Upload
others
View
36
Download
2
Embed Size (px)
Citation preview
KUMKUMBUKA ALLAH (DHIKR - E
ILAAHI)
HOTUBA ILIYOTOLEWA NA
HADHRAT MIRZA BASHIRUDDIN MAHMOOD
AHMAD(RA)
KHALIFAT-UL- MASIH II
_______ Mfasiri:
MUSA A. MPINGA - DAR ES SALAAM
KUMKUMBUKA ‘ALLAH’ (Dhikr-e ilaahi)
Napenda kuelezea masuala yafuatayo:-
- Dhikr-e -ilaahi au kumkumbuka Allah ni nini?
- Kwa nini Dhikr-e -ilaahi ni muhimu?
- Namna mbalimbali za Dhikr-e -ilaahi
- Tahadhari za kuchukua katika kufanya Dhikr-e -ilaahi
- Makosa ya kawaida ya uelewa kuhusu Dhikr-e -ilaahi
- Njia za kukomesha athari za shetani na kuendeleza umakini katika sala
Somo hili lina umuhimu mpana. Linawahusu binadamu wote, wa juu na chini,
matajiri na masikini, wachanga na wazee. Pale utakapotekeleza kwa matendo
mawazo ninayokusudia kuyatoa leo, matokeo yenye manufaa ya Dhikr-e -ilaahi
yatakuwa bayana.
Dhikr-e -ilaahi au kumkumbuka Allah ni nini?
Dhikri, ni neno la kiarabu, maana yake ni kukumbuka. Pale linapotumika kumhusu
Allah, linamaanisha njia za kumkumbuka Allah, kuweka sifa zake akilini, kuzitaja
tena na tena, kuzikubali kwa hamu na ukweli wa moyo, na kutafakari juu ya uweza
wake na nguvu yake.
Umuhimu wa mada hii Dhikr-e -ilaahi ni muhimu kiasi gani? Kwa kifupi somo hili ni nyeti na ni la
umuhimu mkubwa. Sisemi umuhimu mkubwa kwa sababu ya kauli tu, bali kwa
sababu Allah Mwenyewe Ameliita hivyo. Allah Anasema;
Na kwa yakini kumbuko la Allah ni (jambo) kubwa kabisa. (Kurani Tukufu 29:46).
Yaani kumkumbuka Allah kuna daraja la juu zaidi kuliko matendo mengine yote
ya ibada. Kwa hiyo kauli ya kwamba somo hili ni la muhimu sio yangu mimi, ni
tamko la Allah Mwenyewe.
Kwa nini Dhikr-e-illahi ni jambo la lazima?
Kama suala ni la umuhimu mkubwa kiasi hiki, ni dhahiri Islam itaweka mkazo
endelevu juu yake. Na hivi ndivyo hasa ilivyo. Tunaona ukumbusho wa mara kwa
mara juu ya jambo hili katika Kurani Tukufu, kwa mfano:-
Na likumbuke jina la Mola wako asubuhi na jioni (76:26)
Hali kadhalika kuna Hadithi ambamo Mtume Mtukufu (saw) amesema; “Pale watu
wanapokusanyika pamoja kwa ajili ya kumkumbuka Allah, wanazungukwa na
malaika na kufunikwa na rehema kutoka kwa Mola.
Hii ndiyo sababu ya kuchagua mada hii kwa ajili ya mkutano wa mwaka. Maelfu
kati yenu mmekuja kutoka mbali sana ili kuhudhuria mkusanyiko huu.
Nitakapokuwa naelezea mada hii, malaika watakuwa wanawamiminieni rehema
za Mungu. Mtakaporejea nyumbani na kuyafikisha mliyoyasikia, wasikilizaji
watapata rehema, na kwa jinsi hii rehema zitawafikia Wanajumuiyya wote.
Hadithi niliyoitaja mapema inaonyesha kwamba kumkumbuka Allah katika
mkusanyiko ni jambo la baraka. Linavutia malaika ambao pamoja nao, huja na
rehema na msaada wa Allah, kwa hiyo umuhimu wa Dhikri wapaswa kuwa wazi.
Bila shaka malaika watamuauni mtu ambaye kwa kufanya kwake Dhikri, anavutia
upamoja nao mara kwa mara, na kila mara atakumbushwa nao kutenda matendo
mema.
Kuwepo kwa malaika sio utungo wa fikra ya kibinadamu, bali ni ukweli. Mimi
Mwenyewe ninawaona malaika. Nilipata mara moja kuongea nao kirafiki kabisa.
Kwa kuja kwao mara kwa mara, malaika hujenga mapenzi na urafiki na wale
wamkumbukao Allah. Mwenyezi Mungu Anasema;
Enyi mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu wala watoto wenu kumkumbuka
Allah (63:10).
Enyi mlioamini, mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na mtukuzeni asubuhi
na jioni. (33:42 - 43)
Mtume Mtukufu (saw) ametilia mkazo umuhimu wa Dhikri katika hadithi zake.
Hadhrat Abu Musa Ash’ari anasimulia kwamba Mtume Mtukufu (saw) anasema,
“Mfano wa mtu anayemkumbuka Mola wake na yule asiyemkumbuka, ni kama
aliye hai na mfu”. Yule amkumbukaye Allah yuko hai, na yule asiyemkumbuka
amekufa”.
Hadhrat Abi Darda’a anasimulia ya kuwa Mtume Mtukufu (saw) amesema, “Je
nikuambieni juu ya tendo jema na takatifu kabisa hata kwa wafalme, ambalo
huinua daraja lenu, ambalo ni bora zaidi kuliko kutoa dhahabu na madini ya fedha,
ambalo ni bora zaidi kuliko kukutana na maadui na kukata shingo zao, au ninyi
wenyewe kuupata ushahidi? Masahaba wakajibu, Naam, tueleze tafadhali. Mtume
Mtukufu (saw) akasema; “Ni kumkumbuka Allah”.
Sawa na Hadithi nyingine Mtume Mtukufu (saw) amesema; kumkumbuka Allah
kuna malipo makubwa. Masahaba wakauliza, Ewe Mjumbe wa Allah, jambo hili ni
bora kwa malipo kuliko kujitahidi katika njia ya Allah? Akajibu ndio, kwa vile ni
kumkumbuka Allah ndiko kunakomhimiza mtu kuifanya hiyo juhudi.
Haja ya kuzingatia kwa mkazo zaidi Dhikri katika Jamaat yetu.
Huo ndio umuhimu wa Zikri. Hata hivyo, kwa namna fulani baadhi ya
Wanajumuiyya wa Jamaat yetu hawatilii mkazo jambo hili. Mungu Mwenye Enzi
Ameielekeza fahamu yangu katika kutafakari na kuliwazia jambo hili. Nimewaza
juu ya jambo hili tangu nikiwa kijana mdogo na hadi leo nafikirishwa na jambo hili
kama nilivyokuwa wakati ule. Uvivu wowote uliopo katika Jamaat yetu katika
kumkumbuka Allah ni lazima uondolewe. Masihi Aliyeahidiwa (as) ameweka
mkazo mkubwa katika sala. Kwa msaada wa Mungu, Jamaat yetu inaangalia sana
wajibu huu. Masihi Aliyeahidiwa (as) amesisitiza pia umuhimu wa kumkumbuka
Allah, lakini Jamaat bado haijalipa suala hili uzito unaotakiwa. Uvivu katika
kumkumbuka Mungu hutokana na athari ya elimu ya kimagharibi kwa kiasi fulani.
Watu wengi wanafikiri hakuna haja ya mtu kukaa peke yake na kusema ‘Laa Ilaha
Ilallah’ (Hakuna apasaye kuabudiwa ila Allah) au kutaja sifa za Mungu kama
Qudduus (Mtakatifu), ‘Aliim (Mwenye elimu), Khabiir (Mwenye habari), Qadiir
(Mwenye nguvu) au Khaaliq (Muumbaji). Wengi wa Wanajumuiyya wetu
waliopata elimu ya kimagharibi, wameathirika na mawazo haya.
Wakulima huunda kundi jingine kubwa katika Jamaat yetu. Zamani hawakuwahi
kupata habari za kutosha juu ya dhana ya Dhikr na faida zake. Kwa hiyo nao
wanakosa tabia ya kufanya Dhikr. Mpaka pale Jamii ya wakulima itakapopata
habari za kutosha na kufundishwa vilivyo, haiwezi kutazamiwa (wao) kuzingatia
barabbara kumbuko la Allah.
Salat (kusali sala tano zilizopangwa katika siku) pia ni kumkumbuka Allah. Kwa
msaada wa Allah Jamaat yetu inafuatilia vyema kabisa sala. Hata hivyo, kuna njia
nyingine muhimu za kumkumbuka Mungu tofauti na sala. Ingawa si kwamba
hazishikwi kabisa katika Jamaat, bali mkazo wa kutosha hauwekwi kwenye njia
hizi.
Baadhi ya Wanajumuiyya wanakosa kabisa tabia ya kumkumbuka Allah pamoja na
Salat, hili ni kosa kubwa. Ikiwa mtu ni mzuri mno wa sura lakini ana macho
mabovu, au masikio au pua mbaya, ataitwa mzuri? Hapana kabisa. Kila mtu
atasema anachukiza. Kwa maneno mengine Mwanajumuiyya ambaye hatumii
baadhi ya njia za kumkumbuka Allah ni kama mtu ambaye amevaa koti la gharama
sana, shati, jacket na suruali, lakini anakosa viatu au kofia. Bila kujali nguo zake
zilizoshonwa vizuri, kukosa kwake viatu au kofia kunafanya muonekano wake
kuwa na kasoro. Ukosefu wa tabia ya kumkumbuka Allah ni kasoro, na watu
wenye onjo zuri hawapendi kasoro yoyote binafsi.
Nitathibitisha kwamba pamoja na Salat, njia nyingine za kumkumbuka Allah
zimehimizwa na Allah na Mtume wake (saw). Ikiwa mtu anaelewa falsafa ya
mahimizo haya au la, ni wajibu kuyafuata ili kupata maendeleo ya kiroho.
Baadhi ya Wanajumuiyya wa Jamaat yetu wanadhani kwamba kwa kutimiza ibada
za faradhi wametimiza wajibu wao na hakuna haja ya Nawafil, yaani sala za ziada.
Hii ni dhana potofu. Mtume Mtukufu (saw) anasema kwamba Mungu Mwenye
Enzi Amemuambia kuwa, kwa kusali Nawafil Mtumishi wangu anakuwa karibu
mno nami kiasi ya kwamba ninakuwa masikio ambayo kwayo husikilia, macho
ambayo kwayo huonea, mikono ambayo kwayo hushikia na miguu ambayo kwayo
hutembelea.
Hadithi hii inafichua thamani iliyopewa Nawafil na Allah, na ukubwa wa daraja la
mtu anayezishika. Allah humwinua juu sana kiasi ya kwamba anaanza kuakisi sifa
zake. Nawafil si jambo la kawaida, kwa hiyo kukosa kuzingatia kuzitimiza ni
sababu ya masikitiko makubwa.
Mwanadamu ana asili ya uvivu na kutopenda kufanya juhudi. Anatamani
akabiliane na ugumu na nidhamu ndogo kadiri iwezekanavyo. Mwenyezi Mungu
Ambae Anatambua udhaifu wa viumbe vyake, kwa rehema Zake, Ameteua baadhi
ya matendo ya ibada kuwa faradhi na mengine kuwa ya ziada.
Ibada za faradhi zinaweka kiwango cha ibada zinazomwezesha mtu kukubalika.
Yeyote anayezitimiza kikamilifu anakuwa hana lawama. Imesimuliwa kwamba
mtu mmoja alimjia Mtume Mtukufu (saw), na akauliza juu ya Islam. Akajibu
Mtume (saw), Sala tano kila siku mchana na usiku. Akauliza, kuna Sala zozote
zingine baada ya hizi? Mtume Mtukufu (saw) akajibu, hakuna mpaka wewe
mwenyewe upende. Kisha, Mtume Mtukufu (saw) akaendelea; kufunga katika
mwezi wa ramadhani, tena yule mtu akauliza, kuna funga zozote nyingine baada
ya hii? Mtume Mtukufu (saw) akajibu hapana mpaka wewe mwenyewe upende.
Kisha Mtume Mtukufu (saw) akamwambia juu ya Zakat, wajibu wa kifedha wa
Waislam, yule mtu akarudia swali lile lile na akapewa jibu lile lile. Yule mtu
akaondoka akisema, naahidi kwa jina la Allah sitaongeza chochote katika haya, na
sitapunguza chochote. Mtume Mtukufu (saw) akasema, kama amesema kweli
(kama atatimiza ahadi yake hii), ameshafanikiwa.
Kwa kifupi ibada za faradhi zikifanywa kwa makini, zinahakikisha ufaulu. Lakini
waangalifu na wenye busara hawajibani kwenye ibada za faradhi pekee.
Wanauingia uwanja wa Nawafil ili kujazia upungufu unaoweza kuwapo katika
ibada zao za faradhi. Kwa mfano sala tano kila siku zimefaradhishwa, hata hivyo
kusahau au mghafiliko waweza kutokea katika mojawapo ya hizo na kuzifanya
kuwa batili. Kutakuwa na wajibu utakaodaiwa siku ya malipo kwa mapungufu
kama haya katika sala. Nawafil itajaziliza faradhi kama hizi.
Inasimuliwa kwamba Mtume Mtukufu (saw) mara moja alimwona mmoja wa
masahaba zake akisali. Akamwamuru kurudia sala, nae akarudia, lakini Mtume
Mtukufu (saw) akamtaka kurudia tena mara ya pili na ya tatu. Yule sahaba
akaomba Ewe Mjumbe wa Allah sifahamu namna ya kusali vyema zaidi, tafadhali
nifundishe. Mtume Mtukufu (saw) akajibu, ulikuwa unaharakisha mno katika
kusali, hivyo haiwezi kukubaliwa na Allah, sali pole pole na sala yako
itapokelewa.
Hebu nifafanue hoja hii, kwa mfano mwanafunzi anafanya mtihani ambao anahitaji
maksi hamsini ili kufaulu. Ikiwa atajibu maswali yawezayo kumpa maksi hamsini
tu, hawezi kuwa na hakika ya ufaulu wake. Anaweza kufeli kwa sababu mojawapo
ya maswali hakulijibu sawa sawa. Au fikiria msafiri anayejiandaa kufanya safari
ndefu. Anaweza kukadiria fedha zinazohitajika wakati wa safari, lakini wakati wa
safari anaweza kukabiliana na dharura inayohitaji fedha zaidi. Nawafil ni kama
fedha za ziada kwa ajili ya dharura. Ni za muhimu na zapaswa kupewa mkazo
maalum.
DHANA POTOFU JUU YA DHIKR
Kuna dhana potofu iliyoenea juu ya Dhikri katika Jamaat yetu. Kwa kuwa
inaonekana inapelekea kupuuzia Dhikri, nataka kuondoa dhana hii potofu. Masihi
Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu Masufi (wale wajiitao Madaruweshi) wa zama zake
ambao waliingiza bidaa nyingi katika Islam. Alibainisha kurudia rudia kwao
kikasuku maneno mbalimbali ya Dhikr kulikuwa hakuna maana, kwani huo
ulikuwa ni wakati wa kuuhami Uislam kutokana na mashambulizi ya maadui.
Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu - na hili walilistahili, lakini baadhi ya
Waahmadiyya walimwelewa vibaya.
Dhana kwamba kukaa mahala kwa ajili ya kumkumbuka Allah hakuna maana ni
potofu kabisa. Aina zote za Dhikr zakusudiwa kumsifu Allah na kuzitukuza sifa
zake. Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu wale waliokuwa wanazitaja sifa za
utukufu wa Mungu wakiwa wamejifungia majumbani mwao, lakini wasithubutu
kuwakabili maadui waliokuwa wakimimina matusi katika jina lake tukufu.
Aliwaasa kwa kuwa walikuwa waoga. Walikuwa hawatimizi wajibu wao wa
kuwaita watu kwenye wema na kukataza mabaya. Matendo yao yalikuwa ni
unafiki, kama wangekuwa waaminifu ki-ukweli katika kumtukuza kwao Mungu,
kwa nini hawakuyakabili mashambulizi ya maadui?
Kwa nini hawakumtukuza Allah hadharani kama walivyofanya katika kona
zilizonyamaa za nyumba zao?
Zaidi ya hayo, Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu kwa kuwa waliiharibu dhana
ya Dhikr. Matendo yao hayakuwa na alama yoyote ya dhana ya kumkumbuka
Mungu katika uhalisia wake.
AINA ZA DHIKRI ZILIZOPOTOKA
Aina kadhaa potofu za Dhikr zinapatikana kati ya Masufi. Wanalia kilio kutoka
nyoyoni mwao na wanakipeleka kichwani mwao na kupiga kelele kwa sauti kiasi
hiki kwamba hakuna yeyote jirani nao anaweza kulala au kumakinika katika ibada.
