15
Wanawake wa Biblia Diocese-Based Leadership Training Program Mennonite Churches of East Africa (KMC/KMT) Gloria Bontrager ©2014

Wanawake wa Biblia - equip4change.orgequip4change.org/pdf/swahili/level1/Wanawake-wa-Biblia.pdf · 4. Inaonekana kwamba mara nyingi imani na uvumilivu zinaenda pamoja. Kwa nini tusitegemee

Embed Size (px)

Citation preview

Wanawake wa Biblia

Diocese-Based Leadership Training Program Mennonite Churches of East Africa (KMC/KMT)

Gloria Bontrager ©2014

uk. 2

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Yaliyomo

Somo la 1 Uumbaji wa mwanamke – “Hawa, mama yao wote walio hai” 3

Somo la 2 Sara – Kielelezo cha Imani, Utii, Heshima 4

Somo la 3 Hana – Mwanamke wa Imani na Maombi 5

Somo la 4 Mariamu wa Bethania, Mwanmke Aliyependa Sana 6

Somo la 5 Mariamu, Mama wa Yesu, Usafi wa Maisha na Tayari Kupokea Mapenzi ya Mungu

7

Somo la 6 Mke wa Potifa: Mwanamke wa Tabia Mbaya 8

Somo la 7 Abigaili - Mke wa Mpagani na Mpatanishi wa Amani 10

Somo la 8 Ukarimu, Matendo Mema na Uchaji wa Mungu 12

Somo la 9 Mateso – Mjane wa Sarepta 13

Somo la 10 Sara – Kielelezo cha Imani, Utii, Heshima 14

uk. 3

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 1. Uumbaji wa mwanamke – “Hawa, mama yao wote walio hai”

(Soma katika Biblia Mwanzo 1:27-28; 2:18, 20-25)

1. Uumbaji wa Adamu na Hawa ulikuwa ni “mzuri sana” kwa sababu walikuwa na ushirika, upendo, ukamilifu, na utulivu kati yao na Mungu.

2. Hawa aliumbwa kuwa mwenza wa Adamu. Wote wawili walipewa kazi sawa ya kuitunza bustani. Mungu aliwaumba katika sura yake na aliwataka wasaidiane (Mwanzo 1:27). Hawa, mwenza wake Adamu, alikuwa na uwezo sawa wa akili na mshiriki katika jamii na masuala yote ya uzazi. Walipendana, kuheshimiana, na kumheshimu Mungu. Hawa aliishi katika ulimwengu uliokamilika.

3. (Soma Mwanzo 3:1-20) Hawa alidanganywa na Shetani aliyemfanya awe na mashaka na mambo yale aliyoambiwa na Mungu. Aliamua na kukubali kuzungumza na Shetani, katika kumweleza yale Mungu aliyowaagiza, Shetani alipata ujasiri wa kumshauri kuwa, Mungu hakuwatakia mema, bali aliwadanganya.

4. Mwanamke Hawa alisukumwa na mataminio (ya lile tunda) naye akafanya uamuzi (nje ya mapenzi ya Mungu) na kumwingiza mumewe katika dhambi yake. Akampa tunda, naye kwa hiari yake akala tunda walilokatazwa. Licha ya kumtii Mungu kutokana na upendo wake kwa Mungu, Hawa aliamua kuasi na kumshirikisha mumewe pia. Hali ya uasi ilileta madhara makubwa sana katika ulimwengu wao.

5. Dhambi ya kutotii ilileta mabadiliko mabaya na makubwa kwao na kwa ulimwengu alioumba Mungu. Nyoka alilaaniwa, na ardhi ililaaniwa kwa kuzaa miiba na michongoma, chakula chao kitakuwa ni kwa uchungu na kwa jasho lao, mwanamke atazaa kwa uchungu mwingi na hakika watakufa. Mungu akawafukuza kutoka mazingira hayo mazuri ya bustani. Dhambi iliharibu mahusiano mazuri yaliyokuwapo kati yao na Mungu. Tangu hapo binadamu anahangaika na kutafuta namna ya kurudisha tena mahusiano na Mungu.

Maswali ya majadiliano:

1. Ni katika tabia gani za mwanamke tunaona mfano wa Mungu? Je, ni tofauti na mwanaume kwa jinsi tunavyoona mfano wa Mungu katika tabia zake? (Isaya 66:12-13; Isaya 42:14; 46:3-4; 49:15; Zaburi 22:9-10; Zaburi 71:6) (Isaya 1:2; Kumbukumbu la Torati 8:15-16; Isaya 40:11)

2. Jadili usemi huu: Mwanamke hakuumbwa kutoka kichwa cha mwanamume, ili kumtawala, au kutoka miguuni, ili akanyagwe. Bali aliumbwa kutoka ubavuni, ili awe na usawa naye, na chini ya mkono wake ili alindwe naye, na karibu na moyo wake, ili apendwe naye (Mithali 12:4).

