Upload
others
View
135
Download
2
Embed Size (px)
Citation preview
1
TANGAZO LA SERIKALI Na…………la Tarehe………….
SHERIA YA SERIKALI ZA MITAA (MAMLAKA ZA MIJI)
SURA 288
SHERIA NDOGO
Zimetungwa Chini ya Kifungu cha 89(1) Na 62(1) na (2)
SHERIA NDOGO ZA (UDHIBITI NA USIMAMIZI WA MIFUGO ZA
HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA, 2018
Jina na Mwanzo
wa kuanza
kutumika
1 Sheria ndogo hizi zitajulikana kama Sheria Ndogo za (Udhibiti
na Usimamizi) wa Mifugo za Halmashauri ya Manispaa ya Ilala
za Mwaka 2018 na zitaanza kutumika mara baada ya kutangazwa
katika Gazeti la Serikali.
Matumizi 2 Sheria Ndogo hizi zitatumika eneo lote lililopo chini ya Mamlaka
ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Tafsiri 3 Katika Sheria Ndogo hizi isipokuwa pale itakapoelekezwa
vinginevyo:-
“Afisa Mwidhiniwa” maana yake ni afisa mifugo wa Manispaa,
afisa kilimo pamoja na afisa yeyote wa Halmashauri
atakayeteuliwa kusimamia utekelezaji wa Sheria Ndogo hizi.
“Afya” maana yake ni hali timilifu ya kimwili na kiakili ya
mnyama.
“Halmashauri” maana yake ni Halmashauri ya Manispaa ya
Ilala.
“Kaya” maana yake ni familia ya watu akiwemo baba, mama,
mtoto au watoto na mtu mwingine yeyote anayeishi na familia
hiyo, au watu wanaokaa katika nyumba moja na kuishi kama
familia au mtu yeyote anayeishi peke yake katika chumba au
nyumba.
“Kero au Chukizo” maana yake ni kitu chochote ambacho kipo
katika hali yoyote iwe kinatumika, kimewekwa, kimejengwa au
ni kichafu kiasi cha kusababisha
(a) Hatari kwa viumbe na maisha ya binadamu,
(b) Harufu mbaya ya kuudhi.
2
(c) Kuzaliana kwa wadudu na wanyama hatari kama vile
inzi, mende, sisimizi, panya, nyoka, nyuki, kunguni au
viumbe wengine hatari.
(d) Magonjwa kwa binadamu, kuhifadhi mbu, inzi, panya na
viumbe wenye madhara
“Kibali” maana yake ni ni hati iliyotolewa chini ya sheria ndogo
hizi.
“Mifugo” maana yake ni mifugo yoyote na wanyama wafugwao
na binadamu.
“Mkurugenzi” maana yaje ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala au Afisa yeyote wa umma atakayeteuliwa
kutekeleza majukumu ya Mkurugenzi.
“Ufugaji wa ndani” maana yake ni ufugaji na ulishaji wa
mifugo ndani ya jengo lililoruhusiwa (zero grazing).
“Wakala” maana yake ni mtu binafsi au kikundi cha watu,
kampuni, taasisi au shirika aliyeteuliwa kusimamia utekelezaji
wa Sheria Ndogo hizi.
“Waziri” maana yake ni Waziri mwenye dhamana ya Serikali za
Mitaa.
“Zizi” maana yake ni jengo au eneo lililozungushiwa uzio
ambalo linatumika kuhifadhi mifugo iliyokamatwa ambalo
litatunzwa na kusimamiwa na Halmashauri
Wajibu wa
Halmashauri
4 Ni wajibu wa kila Halmashauri:
(a) Kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya ufugaji
(b) Kuelekeza idadi ya mifugo ambayo kila mfugaji
anaruhusiwa kufuga.
(c) Kujenga majosho ya mifugo kwa kushirikiana na
wananchi.
(d) Kutoa elimu ya ufugaji bora kwa jamii ili kuongeza tija.