Hii inaitwa kuupenya moyo - kama vile La ilaha ilallah itaingia nyoyoni mwao
ikiwa tu itagongelewa iingie ndani. Ingawa wanasema kwamba wanakusanyika
kwa ajili ya Dhikr, wanajitia tu wazimu kwa sauti tupu za Allah, Allah.
Kuna matendo ya namna nyingi, mbalimbali;
- Baadhi wanabarizi tu na nyimbo, vibwagizo na kucheza na wasichana makahaba,
eti wanaiita hali hii kuwa ni kikao cha Dhikr kwa sababu tu neno Allah linatajwa
mara kwa mara.
- Wengine ‘Wanazipenya’ nyoyo zao
- Wengine hutoa ukelele kutoka rohoni mwao
- Wengine eti huitoa Dhikr kutoka katika nyoyo zao na inarejea baada ya kusujudu
katika Arsh - Kiti cha Enzi cha Allah.
- Wengine hucheza kwa kuifuata sauti ya usomaji wa Kurani Tukufu huku
wengine wakirukaruka na kusoma ushairi, hujifanya wanapandisha madadi na
kupoteza fahamu. Hapo ndipo mmoja wao huruka katikati ya mkusanyiko na kutoa
sauti za kifuani za Allah, Allah.
Kwa kifupi, mambo mengi yasiyofaa na machafu yameingizwa katika dhana ya
Dhikri. Hakuna lolote kati ya hayo lenye kulandana na mafundisho ya kweli ya
Islam. Tunazilaani bidaa hizi, lakini hatuwezi kuiacha Dhikr kwa sababu ya haya.
Mtume Mtukufu (saw) amesema kila ubunifu (bidaa) humpeleka mtu mbali na njia
ya Allah na zote hizo zinaelekeza motoni. Hii ndiyo sababu Dhikr kama hii
haiwapeleki watu hawa karibu na Allah, badala yake inawaweka mbali Naye.
Tangu aina hii ya Dhikr ilipoanzishwa, Waislam wameenda mbali na Allah.
Hii haishangazi, matendo yaliyo kinyume na mwongozo wa Allah na Mtume wake
ilikuwa ni lazima yahafifishe hali ya kiroho. Ubunifu (bidaa) wote ulioingizwa
katika Dhikr una vionjo vya starehe, lakini starehe yenyewe ni ya kiini macho. Mtu
anayeiangukia starehe hii na kuacha starehe ya kweli ameharibikiwa. Ni kama mtu
anayeugua maumivu ya tumbo na badala ya kutafuta tiba ya kweli, anajitia
usingizini kwa dawa ya usingizi. Nguvu ya kuzuia maumivu inaleta nafuu ya
muda, lakini kwahakika anajiua mwenyewe. Muda utawadia upesi ambapo
ugonjwa utafanya uharibifu wake.
DHIKRI DHIDI YA VIINI MACHO
Kile kinachoitwa Dhikr na watu hawa kwa kweli ni kiini macho na pumbazo la
akili (mesmerism & hypnotism). Haina uhusiano wowote na hali ya kiroho, bali
inahusiana na hudhurisho la mawazo. Mungu Mwenye Enzi Ameweka katika dhati
ya mwanadamu nguvu ya kuleta athari kubwa kwa njia ya kukazia mawazo
kwenye jambo fulani. Hisia za burudiko kama zile zitokanazo na madawa ya
kulevya kama opium, cocaine na bangi zinaweza kupatikana kutokana na mkazio
huu wa mawazo. Hisia hizi sio burudiko la kweli bali ni hali ya pumbazo. Watu
kama hawa wanajidanganya wenyewe katika kuamini kwamba wanapata burudiko
kwa kutaja jina la Allah. Kwa kweli hata wangetaja Ram, katika wakati ule wa
kazio la mawazo hisia zao zisingekuwa tofauti.
Inasimuliwa kwamba Mwislam mwenye heshima alikuwa anasafiri katika boti.
Akaanza kudhikiri kwa mkazo kamilifu. Wengine, hasa Wahindu wakajiunga nae
katika kusema Allah, Allah. Hata hivyo Mhindu mmoja hakuathirika, yule
Mwislam akaanza kukazia mawazo yake kwa yule Mhindu na yule Mhindu nae
akaanza kukazia mawazo yake kwa Mwislam kwa nguvu zaidi. Badala ya
kumuathiri Mhindu, Mwislam akaathirika mwenyewe. Bila kutaka akaanza
kutamka Ram, Ram. Mwislam alipigwa na butwaa na akang’amua kuwa kufanya
Dhikri kwa njia hii kulikuwa sio sahihi. Alitubu na akaachana na mazoea haya.
Aligundua kwamba matokeo hutokana tu na utumiaji wa ujuzi, na sio
kumkumbuka Allah, kama baraka ya kutamka Allah ilikuwa ndio chimbuko la
burudiko lake, kutaja Ram kusingeweza kuleta hisia ile ile.
Wale wanaofanya jinadi kama hizi hali yao ni kama msafiri jangwani. Akiona
kapu limejaa mchanga, anadhani lina chakula. Mtu afanyae nyiradi zisizo na
maana anaamini anapata ukaribu na Mungu, lakini kwa kweli yumo katika hali ya
mdanganyiko. Fahamu zake zimepumbazika. Anafikiri kwamba amefikia hali ya
kiroho ya juu, lakini kwa kweli hali ya moyo wake inabaki na uchafu.
BURUDIKO KUTOKANA NA DHIKRI
Mu Ahmadiyya mmoja mkweli wa moyo alipata kuniambia kwamba burudiko
kubwa lapatikana katika matendo kama haya. Nilimwambia kwamba faraja hiyo
inafanana na ile ipatikanayo kwa kutumia opium na cocaine. Ushahidi kamili ni
kwamba Dhikr za aina hii hazileti usafi wa kiroho. Alikubali na akanieleza kuwa
alimfahamu mtu mmoja aliyekuwa mahiri wa nyiradi zote hizo, lakini alikuwa
akiomba omba chakula mitaani. Yule Mu-Ahmadiyya aliongeza kusema kwamba
alikuwa akishangaa, kama mtu huyu amefikia hali ya juu ya kiroho anayoidai kwa
nini anahitaji kuomba omba?
Masihi Aliyeahidiwa (as) amesimulia hadithi ya mtu mmoja aliyedai kuwa ni mcha
Mungu aliyefikia hali ya juu ya kiroho. Siku moja mtu huyu alimtembelea mfuasi
wakekatika kipindi cha njaa, na akamdai “nipe karadha (hadhi) yangu”, yule
mfuasi hakuwa nacho cha kumpa, hivyo akaomba asamehewe, lakini yule mtu
aliendelea kusisitiza madai yake. Mwishowe yule mfuasi alilazimika kuuza baadhi
ya vitu vyake vya ndani ili kukidhi madai ya mcha Mungu yule.
Kwa kifupi mapungufu mengi na uchafu wa moyo vinaonekana kwa watu
wanaojionyesha kama wameshakuwa wacha Mungu kwa njia potofu za Dhikri.
TOFAUTI KATI YA DHIKRI NA ATHIRIKO TU LA MAWAZO
Mungu Mwenye Enzi Ameweka katika sauti na mawazo ya binadamu nguvu
maalum. Kama mtu ataendelea kufikiri kwamba jambo fulani limetokea basi akili
yake itapatwa na athari hiyo hiyo. Vile vile, kama mtu anaanza kuwaza kwamba
moyoni mwake anatoa sauti ya Allah, anaanza kuisikia sauti hiyo. Swali linazuka;
kama moyo kweli unatoa sauti hiyo, kwa nini usitakaswe?
Kuna tofauti ya muhimu kati ya wale ambao kweli wanampenda Mungu na wale
wanaofanya ujanja tu. Tofauti ni rahisi, lakini kushindwa kuitambua kunamfanya
mtu asijali kuhusu kujirekebisha. Anaweza kuamini kwamba amemfikia Allah,
wakati kwa kweli hajamfikia. Kama mtu aliyefika mahali tofauti na alikokusudia
kwenda, lakini akaamini amefika kwenye lengo lake, atakaa pale na kupata hasara
yake. Wale wanaojiingiza katika matendo yaliyopotoka, wanadhani wamefikia
lengo lao la kweli, lakini kwa kweli wako mbali nalo kwa maili nyingi. Kama
ilivyo kwa mtumiaji wa madawa ya kulevya, wako katika hali ya ganzi ya ulevi na
pumbaziko la fahamu.
Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwahimiza wafuasi wake kukaa mbali na aina potofu za
Dhikri. Aliwalaumu wale waliokuwa wakizifanya. “Inawezekanaje mambo haya
yakaitwa kumbuko la Allah katika maana yake ya kweli ikiwa hata Wahindu na
Wakristo wanaweza nao kuyatenda?” Alihoji
KUTAMKA DHIKRI KWA SAUTI
Vipi kuhusu kutamka Dhikri kwa sauti au kusikiliza nyimbo na muziki. Kama
nilivyotaja mapema, mfumo wa neva wa binadamu umepewa nguvu ya kuathiri na
vile vile kuathirika. Masikio yanatoa mojawapo ya njia zielekeazo kwenye mfumo
wa neva. Husisimka kwa sauti zenye kuleta faraja. Hii inahusika sio tu kwa
binadamu bali kwa viumbe vingine pia. Mpigie nyoka zumari na ataanza kucheza.
Je utaweza kusema yupo kwenye athiriko la kiroho, la, bali ni hisia zake tu
zimeathirika. Yeyote anayeamini kwamba kuimba kuna athari ya kiroho amekosea,
kama ambavyo nyoka hucheza kufuata sauti ya zumari, vivyo hivyo Masufi wa leo
husisimka kwa nyimbo na muziki. Zaidi ya hapo, ni bidaa katika imani ya Islam
kufanya Dhikri kwa sauti.
Masufi wa leo wanaenda kinyume na miongozo ya Mtume Mtukufu (saw)
wanapofanyamkutano wa Dhikri, eneo lote walipo linajaa kelele. Wanadhania ni
tendo la wema, wakati kwa kweli, wanaenda kinyume na ‘Sharia’ (sheria ya
Islam). Matendo yao, kucheza, kupiga kelele, kuanguka, na kuzungusha vichwa
vyao hayaendani na mafundisho ya Islam.
JE MASHAIRI NI DHIKRI?
Inasemwa kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisikiliza mashairi, lakini hakuna
awezaye kuthibitisha kwamba alisikiliza mashairi kama njia ya kumkumbuka
Allah. Wakati fulani Hadhrat Hassan (ra) alimjia na kumwambia, Ewe Mjumbe wa
Allah, mpinzani ametunga mashairi dhidi yako nami nimeandaa majibu haya.
Alisikiliza yale majibu. Hivyo hivyo siku moja mtu ambae alikuwa amemuhukumu
kuuawa, alikuja mbele yake na baada ya kupata ruhusa, akasoma beti kadhaa
akiomba msamaha. Mtume Mtukufu (saw) akatandika “kitambaa” chake juu ya
yule mtu kuashiria msamaha. Baadae yule mtu akasema, “sikuwa naogopa kifo,
lakini niliutambua ukweli wa Islam na sikutaka nife ningali kafiri”. Katika tukio
jingine, sahaba fulani aliandika utenzi wakati wa vita ambamo alisema; “leo
tutashinda au tutakubali kufa, lakini hatutarudi nyuma”
Hakuna katika haya tukio linaloonyesha kwamba kumkumbuka Allah kulichukua
sura ya nyimbo au kusoma mashairi, na wala hayathibitishi kwamba masahaba
walicheza au walilewa kwa madadi. Matendo haya yote ni bidaa. Tabia
inayochochewa na nyimbo hizi ni pujufu na isiyo ya Kiislam. Islam haiafiki
mwenendo huo kabisa.
SIFA ZA DHIKRI YA KWELI KUFUATANA NA MAFUNDISHO YA
ISLAM
Anachosema Allah juu ya Dhikr e-laahi ni hiki kifuatacho:-
Hakika waaminio ni wale ambao Anapotajwa Mwenyezi Mungu, mioyo yao hujaa
hofu (Kurani Tukufu 8:3)
Husisimka kwayo ngozi za wale wanaomwogopa Mola wao, kisha ngozi zao na
mioyo yao huwa laini kwa kumkumbuka Mola wao. (Kurani Tukufu 39:24)
Wanaposomewa aya za rahmani huanguka kusujudu na kulia. (Kurani Tukufu
19:55)
Kwa mujibu wa aya hizi hali ya wale ambao humkumbuka Allah kwa ukweli ni
kamaifuatavyo:-
1. Nyoyo zao zinajaa hofu kwa kumwogopa Allah kwa sababu wanakumbushwa
ukubwa na utukufu wa Mola wao.
2. Ngozi zao husisimka yaani nywele za mwilini mwao husimama kwa sababu ya
hali yao ya hofu.
3. Miili yao hulainika, nyoyo zao huwa nyenyekevu
4. Wanasujudu, yaani wanaanza kumwabudu Mungu
5. Wanalia au kugugumia.
Hizi ndizo hali tano zilizotajwa katika Kurani Tukufu. Kama kucheza, kurukaruka,
kuanguka kwa kuzimia kwa madadi na kuyowayowa kungekuwa ni hali sahihi kwa
ajili ya Dhikri, Mungu Mwenye Enzi bila shaka angalizizungumzia pia. Hataji hali
yoyote kati ya hizo, hivyo, hazina uhusiano wowote na kumkumbuka Allah.
KATIKA DHIKRI YA KWELI HAKUNA NAFASI YA KUCHEZA NA
KUPIGA KELELE
Hakuna anayeweza kudai kuwa matendo haya ya siku hizi ni nyongeza za halali
kwenye yale yaliyobainishwa na Allah, kwa sababu maneno yaliyotumika na Allah
hayatoi nafasi kabisa kwa matendo kama haya. Maneno yaliyotumika ni ‘Wajl’,
‘iqshirar’, ‘ta’liin’, na ‘juluud’. Mojawapo ya maana za ‘Wajl’ ni ulaini na
kumong’onyoka. Haya yanahitajia hali ya utulivu. Lakini Masufi wa leo wanaenda
wakizunguka katika hali ya kupagawa, ambayo ni kinyume na dhana hii. Hali
kadhalika, ‘iqshirar’ inatokea pale ngozi inaposisimka kwa ajili ya hofu. Hii pia
inataka hali ya utulivu, kwa kuwa katika hali ya hofu mtu anafadhaika na nyendo
zinakuwa haba. Maneno ‘taliin’ na ‘juluud’ vilevile huhitaji hali ya kutulia.
Neno sahihi la kiarabu kuashiria nyendo ni ‘turb’. Hutumika kwa kushangilia na
kurukaruka kwa furaha. Neno hili halijatumika katika Kurani Tukufu kwa
kumkumbuka Allah. Kamusi zinasema hali ya ‘turb’ ni kinyume cha hali ya upole
na unyenyekevu, ambazo kwa mujibu wa Kurani Tukufu ni matokeo ya
kumkumbuka Allah. Hivyo kurukaruka na kutembea tembea haviwezi kuwa ni
matokeo ya kumkumbuka Allah kwa kweli. Haya yatakuwa ni ‘turb’ ambayo ni
kinyume na upole na unyenyekevu, yaliyo matokeo sahihi ya kumkumbuka Allah.
Islam inafundisha tafakari, busara na umuhimu wa kufuata njia iliyonyooka - sio
wehu na ujinga ambao hupelekea kuruka ruka na kupiga kelele. Haya hayawezi
kuwa mafundisho ya Islam.
KUPOTEZA FAHAMU SIO MATOKEO SAHIHI YA DIKRI
Kuanguka kwa kupoteza fahamu (kwa kupandisha mdadi) sio matokeo sahihi ya
Kiislam katika hisia ya hali ya juu. Mwislam katika huzuni ya kufiwa anaruhusiwa
kutokwa machozi kwa huzuni, lakini sio kulia kwa sauti na ukelele wa wazi au
kupoteza fahamu. Wakati fulani Mtume Mtukufu (saw), alipita karibu na
mwanamke mmoja aliyekuwa akionyesha huzuni isiyofichika karibu na kaburi la
mtoto wake. Alimshauri kuwa na subira, (mwanamke yule) akasema: kama mtoto
wako angekuwa amekufa ungefahamu ni vigumu kiasi gani kuwa na subira.