3. Ndoa ya kwanza ilianzishwa katika Mwanzo 2:24. Ni tabia gani za ndoa yaliyomo katika kifungu hiki?

4. Taja dhambi za Hawa. Na linganisha dhambi zake na kifungu cha Wafilipi 2:1-8.

5. Dhambi zetu tunazozitenda siku hizi, je, zinatokeza matokeo gani?

uk. 4

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 2. Sara – Kielelezo cha Imani, Utii, Heshima

Mwanzo 12:1-5; 18:1-15; 21:1-13; Waebrania 11:11; 1 Petro 3:5-6

1. Imani na utii (Mwanzo 12:1-5). Sara alikuwa mke mzuri wa mwanamume tajiri Ibrahimu aliyeheshimika katika mji mkubwa. Kwa kuwa mumewe alikutana na Mungu aliye Hai na kumwamini, Sara alikubali kuondoka na kumsindikiza mumewe kwenda mahali wasikokujua, jinsi Mungu alivyowaagiza. Kwa kumtii Mungu, waliahidiwa kwamba kupitia uzao wao, taifa kubwa litaundwa, na kupitia kwao mataifa yote watabarikiwa. Sara alifuata uongozi wa kiroho wa mumewe na wa Mungu aliyesema naye, hivyo alitii kila aliloambiwa, aliondoka na mumewe kwenda katika mazingira mapya wasiyoyajua.

2. Kuvumilia hali ngumu kwa heshima na imani (Mwanzo 12:10-20). Ibrahimu alifanya uamuzi mbaya wa kudanganya juu ya hadhi ya Sara kama mkewe na kunweka katika hali ya hatari. Hata hivyo, Mungu akawa msaada wake Sara na kuingilia hali hiyo. Mungu huwaheshimu na kuwabariki wanawake wanaoheshimu na kutii waume wao, bila kujali udhaifu au kushindwa kwao. Mungu hutumia uzoefu huo kuongeza imani na utii wetu kwake. Sara ni kielelezo cha imani. Biblia inasema kuwa, alijipamba kwa kumtumaini Mungu na kukubali mamlaka ya mumewe na kumtii bila hofu yoyote (1Petro 3:5-6).

3. Kutovumilia huleta shida (Mwanzo 16:1-6). Ahadi ya kupata mtoto ilipochelewa, Sara alifuata busara yake mwenyewe, akamshauri mumewe Ibrahimu kumwingilia mjakazi ili apate uzao kwake na hivyo kutimiza ahadi ya Mungu. Dhambi ya Sara ya kutoamini ahadi ya Mungu na kutovumilia ilileta huzuni, migongano na mashindano katika familia. Sara aliposhindwa kungojea mpango wa Mungu matokeo yake ni lawama, wivu, utengano na kudhalilishana kati ya wanawake hao wawili. Ingawa Ibrahimu aliwapenda Hajiri na kijana wake, lakini alikubali Sara akawafukuza, jambo ambalo lilileta mgogoro wa kudumu kati ya koo mbili za uzao wa Ibrahimu.

4. Licha ya wateule wa Mungu kushindwa Mungu alishika Agano lake. (soma Mwanzo 18, 20 na 21). Mungu alitimiza ahadi zake kwa wakati wake, hata waliposhindwa na kuyumba katika imani yao. Ibrahimu na Sara wote wanatajwa katika Agano Jipya kama ni watu wa imani. Wamewekwa kuwa kielelezo kwa jinsi walivyotembea katika imani na kumtii Mungu (Waebrania 12:8-12; 1Petro 3:6).

Maswali ya majadiliano:

1. Imani inawezaje kutuongoza katika mahangaiko ya ndoa zetu? Toa mifano kutoka katika maisha ya Sara na Ibrahimu.

2. Maisha ya Sara yanatufundisha nini kuhusu uaminifu na upendo wa Mungu, hata kama tunaenda kinyume naye na kufuata njia zetu wenyewe?

3. Kwa nini hofu ni jambo kubwa kwa wanawake? Tufanyeje ili kushinda hofu zetu?

4. Inaonekana kwamba mara nyingi imani na uvumilivu zinaenda pamoja. Kwa nini tusitegemee hekima yetu wakati wa mashaka au matatizo? Tufanyeje ili kuimarisha subira na uvumilivu katika maisha yetu?

5. Eleza maana ya kujipamba inavyoelezwa katika 1 Petro 3:4.

6. Tunawezaje kujenga roho ya utulivu na upole?

uk. 5

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo La 3. Hana – Mwanamke wa Imani na Maombi

(Soma 1 Samweli 1:9-28)

1. Ndoa ya Hana yapata matatizo. Hana alikuwa ni mke wa kwanza wa mwanamume aliyempenda Mungu. Ingawaje Hana alikuwa mgumba, lakini mumewe alimpenda sana. Mke mwenza alikuwa na watoto, mara kwa mara alimsumbua kwa kumkumbusha hali yake ya ugumba. Alitowesha amani katika familia kutokana na vurugu. Mume alifanya mambo kuwa magumu zaidi kwa Hana kwa kuonyesha upendeleo, jambo ambalo liliongeza wivu na kutoelewana.

2. Hana alilia mara kwa mara, hata akakataa kula, akiomba na kumlilia Mungu kuhusu hali yake. Kutokana na historia ya viongozi wakubwa kama Ibrahimu na Isaka, Hana alimjua Mungu kuwa ni wa miujiza. Alimjua kuwa ni msikivu, mwaminifu kwa watu wake, hivyo akaamua kumimina roho yake ya huzuni mbele za Mungu, akimwomba ampe mtoto wa kiume.

3. Sara alizoea kuingia hekaluni kila mwaka kuabudu. Alipojiweka mbele ya Bwana akaanza kulia mbele ya watu kwa sababu ya uchungu wake. Aliamua kuchukua hatua ya ujasiri ya kuweka nadhiri iliyoonyesha ukweli wa imani ya moyo wake. Akamwitia Mungu kwa ujasiri, “Ee Bwana wa Majeshi” na pia kutambua unyonge wake na moyo wa utumishi. Aliahidi kumweka mtoto atakayepewa, wakfu kwa Bwana, siku zote za maisha yake. Baada ya maombi hayo, aliondoka katika hekalu akiwa na amani na kuamini kuwa Mungu amemsikia na atafanya.