(e) Kufanya sensa ya mifugo, kuweka alama na kutoa kadi
za mifugo
(f) Kutoa chanjo kwa kushirikiana na wafugaji ili kudhibiti
magonjwa ya mifugo.
(g) Kudhibiti uzururaji holela wa mifugo na wanyama katika
Halmashauri kwa mujibu wa Sheria.
Wajibu wa
mfugaji
Itakuwa wajibu wa kila mfugaji chini ya Sheria Ndogo hizi
kuhakikisha kwamba:-
3
(a) Anaogesha mifugo yake ili kudhibiti magonjwa ya
wanyama kama atakavyoagizwa na Halmashauri.
(b) Anapeleka mifugo yake katika vituo vya chanjo kama
itakavyoamriwa na Halmashauri na atalipia chanjo hiyo
kama atatakiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa viwango
vitakavyoainishwa na Sheria ndogo za Ada na Ushuru za
Halmashauri.
(c) Kuhakikisha Mifugo yake inawekwa alama maalumu
(Branding, ear tags) zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria
ya Mifugo
(d) Anafuga idadi ya mifugo katika jengo lililoidhinishwa
kulingana na maelekezo ya Sheria Ndogo hizi.
(e) Anakuwa na kadi ya mifugo itakayoonesha idadi na aina
ya mifugo aliyonayo.
(f) Anaipatia mifugo yake malisho na maji ya kutosha kwa
kuzingatia kanuni bora za ufugaji.
(g) Anakuwa na kibali cha kusafirisha mifugo na mazao
yake na kuhakikisha Sheria na Kanuni za usafirishaji
mifugo zinazingatiwa.
(h) Anafuga kwa kuzingatia mipango ya matumizi bora ya
ardhi.
(i) Anahudhuria mafunzo ya ufugaji kama atakavyo hitajiwa
na Halmashauri.
(j) Anauza mifugo yake katika masoko na minada
iliyoidhinishwa tu.
Kibali cha kufuga
mifugo
6 1 Mtu yeyote atakayetaka kufuga mifugo atalazimika kupata kibali
cha kufuga kutoka kwa Halmashauri kama ilivyoainishwa katika
jedwali la kwanza la Sheria ndogo hizi.
2 Kibali kilichotajwa katika kifungu cha 6 (1) cha Sheria Ndogo
hizi hakitakuwa na gharama na hakitozidi miaka mitano
kulingana na aina ya mifugo kuanzia tarehe kilipotolewa.
3 Kaya itaruhusiwa kufuga mifugo ndani ya eneo la Halmashauri
kama ilivyoainishwa katika jedwali la pili la Sheria Ndogo hizi.
4
Masharti kwa
Mfugaji
7 Ni marufuku kwa mfugaji au mtu yeyote
1 Kuchunga, kulisha,au kunywesha maji mifugo katika maeneo
ambayo hayakutengwa kwa shughuli hiyo
2 Kusafirisha mifugo kwa kuiswaga barabarani
3 Kusafirisha au kuhamisha mifugo kutoka eneo moja hadi lingine
bila kibali kutoka kwa Halmashauri
4 Kuingiza mifugo katika eneo la Halmashauri bila kibali
5 Kuuza au kununua mifugo katika maeneo ambayo siyo mnada,
masoko au magulio ya mifugo yaliyoaidhinishwa na
Halmashauri.
6 Kufuga mifugo zaidi ya idadi iliyoainishwa katika Sheria
Ndogo hizi,
7 Kununua, kuuza au kufanya Biashara ya kubadilishana aina
yoyote ya mifugo katika eneo lolote la Halmashauri isipokuwa
kwenye minada au magulio yaliyotengwa kwa shughuli hiyo na
Halmashauri.