(Alisema hivyo kwa kutofahamu, maana Mtume Mtukufu (saw) alishapoteza
watoto kadhaa). Kwa kifupi kulia kwa mayowe na kupoteza fahamu hutokana na
kukosa subira na kukosa matumaini, wakati mwingine kukosa subira hutokana na
udhaifu wa moyo, hata hapo pia haitakiwi. Katika nyakati za Hadhrat Junaid,
kulikuwepo na Mwanazuoni mkongwe ambaye alikuwa akipoteza fahamu asikiapo
kumbuko la Allah. Wanafunzi wake walipomuuliza juu ya hili, aliwajibu
nimekuwa mkongwe na hivyo napoteza fahamu. Tazama hakuhusisha kuzimia
kwake na hali fulani ya juu ya kiroho bali (alikuhusisha) na udhaifu wake tu wa
kimwili.
Kuhusiana na kupoteza fahamu kwa kukata tamaa na kukosa tumaini, Allah
Anasema;
Wala msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, hakika hawakati tamaa na
rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri. (Kurani Tukufu 12:88).
Yeyote anayepoteza fahamu kwa kukosa tumaini anatenda kitendo cha kufuru.
Kama akifanya hivyo kwa sababu ya udhaifu wa moyo, anaumwa. Hakuna busara
iliyomo ndani ya yoyote ya hali hizi zote.
Swala la kupoteza fahamu lilijadiliwa wakati wa Masahaba wa Mtume Mtukufu
(saw). Hadhrat Abdullah bin Zubeir r.a. alimuuliza Hadhrat Asma’a r.a. kuhusu
kupoteza fahamu. Alijibu, “Najikinga kwa Allah kutoka kwa shetani
arujumiwaye”. Mtoto wa Hadhrat Abdullah bin Zubeir r.a. alisimulia kwamba
aliwaona watu wakizimia kwa kusikia Kurani Tukufu ikisomwa. Hadhrat Asma’a,
r.a. aliyekuwa mtoto wa Hadhrat Abu Bakar r.a. na akiwa pia ni sahaba, alijibu,
kama aliona jambo hili aliona tendo la kishetani.
Ibn Sirini, mwandishi wa kitabu maarufu cha tafsiri za ndoto, alikuwa ni mkwe wa
Hadhrat Abu Huraira (ra). Aliwahi, wakati fulani, kuambiwa habari za mtu mmoja
aliyezimia baada ya kusikia aya ya Kurani Tukufu ikisomwa. Alijibu, “mwekeni
juu ya ukuta mrefu kisha msomeeni Kurani yote, sio aya moja tu, kama atazimia
nitakubali kwamba anaathirika na kusomwa kwa Kurani Tukufu”.
Hata sasa wale wanaopoteza fahamu huwa waangalifu wasiumie, isipokuwa kwa
bahati mbaya. Hawaanguki kutoka kwenye paa au kuangukia mahala wanapoweza
kuumia. Mara nyingi huwaangukia watu wengine katika kundi.
Kwa kifupi bidaa zote zilizoingizwa katika Dhikri ni potofu na zimekatazwa.
Zinastahili kulaumiwa kwa sababu zinauharibu ucha Mungu. Zinawashusha watu
kuwa daraja la manyani na mbwa. Islam inataka kumwinua mtu kupita daraja la
malaika na inayaona matendo haya kuwa hayana maana na yasiyofaa.
AINA NNE ZA DHIKRI ZILIZOAMRISHWA KATIKA ISLAM
Dhikri, kama ilivyoamrishwa na Kurani Tukufu ni za aina nne. Aina hizi zote
zapaswa kutekelezwa kwa makini, kukosa kutekeleza yeyote kati ya hizi
humnyima mtu baraka kubwa. Nazo ni kama ifuatavyo:-
1. Sala zilizoamrishwa
2. Kusoma Kurani Tukufu
3. Kutaja sifa za Allah, kukiri ukweli wa sifa hizo, kuzisherehesha sifa hizo, na
4. Kuwatangazia watu sifa za Allah
Umuhimu wa aina hizi nne za Dhikri umeainishwa vyema katika Kurani Tukufu.
Dhikri hizi ni muhimu bali ni za lazima katika kupata maendeleo ya kiroho.
Sasa nitathibitisha kwamba aina hizi nne zimeamrishwa na Kurani Tukufu. Mungu
Mwenye Enzi Anasema juu ya sala;
Kwa yakini mimi Ndiye Allah, hakuna aabudiwaye ila Mimi, basi niabuduni na
msimamishe sala kwa kunitaja. (Kurani Tukufu 20:15).
Aya hii inaonyesha kwamba pale Allah Anaposema Mnikumbuke Mimi,
Anamaanisha ushike sala. Kisha Allah Anasema;
Na kama mkiwa na hofu basi (salini) mkitembea, au mmepanda (wanyama), na
mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama
Alivyowafundisheni yale mliyokuwa hamyajui. (Kurani Tukufu 2:240).
Katika aya hii kusali kumeitwa kumkumbuka Allah. Kuna aya nyingine nyingi,
lakini hizi mbili zitatosha kwa sasa.
Dhikri ya pili ni kusoma Kurani Tukufu.
Allah Anasema;
Hakika Sisi Tunateremsha ukumbusho na hakika sisi ndio tuulindao (Kurani
15:10)
Katika aya hii ufunuo wa Kurani Tukufu umeitwa teremsho la ukumbusho - Dhikri
katika kiarabu. Hivyo, pale Allah Asemapo Mkumbuke Allah, Anamaanisha pia
usome Kurani Tukufu. Kisha Allah Anasema;
Na huu ni ukumbusho uliobarikiwa ambao Tumeuteremsha. Je ninyi mtaukataa?
(Kurani Tukufu 21:51).
Aya hii inaiita Kurani Tukufu ni ukumbusho, neno la kiarabu lililotumika hapa pia
ni Zikr.
Aina ya tatu ya Dhikri ni kuzitaja sifa za Allah, na kuukiri ukweli wa sifa hizo.
Baadhi ya watu wanaamini inatosha kuzitaja sifa za Allah wakati wa sala. Hayo ni
makosa. Kumkumbuka Allah kwa nyongeza juu ya sala kumeamrishwa wazi wazi
na Kurani Tukufu. Allah Anasema;
Basi mwishapo kusali mkumbukeni Mwenyezi Mungu kila msimamapo na mkaapo
na mlalapo kibavu. (Kurani Tukufu 4:104).
Ni dhahiri, Dhikri inayotajwa hapa ni ya nyongeza juu ya salat. Kisha Anasema;
Watu ambao haiwasahaulishi biashara wala uchumi katika kumkumbuka
Mwenyezi Mungu na kusimamisha sala na kutoa zaka, wakiogopa siku ambayo
mioyo itapinduka na macho (pia) (Kurani Tukufu 24:38). Hapa tena kumkumbuka
Allah ni mbali ya sala.
Aina ya nne ya Dhikri ni kuwatangazia watu sifa za Allah. Anasema;
Ewe uliyevaa. Simama na uonye. Na Mola wako umtukuze, na nguo zako
uzitakase. Na uchafu uuondoe. Wala usiwafanyie ihsani ili upate zaidi. Na kwa
ajili ya Mola wako fanya subira. (Kurani Tukufu 74:2 -8)
NJIA ZA KUFANYA DHIKRI
Ni zipi njia sahihi za kufanya aina hizi za Dhikri?
Kwa kuzingatia mahitajio ya Jamaat, nitashughulikia baadhi tu ya yaliyomo katika
mnasaba wa somo hili.
Aina hizi mbali mbali za Dhikri zaweza kugawanywa kwenye mafungu mawili.
Faradhi na Nafali. Kwa rehema za Mungu, Jamaat yetu inazingatia sana Dhikri za
faradhi, sitaijadili hii sana. Baadae katika mjadala huu nitasema kitu fulani kuhusu
Nawafil, Dhikri za ziada, ambazo zinahitaji mjadala mpana. Hebu nianzie na
namna ambavyo Kurani Tukufu yapaswa kusomwa.
USOMAJI WA KURANI TUKUFU
1. Kurani Tukufu yapaswa kusomwa kwa mfululizo na kwa kuufuata mpango
uliowekwa. Panga kipande kwa ajili ya usomaji wa kila siku badala ya kuichukua
Kurani Tukufu mara moja moja na kusoma chochote utakacho. Usomaji usio na
mpangilio hauleti faida yoyote. Kama unaamua kusoma nusu ya fungu, au fungu
zima au mafungu kadhaa kila siku ni lazima usome kiasi hicho hicho siku zote bila
uvivu wowote.
Mtume Mtukufu (saw), anasema Allah Anapenda ibada inayofanywa mfululizo,
bila kukosa. Kukosa mpangilio kunaashiria kukosekana hamasa, na moyo hauwezi
kutakaswa bila hamasa na mapenzi ya kweli. Uzoefu wangu binafsi unathibitisha
hoja hii. Kila ninapokuwa na shughuli nyingi mno kama kuandika kitabu au
shughuli nyingine na nikawa siwezi kusoma Kurani Tukufu, moyo wangu
unajisikia sononeko na aina nyingine za ibada pia zinapata athari mbaya. Kwa
kifupi Kurani Tukufu yapaswa kusomwa kila siku.
2. Jaribu kuelewa unachokisoma. Kurani Tukufu haipaswi kusomwa kwa haraka.
Kusoma polepole kutakuwezesha kuelewa na kutaonyesha heshima stahiki kwa
Kurani Tukufu.
Muahmadiyya mmoja ameuliza nini kifanyike kama mtu haielewi Kurani Tukufu.
Watu kama hao wapaswa kujifunza maana ya sehemu fulani ya Kurani Tukufu na
kuiingiza sehemu ile pia katika kila usomaji waufanyao katika Kurani Tukufu.
Waweza kukuuliza, kuna maana gani kuzisoma sehemu ambazo hatuzielewi?
Kumbuka wakati kitu kinafanywa kwa uaminifu wa moyo na nia njema, Allah bila
shaka hutoa malipo. Kama unasoma kwa ajili ya Mungu bila kujua maana, bila
shaka Atakubariki sawa na uaminifu wa moyo wako. Zaidi ya hapo yale maneno
(ya Kurani Tukufu) yanayo athari. Mtume Mtukufu (saw) ameamuru kwamba
adhana isomwe kwenye masikio ya mtoto mchanga mara baada ya kuzaliwa.
Mtoto hana uwezo wa kuelewa au kufahamu chochote wakati ule, lakini
anaathiriwa na maneno ya adhana.
3. Kwa kadri iwezekanavyo, chukua udhu kabla ya kusoma Kurani Tukufu. Nina
imani kwamba inaruhusiwa kusoma Kurani Tukufu bila kuchukua udhu, lakini
baadhi ya wanazuoni wanaona haifai. Bila shaka ni sahihi zaidi kuchukua udhu ili
kupata faida zaidi na kupata malipo zaidi.
KUMSIFU ALLAH KWA UKUBWA WAKE, NA KWA UTUKUFU WAKE
NA KUMSHUKURU
Aina nyingine ya Dhikri inajengwa na tasbiih (kutamka utukufu wa Allah) na
tahmiid (kutamka shukrani kwa Allah) na takbiir (kutamka ukubwa wa Allah).
Dhikri hizi zaweza kufanywa moja moja au kwa ujumuisho.
Wakati mwingine Dhikri hizi ni faradhi, kama kusema takbiir, yaani Allah-u-Akbar
(Allah ni mkuu kabisa). Wakati wa kuchinja mnyama. Kama takbiir haikutamkwa
uchinjaji hautaafikiana na maelekezo ya Islam. Lakini tasbiih na tahmiid
hutamkwa pia kwa sauti ya chini katika kumkumbuka Allah.
Mtume Mtukufu (saw) amefundisha aina fulani ya Dhikri kwa ajili ya kila tukio.
Wakati wa kuanza kula, ametufundisha kusema;
Bismillaahir rahmaanir Rahiim. Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwingi
wa Ukarimu.
Yeyote asiyesoma Bismillah atakuwa pia amejaza tumbo lake, lakini kusudio hasa
la kula litakuwa limetimizwa kwa kuanza na Bismillah. Kutakuwa na manufaa ya
kiroho ndani ya chakula hicho.
Tumalizapo shughuli yoyote Mtume s.a.w. alitufundisha tuseme:
Sifa zote njema zinamhusu Allah Mola wa walimwengu (1:2)
Alhamdulillah pia husomwa wakati wa kuvaa nguo mpya au wakati wa kupata
neema yoyote.
Katika kila wakati wa huzuni twafundishwa kuomba:
Sisi ni wa Allah na Kwake tutarejea
Anapokumbwa na jambo lililo nje ya uwezo wake, mwislamu amefundishwa
kuomba:
Hakuna mpango wala uwezo ila kwa msaada wa Allah
Aina hizi za Dhikri zimejumuisha nyanja zote za maisha. Furaha au huzuni yaweza
kupatikana wakati wa mchana. Anapokumbana na furaha Mwislamu husema
Alhamdulillaahi Rabbil ‘Aalamiin. Kama akiwa katika huzuni husema Innaa
lillaahi wa innaa ilaihi raaji’uun.
Mtume Mtukufu (saw) amefundisha Dhikri kwa kila tukio kwa kufuata amri ya
Mungu Mwenye Enzi, Ambae Amesema;
Mkumbukeni Mwenyezi Mungu kila msimamapo na mkaapo na (mlalapo) kibavu.
(Kurani Tukufu 4:104).
Ikiwa mtafuata maelekezo haya wakati wote mtakuwa katika kumkumbuka Allah.
Ikiwa utasikia habari njema wakati uko Ofisini kwako unafanya kazi sema
Alhamdulillah. Ukisikia habari kama hizo wakati unatembea sema Alhamdulillah.
Tamka Tahmiid kama habari hizo njema zitakufikia ukiwa umejilaza. Hivyo
kumkumbuka Allah kutaendelea katika kila hali.
Dhikri ya kutamka umoja wa Allah
Mtume Mtukufu (saw) amesema pia kwamba njia ya kwanza na iliyo bora zaidi ya
kumkumbuka Allah ni kutamka;
Laa ilaha illallah - Hakuna apasaye kuabudiwa ila Allah. (Imesimuliwa na Jabir
katika kitabu cha Tirmidhi)
Matamko mengine; Kuna aina nyingine za Dhikri ambazo zinakubalika sana. Tamko la muhimu ni hili;
Subhanallahi wa bi Hamdihi, Subhana Allahil ‘Adhiim.
Utukufu ni wa Allah, kwa sifa zake, Utukufu ni wa Allah kwa ukuu wake.
Kuhusiana na tamko hili, Mtume Mtukufu (saw) amesema; “Kuna maneno mawili
ambayo ni rahisi kuyatamka, lakini yana uzito mkubwa kwenye mizani ya matendo
mema siku ya Hukumu. Yanapendwa sana na Mola wa rehema. Yanafanyiza
Dhikri ya hali ya juu.
Siku moja Masihi Aliyeahidiwa (as) alikuwa hajisikii vizuri, lakini aliamka kwa
ajili ya Tahajjud. Alipata ufunuo kwamba angeweza tu kusoma Dhikri hiyo hapo
juu badala ya Tahajjud katika hali kama hiyo. Kwa mujibu wa Hadithi, Mtume
Mtukufu (saw) alikuwa akiisoma Dhikri hii mara kwa mara.
Mtume Mtukufu (saw), ametuambia juu ya ubora wa aina hizi za Dhikri. Kuna
tamko jingine ambalo pia linakubaliwa sana. Ingawa hakuna hadithi iliyohifadhiwa
juu yake, Tafakari inatuongoza kwenye ubora wake. Dhikri hiyo inahusu kusoma
aya za Kurani Tukufu kama vile vile tufanyavyo wakati wa kutamka Dhikri.
Tahadhari na nyakati sahihi kwa aina hii ya Dhikri
Baada ya kueleza wasifu na aina za Dhikri sasa nitashughulikia tahadhari za lazima
na nyakati zifaazo kwa kufanya Dhikri.
Tahadhari za lazima kwa Dhikri 1. Mtume Mtukufu (saw) ametuelekeza tusirefushe mno Dhikri mpaka ikaleta
uchovu
2. Usiingie katika Dhikri wakati akili haijatulia. Kujaribu kufanya Dhikri ilhali una
majukumu ya muhimu haishauriwi. Jitihada kama hii itafanywa na moyo nusu na
hali kama hii ni utovu wa heshima kwa meneno ya Mungu, itahesabiwa kama
dhambi. Kwa kifupi, fanya Dhikri kwa ufupi na kwa umakini kamili.
Wakati fulani Mtume Mtukufu (saw), aliporudi nyumbani kwake, Hadhrat Aisha
(ra) alikuwa anaongea na mwanamke fulani. Hadhrat Aisha (ra) alimwambia
Mtume Mtukufu (saw) kwamba yule mama alikuwa anatumia masaa mengi katika
ibada. Alimjibu, hakuna ubora wowote katika kufanya ibada ya kupitiliza kiasi
kama hiyo. Allah Anapendezwa na ibada inayofanyika mfululizo. Allah Hapatwi
na uchovu lakini mtu huchoshwa na ibada ya kupita kiasi. Baada ya kuchoka ibada
yake inafanyika bila mazingatio wala furaha na haipati kupokelewa. Ikiwa mtu
atapitiliza kiasi, anajiletea mwenyewe fadhaa.