4. Ombi la Hana lapatiwa jibu na kwa shukrani kuu, anatimiza ahadi yake kwa Mungu. Alimleta mtoto hekaluni mbele ya Mungu na kumtoa amtumikie kwa muda wote wa uhai wake (1 Samweli 1:26-28). Soma sala yake ya shukrani katika 1 Samweli 2:1-10.

Maswali ya Majadiliano:

1. Mungu huona mateso yetu na husikia kilo chetu (Kutoka 2:23-25). Kwa nini Mungu hatujibu mara moja tunapomwendea?

2. Kujua jinsi Mungu alivyofanya kazi katika maisha ya watu wa zamani, inatusaidiaje kumwamini kuwa atajibu haja zetu?

3. Je, maneno gani katika ombi la Hana katika 1 Samweli 1:11 ni mfano kwetu wa namna ya kumwomba Mungu?

4. Je, ni vizuri kumwomba Mungu kwa kudumu na kwa ujasiri (kwa mfano kuweka ahadi na nadhiri) katika maombi yetu leo? (Soma Waebrania 10:19-23).

5. Soma sala ya sifa ya Hana katika 1 Samweli 2. Maomi yetu yakipata jibu, je, ni vizuri tuitikiaje?

6. Eleza uchungu wa ugumba. Tunawezaje kusaidia na kufariji mtu mgumba badala ya kumlaumu au kumshtaki?

uk. 6

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 4. Mariamu wa Bethania, Mwanmke Aliyependa Sana

(Soma Luka 10:38-42)

1. Mariamu alichagua kufanya jambo lisilo la kawaida la kukaa miguuni pake Yesu akisikiliza maneno yake, badala ya kushugulika na ukarimu kama alivyofanya dada yake Martha. Na Martha alipomnung’unikia Mariamu kwamba hakutekeleza wajibu wake, Yesu alithibitisha uchaguzi wake Mariamu kwamba amechagua yaliyo bora, na kumwonya Martha kwa jinsi alivyomhukumu dada yake.

2. Katika Yohana 11:17-37, Mariamu anaomboleza kifo cha ndugu yake na kusikitika kwa nini Yesu alikawia kuja, wakati aliarifiwa ugonjwa wake. Alikuwa na imani juu ya uwezo wa Jesu kuponya rafiki yake mpendwa, kwa nini hakuzuia kifo chake? Ingawa hakuelewa kutokana na kuumizwa na tukio hili, upendo na imani yake kwa Yesu haikuyumba. Upeno mkuu wa Yesu kwa familia ya Mariamu ni dhahiri kwa jinsi alivyoomboleza nao. Lakini dhumuni la Mungu (kuimarisha imani yao) lilikamilika vizuri zaidi kupitia kifo cha Lazaro na kufufuliwa kwake kutoka wafu.

3. Upendo mkuu wa Mariamu unaoneshwa zaidi pale Yesu alipowatembelea tena nyumbani kwao (Yohana 12:1-8). Alipata nafasi tena ya kuonyesha upendo wake bila kujali atakavyoeleka kwa matendo yake. Mariamu alichukua marashi yake ya gharama akampaka miguuni mwa Yesu na kufuta kwa nywele zake. Matendo hayo ya kumwabudi Yesu, yalithibitisha imani yake kwa Yesu kuwa ni Masihi, na kumshukuru Yesu kwa mabadiliko aliyomfanyia katika maisha yake. Alikumbuka jinsi Yesu alivyozungumzia juu ya mateso yake yatakavyokuwa, akajua muda umefika. Kutokana na upendo mkuu aliokuwa nao kwake, aliupaka mwili wake Yesu mafuta kama tendo la upendo la mwisho.

Maswali ya Majadiliano:

1. Eleza maana ya kumpenda Mungu, au kumpenda Yesu, jinsi unavyoelewa?

2. Je, ni matendo yetu gani huonyesha upendo wetu kwa Yesu leo?

3. Je, tunafanyaje ikiwa maombi yetu hayajibiwi, au yanajibiwa kwa njia tofauti?

4. Je, unaonaje kifo cha mpendwa? Mara nyingi huonekana kama hukumu ya Mungu au kutopendwa na Mungu. Mtazamo sahihi kuhusu kifo ni upi? (1 Wakorintho 5:1-10; 1Wakorintho 15:1-58).

5. Je, tunawezaje kuonesha upendo wetu kwa Yesu kwa njia inavyostahili?

6. Toa mifano kuhusu jinsi tunavyoweza tusieleweke katika kumtumikia Yesu.

uk. 7

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 5: Mariamu, Mama wa Yesu, Usafi wa Maisha na Tayari Kupokea Mapenzi ya Mungu

(Soma Luka 1:26-38; 2:6-14, 17-19; Mathayo 1:18-25)

1. Mariamu alikuwa ni msichana wa kawaida, bikira, mtulivu, mnyenyekevu na asiyejulikana, aliyeishi Nazareti. Pamoja na hayo, alitokewa na malaika Gabrieli, na kumwambia amejaliwa, na “Bwana yu pamoja nawe.” Mariamu alishangaa na kufadhaika kwa salamu hiyo. Kwa uhakika Mariamu alithamini mahusiano yake na Mungu. Kila mwanamke Myahudi alitamani kumzaa Masihi aliyeahidwa. Mariamu ni binti mcha Mungu aliyejua maandiko matakatifu na aliyetegemea kuona ukombozi wa Israeli. Zaidi ya yote alikuwa na moyo wa utashi wa kutumiwa na Mungu. Alipoambiwa na malaika kwamba alichaguliwa kumzaa Mwkozi wa ulimwengu, aliuliza itakuwaje hali yeye ni bikira. Aliamini neno la Mungu, akajitoa kikamilifu kwa mapenzi yake bila kusita.