Kibali cha
kusafirisha
mifugo
8 1 Itakuwa ni wajibu kwa mtu yeyote anayetaka kusafirisha mifugo
na mazao yake kutoka au kuingia katika eneo la halmashauri
kuwa na kibali maalumu kitakachoruhusu kusafirisha mifugo
hiyo kama ilivyoainishwa katika Sheria Ndogo hizi na Sheria
zilizotungwa na Bunge
2 Kibali cha kusafirisha mifugo au mazao ya mifugo au vyote kwa
pamoja nje na ndani ya Halmashauri kitatolewa na Halmashauri
baada ya kujiridhisha kuwa mifugo hiyo ina afya nzuri,
imeogeshwa na kupatiwa chanjo kabla ya kusafirishwa.
3 Halmashauri itatoa kibali cha usafirishaji mifugo kwa kuweka
utaratibu ikiwa ni pamoja na:
(a) Mfugaji kutoa uthibitisho wa kumiliki mifugo au
mnyama huyo kutoka kwa Mtendaji wa Mtaa.
(b) Kukagua vibali vyote vya usafirishaji mifugo.
4 Afisa Mwidhiniwa atakuwa na uwezo wa kukamata na kutoza
faini na adhabu kwa mifugo yoyote inayosafirishwa kinyume na
Sheria Ndogo hizi au Sheria yeyote iliyotungwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Taratibu za
ufugaji
9 Wafugaji wote watatakiwa kuzingatia masharti ya kufuga kama
yalivyo katika Sheria Ndogo hizi au Sheria yoyote iliyotungwa
na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
5
Kudhibiti mifugo
inayozurura
hovyo
10 1 Halmashauri itakamata mifugo au mfugo wowote
Utakaoonekana unazurura hovyo katika eneo la Halmashauri na
utahifadhiwa katika zizi.
2 Mfugo wowote utakaokamatwa utalipiwa faini ya shilingi elfu
kumi (10,000/=) kwa kila siku na gharama nyingine
zitakazojitokeza kama itakavyoamriwa na Halmashauri na baada
ya kulipia hizo gharama atarudishiwa mifugo yake.
3 Endapo mifugo iliyokamatwa haitachukuliwa na mmiliki ndani
ya kipindi cha siku saba (7) tangu kukamatwa kwa mifugo hiyo,
Halmashauri itakuwa na haki ya kuuza kwa mnada mfugo au
mifugo hiyo baada ya kupata idhini ya Mahakama.
4 Halmashauri itatoa tangazo la mnada kwa njia ya vyombo vya
habari au kadri atakavyoona inafaa
5 Baada ya mauzo, Halmashauri itakata fedha za faini, gharama za
mnada na gharama za ulinzi na fedha zitakazobaki atapewa
mwenye mifugo na kama hataonekana ndani ya siku kumi na nne
fedha hizo zitaingizwa katika vyanzo vya mapato vya
Halmashauri.
6 Endapo mwenye mifugo hiyo atakuwa na sababu za msingi za
kutofika kwake katika muda uliopangwa na Halmashauri,
Halmashauri itarudisha fedha zake.
7 Endapo kutatokea kufa kwa mifugo au mfugo kutokana na
sababu yoyote ile, Halmashauri haitawajibika na ulipaji wa
gharama zozote.
Ukaguzi wa
mifugo na bidhaa
za mifugo
11 1 Afisa mwidhiniwa atakuwa na uwezo wa kukataa aina yoyote ya
mifugo au bidhaa kuingia au kuuzwa ndani ya eneo la
Halmashauri iwapo mifugo hiyo au bidhaa hizo zinaweza
kuhatarisha afya au usalama wa mifugo mingine au watumiaji
wengine.
2 Itakuwa halali kwa Afisa Mwidhiniwa wa Halmashauri
atakayeteuliwa kusimamia utekelezaji wa Sheria Ndogo hizi
kuingia katika nyumba au jengo lolote wakati wowote kwa
madhumuni ya kukagua kwa kadri atakavyoona inafaa.
3 Mtu yeyote atakaye wazuia maafisa waidhiniwa kutekeleza
wajibu wao chini ya Sheria Ndogo hizi au Sheria nyingine
yoyote iliyotungwa na Bunge atakuwa ametenda kosa.