Hadhrat Abdullah bin Umar bin Aus alikuwa mtu mwenye afya. Alisali usiku
kucha, akafunga mchana, na akasoma Kurani Tukufu yote ndani ya siku moja.
Aliposikia jambo hili, Mtume Mtukufu (saw) alisema, hii sio sawa, salini katika
moja ya sita, au theluthi moja, au sana sana nusu ya usiku. Fungeni kwa
kupishanisha siku, msimalize kusoma Kurani Tukufu chini ya siku tatu. Abdullah
bin Umar bin Aus aliomba zaidi, lakini hakuruhusiwa. Akaapa kutimiza haya kwa
kiwango cha juu kilichoruhusiwa. Akatimiza ahadi yake kwa muda mrefu, lakini
katika uzee alisikitika ya kwamba hakuitumia ruhusa ya ziada iliyokuwa
imetolewa.
Jambo lolote likifanywa kupita kiasi huleta matatizo. Ziada ya chakula kizuri
italichagiza tumbo, hali kadhalika, ziada ya Dhikri husababisha uchovu na
kupoteza hamu. Ongeza juhudi yako pole pole na uibakishe ndani ya uwezo wako.
3. Kama huwezi kuwa makini mwanzoni vumilia na malizia kiwango chako hata
kama kutakuwa na athari za shetani. Kwa kutia nia ya dhati, unaweza kuyashinda
mapungufuyako. Tacon, aliyekuwa wakili maarufu, wakati fulani alikuwa
anasimamia kesi, wakili wa upande wa pili, kwa hofu kwamba Tacon atashinda
kesi, akatunga ujanja. Akamwambia Hakimu kwamba ‘Tacon anadai kwamba
anaweza kupata hukumu nzuri kutoka kwa Hakimu yeyote, bila kujali haki iliyoko
kwenye kesi. Hakimu akafanya uamuzi akilini mwake kutomsikiliza Tacon. Kesi
ilipoanza kusikilizwa, Hakimu alikataa kila hoja ambayo ililetwa na Tacon.
Mwishowe alipitisha hukumu iliyotoa haki kwa upande pinzani. Kwa hitimisho,
hakuna mtu awezaye kumuathiri mtu aliyedhamiria kutoathiriwa. Katika hatua za
mwanzo za kujipatia tabia ya Dhikri, jenga mazoea ya umakini kuepuka athari zote
za nje.
4. Usifanye Dhikri ilhali unayo maumivu ya kimwili. Kama kitu fulani kinakuuma,
kiondoshe kwanza kabla ya kuanza Dhikri.
5. Pokea kwa furaha chochote unachopewa. Hata kama hupati kumakinika
barabbara mwanzoni, wakati utafika ambapo tabia ya Dhikri itakuwa imeimarika.
6. Fanya Dhikri kwa unyenyekevu na hofu ya Allah. Kama hujisikii kupata
unyenyekevu wa kweli, basi jifanyizie usoni katika hali ifananayo, hali itakiwayo
ya moyo itafuatia. Inatokea mara nyingi kwamba mtu anachukua mazoea fulani
bila mashiko halisi, lakini polepole anayachukua na yanakuwa hali yake ya asili ya
kimapokeo. Kama akijifanya mnyenyekevu na akajiliza, basi karibuni ataupata
unyenyekevu wa kweli wa roho.
Inasimuliwa kwamba Profesa mmoja alikuwa na moyo wa upole sana, lakini
baadae akaja kuwa mkatili sana. Hivi ndivyo ilivyotokea. Kwa sababu ya hali yake
ya upole, siku moja alipata hasara na akaamua tangu hapo kuwa mkali. Basi
akajifanyiza tabia ya ukali ingawa ndani yake bado alikuwa na moyo wa upole.
Pole pole ukali ukajengeka katika mwenendo wake. Profesa aliingia katika (silika
ya) ubaya kwa kutumia kanuni ya kujifanyiza, lakini hii yaweza kutumika
kuuelekea wema pia. Katika siku ya mwanzo unyenyekevu wa kweli waweza
kutokeza kwa muda wa kufumba na kufumbua tu, siku ya pili utabaki kwa muda
zaidi. Kadri muda unavyokwenda matokeo ya juhudi ya kudumu yatakuwa bayana
kabisa.
Kuna mazingatio mengine ambayo yapaswa kuelezwa. Isipokuwa kwa matukio
yaliyoruhusiwa katika hadithi, usifanye Dhikri kwa sauti. Hii yaweza kuzua (hali
ya) kujionyesha, na kuwazuia wengine kufanya Dhikri au kusali.
Kumbuka kwamba vitendo vipya ni vigumu kuvizoea, kuvizoea kunachukua muda.
Watu wengi wanalalamika kwamba hawawezi kuziweka nyoyo zao katika Dhikri.
Sasa mnafikiria yeyote anaweza kumahirika katika ujuzi kwa siku moja? Sivyo
kabisa. Inachukua muda wa subira. Hivyo kama muone ugumu mwanzoni, msikate
tamaa, mtazoea polepole. Sharti ni moja tu kwamba msirudi nyuma.
Wengine wanasema wanaipenda Dhikri. Hawapaswi kutafuta starehe ndani ya
Dhikri, bali waifanye kama ibada, ambalo ndilo lengo lake. Ibada inakubaliwa tu
pale ifanywapo kwa nia hiyo (ya kufanya ibada).
Wengine wanalalamika kwamba wanajisikia kutotamani kwa siku kadhaa halafu
baadae wanajisikia kutamani kufanya Dhikri. Kwao ushauri wangu ni kwamba
wasikate tamaa, kwa maana hilo ni jambo la kawaida.
Siku moja sahaba fulani alimjia Mtume Mtukufu (saw) na kusema Ewe Bwana
wangu, mimi ni mnafiki. Akajibu hapana wewe ni Mwislam. Akasema nijapo
kwako naweza kuishuhudia pepo, na jahannam, lakini ninapoondoka ninapoteza
hali hiyo yote. Akasema ukibaki katika hali ile ile wakati wote utakufa muda si
mrefu. Kubakia katika hali moja kunafudikiza uwezo wa kusonga mbele. Wakati
mwingine Mungu Mwenye Enzi humshusha mtu kutoka katika daraja lake la
kweli, hali kadhalika, wakati mwingine humfanya afaidi daraja la juu zaidi ambalo
hajalifikia ili kumtia moyo kulipata daraja hilo kwa kudumu.
Kukosekana kwa hamasa, hata hivyo kunaweza kuwa hakuna madhara au kukawa
na madhara. Tofauti baina ya matokeo haya mawili yaweza kuonekana. Fikiria
kwamba kuna madaraja ya hamasa katika kufanya Dhikri, sifuri ikiashiria
kukosekana kabisa kwa hamasa na madaraja moja, mbili, tatu, nne na tano
yakiashiria madaraja ya kupanda kwa kuelekea hatua za juu. Kama uko katika
daraja la pili na kukosekana kwa hamasa hakukushushi chini ya daraja la kwanza,
hali hii haina madhara. Kama uko daraja la tatu na kukosa hamasa hakukushushi
chini ya daraja la pili, hali hii pia haina madhara. Lakini kama hali ya kukosa
hamasa inakushusha katika Dhikri kutoka daraja la tatu ukaja chini mpaka daraja la
kwanza au sifuri, wapaswa kuingiwa na shaka na kufanya jitihada ya ziada ili
kuihifadhi hatua uliyoifikia.
Nyakati sahihi za Dhikri Hali hiyo imeyotajwa hapo juu yathibitisha kwamba Dhikri ni jambo la muhimu
sana. Kama nilivyosema hapo awali kwamba Mwenyezi Mungu Anasema:
Basi mwishapo kusali mkumbukeni Allah kila msimamapo na mkaapo na mlalapo
kibavu. (Kurani Tukufu 4:104).
Swali la muhimu linazuka. Ni zipi nyakati sahihi za Dhikri? Kwa maana moja
Allah inabidi akumbukwe wakati wote. Hadhrat Aisha (ra) anasema kwamba
Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akimkumbuka Allah wakati wote. Lakini nyakati
fulani zimetajwa ndaniya Kurani Tukufu. Kwa mfano;
Na likumbuke jina la Mola wako katika nyakati za ‘Bukratan’ na ‘Aswiila’
(76:26).
Nyakati zilizotajwa katika aya hii ni za muhimu sana. ‘Bukra’, katika kiarabu
inamaanisha kutoka mwanzo wa pambazuko mpaka kuchomoza jua. Kwa maneno
mengine Allah Apaswa kukumbukwa tangu baada ya sala ya asubuhi mpaka jua
kuchomoza. ‘Aswiila’, wakati mwingine uliotajwa kwa Dhikri, ni kuanzia wakati
wa sala ya Asr mpaka kuchwa jua. Mungu Mwenye Enzi Anasema pia;
Basi yavumilie hayo wayasemayo, na utukuze kwa sifa za Mola wako kabla
halijatoka jua na kabla halijatua, na nyakati za usiku pia umtukuze, na katikati ya
mchana ili uliridhike. (20:131)
Aya hii inaainisha nyakati tatu zaidi kwa ajili ya kumkumbuka Allah. Wakati wa
kuchomoza jua, na wakati wa mwanzo wa usiku na wakati wa mwisho wa usiku.
Wakati wa sita wa kumkumbuka Allah ni mara baada ya kila sala ya faradhi.
Mtume Mtukufu (saw) alikuwa anazingatia sana kufanya Dhikri katika wakati huo.
Kufanya Dhikri katika wakati huo ni desturi yake (Sunnah). Hadhrat Ibn-i-Abbas
(ra) anasema kwamba Masahaba waliokuwa wamechelewa wakati wa sala
waliweza kutambua kwamba sala imeshamalizika kwa kuisikia sauti hii ya Dhikri.
Wewe ni Amani, Oh Allah, na amani yote yatoka kwako, Ewe Mwenye utukufu na
ukuu
Aina nyingine ya Dhikri baada ya sala ni kusoma;
Subhan -Allah (Utukufu wote ni wake Allah).
Al Hamdu lillah (Sifa zote njema zinamhusu Allah).
Allahu Akbar (Allah ni Mkuu kabisa)
Kuna hadithi kadhaa juu ya aina hii ya Dhikri. Njia bora zaidi ya kuifanya Dhikri
(hii) ni kuyasoma maneno ya mwanzo hapo juu mara thelathini na tatu (x33),
kisha yale ya pili mara thelathini na tatu (x33) na mwisho maneno ya tatu mara
thelathini na nne (x34).
Muda wa baada ya sala unakubaliwa sana na yapasa utumike kikamilifu kwa ajili
ya Dhikri. Baadhi ya watu wanaweza kudhani ya kwamba mimi siifanyi Dhikri hii
au kwamba Hadhrat Khalifatul Masihi -I (ra) hakuifanya. Hili ni kosa. Ninaifanya,
na Hadhrat Khalifatul Masihi -I (ra) pia aliifanya. Hata hivyo hakuifanya kwa sauti
na ndivyo ilivyo kwangu pia. Nanyi pia ifanyeni hii kuwa tabia yenu.
SALA Sasa nitaigeukia Dhikri ya muhimu kupita zote, (yaani) sala za faradhi. Katika sala
Muislam anafanya Dhikri katika mikao yote ya mwili, kusimama - Qiyam,
Kuinama - Ruku, Kusujudu - Sajda na kukaa - Qada.
Anaisoma Kurani Tukufu na kuzifanya aina nyingine za Dhikri. Sala ni mjumuiko
wa aina zote za Dhikri.
Falsafa ya kuwekwa sala za Sunnah na Nafali Sala tulizopangiwa zina sehemu tatu:-
1. Faradhi, sala za lazima
2. Sunnah, sala zilizosaliwa mara kwa mara na Mtume Mtukufu (saw) na
3. Nafal, sala za ziada
Sunnah zimepangwa ili kujaziliza mapungufu katika sala za faradhi. Allah
hazipokei sala zenye mapungufu, anapokea tu zisizo na chembe ya upungufu.
Lakini Anapokea Sunnah mahali pa mapungufu katika sala za faradhi, ikiwa
mojawapo ya rakaa katika faradhi inakosa umakini, au imeharibiwa na mpepesuko
wa mawazo, haitakubaliwa. Lakini hasara itajazilizwa na sunnah. Mtume Mtukufu
(saw) alitambua sana hali ya asili ya binadamu na madhaifu yake. Amefanya hisani
kubwa kwa wafuasi wake kwa kuongeza sunnah katika sala.
Halafu kuna Nafali, hizi ndio njia ya kupata ukaribu na Mungu. Zinamwinua mtu
kupita hatua ya ‘Najat’ (kuondokana na dhambi). Yeyote anayetaka ukaribu na
Allah apaswa kuweka zingatio la kipekee katika Nafali. Baadhi ya Nafali
hufanywa wakati wa mchana, nyingine hufanywa wakati wa usiku. Zile
zifanywazo usiku huitwa Tahajjud. Hii hubeba baraka za kipekee. Mungu Mwenye
Enzi Anasema;
Hakika kuamka usiku (kwa ibada) ni bora zaidi kwa kuikanyaga [kuishinda]
(nafsi) na vizuri zaidi kutamka. (Kurani Tukufu 73:7).
Nafsi inaweza kurekebishwa, na hatua za juu za kiroho zikafikiwa kwa njia ya
Tahajjud. Yeyote anayeitekeleza atabaini umuhimu wake. Masahaba wa Mtume
Mtukufu (saw) walikuwa hawakosi kabisa kusali Tahajjud. Ingawa ni ya ziada,
Mtume Mtukufu (saw), alikuwa akiwazungukia kuona nani aliitekeleza. Siku moja
sifa njema za Hadhrat Abdullah bin Umar (ra) zilikuwa zinasimuliwa. Mtume
Mtukufu (saw) akasema; Ndio ni mwema sana, lakini anapaswa kusali Tahajjud
vilevile. Alikuwa ni kijana mdogo na alikuwa mvivu katika Tahajjud. Mtume
Mtukufu (saw) alimkumbusha kwayo, juu ya uvivu wake katika kusali Tahajjud.
Mtume Mtukufu (saw) anasema, Allah na Awarehemu mume na mke ambao
huamshana kwa ajili ya sala usiku. Ikiwa mume ameamka basi asali Tahajjud kisha
amwamshe mke wake, ikiwa haamki basi amdondoshee matone ya maji usoni
kwake. Hali kadhalika ikiwa mke ataamka basi afanye vile vile, yaani asali
Tahajjud na kumwamsha mumewe kwa kumdondoshea maji usoni kwake. Mtume
Mtukufu (saw) amemwamuru mke kumuheshimu mumewe, lakini pamoja na hayo
amemruhusu kumdondoshea maji ikihitajika, katika kumwamsha kwa ajili ya
Tahajjud. Ni dhahiri, ameweka umuhimu mkubwa katika Tahajjud.
Kurani Tukufu inatuambia kwamba kuamka usiku kwa ajili ya sala kunaikanyaga
(kunaidhibiti) nafsi. Kufuatana na hilo Mtume Mtukufu (saw) anasema ni lazima
tuamke usiku kwa ajili ya Tahajjud, hata ikiwa ni kwa rakaa mbili tu. Anasema pia
kwamba Mungu Mwenye Enzi Anapokea kwa wingi maombi wakati wa mwishilio
wa usiku. Tahajjud, kwa hiyo, ni muhimu sana na yenye manufaa.
Njia ya kuamka usiku kwa ajili ya Tahajjud Njia mojawapo isiyofaa sana kwa maoni yangu ni kutumia kengele ya saa. Njia hii
huleta tegemezi, na hushindwa kuleta utashi thabiti. Kama ukienda kulala ukiwa
umekusudia kuamka kwa Tahajjud, utakuwa katika hali ya ibada usiku wote. Kwa
vile umedhamiria, utaamka. Wale wanaotegemea kengele ya saa, lakini hawana
dhamira thabiti, mara nyingi wataizima kengele iliapo na kurejea kwenye usingizi.
Ikiwa wataamka kwa ujumla watajisikia wanasinzia katika kusali. Utegemezi wao
unawazuia kuamka barabara na kuwa na umakini katika sala. Katika hali fulani
fulani, hata hivyo, saa ya kengele yaweza kutumiwa na wanaojifunza au wengine.
Kuna njia kumi na tatu ambazo zaweza kusaidia katika kuamka usiku. Yeyote
ambaye atazijaribu kwa uaminifu wa moyo, Mungu Akipenda atafaidika nazo.
Kunaweza kuwapo ugumu mwanzoni lakini hatimaye njia hizi zitathibitika kuwa
ni zenye manufaa. Nimezikokotoa njia hizi kutoka katika Kurani Tukufu na
hadithi. Ni rehema ya Allah kwamba njia hizi ambazo ziliendelea kufichika kwa
wengine, zimebainishwa kwangu. Ili kutopoteza wakati nitazieleza kama
nilivyoelewa bila kutaja rejeleo.