2. Je, Mariamu alifikiria yale ambayo yangempata katika kujitoa katika mapenzi ya Mungu? Utaratibu wa Kiyahudi uliruhusu mwanamke akipatwa na mimba kabla hajaolewa kuuawa kwa kupigwa mawe. Lakini ukubali wa Mariamu wa heshima pekee wa kuwa mama wa Masihi umeandikwa katika Luka 1:46-55. Wimbo wake unamtukuza Mungu, umejaa sifa na shukrani za kuchaguliwa kuleta ukombozi kwa watu wa Mungu.

3. Mariamu, mama wa Masihi angeweza kushangazwa na kuogopa matukio yote yaliyohusu kuzaliwa kwake Yesu. Badala yake alikubali na kukumbuka ahadi zilizotolewa huko nyuma kumhusu na akaamini Mungu kuzitimiza (Luka 2:19). Alipatwa na changamoto katika malezi, lakini alizikabili na kumlea Yesu. Akakua, akawa mwenye nguvu, hekima na kufunikwa na neema ya Mungu (Luka 2:40). Mariamu alielewa uwezo wa Yesu ulivyo mkuu, na alifanya bidii kuwashawishi wa kuwasaidia watu kumwelewa Yesu joins alivyo (Johana 2:1-11). Imani yake na kujitoa katika mapenzi ya Mungu ilimjenga na kumwezesha kuvumilia mambo magumu aliyopitia wakati wa maisha ya Yesu. Yesu alipotamka kwamba jamaa yake wa kidunia hawapawi umuhimu wa kwanza, mama yake hakujali aliendelea kumtia moyo katika huduma yake ( Mathayo 12:46). Mwishowe, Mariamu alisimama karibu na msalaba akishuhidia matusi, dhihaka, mateso na kufa kama mhalifu. Hata baada ya kifo, Mariamu ametajwa pamoja na wanafunzi wa Yesu wakisali chumbani (Mtendo 1:14). Wakati wa kifo cha mwanaye, Mariamu hakudumu katika maombolezo bali aliendelea kufuatana na wengine katika huduma ya Mungu.

Maswali ya majadiliano:

1. Je, Mariamu alikuwa na sifa gani katika roho yake zilizomfanya aweze kufaa kwa madhumuni yake Mungu?

2. Mariamu alioynesha mashaka yake kwa malaika. Je, ni sawa kuwa na mashaka kuhusu yale Mungu anayosema?

3. Ni vipi tunaweza kuwa imara na kufanya maamuzi ya ukweli, hata kama tunajua kwamba wengine hawatatuelewa?

4. Ni nini tunajifunza kwa Mariamu, pale ambapo Mungu anataka tupitie mambo magumu?

5. Faida ya mateso na magumu katika maisha ya wanafunzi wa kweli ni nini? (Warumi 5:3).

6. Kwa nini Mariamu alisema maneno haya: “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema” (Luka 1:38).

uk. 8

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 6 Mke wa Potifa: Mwanamke wa Tabia Mbaya

(Soma Mwanzo 39:1-20)

1. Mke wa Potifa alikuwa na kila kitu. Alikuwana mume Afisa mkuu katika nchi ya Misri, walikaa katika nyumba kubwa iliyojaa samani nyingi nzuri zenye gharama kubwa na kuvaa nguo nzuri za thamani. Pamoja na hivyo vyote alikuwa na utupu ndani yake, ili kuujaza utupu huo, alijaribu sana na hata kumbembeleza Yusufu, mtumishi wa mume wake, ili alale naye. Alijaribu hata kumbaka ili atosheleze mwili wake. Lakini heshima ya Yusufu kwa Mungu na kwa bwana wake ilimzuia. Mwanamke huyo aliposhindwa kumpata Yusufu, alitafuta njia mbadala ya kumsingizia na kumtuhumu Yusufu mbele ya Potifa, ndipo Yusufu akafungwa. Dhambi ya kwanza ya uchu ilimpeleka kwa dhambi zingine za uongo, usingiziaje na usaliti.

2. Kujamiiana ni mpango wa Mungu kwa ndoa tangu mwanzo. Hujenga hali ya usalama na utulivu katika ndoa, na kufanya wenzi katika ndoa kuelewana na kupendana kwa ndani zaidi (Mwanzo 2:24-25; Mathayo 19:4-6; Waefeso 5:31). Kujamiiana kwa halali ni tendo la heshima na hakupaswi kuonewa aibu, wala kuchafuliwa (Waebrania 13:4). Biblia intunashauri kujifurahia raha za matendo yaambatanayo na ngono katika ndoa halali (Mithali 5:15-19). Paulo alihimiza Wakristo kutumia haki zao za ngono ili kuepa uasherati na uchafu ndani ya kanisa (1 Kor. 7:2-9). Ndoa ya aina hiyo inadhibiti tamaa ya ngono na kujenga nidhamu.

3. Mafarisayo walimlaumu Yesu jinsi alivyokutana na mwanmke wa tabia mbaya kwa sababu alimkubalia mwanamke huyo kumgusa (Luka 7:36-50). Lakini Yesus alitambua hitaji lake la kweli la kukubalika na kusamehewa. Yesu alimkubali, akamsamehe dhambi zote kwa sababu ya upendo wake mkuu.