6
Taratibu ya
biashara ya
mifugo na mazao
yake
12 1 Mfanyabiashara wa mifugo na mazao ya mifugo anatakiwa kuwa
na leseni ya mifugo, utambulisho na vibali vilivyotolewa na
Mamlaka nyingine za Serikali kabla ya kuanza biashara ya kuuza
na kununua mifugo na mazao ya mifugo na atatakiwa
kuwasilisha vibali vyake kwa Halmashauri kwa ajili ya uhakiki.
2 Mifugo yoyote itakayosafirishwa kutoka mnadani itapelekwa
machinjioni na itatakiwa kuwa na kibali (movement permit) na
inatakiwa kusafirishwa katika vyombo vya usafiri
vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria.
3 Mifugo yote inayopelekwa mnadani itatakiwa iwe na barua ya
utambulisho kutoka kwenye mamlaka halali inakotoka mifugo
hiyo.
4 Mifugo yote itauzwa na kununuliwa katika minada na masoko
yanayotambulika kwa mujibu wa Sheria.
5
6.
Mifugo itakayokamatwa ikisafirishwa bila kibali au kuuzwa
sehemu isiyosajiliwa kihalali na mamlaka zinazohusika, mhusika
atalazimika kulipa faini ya shilingi elfu 10,000 kwa kila mfugo
au mnyama.
Minada yote ya Mifugo au Magulio ya Mifugo itafanyika kwa
kibali maalumu cha Halmashauri na kwenye maeneo
yaliyoruhusiwa.
Udhibiti wa
bucha na maduka
ya nyama
13 1 Itakuwa ni wajibu wa kila mfanyabiashara ya nyama au mmiliki
wa bucha au duka la kuuza nyama kuhakikisha kwamba:-
(a) Jengo lake la biashara ya nyama limejengwa kwa mujibu
wa Sheria na lina mwanga wa kutosha, umeme, maji safi
na salama, visu, meza, mzani wa kawaida /mzani wa
kielektroniki, na misumeno maalumu ya kukatia nyama.
(b) Kuna kabati la vioo la kuzuia inzi na wadudu wengine
wataambao na jokofu la kuhifadhia nyama.
(c) Kuna pipa la kuhifadhia taka ngumu na nyepesi
(d) Nyama iwe imekaguliwa na mkaguzi aliyeidhinishwa na
kuwekwa muhuri na inauzwa ndani ya jengo
lililothibitishwa na Sheria za mamlaka husika na sio nje
ama mahali popote pa wazi.
(e) Muuzaji anavaa sare nyeupe muda wote ambazo ni
gunboot, koti na kofia
(f) Muuzaji anapima afya yake na kuwa na cheti na
kuhakikisha anapima afya yake kila baada ya miezi
mitatu (3)
(g) Mmiliki au muuzaji wa nyama anatoa ushirikiano wa
kutosha kwa wakaguzi mara atakapotakiwa kufanya
7
hivyo wakati wowote wa ukaguzi.
2 Mmiliki atatakiwa kuwa na leseni halali, kutambuliwa na
kusajiliwa na Mamlaka nyingine za Serikali kwa mujibu wa
Sheria zilizotungwa na Bunge.
3 Kuhakikisha kuwa biashara ya nyama inafanyika katika bucha na
maduka maalumu (super market) na sio vinginevyo.
Magari ya
Kubeba Nyama
14. 1 Nyama zote zinazotoka machinjioni zitabebwa kwa gari
maalumu (meat van) ambazo zitakuwa zimekaguliwa,
zimesajiliwa na kupewa cheti maalumu cha ukaguzi na gari hizo
zitakaguliwa kila baada ya miezi mitatu (3)
2 Ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kusafirisha nyama kwa
kutumia pikipiki au baiskeli
3 Itakuwa ni wajibu wa kila mmiliki wa gari la kubeba nyama
kuhakikisha kwamba gari lake:-
(a) Limesajiliwa na Halmashauri
(b) Lina sanduku la aluminium lenye mfuniko na limepakwa
rangi nyeupe, mstari mwekundu na namba.