1. Ni kanuni ya asili kwamba kila kitu hurejea katika hali yake ya mwanzo ikiwa
mazingira yafananayo na yale ya mwanzo yatatokea tena. Mara nyingi katika
ukongwe, mtu huugua magonjwa yake ya utotoni. Hali hii pia hutokea kwa ndege
na miti. Kanuni hii inaweza kusaidia katika kujenga tabia ya kuamka usiku. Fanya
Dhikri kwa muda, baada ya sala ya Isha. Kadri ufanyavyo Dhikri zaidi, ndivyo
utakavyoamka mapema zaidi kwa ajili ya Dhikri kabla ya asubuhi.
2. Usiongee na mtu yeyote baada ya sala ya Isha. Ingawa wakati mwingine Mtume
Mtukufu (saw) aliendelea na mazungumzo baada ya Isha, lakini kwa kanuni ya
jumla alikataza jambo hili. Kuna sababu mbili (a) Ikiwa utaanza kuongea
utachelewa kulala na utashindwa kuamka usiku, na (b) Ikiwa maongezi yatahusu
mambo yasiyo ya kiimani, fikra zako zitaelekea kwingine. Wapaswa kulala wakati
unaifikiria imani yako, (ndipo) uta amka ukiwa na mawazo hayo hayo. Haikatazwi
kufanya kazi za Ofisini au majukumu mengine ya muhimu baaada ya Isha. Lakini
katika hali hiyo ni vyema kutumia muda kidogo kufanya Dhikri kabla ya kuingia
kulala.
3. Tawadha kabla ya kwenda kitandani, hata kama ungali na udhu. Inaathiri moyo
na huleta umurua wa kipekee mwilini. Kama ukienda kulala katika hali hiyo ya
umurua, utaamka na hali hiyo hiyo. Hili ni jambo lionekanalo mara nyingi. Mtu
akiwa anatabasamu wakati wa kulala kwa kawaida hutabasamu wakati anaamka,
yule anayelia anaamka analia. Kwa kutawadha, utakuwa murua wakati unalala na
murua wakati unaamka. Itakusaidia pia katika kuamka.
4. Soma Dhikri fulani kabla hujapitiwa na usingizi. Hii itasababisha uamke tena
kwa ajili ya Dhikri usiku. Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akisoma Dhikri ifuatayo
kabla ya kupitiwa na usingizi; Alisoma Ayat-ul-Kursi (Aya 2:256) na sura tatu za
mwisho za Kurani Tukufu, kisha alipulizia polepole mikononi mwake na kisha
kuipitisha mikono yake kwa kujipakaza mwilini mara tatu, kisha aligeukia kulia
na kusema;
Oh! Allah, najiweka katika ulinzi wako, na nageuza uso wangu kuelekea kwako na
kuacha masuala yangu yote kwako, kwa upendo halisi na hofu juu yako, hakuna
kimbilio wala ulinzi kutoka kwako isipokuwa kwako mwenyewe. Naamini kitabu
chako ulichokiteremsha na Mtume wako uliyemtuma.
Waumini wote wapaswa kufanya Dhikri hii na kisha kuendelea na Dhikri zingine
mpakausingizi uwachukue. Usomaji wa muhimu katika wakati huu ni:
(Subhaana llaahi wa bi Hamdihi Subhaana Allah hil ‘Adhwiim)
Mtakatifu ni Allah, kwa sifa zake, Mtakatifu ni Allah kwa ukuu wake.
Hali ambayo mtu huingia nayo usingizini hubakia nayo usiku wote, ikiwa mtu
analala wakati anafanya Tasbiih (kumtukuza Allah) na Tahmiid (kumsifu Allah)
atabaki katika hali hiyo ya kiroho usiku wote. Ni jambo la mazoea kwamba
wanawake au watoto ambao wamesumbuliwa au wana maumivu wakati wa kulala,
hulia wanapojigeuza upande wakiwa usingizini. Hali kadhalika ikiwa mtu anaenda
kulala akiwa anaisoma Tasbiih, basi ataisoma Tasbiih atakapojigeuza upande.
Mungu Mwenye Enzi Anasema:
Huinuka mbavu zao kutoka vitandani kumwomba Mola wao kwa hofu na tumaini,
na hutoa katika yale tuliyowapa (32:17).
Kwa mtazamaji wa kijuu juu, inaweza isionekane kwamba Waislam wanakaa
mbali na vitanda vyao. Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akilala na hali kadhalika
Waislam wote hulala. Lakini kwa kweli kulala kwao sio kulala, ni aina fulani ya
Tasbiih. Wanaonekana wamelala, lakini kwa kweli hawajalala. Mbavu zao huinuka
kutoka vitandani mwao, wako shughulini katika kumkumbuka Mola wao.
5. Kaza kabisa nia wakati wa kulala, kwamba utaamka kwa ajili ya Tahajjud.
Mungu Mwenye Enzi Amempa mwanadamu nguvu ya kufanya fahamu yake itii
utashi wake. Wanafalsafa wamekubaliana na kanuni hii. Azimia kwa dhati
kwamba utaamka kwa Tahajjud, wakati mwili wako umelala fahamu yako itakuwa
macho. Itakuamsha wakati ule ule ulioutaka.
6. Njia ya sita ni kwa walioimarika katika imani. Badala ya kusali Witr (rakaa tatu
za wajibu) baada ya Isha, ahirisha Witr kwa ajili ya kuijumuisha na Tahajjud. Kwa
ujumla watu ni wazingativu katika kufanya ibada za faradhi lakini huwa
wanalegalega katika ibada za ziada. Witr ni wajibu sio faradhi lakini ni muhimu
kuliko sala za ziada. Wakati wajibu inaunganishwa na Nafali itaongeza mkazo wa
dhamira ya kuzitekeleza zote. Roho haitatulia mpaka wajibu umetimizwa. Kwa
njia hii Nafali pia itatimizwa.
Mtu ambae ameshasali Witr anaweza asiamke kwa Tahajjud hata kama yuko
macho. Roho yake itajisikia amani. Lakini kama bado Witr inadai, Roho haitatulia
na itamuamsha. Wale tu walio imarika katika imani wanaweza kutumia njia hii.
Walio dhaifu wanaweza kujikosesha hata Witr kwa kuijaribu njia hii.
7. Njia ya saba pia ni kwa ajili ya waliopiga hatua kubwa katika imani. Waanze
kusali Nafali baada ya sala ya Isha na kuendelea mpaka waanze kusinzia katika
sala na kuelemewa na usingizi. Ingawa muda wao wa kulala utapungua watajikuta
wako macho wakati wa Tahajjud. Njia hii ni mazoezi kwa ajili ya Roho.
8. Njia ya nane imetumiwa na Masufi wengi. Sijasikia haja ya njia hii mimi
mwenyewe, lakini inaelekea inafaa. Kama unayotabia ya kulala fofofo, badilisha
kitanda laini utumie kigumu.
9. Kula chakula cha jioni masaa kadhaa kabla ya kulala. Kula kabla ya Maghrib au
mara baada ya Maghrib. Wakati mwingine roho iko tayari, lakini mwili hauko
tayari. Mwili ni kama kiini, kama kiini ni kizito mno kinainyonga roho. Tumbo
lisiwe limejaa wakati wa kulala. Hii ina athari mbaya kwa moyo na humfanya mtu
kuwa mvivu.
10. Usilale ukiwa mchafu. Malaika wanashirikiana na wale walio safi,
hawawaendei waliochafuka. Siku moja Mtume Mtukufu (saw) alipewa kitu fulani
chenye harufu kali. Hakukila lakini aliwapatia Masahaba wake kukila. Alieleza
kwamba malaika ambao humtembelea yeye mara kwa mara hawapendi harufu
kama ile. Malaika wanachukia uchafu. Siku moja Hadhrat Khalifatul Masih -I (ra)
alienda kulala bila kuosha mikono baada ya chakula cha jioni. Aliona ndoto, kaka
yake alitaka kumpatia Kurani Tukufu, lakini alipokaribia kuigusa kaka yake
aliiondoa na akasema, usiguse Kurani Tukufu, mikono yako ni michafu. Unadhifu
wa mwili unaathiri utakaso wa moyo. Walio safi watapata malaika kuwasaidia
kuamka, walio wachafu hawatakaribiwa na malaika. Kwa hiyo wekeni miili yenu
safi.
11. Kitanda chapaswa kuwa safi. Watu wengi hupuuzia jambo hili. Kumbukeni
hali ya kiroho huathirika moja kwa moja na usafi wa kitanda. Wekeni uangalifu wa
kipekee katika jambo hili.
12. Mume na mke waepuke kulala pamoja. Miongoni mwa Waislam wa kawaida
jambo hili la kulala pamoja laweza kudhuru hali ya roho, lakini haiwadhuru wale
walioendelea kiroho. Mtume Mtukufu (saw) alilala katika kitanda kimoja na wake
zake. Alikuwa na daraja la juu mno la kiroho na hali yake ya kiroho isingeweza
kutikiswa. Waislam wa kawaida wanapaswa kuwa waangalifu. Matamanio ya
kimwili huathiri vibaya hali ya kiroho. Ndio maana Islam inafundisha;
Kuleni na kunyweni lakini msipite kiasi (Kurani Tukufu 7:32)
Kwa nini Islam inatukataza tusipite kiasi? Kwa sababu isirafu inadhuru hali ya
kiroho. Watu wenye uwezo wa kuzitawala hisia zao hawatadhurika kwa kulala
pamoja, lakini Waislam wa kawaida watakuta kwamba hali hii inazifanya fahamu
zao zielemee kwenyematamanio. Hii huidhuru hali ya kiroho na kuwazuia kuamka.
13. Njia ya mwisho ni bora kwa zote. Inasaidia kwa ajili ya kuamka kwa Tahajjud
na humwokoa mtu katika madhambi mengi na udhaifu. Kabla ya kulala, tafakari
kama unayo bughudha au unayo chuki moyoni au mgongano na mtu yeyote. Kama
hali kama hizo zipo ziondoshe moyoni mwako. Takasiko lipatikanalo kwa zoezi
hili litakuwezesha kuamka kwa ajili ya Tahajjud.
Moyo wapaswa kuwa safi kabisa wakati wa kulala. Yeyote anayedhani bado anayo
haja ya kubaki na kero alizo nazo, apaswa kujikumbusha kwamba ataweza kuwa
huru kuendelea na mawazo kama hayo wakati wa mchana, lakini hayahitaji usiku.
Kwa vyovyote haitarajiwi kwamba atapigana na yeyote usiku ule wakati tayari
analala.
Baada ya kung’olewa, mawazo kama hayo, kwa ujumla, hayarejei. Hata yakirejea,
madhara yake hayatakuwa makubwa sana. Matokeo ya jambo hutegemea ni kwa
muda gani limeathiriwa na jambo jingine. Ukipangusa kitu na sponji kitapata
unyevu lakini ukiiloweka sponji kwa muda mrefu itajaa maji. Mawazo ambayo
hudumu na yanarudiwarudiwa fikrani mwako usiku wote yatauelemea moyo wako.
Mawazo kama hayo hayataweza kuleta madhara makubwa wakati wa mchana kwa
sababu fikra zako zimemezwa na shughuli nyingine. Lakini wakati wa usiku fikra
inayo wasaa wa kuweza kuathiriwa. Ondosha mawazo yote mabaya juu ya
wengine yanayotokea wakati wa kulala yasije yakajengeka. Kuyaondosha wakati
huu haitakuwa vigumu. Zaidi ya hapo, ikiwa utafariki usiku huo (kabla
hujayaondosha mawazo kama hayo) utakosa nafasi ya kuomba msamaha kwa
dhambi hii.
Ikiwa utaiondosha chuki mara moja, utakuwa huru kwa kudumu. Ukijisafisha kwa
njia hii usiku, bila ya shaka utapata baraka ya nafasi ya kuamka kwa ajili ya
Tahajjud.
Kumakinika katika sala.
Sasa nitazungumzia juu ya kuwa na umakini katika sala. Somo ambalo nimeulizwa
mara nyingi juu yake. Mnaweza mkawa tayari mnazitumia njia nitakazozieleza.
Kama mmezitenda kwa ukamilifu wake, ni lazima mtakuwa mmeonja matokeo
yake mazuri.
Kama sehemu ya maamrisho katika sala, sharia (sheria ya Islam) imeweka baadhi
ya kanuni kwa ajili ya kuhakikisha umakini unakuwapo. Kwa sababu ya ujinga
wao wenyewe, watu wengi hawapati faida yoyote kutokana na kanuni hizi.
Nitaongeza baadhi ya mbinu ambazo kwa ujumla hazifahamiwi lakini zaweza
kusaidia. Hebu nianze kwa kanuni ya jumla. Mtu anapoiamini mbinu anayoitumia,
hunufaika zaidi na mbinu hiyo. Sardo alikuwa mtunisha misuli mahiri huko Ulaya.
Alisema kwamba mazoezi ni muhimu kwa afya, wakati huo huo ni lazima uamini
kwamba mikono yako na misuli inaendelea kuwa na nguvu zaidi na kutuna.
Mikono huwa na nguvu zaidi kwa mazoezi, lakini unapoongeza imani kwamba
mwili unafaidika, kiasili unaathirika. Bila imani kama hizi, sehemu kubwa ya
athari ambayo ingeweza kutokea hupotea na manufaa hupungua.
Kanuni ndani ya sheria ya Islam ambazo zinasaidia umakini katika sala.
Baadhi ya kanuni zilizomo katika sheria ya Islam kwa ajili ya kuhakikisha umakini
ni kama zifuatazo:-
1. Kutawadha ni muhimu kabla ya kila sala. Mungu Mwenye Enzi Ameumba njia
za kuwasilisha mawazo na hisia. Moja ya njia hizi ni mfumo wa neva. Hufanya
kazi kama mfereji wa kupitisha hisia za mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mtume Mtukufu (saw) alisoma Ayatul Kursii na kisha akapulizia mikono yake na
kuipitisha pole pole kwenye mwili wake. Unadhani kwamba tendo hili lilikuwa
halina maana yoyote? Hapana. Ukweli ni kwamba mawazo husafirishwa kutoka
kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia mfumo wa neva na vilevile kupitia
sauti, na pumzi. Mtume Mtukufu (saw) alizitiisha njia hizo zote za mawasiliano
kwa kusoma Ayatul Kursii kwa ulimi wake, kisha kupulizia pumzi mikononi
mwake, na halafu kuipitisha mikono yake juu ya mwili wake.
Kwa kifupi, sauti, mfumo wa neva, kuona, na pumzi zote hizi ni njia za
kuwasilishia mawazo. Hii ndio maana Waislam wacha Mungu, akiwemo Mtume
Mtukufu (saw), waliyasoma maneno maalum na wakayapata manufaa kamili ya
kiroho kwa kupulizia au kuigusa miili.
Kwa kuwa mfumo wa neva ni njia ya kuwasilishia mawazo. Mtume Mtukufu (saw)
ametuelekeza tutawadhe ili kusafisha mawazo yetu. Njia kuu za kutolea mawazo ni
vinywa, mikono na miguu. Zinatakiwa ziwe safi. Majaribio yameonyesha kwamba
pale mdomo, mikono na miguu inapooshwa na maji, mlolongo wa mawazo
machafu hukatika. Kutawadha kunakata mlolongo wa fikra za nje na huleta utulivu
na raha. Hii kwa upande wake, husaidia katika umakini. Unapotawadha, dhamiria
kwa dhati kuwa udhu ulioupata utayadhibiti mawazo yote yanayokutoa katika
umakini. Ukiwa na msimamo huu utahisi raha ya ziada na mawazo yako
hayatapepesuka.
2. Njia nyingine ya kufikia umakini katika sala ni kusali katika jamaa msikitini.
Fikra ya binadamu hufanya kazi kupitia mchakato wa mahusishano. Tom
anapokutana na Dick humuuliza juu ya mtoto wake Harry. Ingawaje Harry hayupo,
kukutana na Dick kunamkumbusha Harry. Hivyo ndivyo akili ya binadamu
ifanyavyo kazi. Unapoona kitu fulani, unakumbuka pia vitu vingine
vinavyohusiana na kitu kile. Ikiwa mtu atasali katika mahala paitwapo nyumba ya
Mungu, ambapo sala husaliwa usiku na mchana, ni hakika kabisa kwamba,
atafikiria kwamba anasimama mbele ya Mungu Ambaye kwa ajili ya kumwabudu
yeye sehemu ile imejengwa. Kwa hiyo atajisikia ni lazima amtii Mola Wake kwa
moyo wa kweli. Mtume Mtukufu (saw) ameelekeza kwamba Waislam ni lazima
watenge mahali kwa ajili ya sala majumbani mwao. Kusalia pale kutawakumbusha
kwamba mahali pale pametengwa kwa ajili ya ibada. Wanaweza kuwepo baadhi
kati yetu ambao hawajawahi kuhisi mawazo kama hayo misikitini. Lakini sasa kwa
kuwa hekima hii imewekwa wazi mtaweza kwenda Misikitini mkiwa na hisia hizi.
