea maazimio ya MVIWATA wakati wa tafakari ya miaka 50 ya Uhuru, na mustakabali wa wakulima wadogo. Ndiyo maana mwandishi wa kitabu hiki alipenda kizinduliwe kwa mara ya pili na MVIWATA kwani kitabu hicho ni kama mali ya MVIWATA.

Mgeni Rasmi akizindua Kitabu

Page 10: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

10

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

3. Mawasilisho ya Mada

3.1 Mada ya Kwanza: Mchakato wa Ukusanyaji wa Maoni ya Katiba Mpya na Nafasi ya Wakulima Wadogo:- Ndugu Deus Kibamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania.

Historia ya Mchakato wa KatibaMwasilishaji, Ndugu Deus Kibamba alianza kwa kuwasilisha historia ya mchakato wa upatikanaji wa katiba, na kueleza kwamba vuguvugu la kudai katiba mpya lilianza miaka ya 1960 na baadhi ya watu waliokuwa wakiidai katiba walipelekwa jela. Hata hivyo, alisema kuwa wakati wa uongozi wa Rais Mwinyi na Mkapa walilifumbia macho suala la Katiba.

Alisema kwamba katika ma-Rais wote ni Rais Kikwete peke yake ambaye ameweza kuruhusu suala la mabadiliko ya katiba na ukweli unaonyesha kuwa anapata wakati mgumu katika mchakato huu wa uundaji katiba mpya.

Ndugu Deus Kibamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania akiwasilisha mada katika Warsha na Mkutano Mkuu wa 17 wa MVIWATA.

Madai ya katiba mpya yameongezeka kutokana na kukithiri kwa mapungufu katika katiba ya sasa na alitaja mfano wa suala la muungano, na kudai kwamba kuzuia kuujadili siyo suluhisho la matatizo yaliyopo sasa.

Alisisitiza kuwa wengi wanaoguswa na wanaopenda katiba ibadilishwe ni wale wenye maisha magumu, lakini kwa wale wenye maisha bora wanaonufaika na

Page 11: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

11

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

mapungufu yaliyomo kwenye katiba ya sasa hawapendi katiba ibadilishwe kwa sababu mabadiliko yanaweza kuathiri maslahi yao.

Majukumu ya Jukwaa la Katiba TanzaniaAlitaja kuwa majukumu ya Jukwaa la Katiba ni kutoa elimu, kuwahamasisha watu kushiriki katika mchakato mzima wa utoaji maoni juu ya katiba mpya na kufuatilia tume ya ukusanyaji maoni ili wasivunje katiba. Akielezea baadhi ya changamoto alisema kuwa mwitikio wa wananchi katika kutoa maoni upo chini sana, na pia makao makuu ya Tume yapo karibu na ofisi za makao makuu ya polisi hivyo kuleta hofu kwa wananchi katika mchakato mzima wa utoaji maoni. Sheria ya katiba ya maoni inapingana na katiba yenyewe, mfano: sheria inazuia kutoa elimu ya katiba kwa wananchi na ukikutwa umetoa elimu bila kibali cha Tume adhabu yake ni kifungo cha miaka 5. Sheria hii ipo kwenye mchakato wa marekebisho na Rais amekubali kubadilisha ila utekelezaji wake umechukua muda mrefu.

Hatua za Mchakato wa upatikanaji wa katiba.Alizielezea hatua za upatikanaji wa Katiba kuwa ni: Tangazo kwenye gazeti la serikali Kutunga sheria ya marekebisho ya Katiba Uteuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba; makundi mbalimbali yalitakiwa

kupeleka majina ya wawakilishi ili kupata wajumbe wa tume. Unapotokea ugumu katika sheria ya katiba basi hata utekelezaji unakuwa na changamoto.

Akielezea tume iliyoundwa alisema kuwa tume hii ni huru ambayo imeshirikisha makundi mengi.

Hata hivyo, alisema kuwa ugumu ulitokea wakati wa uundaji wenyewe wa kamati hiyo kwani majina mengi yaliwasilishwa na hivyo kupata ugumu wa kuchagua nani awakilishe mwingine.

Kazi ya tume ni kubwa na inatakiwa wajumbe watumie muda mwingi kutafakari maoni ya wananchi, hata hivyo inashangaza kuona baadhi ya wajumbe waliochaguliwa ndani ya tume wanatumia muda mrefu wakiwa nje ya shughuli za Tume huku wakiendelea na shughuli zao kama kawaida kitu ambacho hakiruhusiwi. Kuunda Bunge Maalum la Katiba: Bunge hili litakuwa na wawakilishi kutoka

makundi mbali mbali hata hivyo haiko wazi wajumbe wanapatikanaje. Bunge hili litajadiliana rasimu ya katiba iliyopitiwa na wananchi

Kupiga kura ya maoni/maamuzi: Baada ya bunge kupitisha rasimu ya katiba, wananchi watatakiwa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha katiba.