(c) Halibebi kitu kingine kinachoweza kuleta madhara/athari
kwa afya ya mlaji.
(d) Atalipia gharama za usafirishaji kama zilivyowekwa na
Halmashauri.
Udhibiti wa
uchinjaji
machinjioni
15 1 Watu wote wanaohusika na shughuli za machinjio, watatakiwa
kupima afya kwa mganga au tabibu aliyeteuliwa na watapima
afya kila baada ya miezi 3 katika Hospitali au Vituo vya Afya
vilivyoteuliwa na Serikali kufanya kazi hiyo.
2 Watu wanaohusika na machinjio wanatakiwa kuwa wasafi, na
kuvaa mavazi maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
3 Hairuhusiwi kukaa au kufanya mkusanyiko wa aina yoyote
katika eneo la machinjio ya Halmashauri isipokuwa kwa kibali
maalumu kitakachotolewa na Halmashauri.
4 Machinjio mpya zitaanzishwa kwa kufuata kanuni, taratibu na
sheria zilizowekwa.
5 Uendeshaji wa machinjio utafuata sheria na taratibu zilizowekwa
na Mamlaka husika.
6 Hairuhusiwi kufanya biashara ya aina yoyote katika eneo la
machinjio.
7 Hairuhusiwi kuweka Bucha au duka la nyama ndani ya mita 200
8
kutoka eneo la Machinjio
8 Mfanyabiashara ya nyama anapaswa kuwa na leseni halali ya
biashara
9 Mifugo yote itachinjwa katika machinjio na hakuna kulaza
mifugo katika machinjio isipokuwa kwa idhini maalumu ya
mamlaka husika.
10 Kila mfanyabiashara ya nyama anapaswa kutumia leseni yake ya
biashara ya nyama yeye mwenyewe.
11 Hakuna nyama itakayoruhusiwa kutumika kwa matumizi ya
binadamu bila kufanyiwa ukaguzi wa mwisho (Post-mortem
meat Inspection)
12 Hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuingiza Mifugo katika
Machinjio ya Manispaa kwa ajili ya kuchinjwa baada ya saa
11:00 jioni isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka katika
mamlaka husika.
13 Mifugo yote haitachinjwa bila kufanyiwa ukaguzi wa awali
(Ante mortem inspection)
14 Hairuhusiwi kutoa lugha za kashfa, kuudhi, kudhalilisha au
matusi kwa Mtaalamu au mtu yeyote katika eneo la machinjio
15 Kila mfugaji atatakiwa kupeleka mfugo/mnyama wake
machinjioni au mahali huduma hiyo inapopatikana. Hairuhusiwi
mtu yeyote kuchinjia nyama mahali pengine popote.
Udhibiti ufugaji
mbwa na paka
16 1 Hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kufuga katika eneo la
Halmashauri bila kibali cha ufugaji toka Halmashauri.
2 Kibali cha ufugaji kitatolewa bure na kitadumu kwa mwaka
mmoja tu,
3 Kila mfugaji atawajibika kumpatia chanjo mnyama wake na
atawajibika kulipia ada ya chanjo pale atakavyoelekezwa na
Halmashauri.
4 Mfugaji atalazimika kuonesha cheti cha chanjo ya kichaa cha
mbwa wake kabla ya kupata kibali au kuhuisha kibali kilichoisha
muda wake.
5 Mfugaji atawajibika kumfungia mbwa wake wakati wote wa
mchana na atawafungulia wakati wa usiku kuanzia saa nne na
kuwafungia saa 11 alfajiri.
9
6 Mfugaji atatakiwa kuogesha mnyama wake kila baada ya siku 7
ili kudhibiti magonjwa na wadudu wasumbufu kwa gharama
zake ama kama atakavyoelekezwa na Halmashauri.