Hii itawasaidieni kudhibiti mawazo yanayojiingiza ingiza na kumakinika katika
kitendo chenu cha ibada na kupata amani ya kweli.
3. Agizo la kuelekea Ka’aba, (nyumba ya kwanza ya Mungu iliyojengwa Maka),
vile vile husaidia katika kupata umakini. Jiji la Maka lina sifa nyingi njema.
Ilikuwa ni hapa ambapo kwa kutii amri ya Mungu, mpendwa mmoja wa Allah,
Ibrahim (as), alimuacha mke wake na mtoto bila chakula wala ulinzi.
Kwa kuwa alifanya hivi kwa ajjili ya Mungu, Mungu Alikiongeza kizazi chake,
ambacho kinahesabika kama nyota mbinguni. Manabii wengi walizaliwa katika
uzao wake. Hatimaye, mtu aliyekusudiwa kuwaongoza binadamu wote aliinuliwa
pia katika kizazi chake.
Mtu anapotambua hekima ya kugeuza uso wake kuelekea Makka, anahamasishwa
na kujitolea kulikofanywa na Ismail (as). Mawazo yake yataelekea kwenye ukweli
kwamba Mungu Ambaye, kwa ajili ya ibada yake Amesimama hivi sasa, ni Mola
wa Heshima kubwa na utukufu. Utambuzi huu husaidia kuondoa mawazo potoshi
na kumuongoza mtu katika kutambua adhama na utukufu wa Allah.
4. Mwito wa adhana husaidia vile vile katika umakini. Mwito wa Allah-o-Akbar,
Allah-o-Akbar (Mungu ni Mkuu kabisa, Mungu ni Mkuu kabisa) huwakumbusha
waabuduo kwamba Mungu Ambaye wanaitwa kwenda mbele yake ni Mkuu kuliko
wote. Hii itahimiza umakini katika sala yao. Mtume Mtukufu (saw) anasema
adhana hutolewa ili kumfukuza shetani.
5. Iqamat (kifupisho cha adhana kinachosomwa wakati wa kuanza sala ya jamaa)
vile vile huzielekeza fikra kwenye ukubwa na utukufu wa Mungu. Hekima yote
iliyoko kwenye adhana inaihusu pia Iqamat, Mtume Mtukufu (saw) anasema
Iqamat pia humfukuza shetani. Alimaanisha kwamba Iqama huondoa miegamo
mibaya ya fikra na kuhamasisha umakini katika ibada.
6. Utulivu katika mipangilio ya nje huzalisha utulivu katika mawazo na
hauyaruhusu kutawanyika. Wakati mistari inaponyooshwa kwa ajili ya sala,
mawazo ya ndani pia hupangika. Na inatisha kiasi gani hali inayowakilishwa na
mistari iliyonyooka wakati wa sala - kila mmoja akiwa amesimama mbele ya
Mfalme wa Wafalme kimya kabisa! Mtume Mtukufu (saw) anasema, hakikisheni
mistari yenu imenyooka zisije zikapindama nyoyo zenu. Nini umuhimu wa
mistari? Ni huu tu kwamba kupinda pinda kwa njekusilete athari mbaya katika
utulivu wa kiroho.
7. Njia ya saba ya kufikia umakini katika sala ni Niyat (kukusudia), kwa sababu
unapoiamuru fahamu yako kufanya kitu fulani inakifanya. Niyat haina maana
unatakiwa kutaja jina la Imam, idadi ya rakaa na kuelekea ka’aba. Azma ya
kufanya ibada ya sala inatakiwa ipitishwe nyoyoni. Inasemwa mtu fulani alipata
ugonjwa wa kuogopa Niyat na hususan juu ya kutaja jina la Imam (yule
anayeongoza sala). Aliposimama katika mstari nyuma ya wengine, hakutosheka na
kutamka ‘nyuma ya Imam huyu’. Alikuwa na shaka kwamba kwa vile walikuwapo
watu wengine kati yake na Imam, basi hakuwa hasa nyuma ya yule Imam. Kwa
hiyo alisonga mbele na kusema nyuma ya Imam huyu, lakini bado hakutosheka,
alisonga mbele zaidi mpaka alipomgusa Imam na kusema nyuma ya Imam huyu.
Wale wanaoingiza katika imani bidaa potofu kama hizi wamekosea. Wanadhurika
na matokeo yake. Niyat inageuzwa kuwa mzigo usio wa lazima. Kwa kweli nia
inahusiana na moyo. Unaposimama kwa sala, fikra zako ziwe macho juu ya sala.
Jikumbushe unachojiandaa kukifanya. Mara unapolielewa hili, utaanza
kunyenyekea na kuwa makini.
8. Katika sala za Jamaa, Imam anarudia rudia maneno ambayo huleta hofu ya
Allah. Yeyote anayepotelewa na mawazo hutikiswa na kuamshwa. Pale Allah-u-
Akbar inapotamkwa anaonywa, simama kwa ukamilifu wa adabu kwa sababu yule
uliyeko mbele yake ni mkuu kuliko wote. Halafu baada ya muda kidogo mawazo
tena yanapoteleza, Imam hurudia ukumbusho huo huo. Tena baadae kidogo,
anaambiwa, ‘Sami Allahu li man Hamida (Mungu Humsikiliza yule anayemsifu).
Kumkumbusha kwamba ili kunufaika na sala, ni lazima atumie muda wa sala
katika kumsifu Allah, vinginevyo, anapoteza muda wake.
Ukumbusho wa mara kwa mara kutoka kwa Imam huwafanya wafuasi kuwa
macho na wasikivu. Hii ndiyo sababu Imam anayo daraja juu ya wafuasi,
anawakumbusha tena na tena kwamba wamesimama mbele ya mkuu kabisa katika
Wafalme, na kwa hiyo ni lazima wasimame kwa utulivu kamilifu.
9. Islam haikuchukua mkao mmoja tu kwa ajili ya sala, bali mikao mbalimbali.
Ikiwa mtu atazama katika mawazo mengine, kwenda kwake kwenye Ruk’u
(kiinamo), Sajda kunamkumbusha. Hata mtu akienda katika mikao hii kama
mazoea, ile miondoko ya kuiendea mikao hii huifanya fahamu kuwa macho. Ibada
katika dini nyingine hainazo sifa hizi, Islam ni pekee kwa kuwa na sifa hizi za sala.
10. Kusali sunnah kabla na baada ya faradhi vile vile husaidia kufikia umakini,
hususan wakati wa sala ya faradhi. Ni kanuni ya kimaumbile kwamba dalili ya
matukio yajayo huanza kuonekana kabla ya matukio yenyewe, na athari zake
huendelea kuonekana baada ya matukio kutokea. Kwa mfano, mwangaza huenea
kabla jua halijaonekanaasubuhi na huendelea kuonekana baada ya jua kuzama
jioni. Tunaona pia kuwa aina fulani za hofu hujaza mioyo na kuhafifisha mawazo
mengineyo.
Masuala ambayo huendana na matakwa ya mtu, au yale yamleteayo furaha, au yale
ambayo kukosekana kwake kwaweza kuleta madhara, hufunika masuala mengine
na huchukua nafasi kubwa katika fikra. Ikiwa mtu ameshika kazi ambayo
haionekani kuwa na manufaa sana kwake, na kama inabidi afanye jambo ambalo
linaelekea kuwa na manufaa kwake au atadhurika kama halikufanyika, au lina
mvuto wa kipekee kwake, mawazo yake yatazama kwenye shughuli hii ya pili hata
anapokuwa anaifanya shughuli ile ya mwanzo. Chukulia kwa mfano mfanyakazi
ofisini, kama inabidi afanye shughuli yake binafsi baada ya masaa ya kazi, ataanza
kuifikiria shughuli hiyo saa moja au masaa mawili kabla ya muda wa ofisi kwisha,
kinyume chake ikiwa ameshika shughuli muhimu ofisini, ataendelea kuiwazia
shughuli hiyo baada ya kuondoka ofisini. Ni baada ya muda fulani kupita ndipo
ataweza kuweka mawazo yake yote kwenye shughuli nyingine.
Mtume Mtukufu (saw), ameweka sunnah kabla na baada ya sala za faradhi
kuhakikisha kwamba faradhi haziingiliwi na mlolongo wa mawazo. Kuyumba
kama huko kunadhibitiwa wakati wa kusali sala za sunnah na kumfanya mtu
kujiandaa kikamilifu na kupata utulivu wa mawazo wakati wa kusali faradhi.
Hivyo hivyo, Sunnah zimewekwa baada ya sala ya faradhi ili kuzuia mawazo ya
shughuli zinazongojwa kufanywa kuingilia sehemu ya mwisho ya sala za faradhi.
Hivyo sala yote ya faradhi imelindwa. Kama nilivyosema, mawazo potoshi, kwa
ujumla, huzuka wakati shughuli ya mwanzo inakaribia kumalizwa, na fahamu
inatayarishwa kwa shughuli ya pili. Kama mtu anaamini mwishoni mwa sala yake
ya faradhi, kwamba bado hajamaliza - suna bado zimebaki, mawazo yake
yataendelea kubaki yamedhibitiwa. Hii ni moja wapo ya sababu kubwa ya
kuwekwa sala za sunna. Mtume Mtukufu (saw) ameweka idadi ya sala za sunna
kulingana na mahitaji ya wakati. Wakati wa sala ya Dhuhur ni wakati wa
mishughuliko mingi katika kazi nyingi. Kwa hiyo ameweka rakaa mbili au nne
kabla na baada ya faradhi. Ameweka walinzi wawili kulinda sala ya faradhi kutoka
kwenye mtangotango wowote wa mawazo.
Hakuna sunna kabla ya sala ya Asr lakini ziko Nafali. Mtu anaweza kuzisali au
kuziacha, kwa kuwa ni wakati wa kumaliza shughuli za kikazi. Sala ya wakati huu
kwa hiyo ni fupi sana. Lakini kuna Dhikri kati ya Asr na sala ya Maghrib.
Hakuna sunna kabla ya sala ya Maghrib kwa sababu kwa ujumla muda ni mfupi
sana, lakini sunna zipo baada ya sala ya maghrib. Chakula cha jioni kwa ujumla
huliwa baada ya sala ya maghrib. Raka’a mbili za sunna huilinda fahamu isizame
katika mawazo juu ya chakula au mambo kama hayo.
Hakuna sunna kabla ya sala ya Isha kwa sababu, aina ya mshughuliko ulioko kabla
ya Isha, hauyamezi mawazo kwa muda mrefu, lakini kuna sunna na Witr baada ya
Isha kuilinda fahamu na mawazo ya kulala. Witr yaweza pia kusaliwa baadae.
Kuna rakaa mbili za sunna kabla ya Alfajr kazi yake ni kuondoa usingizi. Hakuna
sunna baada ya Alfajr kwa sababu kwa ujumla hakuna shughuli za kuweza
kuyachukua mawazo ya mtu baada ya Alfajr. Lakini Dhikri imewekwa kati ya
Alfajr na kuchomoza jua.
Njia zote hizo hapo juu zimewekwa katika sheria. Waweza kufaidika nazo
kikamilifu, ukielewa falsafa yake na kuendelea kujikumbusha juu ya hekima zake.
Nimezielezea njia hizi kwa kirefu kuwawezesheni kuzielewa kikamilifu. Mungu
Apendapo wale watakaozitekeleza, wakizingatia ipasavyo falsafa yake, watapata
manufaa makubwa.
Yapasa pia ikumbukwe kwamba kama ambavyo mwili wa binadamu una viungo,
ndivyo ilivyo kwa sala. Viungo vya sala ni yale maneno yasomwayo wakati wa
kusimama, kurukuu (kuinama), na kusujudu. Vipeni uzito wa kipekee viungo hivi
kuifanya sala yenu iwe yenye nguvu sawa sawa na iliyo simama imara, vinginevyo
itaanguka.
Njia nyingine za kuhifadhi umakini. Nitageukia njia ambazo hazikuwekwa katika sheria lakini zinaweza kusaidia
kuhifadhi umakini katika sala.
11. Kama huwezi kumakinika, soma maneno ya sala polepole. Akili ya binadamu
haraka hukumbuka mambo ambayo imeyaona mara nyingi, lakini hupata ugumu
katika kuyakumbuka mambo ambayo imeyaona mara chache. Kama unamwona
Tom kila siku taswira yake itakujia mara moja unapomfikiria, lakini kama
unamwona mara moja moja taswira yake itakuja baada ya muda kidogo, na hapo
pia sio wazi wazi sana. Vivyo hivyo, kama ukijifunza lugha katika utoto, taswira
zafanyika mara moja pale maneno yanapotamkwa. Wakati maneno kwa ajili ya
maji na mkate yanapotamkwa, haraka huamsha katika fahamu vitu halisi
yanayoyawakilisha. Hali sio hiyo kwa lugha za kigeni. Fahamu inajiwa na taswira
baada ya muda kidogo. Wakati watoto wanajifunza kiingereza na kutamka neno
kama paka, litaonekana kuwa sio kitu zaidi ya neno tu kwao. Lakini wakati neno
kama hilo linatamkwa katika lugha yao ya asili, fahamu zao mara moja huunda
taswira ya paka.
Wengi wa Waislam wasiokuwa na mazoea na Kiarabu hawawezi kuwa makini
kikamilifu katika sala. Umakini unahitaji maana za maneno ziwe zimehifadhiwa
katika fahamu zao. Bila hivyo hawawezi kuvuta taswira papo kwa papo.
Wanaweza kuwa wanasoma aya ya nne ya sura Al-Fatiha; ‘Iyyaka Na’abodo’
(wewe tu twakuabudu), wakati fahamu zao ingali bado kwenye mchakato wa
kuvuta taswira za aya ya pili; ‘Ar-RahmanirRahim’ Mwingi wa rehema mwingi wa
ukarimu). Hivyo, umakini wao unaathirika na manufaa ya sala yanapungua. Ni
muhimu kwa wale ambao uwezo wao wa Kiarabu ni hafifu kuyasoma maneno
polepole. Mpaka fahamu zao zinapokuwa zimevuta taswira kamili ya mstari
mmoja, ndipo waendelee na mstari unaofuata. Yawabidi kusema Bismillaahir
Rahmaanir Rahiim (Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, mwingi wa ukarimu)
na kujaribu kuvuta taswira kamili ya maana yake ya kweli. Haiwapasi kuendelea
kwenye Alhamdulillahi Rabbil Aalamiin (Sifa zote njema zinamhusu Allah, Mola
wa Walimwengu) mpaka taswira ya mstari uliopita imekuwa bayana na murua.
Iwe hivyo hivyo kwa mstari unaofuata, Maaliki yaumiddiin (Mmiliki wa siku ya
malipo). Bila kuishika tabia ya kusoma pole pole na kwa tafakari kama hivi,
maneno kwenye vinywa vyao yatakuwa tofauti na taswira kwenye fahamu zao.
Hata wale wanaoelewa Kiarabu watanufaika na usomaji wa pole pole. Ingawa
wataweza kuziita taswira haraka, usomaji wa haraka hautatoa muda kwa ajili ya
kuingiza moyoni hisia zinazoletwa na maneno yanayotamkwa. Wapaswa pia
kuisoma Kurani Tukufu pole pole na kuigawa kwa vituo vya mara kwa mara.
Usomaji wa pole pole ni mazoea mazuri, sio tu katika kusoma Kurani Tukufu,
lakini pia kwenye maongezi ya kawaida, wakati wa kutoa na kupokea ushauri na
mawaidha. Siku moja Hadhrat Abu Huraira (ra), alikuwa anasimulia hadithi kwa
haraka na sauti ya juu. Hadhrat Aisha (ra) alimuuliza yeye ni nani na alikuwa
anafanya nini. Alitaja jina lake na kueleza kwamba alikuwa anasimulia hadithi ya
Mtume Mtukufu (saw). Akamuuliza “Hivi ndivyo Mtume Mtukufu (saw)
alivyokuwa akifanya katika mazungumzo yake?”. Alikuwa hana jibu.
Njia ya Mtume Mtukufu (saw) ilikuwa ni kuongea kwa polepole, sio tu katika
usomaji, lakini pia kwenye maongezi ya kawaida. Fuateni njia yake itaondoa
mkanganyiko kati ya maneno mnayoyasema, na taswira zinazojengeka katika
fahamu zenu. Ni njia bora kabisa ya kuhifadhi umakini.