Uzoefu mpaka sasa na mapungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoniBaadhi ya mapungufu yaliyoonekana mpaka sasa katika ukusanyaji wa maoni ya katiba ni kama ifuatavyo: Kwa baadhi ya mambo (suala la muungano) kuzuiliwa kujadiliwa wakati wa

mchakato huu, Muda mdogo wa utoaji elimu kwa wananchi juu ya katiba na mchakato wa

kuunda katiba mpya (Ilihitajika mwaka 1 au 2 kujadiliana juu ya katiba). Kuna uhamasishaji duni, muda wa uhamasishiji ungefanyika jioni na siyo asubuhi.

Page 12: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

12

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

Ukusanyaji wa maoni kutowafikia wananchi wote na wakati mwingine kuwepo kwa uhuru mdogo kwa wananchi kutoa maoni yao. Ratiba haitolewi kwa wakati, haipo wazi ni siri, na muda mfupi sana hutumika kukusanya maoni

TuendakoAlimalizia mawasilisho yake kwa kusema kuwa lazima tuvunje ukimya, mijadala ifanyike kila kona na kwa kuwa wakulima ndiyo wengi basi washiriki kikamilifu kutoa maoni yao katika mchakato huu wa uundaji katiba mpya.

3.2 Mada ya Pili: Masuala muhimu/ mahususi yanayohusu wakulima katika katibaMada hii iliwasilishwa na Mwalimu Bashiru Ally, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisisitiza kwamba mchakato wa kutunga katiba ni muhimu sana na kila mwananchi anapaswa kushiriki pasipo kubaguliwa kwa namna wala sababu yoyote.

Umuhimu wa utungaji katiba: Alieleza kuwa mchakato huu usitenganishe mtu mmoja na mwingine kwa sababu ya elimu, vipaji, vyeo na mali, kitu muhimu ni kuwa Mtanzania ashiriki. Mihadhara hii inatakiwa kuwa ya kuelimishana, kuhamasishana na kushirikishana na siyo ya kutengana na kubaguana hivyo inatupasa kusimama na kushiriki kwa pamoja kutoa mapendekezo katika mchakato wa kupata katiba mpya. Mchakato huu ulifananishwa na mchakato wa kutunga mimba ambapo hauna vigezo zaidi ya sifa za kutekeleza.

Katiba iguse mfumo wa uzalishaji mali: Mwezeshaji alisema kwamba kwa upande wa wakulima, katiba inapaswa kugusa sehemu ya uzalishaji mali kwa kutoa fursa sawa kwa upatikanaji wa rasilimali ardhi, maji na misitu na si vinginevyo. Rasilimali za taifa kama madini, misitu na wanyama visibinafsishwe na kama kutakuwa na haja basi taifa liweze kumiliki hisa au kuwa na mfumo wa kampuni ambapo utaiwezesha nchi kupata faida kutokana na kuwepo kwa

Page 13: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

13

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

rasilimali hizo. Suala la upatikanaji wa pembejeo na mikopo kwa wakulima liwe jukumu la serikali kwenye taasisi za kifedha kisha iwawezeshe wakulima kuzalisha kwa mfumo ulio bora ili pindi panapotokea mabadiliko ya tabia nchi au hali ya hewa kubadilika basi wakulima wapate mtetezi wa kuwasemea kwenye vyombo vya fedha kutokana na mavuno madogo yanayopatikana kutokana.

Katiba pia inapaswa kuangalia ustawi na hifadhi ya jamii: Katiba inatakiwa kuonesha mfumo wa haki na usawa wetu kama jamii ili kila mwananchi aweze kupata huduma ya elimu, afya na kujitawala hivyo tuwe na vipaumbele ambavyo vitakuwa na faida kwetu. Hakuna huduma yoyote leo hii inayotolewa kwa mkulima maskini bali huduma zote zimezibwa na matajiri kwa kila nyanja.

Alisisitiza katiba ilinde demokrasia ya Watanzania: Katiba isiangalie uchaguzi tu, bali iguse haki za kila raia bila kuangalia jinsia, elimu, wala uwezo. Alisema kwamba ni vyema kukawa na watendaji vijijini wanaowajibika kwa wananchi. Alishauri katiba izuie watu wachache kujilimbikizia mali, hasa kwa njia haramu ili kujenga mfumo wa uchumi wa usawa.