4. Wakati mwingine Yesu aliletewa mwanamke katika fumanizi la uzinzi (Yohana 8:3-11). Yesu aliwajibu washtaki wa mwanamke huyo, maneno yaliyowaonyesha dhambi zao wenyewe, wakaondoka. Yesu hakumhukumu yule mwamamke, alimwagiza kwenda na kutotenda dhambi tena.

5. Yesu alifundisha kuhusu uzinzi na talaka (Mathayo 5: 27). Alieleza kwamba, hata kumtazama mtu kwa tamaa, ni sawa kama umezini. Sisi kama viungo vya mwili wa Kristo na hekalu la Roho Mtakitifu tusitoe miili yetu katika matendo ya uasherati na hivyo kuchafua mwili wa Kristo na roho zetu. Bali tutoe miili yetu kwa utukufu wa Mungu (1 Wakorintho 6:13b-20). Miili yetu ni hekalu la Mungu aliye Hai, hivyo haipaswi kuchafuliwa na mahusiano yasiyomjua Mungu (2 Wakorintho 6:14). Wanandoa wasipojitoa kikamilifu katika ndoa yao, uchu wa ngono utaleta tamaa mbaya na kuishia kuangamizana (Mithali 6:32). Ngono inapofanyika katika udanganyifu na katika hali isiyo halali husababisha hatia, lawama, chuki, aibu, tena kuongeza upweke na matatizo mengi ya kujirudia katika ndoa (Mithali 5:3-6; 23:27-28; 6:27-29). Wote wanoshiriki katika matendo ya mwili yakiwamo uzinzi na uasherati hawataurithi ufalme wa Mungu (Wagalatia 5:19-21). Sisi Wakristo tunaamriwa kujitakasa na kuepukana na uchafu wowote wa miili na roho zetu, tuwe wacha Mungu na watakatifu (2 Wakorintho 7:1).

uk. 9

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Maswali na Majadiliano:

1. Matendo ni tunda la fikira. Mtu hufanya kufuatana na mawazo yake na roho yake (Mithali 23:7). Jadili jinsi dhambi ya mke wa Potifa ilivyoanza na kuendelea hatua kwa hatua hadi ya kuwa matendo.

2. Kwa kawaida unafikiria tamaa ya ngono ni tatizo la mwanamume. Je, pia hili ni tatizo kwa wanawake wa siku hizi?

3. Je, una mawazo gani kuhusu ngono? Tabia ya kiungwana ya mwanamke inawezaje kutunza mahusiano mazuri yenye mipaka kati ya wanaume na wanawake?

4. Je, sisi Wakristo tufanyeje kwa wale wanoshikwa katika uasherati na uzinzi?

5. Ni kawaida kuona ngono kuwa ni uchafu, ufisadi na hata uovu. Je, maoni hayo ni ya kibiblia? Katika hali gani inaweza kuwa safi na takatifu?

6. Sisi wanawake wa kanisa tunawezaje kuitikia uchafu wa ngono ndani ya kanisa?

uk. 10

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 7 Abigaili - Mke wa Mpagani na Mpatanishi wa Amani

(Soma 1 Samweli 25:2-31)

1. Abigaili alikwa mzuri tena mjanja. Nabali, mumewe alikuwa tajiri, lakini mkorofi na mpumbavu. Daudi alikuwa ametawazwa kuwa mfalme wa Israeli, lakini alimkimbilia Sauli na kutangatanga na watu wake nyikani. Walitoa ulinzi kwa watumishi wa Nabali waliokuwa wakikata manyoya ya kondoo. Daudi alitoa maagizo kwa watu wake, kumwedea Nabai kwa amani, kuomba chakula kwa sherehe yao. Nabali aliwajibu vibaya sana tena kwa kejeli na hata kumkashifu Daudi. Daudi alipoambiwa yaliyotokea, alikasirika na kujitayarisha kwenda kumwangamiza Nabali na familia yake.

2. Mmoja wa vijana alitambua mabaya ambayo yangetokea, akaenda kumwarifu Abigaili yote yaliyofanywa na mumewe. Abigaili akatayarisha sadaka ya amani na kuondoka mara moja kumwendea Daudi. Akamkabili Daudi na kukiri hatia na upumbavu wa mumewe alioufanya na kuomba msamaha. Alimshauri pia, kufikiria hasara atakayopata ya kulipi za kisasi kwa kumwaga damu kwa mikono yake, bali baraka za amani atakazopata kwa kutofanya hivyo. Pia alimkumbusha wito na utume wake kwa Bwana. Busara yake ilimsaidia Daudi kutuliza hasira na kuacha kuua.

3. Tabia ya Abigaili na jinsi alivyonena ilileta mabadiliko ya haraka katika utata uliokuwepo. Inategemea ni kwa namna gani wanawake hutumia ndimi zao kwani huweza kuleta au kuzuia mtikisiko. Zaburi inatoa ushauri wa kuzuia ndimi kwa mabaya ili kuleta amani kuliko ugomvi (Zaburi 34:13-14). Pia, kujua nyakati za kusema na kujizuia (Mhubiri 4:7 na Zaburi 39:1-3). Maneno mazuri ni kama inayokubalika na huleta uponyaji mioyoni (Mithali 10:20), na maneno mabaya ni kama upanga mkali uchomao moyo au mshale wa sumu uuao (Mithali 12:18). Mtume Yakobo anazumgumzia matatizo ya kutozuia na kutotawala ulimi (Yakobo 1:26; 3:5-12; 4:11). Ulimi huo huo hulaani, hubariki, husingizia, hutukana na hutoa maneno maovu kwa ndugu na dada, ulimi pia hukemea kwa ukali (1 Timotheo 5:1). Mambo hayo hayatakiwi katika kanisa la Kristo.