12. Njia ya kumi na mbili imeagizwa na Mtume Mtukufu (saw). Ameelekeza
kwamba macho lazima yaangalie mahali pa kusujudia wakati wa sala. Watu wengi
wanapuuzia maelekezo haya. Wanafumba macho yao wakati wa sala wakidhani
kwamba kwa njia hii watapata umakini. Sivyo hivyo, umakini waweza tu
kupatikana kwa kuacha macho wazi. Hii ndio maana Mtume Mtukufu (saw)
ametushauri tufumbue macho yetu. Katika kitabu chake Awariful Ma’arif,
shahabuddin Suherwardi anasema, kwamba wakati wa rukuu macho yaangalie
kwenye nafasi kati ya miguu miwili. Nakubaliana na pendekezo hili, lina manufaa
kwa macho na huleta unyenyekevu.
Kuna hekima kubwa katika kuelekeza macho kwenye nukta moja. Ni tabia
yamwenendo wa mwili wa binadamu kwamba, pale moja wapo ya njia za fahamu
inapokuwa imezama kabisa katika utendaji, njia nyingine za fahamu hupumzika.
Pale macho yanapokuwa makini kabisa, kipawa cha kusikia hakitafanya kazi.
Ikiwa mtu atakuita wakati kama huo hutaisikia sauti yake. Vivyo hivyo, wakati
masikio yamo shughulini, kipawa cha kusikia harufu hakitafanya kazi. Ikiwa moja
wapo ya njia za fahamu imezama kabisa katika shughuli, fahamu nyingine
hazifanyi kazi. Lakini kama hakuna chochote katika njia za fahamu kilichomo
shughulini, aina mbalimbali za mawazo yanayotangatanga yatafurika ndani ya
fahamu. Ikiwa macho yatakuwa mashghuli katika sala, fahamu haitatangatanga
tena. Jambo hili hivi sasa limethibitishwa kwa majaribio katika mwenendo wa
mwili.
Fikiria tu kwamba Mtume Mtukufu (saw) alitoa maelekezo ya kufumbua macho na
kutazama wakati wote katika sehemu ya kusujudia miaka elfu moja mia nne
iliyopita, katika wakati ambapo ugunduzi kama huu wa kisayansi ulikuwa bado
haujafanywa. Zaidi ya hayo aliainisha njia ya fahamu ambayo ni lazima iwe
imekamatwa kikamilifu ili kumlinda mtu na kutanga tanga kwa mawazo.
Vipawa vya kuhisi harufu na kusikia haviwezi kulengwa kwa njia kama hii kwa
kuwa utendaji kazi wao mara nyingi unakuwa ni wa bila hiari. Kutumia kipawa
cha kuhisi harufu kwa ajili ya kulifikia lengo hili kunahitaji mipango ifanywe
kupata manukato ya aina mbalimbali. Ikiwa watu wenye manukato tofauti tofauti
watapita karibu, basi mwelekeo wa mawazo ungeweza kugeuzwa. Hali ni kama
hiyo pia kwa kipawa cha kusikia. Hakuna awezaye kuamua nini anataka kusikia na
nini hataki kukisikia. Ikiwa sauti mbalimbali zinatokeza kwa wakati mmoja mtu ni
lazima azisikie zote. Kwa hakika katika hali kama hiyo hakuna sauti yoyote
itakayosikika vyema. Kwa hiyo ukitumia kipawa cha kusikia, masikio aidha
yatasikia sauti zote au hayatasikia sauti yoyote.
Tofauti na vipawa vya kusikia na kuhisi harufu, kipawa cha kuona chaweza
kutawalika. Mtu anaweza kugeuza macho yake ili asione asichopenda kukiona na
anaweza kukazia macho kile anachokitaka kukiona. Chini ya amri ya Mungu,
Mtume Mtukufu (saw) alichagua kipawa cha kuona kwa ajili ya kupata umakini
katika sala.
Mtume Mtukufu (saw) ameelekeza pia kwamba mahala pa kusujudia papaswa
kuwa palinganifu na pasiwe na mapambo. Wakati Mwislam anakazia macho yake
mahali pa kusujudia matokeo yatakuwa yenye manufaa sana. Mawazo yake
yatakuwa makini kwenye ibada kwa ukumbusho unaoendelea wa kusujudu.
Vipawa vyake vingine ambavyo kikanuni vyaweza kuwa macho au vimesinzia,
vitakuwa vimedhibitiwa. Kwa vile mawazo huamshwa na vichocheo vya nje,
ambavyo navyo huhisiwa kupitia njia za fahamu, ukweli kwamba macho
yamewekwa kazini na njia zingine za fahamu zimesinzia, utamwezesha mtu kuwa
makini katika sala.
Siku moja kitambaa kilichorembwa kiliwekwa mahali ambapo Mtume Mtukufu
(saw) alikuwa akisalia. Aliamuru kiondolewe, alieleza kwamba kitaathiri umakini
katika sala. Maelekezo yake yalikuwa ni kwa faida ya wafuasi wake.
13. Kama nilivyotaja mapema, Niyyat (dhamira) inahitajika mwanzoni mwa sala.
Itasaidia pia ikiwa mwanzoni mwa sala utaazimia kutoruhusu fikra potoshi
zijipenyeze na kupotosha fahamu yako. Kila mtu anajua kwamba mawazo kama
hayo hayatakiwi. Lakini watu ni wenye kusahau na kujikumbusha mwanzoni mwa
kila sala bila shaka kutasaidia.
14. Wakati unamfuata Imam, usomaji afanyao Imam utakuweka macho na makini.
Imam kwa hiyo huwalinda wafuasi wake. Hii kwa bahati yaonyesha ni muhimu
kiasi gani kusali nyuma ya Imam. Unaposali peke yako, inabidi ufuate njia bora
kabisa iliyotumika na Mtume Mtukufu (saw), wafuasi wake na waislam wengi
wacha Mungu. Baadhi ya aya za Kurani ni maalum kwa ajili ya kuleta hali ya
unyenyekevu, rudia hizo mara kwa mara. Kwa mfano unaposoma sura Al-Fatiha,
rudia aya ifuatayo mara kwa mara;
Wewe tu twakuabudu na wewe tu twakuomba msaada (Kurani 1:5).
Hii itaiweka roho katika tubio. Ikiwa itakuwa imepotea katika mawazo
mchanganyiko, roho itarejea kwenye tendo la ibada ikihisi kwamba, kwa kuwa
inadai kumwabudu Mungu pekee, haipaswi kutanga tanga huku na huko.
15. Njia inayofuata ni ya kuwasaidia wale ambao hawawezi kubakia makini kwa
muda mrefu. Kama watoto wadogo ambao hawawezi kuhimili njaa au kukaa na
chakula tumboni kwa muda mrefu, wanahitaji msaada wa mara kwa mara. Njia
inayosaidia kwao ni kuwa makini juu ya mkao mmoja kwa wakati mmoja
wanapokuwa katika Qiyam wanapaswa kuazimia kwamba mawazo yoyote
yasiwasumbue mpaka mwisho wa Qiyam. Wanapoenda kwenye rukuu watie azma
hiyo hiyo mpaka mwisho wa rukuu. Wafanye hivyo hivyo wakati wa kubadili kila
mkao. Hii itawapa nguvu kubwa kuyashinda mawazo yoyote potoshi.
16. Ikiwa utazidiwa nguvu na mawazo mengine ya kidunia, yatakufuatilia , lakini
ikiwa utayakabili mawazo yako na kuazimia kutoyaruhusu yakusumbue,
yatakoma. Kwa hiyo toa upinzani wa nguvu kwa mawazo yoyote kama hayo,
yasimamishe mara moja. Kwa mfano kama wakati wa sala, unamwazia mtoto
wako mgonjwa, acha kumwazia kwa kujiambia kwamba mtoto hatapata nafuu kwa
kumfikiria na wala hali yake haitazidi kuwa mbaya zaidi kama hutamwazia. Kwa
hiyo, azimia kutomwazia. Endelea na zoezi hili kwa kila aina ya wazo mpaka
umekuwa mahiri katika kuyatawala mawazo yote. 17. Unaposali Nafali nyumbani,
tamka maneno kwa sauti ya kutosha kuweza kuyasikia. Kwa kuwa masikio
hayajazibwa, yanaendelea kufanya kazi kwa kiasi fulani. Unapoyasikia maneno,
mawazo yako yataelekea zaidi kwenye kumkumbuka Mungu. Njia hii kwa
kawaida itumike usiku. Ikiwa utayaweka masikio yatumike katika sala wakati wa
mchana, yatavurugwa na aina zote za kelele.
18. Fikra mpya huletwa na miondoko mipya. Miondoko ifanywayo wakati wa sala
ni sehemu ya ibada, na kwa hiyo haisababishi kuleta mawazo ya nje. Lakini ikiwa
mitikisiko mingine itafanywa, itakuondolea umakini katika sala. Mtume Mtukufu
(saw) ameelekeza kwamba mitikisiko isiyo ya lazima isifanywe wakati wa sala. Ni
yakini mitikisiko hutawanya mawazo. Ikiwa mtu kwa bahati mbaya ataligusa koti
lake anaweza kuanza kuwaza kwamba koti lile limekuwa kukuu mno na anahitaji
koti jipya. Kisha anaweza kuzama katika kuwaza jinsi mshahara wake ulivyo
mdogo, au jinsi mshahara wa mwezi uliopita ulivyochelewa, au kama alichelewa
kuupata kwa sababu ya uzembe wa ofisa fulani, ataanza kuwaza jinsi alivyo mbaya
ofisa yule.
Wakati bado yungali amezama katika mawazo kama haya atamsikia Imam
anasema Assalaamo Alaikum wa Rahmatullah na atamaliza sala yake wakati akiwa
hajafanya ibada yoyote ya kweli. Mtume Mtukufu (saw) amekataza mitikisiko ya
aina yoyote nyingine wakati wa sala ambayo sio miondoko iliyowekwa kama
sehemu ya sala. Hata kama kuna mchanga mahala pa kusujudia, haipasi uondolewe
wakati mtu anasali isipokuwa kama inaleta maumivu makali mno, na hapo
uondolewe mara moja tu. Kwa kifupi aina zote za nyendo ambazo hazihusiani na
sala inabidi ziepukwe.
19. Fanya Qiyam, Ruk’u, na Sajda kwa umakini. Unapokuwa umesimama kwa
Qiyam usiweke uzito wako wote kwenye mguu mmoja ukauacha mwingine
ukilegalega. Unapolegalega au kuzembea wewe mwenyewe, adui anaweza
kukuzidi nguvu. Ulegevu wa mwili hupelekea ulegevu wa kiroho.
20. Njia inayofuata inahusiana na kuitiisha nafsi. Inatumika kupita kiasi na baadhi
ya masufi kama Shibli. Sipendi kufanya mambo kwa kupita kiasi. Hata hivyo
nitataja njia hii. Ikitumika kwa kiasi, inaweza kuwa na manufaa. Hadhrat Junaid
wa Baghdad alikuwa mtawa mwenye heshima kubwa. Mmoja wa wafuasi wake
alikuwa ni Shibli, mtu mkweli wa moyo na mcha Mungu. Shibli aliwahi kuwa
Gavana wa Mkoa. Siku moja alipokuwa anahudhuria baraza la Mfalme, Chifu
mmoja wa kabila fulani alipewa zawadi ya joho la Mfalme kwa kutambua huduma
yake. Yule Chifu alipatwa na ugonjwa wa mafua. Ilitokea kwamba wakati ule ule
alipokuwa amesimama mbele ya Mfalme, pua yake ilianza kuvuja. Mfalme
alikuwa hana kitambaa cha mkononi. Alipodhani Mfalme hamwangalii yule chifu
alipangusa pua yake na ile nguo ya Kifalme. Mfalme alimuona na akakasirika
sana, alihisi kwamba vazi la Kifalme limedhalilishwa. Shibli ambaye alikuwa na
ucha Mungu katika moyo wake alishtushwa mno na tukio hili kiasi ya kwamba
akapoteza fahamu. Alipopata fahamu alijiuzulu Ugavana. Alipoulizwa kwanini,
alimjibu Mfalme kwamba ulimpa nguo Chifu na ukakasirika sana alipoitumia
vibaya. Mimi nimepewa neema nyingi mno na Mungu. Ghadhabu yake itakuwa
kubwa kiasi gani ikiwa simshukuru.
Halafu akaenda kwa Hadhrat Junaid na akamwomba amkubali kuwa mwanafunzi
wake. Akasema, siwezi kukukubali uwe mwanafunzi, ulikuwa Gavana na katika
nafasi hiyo ulikuwa mkatili kwa watu wengi mno. Shibli aliomba, je hakuna kitu
ninachoweza kufanya? Junaid alimshauri kwenda katika kila nyumba kwenye eneo
lake kuomba radhi na kutoa fidia kwa makosa aliyokuwa ametenda. Alifanya
kama alivyoshauriwa.
Simulizi za maisha ya Shibli zinarikodi kwamba kila alipoona ulegevu au
mwingiliano wa mawazo wakati anasali Nafali, alikuwa akijicharaza kwa fimbo,
mpaka fimbo inakatika. Halafu anaanza tena. Mwanzoni alikuwa anakaa na fungu
la viboko. Alichokifanya ilikuwa ni kupitiliza kiasi na naamini Islam hairuhusu
kufanya mambo kwa kupitiliza kiasi namna hii. Hata hivyo kwa kuwa jambo
lenyewe lahusika na nafsi yake tu siwezi kumlaumu.
Kuna njia ya kuitiisha nafsi ambayo sio ya kupitiliza kiasi. Kila mawazo yako
yanapopepesuka, urudie kipande ulichokuwa unasoma kabla mawazo hayajaelekea
pembeni. Halafu endelea kukisoma kipande kile, nafsi itatambua kwamba umekaza
nia katika ibada yako kwa Mungu. Utambuzi huu utaondosha mikanganyiko
mingine katika fikra na utapata amani na umakini.
21. Kuna mbinu nyingine bora sana na yenye manufaa. Sifa ya waaminio wa kweli
ni kwamba;
“hujiepusha na yote ambayo ni uupuzi” (23:4). Wale ambao wana tabia ya
kuyaendekeza mawazo ya kipuuzi na yasiyo na maana watavamiwa na mawazo
kama hayo hayo wakati wa sala.
Iwapo wajifundishe kutofikiria mawazo kama hayo kabisa, wataondokana na
kutangatanga kwa mawazo wakati wa sala vile vile. Kuna wengi ambao hujiingiza
katika kupiga soga kama vile kungwi wa soga, Sheikh Chilli wa Iran. Mawazo
kama hayo hayawatendei heri yoyote. Fahamu haipaswi kuruhusiwa kujiingiza
katika fikra za kubuni buni na za juu juu. Bila shaka hakuna dhara katika kufikiria
mambo yenye manufaa na yenye maana. Yaliyozidi kabisa katika upuuzi ni
mawazo juu ya vitu vilivyopita ambavyo mtu hawezi kuvibadilisha. Kuendelea
kuwazia vitu kama hivyo kwa hakika ni kilele cha ujinga.
Itakuwa ni jambo la dhahiri kwamba jitihada ya mwanadamu huelekezwa kwenye
chochote ambacho mawazo yake yamekielekea, kama mtu ataelekeza fikra zake
kwenyemawazo yasiyo na maana, basi atapoteza uwezo wake wa kuelekeza fikra
zake kwenye mawazo yenye manufaa.
Jitahidi kuyadhibiti mawazo yasiyo na maana, na kugeuzia fikra kwenye mawazo
yenye kuleta faida, kama utafanya hivyo, fahamu yako itajenga tabia ya kutafakari
juu ya mambo yenye manufaa. Kufikiria mambo mengine wakati unafanya jambo
jingine ni upuuzi, isipokuwa katika hali fulani fulani. Fahamu ya mtu aliyeizoeza
kujielekeza kwenye heri haitafikiria mambo mengine wakati wa sala.
22. Njia inayofuata inafaa sana. Huupeleka ucha Mungu kwenye kilele chake.
Mtume Mtukufu (saw) aliulizwa siku moja, Ihsani (wema) ni kitu gani? Alijibu,
sali mbele ya Mungu kama vile unamuona, lakini kwa kiwango cha chini kabisa
angalau usali kwa kufikiria kwamba yeye Anakuona.
Unaposimama kwa ajili ya sala, fikiria kwamba unasimama mbele ya Mungu na
kwamba unaweza kumuona, sio katika mwili wake bali katika utukufu wake na
adhama yake. Hii huleta kwenye fahamu ya mtu hofu juu ya ukubwa na uwezo wa
Mungu. Fahamu inashika hadhari isitende jambo lolote la utovu wa adabu katika
wakati ule, kama huwezi kuvuta taswira ya Mungu angalau kwa akali amini
kwamba Anakuangalia. Anaona kila kitu unachokifanya. Fikiria kwa bidii
unaposema Al-hamdulillah (Sifa zote zamhusu Allah), je hali ya moyo wako
inakiri usemi huo? Au moyo umezama katika mawazo mengine kabisa? Kama
fahamu imezama katika uitikio tofauti, jirudi mwenyewe na ufanye moyo wako
uungane na kile kinachotamkwa na ulimi.