7 Mfugaji atalazimika kumfunga mbwa wake kwa mnyororo
maalumu wakati wa kumsafirisha kutoka sehemu moja kwenda
sehemu nyingine kwa mujibu wa Sheria.
Mbwa na paka
wanaozurura
17 Mnyama (mbwa na paka) atakayepatikana anazurura atakamatwa
na kuhifadhiwa katika kizuizi kwa muda usiozidi sikumbili
(masaa 48) na baada ya hapo halmashauri inamtaifisha au
kufanya maamuzi mengine ya kisheria pale itakapoona inafaa.
Makosa 18 1 Mfugaji yeyote atakuwa ametenda kosa iwapo:-
(a) Atashindwa au kukataa kuogesha au kuchanja mifugo
yake ili kuzuia magonjwa au
(b) Atalisha mifugo yake kwenye maeneo yasiyoruhusiwa au
(c) Ataruhusu mifugo yake kuzurura hovyo au
(d) Atakuwa hana utambulisho na kibali cha kufuga au
(e) Atashindwa au atazembea kutoa taarifa juu ya uwepo wa
au dalili za ugonjwa au kifo cha ghafla cha mfugo katika
banda lake au
(f) Atashindwa kutoa ushirikiano wa uwekaji wa alama
kwa mnyama wake au mifugo yake kwa mujibu wa
Sheria Ndogo hizi.
(g) Kumzuia afisa Muidhiniwa kutekeleza majukumu yake
Kufifisha kosa 19 Mkurugenzi atakuwa na uwezo wa kufifilisha kosa kwa kumtoza
faini mtu yeyote aliyetenda kosa kwa mujibu wa Sheria Ndogo
hizi, kiasi kisichopungua shilingi Laki Mbili (200,000) na
kisichozidi laki tano (500,000) iwapo mkosaji atakiri kosa kwa
hiari na kuwa tayari kujaza fomu maalumu iliyoambatanishwa
kwenye jedwali la tatu la Sheria Ndogo hizi.
Adhabu 20 Mtu yeyote atakayekwenda kinyume na masharti ya Sheria
Ndogo hizi atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia
atatozwa faini ya kiasi kisichopungua shilingi laki
mbili(200,000) au kisichozidi Milioni moja (1,000,000) au
kifungo kisichopungua miezi kumi na miwili (12) au kisichozidi
miezi ishirini na nne (24) jela au adhabu zote mbili kwa pamoja.
10
JEDWALI LA KWANZA
KIBALI CHA KUFUGA WANYAMA
(Chini ya kifungu 6 (1))
Jina:…………………………………………….
Anuani:…………………………………………
Ameruhusiwa kufugwa wanyama wafuatao katika eneo la………………………..
Na Aina ya mnyama Idadi
1 Ng’ombe
2 Mbuzi
3 Kondoo
4 Nguruwe
5 Ngamia
6 Punda
7 Paka
8 Farasi
9 Sungura
10 Mbwa
11 Kuku /Bata
12 Wanyama wengine (wataje)
Kibali hiki kitakuwa kwa muda wa miezi kumi na mbili (12) kuanzia tarehe………………..hadi
tarehe…………..
Kimetolewa na :
Jina la Afisa Mwidhiniwa:……………………………………….
Tarehe:………………………………….
Muhuri:
11
JEDWALI LA PILI
KIBALI CHA KUSAFIRISHA WANYAMA
(Chini ya kifungu cha 8(1))
Jina:…………………………………………….
Anuani:…………………………………………
Ameruhusiwa kusafirisha wanyama wafuatao kutoka ………………………kupitia njia
za…………… ………………………………………..hadi……………………..…..
Na Aina ya mnyama Idadi
1 Ng’ombe
2 Mbuzi
3 Kondoo
4 Nguruwe
5 Ngamia
6 Punda
7 Paka
8 Farasi
9 Sungura
10 Mbwa
11 Kuku /Bata
12 Wanyama wengine (wataje)
Kibali hiki kitakuwa cha muda wa siku………….. kuanzia tarehe………………..hadi
tarehe…………..