4. Hali ya amani aliyokuwa nayo kahaba Rahabu ilimsaidia asiangamizwe na waasi (Waebrania 11:31) .Huenda aliwahi kusikia habari za ukuu wa Mungu wa Israeli. Alipopata nafasi ya kushuhudiwa na wapelelezi, aliamini kwa hiari yake na kuwakaribisha kwa amani. Kupitia jambo hili amekuwa miongoni mwa mama wa ukoo wa Kristo.

5. Kuishi kwa amani na mwenza asiyeamini ni changamoto katika ndoa. Hata hivyo, 1 Wakorintho 7:10-16 inashauri kuwa, mwenza aliyeamini anaweza kumsaidia mwenzake na watoto kuokoka kutokana na matendo na imani wanayoona kwake. Katika 1 Petro 3:1 inaelezea kuwa njia ya kumvuta mwenza ni mwenendo kuwa msafi na uchaji wa Mungu, tena haya huzungumza zaidi kuliko maneno. Biblia inakataa kutengana au talaka kutokana na imani tofauti. “Maana Mungu ametuita katika amani” (1 Wakorintho 7:12-15). Yesu alifundisha juu ya talaka (Mathayo 5:31-32). Ingawaje talaka ilikubalika katika sheria ya Musa (Kumbukumbu 24:1-4), lakini mtazamo mwema wa Yesu unakumbusha kuwa, talaka siyo suluhisho sahihi, bali pale tu uzinzi uanpofanyika. Yesu anakataa suala la talaka kwa sababu huwapeleka wahusika kufanya dhambi (Marko 10:11-12; Luka 16:18).

uk. 11

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Mawali ya Majadiliano:

1. Tunatakiwa kuwa na busara kama nyoka na wapole kama hua (Mathayo 10:16). Je. ni kwa vipi Abigaili alionyesha busara na upole?

2. Linganisha matendo ya Abigaili na amani tuambiwayo katika Agano Jipya (Warumi 12:18-21). Je, tunapewa nafasi ya kulipiza kisasi?

3. Kama hatuwezi kuzuia ndimi zetu, Yakobo anasemaje kuhusu dini yetu? (Yakobo 1:26). Athari zipi hutokea tusipozuia ndimi zetu?

4. Soma Mithali 15:1-2; 5:3-4; 6:23-24; 19:13 kuhusu matumizi ya ulimi. Je, ulimi hutumikaje na matokeo yake ni nini?

5. Mtu akiwa na roho ya amani, je, inawezaje kujenga imani yake? Tumia mfano wa Rahabu.

6. Jadili changamoto za kumwoa au kuolewa na asiyeamini. Ni kwa nini Yesu na waandishi wa Agano Jipya wanahimiza uvumilivu katika ndoa kama hiyo? Je, mafundisho hayo yanapatana na 2 Wakorintho 6:14?

7. Ni katika hali gani talaka inakuwa mbadala sahihi?

uk. 12

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 8. Ukarimu, Matendo Mema na Uchaji wa Mungu

1. Mwanamke Mshunami (2 Wafalme 4:8-22, 32-37) alikuwa tajiri na mkarimu kwa Elisha, ila alikuwa hajazaa. Huyo alimtaka ale nao chakula kila mara alipopita. Alimtambua kuwa ni Mtakatifu wa Mungu, hivyo akamshauri mumewe wamtengee chumba cha kupumzikia kila alipopita. Alitafuta njia ya kutumia mali yake kwa hudumu ya Mungu, kwa mali yake alimhudumia mtu wa Mungu. Elisha alipotaka kumbariki kwa ukarimu wake, yeye alimwomba ambariki kwa mtoto.

2. Martha wa Bethania (Luka 10:38-42) alikuwa na mazoea ya kukarimu Yesu na wanafunzi wake, maana ni marafiki wa familia. Ilikuwa ni hesima wapewe mahali pa kupumzika kila walipokuja. Baadaye Martha aliingia katika hali ya mahangaiko kutokana na shughili nyingi za kukaribisha wageni na hata akakosa muda wa kuzungumza nao. Hivyo Martha, alimlaumu na kuhukumu Mariamu kwa kutojali kumsaidia kazi, bali kukaa na kuzungumza tu. Yesu alimshauri Martha kuhusu umuhimu wa kujenga roho yake na kutowahukumu wengine.

3. Dorkasi alikuwa ni mwanafunzi mtenda mema (Matendo 9:36-42) na alijitoa kuwasaidia maskini kwa dhati. Alikuwa na kipaji cha kuwabariki wengine, hasa wajane. Wajane labda walikuwa wengi katika mji wa Yafa, uliokuwa kando ya pwani, kwa sababu ya vifo vya ajali za waume wao waliokuwa wanamaji na wavuvi. Huenda naye alikuwa ni mjane, lakini alitumia uwezo wake kuwatia moyo na kuwasaidia wengine, kimwili na hata kihisia na kiroho. Kutokana na upendo wake mkuu wa kujtoa, alipendwa sana.