Mtume Mtukufu (saw) anasema kwamba mtumishi yeyote wa Mungu Ambaye
anasali rak’a mbili kwa unyenyekevu kiasi hiki kwamba hajiingizi katika
mawasiliano yoyote na nafsi yake, anasamehewa madhambi yake yote. Fikiria basi
daraja la yule ambaye siku zote anakuwepo katika hali kama hiyo. Kwa hiyo
kumakinika kikamilifu katika sala sio jambo la kawaida.
Njia nilizowaelezeni, kwa fadhili za Mungu, hazipaswi kuchukuliwa kiwepesi.
Zifanyieni kazi kwa uaminifu wa moyo. Mkifanya hivyo, mtabarikiwa sana.
Wakati wa kumalizia sala, tunatamka maamkizi yaliyozoeleka ya kiislam
Assalamu Alaikum wa Rahmatullah. Hili ni ashirio la ajabu kwa ajili ya kuhifadhi
umakini. Unasema Assalaamu Alaikum unapokuja kutoka mahala fulani. Mwislam
anaposema Assalamu Alaikum wa Rahmatullah wakati wa kumaliza sala yake,
anaarifu kwamba alikuwa amekwenda kubainisha utii wake na utumishi wake kwa
Mungu na sasa amerejea. Anasema kwamba ameleta ujumbe wa amani na rehema
kwa Waislam wenzake. Kwa kuwa wakati wote alikuwapo kimwili mahali pale,
maana pekee yaweza kuwa kwamba roho yake ilikuwa katika sujda mbele ya
Mungu, alikuwa ameshughulika mno katika ibada kiasi maungano yake na dunia
yalikuwa yamekatwa na hakuwepo. KusemaAssalaamo Alaikum wakati wa
kumaliza sala kunaashiria kwamba ni muhimu kwa Muislam kuwa macho wakati
wa sala, kuichunga sala yake, kwa sababu umo, kwa wakati ule, ndani ya baraza ya
Mungu Mwenye Enzi, ambaye Anasema juu ya Waislam kwamba:
“Nao huzihifadhi sala zao” (6:93) Shetani anataka kuziharibu sala zao lakini
Waislam walio makini huzilinda sala zao dhidi ya shambulio lake.
Kwa hiyo kila mmoja anapaswa kuzilinda sala zake. Unaposali, uweke akilini
kwamba umeingia alipo Mungu. Unaporejea yakupasa ulete habari njema kwa
wale walio kulia na wale walio kushoto kwamba umeleta amani na baraka kwa ajili
yao.
Lakini kama mtu hakuwahi kwenda kwa Mungu, na alikuwa wakati wote
amezingirwa na fumbato la mawazo yake mwenyewe, atakuwa anasema uwongo
mkubwa, wakati anasema Assalamu Alaikum warahmatullah. Anajaribu
kuwaambia watu kwamba amerejea kutoka kwa Mungu, wakati hakuwahi kwenda
Kwake.
Fanya kila jitihada kuzihifadhi sala. Mpe upinzani mkubwa shetani kwa kuwa
anajaribu kukuweka mbali na Mungu. Kumbuka kuwa hata kama sala yako yote
imetumika katika kupambana na humpi ushindi shetani, Allah Atakuhesabu
ulihudhuria mbele yake. Lakini ukijiachia, Atakuacha uende. Endelea na
mapambano yako, hatimae utafanikiwa.
DHIKRI YA KUONGEA KATIKA HADHARA YA WATU:
Mpaka hapa nimezitaja aina tatu za Dhikri; sala, usomaji wa Kurani Tukufu na
Kumkumbuka Allah kwingineko nje ya sala kunakofanywa na mtu peke yake.
Aina moja ya Dhikri inafanywa hadharani na bado inabakia kuwa ni Dhikri.
Inafanyika kwa njia mbili:-
1. Tunapokutana na Waislam wenzetu, yatupasa kuzungumzia mambo yahusuyo
Nguvu ya Mungu, Utukufu Wake na kuzikumbuka baraka Zake, badala ya
kujiingiza katika maongezi ya kipuuzi na yasiyo na manufaa. Hii hutakasa moyo
na picha njema yenye baraka hujengwa katika hisia za ndani kabisa.
Siku moja Mtume Mtukufu (saw) alikwenda nyumbani kwake. Aliona watu
wakiwa wameshughulika katika kusali msikitini, wengine walikuwa wamekaa
kwenye makundi wakiongelea mambo ya imani. Alijiunga na kundi la pili na
kusema kile wanachokifanya hawa ni bora zaidi. Hii yaonyesha kwamba kuongea
hadharani wakati fulani ni bora zaidi kuliko kumkumbuka Allah kipekee pekee.
Kuna nyakati ambapo kumkumbuka kipekee pekee ni muhimu. Lakini wakati watu
wengi wapo inakuwa na manufaa zaidi kuongea hadharani na kubadilishana uzoefu
wakiroho na kila mmoja kujitenga kipekee katika hali kama hizi kwaweza kuleta
hali ya kujikweza. Kueleza maana za Kurani Tukufu kumeunganishwa katika aina
hii ya Dhikri. Hali kadhalika, kuwaalika Waislam wengine katika mambo mema
kunahesabiwa kama Dhikri.
2.Halafu kuna Dhikri ifanywayo katika mikutano na wapinzani. Dini zote
nyinginezo, ukiacha Islam, zinalo kosa la kupunguza au kuongeza wakati wa
kuelezea sifa za Mungu. Kwa hiyo kuelezea sifa sahihi za Mungu katika mikutano
yao ni aina ya Dhikri. Allah Anasema;
Ewe uliyevaa, simama na uonye. Na Mola Wako umtukuze. (74:2-4)
Kuwaonya watu na kuelezea ukubwa wa Mungu mbele yao kumejumuishwa hapa
kama Takbiir, ambayo ni sehemu ya Dhikri.
Kwa kumalizia, kuelezea sifa za Allah kwa watu wengine wa dini zingine ni
Dhikri. Sura ya 87 ya Kurani Tukufu (Sura Al-Ala) pia inabainisha jambo hili.
Neno Dhikri limetumika mahsusi kwa ajili ya shughuli kama hizi katika sura Al-
A’alaa, ambayo inasema;
Basi ukumbushe maana kukumbusha kunafaa (87:10).
FAIDA ZA DHIKRI
Sasa nitageukia faida za Dhikri.
1. Faida kubwa zaidi ya Dhikri ni kuwa inapelekea kupata ridhaa ya Mungu, sio
kama ilivyo kwa tendo jingine jema lolote, bali kwa njia ya kipekee.
Malipo ya tendo hulingana na umuhimu wake. Mungu Mwenye Enzi Anasema juu
ya Dhikri kwamba ndio jambo kubwa kuliko yote. Katika mahala pengine kwenye
Kurani Tukufu, Mungu Anasema:
Mwenyezi Mungu Amewaahidi waaminio wanaume na waaminio wanawake
Bustani zipitazo mito ndani yao kukaa humo, na makao mazuri katika Bustani
zenye kudumu, na radhi ya Mwenyezi Mungu ndiyo kubwa mno. Huo ndio ufaulu
mkuu (9:72).
Zawadi kubwa kuliko zote ni radhi ya Allah. Zawadi kubwa kuliko zote yaweza tu
kutolewa kwa kitendo kikubwa kuliko vyote, ambacho ni Dhikri. Kwa hiyo malipo
ya Dhikri ni radhi ya Allah. Katika aya hiyo hapo juu Mungu Mwenye Enzi
Anatofautisha radhi ya Allah na malipo mengine. Hii yaonyesha kuwa hiki ni kitu
tofauti na ni jambo kubwa kuliko yote.
Kwa hakika, kwa Mwaminio wa kweli hapawezi kuwako malipo ya juu zaidi
kuliko kupata radhi ya Mola Wake. Allah Ameashiria wazi wazi kwamba ikiwa
utafanya Dhikr-e-llahi, tendo kubwa kuliko yote, utapata radhi ya Allah, malipo
makubwa kuliko yote.
2. Kumkumbuka Allah kwaweza kuleta faraja na amani ya moyo. Allah Anasema;
Wale walioamini na ikatulia mioyo yao kwa kumkumbuka Allah. Sikilizeni kwa
kumkumbuka Allah mioyo hutulia. (13:29).
Mioyo hupata farijiko katika Dhikri kwa nini? Kwa sababu wasiwasi
husababishwa na woga wa balaa linalotarajiwa kuja. Kama mtu anaamini kuna
dawa kwa kila ugonjwa, hataogopa. Mtu anapomkumbuka Allah na anatambua
kwamba kwa uwezo wake usio kikomo, anaweza kuondoa aina zote za vikwazo,
moyo wake unamliwaza kwa kumwambia; kwa nini nijali? Ninaye Mungu
Mwenye uwezo wote, bila shaka atayaondosha mashaka yangu yote. Mawazo
kama haya huleta amani ya moyo.
3. Allah huwa rafiki wa yule anayetoa muda wake katika kumkumbuka. Anampatia
nafasi katika Enzi yake hata wakati bado yungali katika dunia hii. Kama
Anavyosema:-
Basi Mnikumbuke, (Nami) Nitawakumbukeni, Na Nishukuruni wala Msinikufuru
(2:153).
Kama ambavyo wafalme wa kidunia huwaalika watu kwenye enzi yao ya kifalme
wanaporidhika nao, ndivyo kama hivyo hufanya Allah.
4. Kumkumbuka Allah humlinda mtu na madhambi. Mungu Mwenye Enzi
Anasema katika Kurani Tukufu;
Soma uliyofunuliwa katika Kitabu na usimamishe sala. Bila shaka sala huzuia
mambo ya aibu na maovu, na kwa yakini kumbuko la Mwenyezi Mungu ni (jambo)
kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu Anajua mnayoyatenda. [29:46].
Sala inakuokoa na mambo ya aibu na uovu. Kama nilivyosema hapo awali
kwamba Sala ni aina ya Dhikr e Ilahi (kumkumbuka Allah). Hivyo kumkumbuka
Allah kunazuia madhambi. Dhikri ni nzito. Inapoanguka juu ya kichwa cha
Shetani, basi Shetani atapondwa na kufa na kutokushawishi tena kwenye maovu.
5. kumkumbuka Allah kunaimarisha mioyo na kukuza ari ya kupambana na
maovu, kama vile Allah Asemavyo:
Enyi mlioamini, mkutanapo na jeshi, basi jiimarisheni, na mumkumbuke Allah kwa
wingi ili mpate kufaulu. [8:46].
Kulingana na aya hii, njia ya kukabiliana na adui mwenye nguvu ni kumkumbuka
sana Allah.
6. Mtu amkumukaye Allah atakuwa ni mwenye kufanikiwa katika mambo yake
yote, kwa sharti kwamba anamkumbuka Allah kwa uaminifu wa hali ya juu kabisa.
Hii yathibitishwa na aya niliyoisoma hapo awali. Allah Anasema:
Na mumkumbuke sana Allah ili mpate kufaulu. [8:46].
7. Mtume s.a.w. alisema: Siku ya Kiama watu wa aina saba watapewa kivuli cha
Huruma ya Allah. Miongoni mwao ni watu wenye kumkumbuka Allah. Mtume
s.a.w. anaongeza kwamba itakuwa ni siku ya majonzi sana. Hakuna yeyote
aliyeona mfano wake. Adhabu ya Allah itakuwa kubwa sana siku hiyo kwa sababu
wadhalimu wote watahudhurishwa mbele Yake. Jua litakuwa linawaka kwa karibu
sana. Kila atakayepewa kivuli cha Rehema ya Allah siku hiyo atakuwa ni mwenye
bahati kweli kweli.
8. Mwenyezi Mungu Hukubali Dua za wale wamkumbukao. Dua zimezotajwa
ndani ya Kurani Tukufu zimeanza na Dhikri, yaani Tasbiih na Tahmiid. Dua ya
kwanza imo ndani ya Sura ya Al Faatiha. Inaanza na aya zenye Dhikri tu.
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwingi wa Ukarimu. Sifa zote njema zin
amhusu Allah, Mola wa walimwengu. Mwingi wa Rehema, Mwingi wa Ukarimu.
Mmiliki wa Siku ya malipo. (1:1- 4).
Halafu inakuja sehemu ambayo sehemu ni ya Allah na sehemu ni ya mwanadamu:
Wewe tu twakuabudu na Wewe tu twakuomba msaada (1:5).
Mwishoni inakuja dua:
Utuongoze kwenye njia iliyonyooka, njia ya wale Uliowaneemesha, sio ya wale
Uliowakasirikia, wala ya wale waliopotea. (1:6-7).
Sura ya Al Faatiha ni dua; lakini Mwenyezi Mungu Anaianza na Dhikri na
Kuimalizia na dua. Twaliona jambo hili hili duniani. Ajapo omba omba huanza
kumsifu bwana mwenye nyumba halafu hutoa maombi yake.
Halikadhalika mtu aendapo kumuomba Allah ni lazima kwanza ayakiri mamlaka
ya Mwenyezi Mungu na kuukiri udhaifu wake binafsi. Nabii Yunus a.s. alifanya
hivyo hivyo alipolia ndani ya kina cha kiza akisema:
Hakuna wa kuabudiwa ila Wewe, Utakatifu ni Wako. Hakiak mimi nilikuwa
miongoni mwa wadhalimu. (21:88).
Kwanza aliutaja utukufu wa Mungu, halafu akaieleza hali aliyojikuta nayo. Zaidi
ya hapo Mtume s.a.w. anainasibisha kauli ifuatayo kwa Allah: “Yule aendeleaye
kunikumbuka hupata zaidi toka Kwangu kuliko yule aniombaye tu.” Hadithi
haimaanishi kwamba usimuombe Mwenyezi Mungu. Sura Al Faatiha, iliyo mama
wa Kitabu, imechanganya Dhikri na dua. Kurani Tukufu na Hadithi, zote
zatufundisha dua nyingi. Hadithi hii yamaanisha hivi tu kwamba yule mtu ambaye
hafanyi Dhikri, bali hupeleka tu maombi na mahitajio hupata kidogo ukilinganisha
na yule adumuye kuomba kile anachohitaji na kutafuta wasaa wa kufanya Dhikri.
9. Dhikri ni njia ya kupata msamaha wa dhmbi toka kwa Allah. Mtume s.a.w.
anasema: yule mtu afanyaye Takbiir, tahmiid na Tasbiih husamehewa madhambi
yake yote, hata kama madhambi yake hayahesabiki kama povu la bahari.
10. Dhikri inaongeza busara. Yule amkumbukaye Allah hugundua ukweli na
nukta za hekima ambazo humstaajabisha hata yeye mwenyewe. Mwenyezi Mungu
Anasema:
Katika uumbaji wa mbingu na ardhi na mfuatano wa usiku na mchana, ziko ishara
kwa wenye akili. Ambao humkumbuka Allah wakiwa wima na wakiwa wamekaa na
wakiwa wamelala kibavu na huutafakari uumbaji wa mbingu na ardhi: Mola
Wetu! Hukuviumba hivi bure tu; Utukufu ni Wako, basi Utuepushe na adhabu ya
moto. (3:191-192).
Kumkumbuka Allah kunaongoza kwenye utawa. Kuna Hadithi fulani ambamo
Mtume s.a.w. anainasibisha kauli ifuatayo kwa Mwenyezi Mungu:
Wakati mja wangu anikumbukapo moyoni, Nami Humkumbuka faraghani na
anikumbukapo hadharani Nami Humkumbuka hadharani..
Hadithi hii yaonyesha kwamba kama, kwa mfano, mtu anasema: “Wewe u
Mtakatifu ewe Allah” Mwenyezi Mungu hurjesha hii kwa kumbariki kwamba:
wewe pia uwe mtakatifu na uliyetakasika. Allah Asemapo hayo, basi utakaso ni
lazima upatikane. Halikadhalika mtu alitukuzapo jina la Allah miongoni mwa watu
wengine, Mungu Naye Hulinyanyua jina lake zuri kwa watu, dunia inamkubali
kuwa ni mtu mwema.
Ni asili ya mwanadamu kwamba unapojihusisha sana na watu fulani, basi penzi
lako kwao huongezeka. Watu huanza hata kuvipenda vijiji au miji waishio. Mtu
amkumbukapo Allah usiku na mchana na kulitaja Jina Lake, penzi lake kwa Allah
litaanza kuongezeka.
Hizi, kwa muhtasari, ndio faida za kumkumbuka Allah. Ni maombi yangu kwamba
Allah Azifanye ziwe zenye faida kwangu na kwenu nyote. Amin.