Barua toka kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa/Afisa Mifugo Mtaa/Kata inayothibitisha uhalali wa
kumiliki mifugo /wanyama hao imeambatanishwa.
Kimetolewa na :
Jina la Afisa Mwidhiniwa:……………………………………….
Tarehe:………………………………….
Muhuli:
12
JEDWALI LA TATU
HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA
(SHERIA NDOGO ZA WANYAMA MWAKA 2018)
KIBALI CHA JUMLA CHA KUSAFIRISHA WANYAMA
Jina:…………………………………………….
Anuani:…………………………………………
Ameruhusiwa kusafirisha wanyama wafuatao
Na Aina ya mnyama Idadi
1 Ng’ombe
2 Mbuzi
3 Kondoo
4 Nguruwe
5 Punda
Kutoka …………………………kwenda………..………………..kupitia………………………..
Kwa muda wote wa masaa ya mchana kwa kipindi cha kuanzia ………………..hadi…………….
Namba ya gari…………………………….Namba ya trela………………………..
Kibali hiki kitakuwa cha muda wa siku………….. kuanzia tarehe………………..hadi
tarehe…………..
Barua toka kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa/Afisa Mifugo Mtaa/Kata inayothibitisha uhalali wa
kumiliki mifugo /wanyama hao imeambatanishwa. Aidha, kibali cha kusafirisha mifugo
Na……………….kimeambatishwa
Kimetolewa na :
Jina la Afisa Mwidhiniwa:……………………………………….
Tarehe:………………………………….
Muhuli:
13
JEDWALI LA NNE
IDADI YA WANYAMA WANAOTAKIWA KUFUGWA
KATIKA ENEO LA HALMASHAURI
(Chini ya kifungu 6 (1))
Na Aina ya mnyama Idadi
1 Ng’ombe 4
2 Mbuzi 4
3 Kondoo 4
4 Nguruwe Kundi moja (flock)
5 Ngamia 4
6 Punda 4
7 Paka 4
8 Farasi 4
9 Sungura Kundi moja (flock)
10 Mbwa 4
11 Kuku /Bata Kundi moja (flock)
12 Wanyama wengine (wataje) Kulingana na aina ya wanyama husika
14
HATI YA KUFIFISHA KOSA
(Limetungwa kwa chini ya kifungu cha 16)
Mimi ……………………………………..nakiri kwa hiari yangu mwenyewe mbele ya
……………………………….……ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala
kwamba mnamo tarehe ……….ya Mwezi………..Mwaka…………nilitenda kosa la kukiuka
masharti ya Sheria Ndogo hizi za Udhibiti na Usimamizi wa Mifugo za Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala za mwaka 2018.
Kwa mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa niko tayari kulipa kiasi cha
shilingi,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,kama faini ninayodaiwa.
NATHIBITISHA KWAMBA MAELEZO HAPO JUU NI YA KWELI NA NIMEYATOA
KWA HIARI YANGU KADRI YA UFAHAMU WANGU
Leo tarehe………………..ya Mwezi…………….Mwaka………….
Jina:………………………………….
Saini:………………………………
Mbele ya:………………………………..
Cheo:……………………………………
Saini:……………………………………
Tarehe:………………………………….
15
Nembo ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imebandikwa kwenye Sheria Ndogo hizi kufuatia
Azimio lililopitishwa kwenye mkutano wa Halmashauri ulioitishwa na kufanyika
Tarehe………………Mwezi……………..2018 mbele ya:-
…………………………..
JUMANNE K. SHAURI
MKURUGENZI WA MANISPAA
HALMASHAURI YA MANISPAA ILALA
…………………………..
CHARLES KUYEKO
MSTAHIKI MEYA
HALMASHAURI YA MANISPAA ILALA
NAKUBALI,
…………………………..
Mhe. SULEIMAN JAFO (MB)
WAZIRI WA NCHI – OR-TAMISEMI
DODOMA
Tarehe……………………..