4. Mwanamke mchaji wa Mungu lazima apambwe na matendo mema na uzuri wa ndani, roho ya upole na utulivu (1 Timotheo 2:9-10; 1 Petro 3:4-5). Mapambo ya nje tu hayaonyeshi uzuri wa mtu, bali ni ule wa ndani ujengwao katika utu wa kweli. Wanawake watakatifu wa Agano la Kale walijipamba kwa kutii wanaume wao (1 Petro 3:5; 1 Timotheo 2:15). Wanawake wahimizwa kudumu katika imani, upendo, utakatifu na unyoofu. Mwonekano wa mtu alivyo kwa nje huonesha tabia yake alivyo, na huashiria mara nyingi kilichomo ndani yake. Ni muhimu kuvaa mavazi ya heshima kwa mwili wetu na kumheshimu Yesu aliye ndani yetu. Tuwe na sifa za ustahimivu, kiasi, uaminifu, maneno ya neema na heshima (1 Timotheo 3:11, 4:7; Tito 2:3; 1 Petro 3:2).

Maswali ya Majadiliano:

1. Soma Waebrania 13:2. Je, ukarimu unaleta faida gani kwa watu wa Mungu? Au kama Mariamu, wakati mwingine ukarimu unaweza kutuzuia tusitunze roho zetu?

2. Je, kuna mahusiano gani kati ya imani na matendo mema? Au inawezekana matendo mema yaweza kuleta hasara? Tafakari mfano wa Mariamu.

3. Katika dunia yetu kuna ushawishi unaotufanya tusisitize uzuri wa nje kuliko ule wa ndani. Ni jinsi gani sifa za kiroho zinaathiri mwonekano wetu mbele ya wengine?

4. Sisi kama wanawake tunaweza kufanyaje ili kujenga uzuri wa ndani zaidi na kupunguza msisitizo wa ule wa nje?

5. Mara nyingi kanisa linahimiza wajibu wa mwanamke wa kunyenyekea na kutojali nafasi za huduma kanisani. Wanawake wanawezaje kutumia vipawa vyao vya huduma kanisani?

uk. 13

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 9. Mateso – Mjane wa Sarepta

(Soma 1 Wafalme 17:7-24)

1. Mwanamke huyu alipita katika wakati mgumu. Alikuwa amefiwa mumewe, halafu ukame ulisababisha ukosefu wa chakula na maji, alikuwa na akiba ya chakula ya siku moja tu. Alipoende kutafuta kuni alikutana na mtu asiyemfahamu, lakini alimtambua ni mcha Mungu kwa mavazi aliyovaa. Alikuwa ni Eliya ambaye pia alikuwa na njaa. Aliyetumwa na Mungu kwa huyo mjane ili kujipatia mahitaji yake. Eliya alimwomba amletee maji ya kunywa na kipande cha mkate. Mjane alipoelezea hali yake, Eliya alimwagiza, “Usiogope, nenda ufanye kama ulivyosema, lakini unifanyie mimi kwanza na kuniletea, kasha ujifanyie wewe na mwanao. Kwa kuwa Bwana Mungu wa Israeli, anaahidi pipa la unga halitapunguka wala chupa ya mafuta haitaisha hadi hapo mvua itakaponyesha”.

2. Mwanamke huyu alikuwa ni mpagani, hakuwa Mwisraeli, huenda aliwahi kusikia habari za Mungu wa Israeli. Hali ngumu aliyokuwa nayo na ahadi alizoambiwa na nabii zilimfanya akubali kufanya aliyoombwa. Hatua ya imani ya kwanza ni ile ya kukubali kuamini alilosema nabii. Ndipo alipotii na kumfanyia kwanza nabii chakula, na alipata mfululizo wa miujiza ya ongezeko la unga na mafuta! Biblia intuambia chakula kiliongezeka na kuwatosheleza watu wote wa kwake na nabii Eliya kwa siku nyingi (1 Wafalme 17:15-16). Hatua yake ya imani kwa Mungu ilikuwa ni msingi wa maisha yake na vile vile kumweka hai mtunishi wa Mungu.

3. Hata hivyo siku moja alipatwa na maafa tena. Mtoto wake aliugua ghafla na kufa. Alikuwa na maswali ya kujiuliza: Je, ni jaribu la kutomwamini Mungu na upendo wake? Kwa nini Mungu amwokoe kutoka kifo cha njaa na afe kwa ugonjwa? Je, arudie maisha yake ya nyuma ya upagani? Je, amemkasirisha Mungu? Katika uzuni yake alifikia hatua ya kumtuhumu mtumishi wa Mungu kuhusika na kifo cha mwanaye. Eliya alileta hali ile mbele ya Mungu na kumwomba arudishe uhai wa yule mwana. Ombi lilijibiwa, mtoto alifufuliwa akwa hai. Suala la kufufuliwa mtoto wake, lilileta msukumo mpya wa imani na upendo wake kwa Mungu. Aidha, jaribu hili lilimjengea uaminifu zaidi kwa Mungu.

Maswali ya Majadiliano:

1. Ukame uliotokea Sarepta uliletea watu wote mahangaiko. Je, kwa nini Mungu alimtuma Eliya kwa huyu mwanamke?

2. Ni mambo gani mawili yaliyomfanya mwanamke awe mwazi na aamini mtu wa Mungu?

3. Je, ni nini ilisababisha mateso hayo?

4. Watu wenye haki nao hupata mateso. Ni msingi gani unaotufanya tufikiri kuwa, tukiishi kwa haki, hatuwezi kuteseka?

5. Toa mifano inayoonyesha jinsi Mungu anavyotumia mateso katika kuwapatia mema wale wampendao. Soma Warumi 8:28.

6. Je, kwa nini Yesu alijaribiwa na kuteswa? Soma Waebrania 2:18.

7. Je, ni nini shabaha ya kuteswa na kujaribiwa? Soma Yakobo 1:3.

uk. 14

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Somo la 10. Nyumba ya Kikristo Inarithisha Imani