Katiba sio kikombe cha babu cha kutibu magonjwa yote sugu kwa mkupuo: Mchakato huu usisababishe kusimama kwa shughuli zingine za kudai haki na maslahi yetu kwa sasa kwa sababu ya kisingizio cha ubovu wa katiba ya sasa. Hivyo suala la kudai haki na maslahi yetu linapaswa kuendelea. Alishauri mikanda ya mihadhara ya Prof.Shivji kwenye vipindi vya televisheni na vitabu vitumike ili kuchochea na kuonesha njia au chachu ya kuendeleza nia thabiti ya kumtetea mkulima mdogo aliye maskini mkubwa katika nchi hii.

Mwisho alitoa msisitizo kwa wakulima akiwaasa kwamba msimu wa kunung’unika na kulalamika umekwisha hivyo ni vyema wakaweka nguvu zao kwenye mchakato huu ili kupata katiba ambayo itasimamia misingi na utaifa wetu kwa kuzingatia maslahi ya watanzania wote kama taifa na akashauri kamwe tusitoe nafasi kwa watu ambao watatuvurugia nafasi hii adhimu tuliyonayo.

3.3 Mapendekezo ya MVIWATA juu ya KatibaMkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA, Stephen A. Ruvuga aliwasilisha mapendekezo ya maoni ya maboresho ya katiba yaliyokuwa yamefanyiwa kazi na kikundi kidogo na kuomba mkutano mkuu kuyaboresha ili baada ya hapo yapelekwe kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba kama mapendekezo ya MVIWATA.

Page 14: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

14

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

Mawasilisho yaliyofanyika yaliongelea vipengele chanya vya katiba, madhaifu yaliyomo katika katiba na kuanisha maeneo yanayopendekezwa kuboreshwa ikiwemo;

Kuwepo kwa dira ya taifa, kupunguza mamlaka ya Rais, wabunge wa kuchaguliwa wasipoteze nafasi zao hata wakipoteza uanachama wa chama, mawaziri na ma-manaibu waziri wasiteuliwe kutokana na wabunge, kuwe na ukomo wa ubunge, ardhi na rasilimali nyingine ziwekwe kwenye katiba kama haki za kila Mtanzania, maeneo yenye utata katika muungano yajadiliwe, mfumo wa uchaguzi wa Rais kwa ushindi wa walau 51% urejee, kuwepo na mgombea binafsi, Spika wa Bunge asitokane na chama chochote, Kuwe na vyombo vya usimamizi wa ardhi na haki sawa katika umiliki na matumizi ya ardhi.

Kufunga warshaWarsha ilifungwa rasmi na Ndugu George Onyango, mwakilishi wa SCC kutoka Nairobi Kenya. Alimshukuru M/kiti kwa kuchagua mada hii ambayo itasaidia wakulima kuchangia katika mchakato wa katiba. Alishangazwa na jinsi watu walivyochangia hasa akina mama, hii ilionyesha ni jinsi gani watu walivyo na uelewa. Aliwahimiza wakulima kutumia nakala za katiba walizopewa katika kujifunza na kuwafundisha wakulima wengine kabla tume haijapita katika maeneo yao. Aliwahimiza wakulima kutoa maoni yao na kutoacha nafasi yao ichukuliwe na watu wengine. Warsha ilifungwa rasmi saa 12:30 jioni.

Page 15: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

15

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

Maazimio ya Warsha

1. Wakulima wawe na utaratibu wa kuelimishana masuala ya katiba ya nchi katika ngazi za vijiji na kata.

2. MVIWATA ifanye utaratibu wa kuwaelemisha wanachama wake juu ya mchakato na juu ya katiba

3. Wakulima wajipange kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni kuhusu katiba mpya4. MVIWATA ihusishe wataalam marafiki zake ili kuboresha mapendekezo yake

kabla ya kuyapeleka kwa Tume. 5. MVIWATA iweke mchakato wake wa ndani wa kukusanya maoni ya wanachama

wake, kuyajumuisha kisha kuyawasilisha katika Tume.

Page 16: Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo Warsha ya ...mviwata.org/wp-content/uploads/2014/09/Taarifa-ya... · ya Katiba katika kila wilaya, kuwawezesha wananchi kutoa maoni juu

16

Katiba Mpya na Mustakabali wa Wakulima wadogo

P.O. Box 3220, Morogoro, TanzaniaTel/fax: +255 23 261 4184. Email: [email protected]

www.mviwata.org