(Soma 2 Timotheo 1:5; Waefeso 5:21-6:4)

1. Kazi muhimu sana waliyo nayo mabibi na mama ni kuweka hali ya mazingira ya nyumbani, iwe mahali watoto wanapojifunza kumpenda Mungu na wenzao. Paulo alitambua kuwa imani ya Timotheo ilianza na kulelewa na wale alioishi nao, bibi yake Loisi na mama yake Eunike (2 Timotheo 2:5). Mazingira ya nyumbani ni mwalimu wake wa kwanza wa kujenga au kuharibu mtoto kitabia. Mama wanao umuhimu mkubwa sana katika miake ya kwanza ya mtoto, kuzaliwa hadi miaka saba, kwa sababu Mama hukaa na mtoto kwa muda mwingi. Katika umri huu, mtoto hujifunza mambo kwa haraka sana. Huiga kutoka kwa mama na wale walio karibu naye. Mama wanapowafundisha wototo simulizi za mashujaa wa imani, au kuwasomea katika Biblia, hupenda sana kusikia simuliza hizi na hunasa katika ubongo, hawasahau. Watoto wenye asili ya mafunzo hayo, hujenga tabia njema, kutokana na yale wanayoambiwa, kusikia na kushuhudia wazazi na wenzake na watu wengine, na watakuwa na misingi imara katika imani.

2. Waraka wa Paulo kwa Waefeso 5:21-6:4 unatoa baadhi ya miongozo katika nyumba ya Kikristo. Familia nyumba iwe mfano wa uhusiano wa upendo wa Yesu kwa kanisa, kama bibi harusi wake. Unyenyekevu wa Kristo alivyotii mapenzi ya Mungu ni kielelezo cha mahusiano yetu ya mume na mke. Wanawake watii na kuheshimu wanaume wao kama wafanyavyo kwa Kristo aliye kichwa cha kanisa. Wanaume wawapende wake zao na kuwaheshimu kama miili yao wenyewe, wawajali, wawatunze bila ubinafsi. Mahusiano ya ndoa yawe mfano wa upendo wa Kristo kwa kanisa bila kujali maisha yake, na yawe mfano wa kanisa linavyonyenyekea kwa hiari na kuongozwa na Kristo kutokana na upend huo. Pia, Paulo anafundisha kwamba, uhusiano wa mume na mke ulivyo juu sana ya mahusiano mengine yoyote yale, kwa maana wao wameunganishwa kuwa mwili mmoja na kujitoa kikamilifu kwa mwenza na watoto wao.

3. Watoto waagizwa kuwatii wazazi wao katika Bwana (Waefeso 6:1-4), wakiwaheshimu kama ilivyoagizwa ili wabarikiwe katika maisha marefu ya kuishi (Kutoka 20:12). Hali bora ya maisha ya watoto hutegemea uhusiano wa upendo wa wazazi wao. Kutii kwa upendo ni matokeo ya ushuhda wa amani na upendo walioonyesha wazazi wao. Inafuata maelekezo ya utulivu na maadili bila kutumia lugha kali, vipigo, na ulazima wa matakwa yao. Mafundisho ya wazazi yawe “kilemba cha neema kichwani” na “mikufu” shingoni mwake (Mithali 1:8-9).

4. Shughuli za ngono katika ndoa huheshimika (Waebrania 13:4). Pale mwanamume na mwanamke wanapokuwa “mwili mmjoa” hali ya nguvu na msisimko isiyozuilika hutokea kwa ndani sana. Paulo anahimiza wenza katika ndoa wapeane haki zao za ndoa, wasinyimane ili kufurahia uhusiano wa ndani wa kimwili kwa sababu unawaunganisha na ni mpango wa Mungu wa kudhibiti tamaa ya mwili (1 Wakorintho 7:2-9; Mithali 18:22).

uk. 15

Wanawake katika Biblia

Diocese-Based TEE, Kenya Mennonite Church, Kanisa la Mennonite Tanzania ©2014 Gloria Bontrager, Theological Education Coordinators

Maswali ya Majadiliano:

1. Ni kwa njia zipi tuanweza kutayarisha vizuri zaidi mioyo ya watoto kumpokea Mungu katika maisha yao?

2. Fikiria na kujadili maneno hayo, je, ni kweli? “Zawadi nzuri zaidi baba awezaye kuwapa watoto wake, ni kumpenda mke wake.”

3. Biblia inamaanisha nini, kunyenyekeana kwa kila mmjoa? Soma Waefeso 5:21.

4. Je wanwake kutii na kuheshimu mamlaka ni vigumu zaidi kuliko wanaume?

5. Je, kumpenda mwingine kama unavyojipenda mwenyewe ni vigumu zaidi kwa mwanamune kuliko mwanamke?

6. Ni mambo gani na matendo gani yanayoonyesha upendo wa Kristo kwa kanisa? Inawezekanaje yakawa kielelezo katika ndoa zetu?

7. Ni katika njia zipi, tunafundisha watoto wetu kuttii? Je, ni vizuri kumlazimisha mtoto kututii?

8. Tunawezaje kujenga mtazamo mzuri wa ngono bila kuathiri heshima yake inayostahili? Tunafundishaje watoto kuhusu ngono?

9. Je, utamsaidaje mume wako ukiona anaanza kubadilika na kuwa mtu asiyekujali?

10. Mfano wa kwanza wa mahari katika Biblia ni Mwanzo 24:42-44, 50-53. Je, ni lazima kuwepo mahari? Faida ya mahari ni nini? Hasara ya mahari ni nini? Je, utafanyaje kama binti yako anataka kuolewa bila mahari?