1
MUHUTASARI WA HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA WENYEVITI WA
KAMATI ZA KUDUMU ZA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA
2015/2016
Mheshimiwa Spika,
Kwanza naomba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutukutanisha tena
hapa tukiwa wazima wenye afya njema, katika kipindi hiki muhimu cha kujadili Bajeti
kuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Bajet hii
itakua na Umuhimu mkubwa kwani itakuwa ni Bajeti ya mwisho katika uhai wa Baraza
hili la Nane ambalo wewe Mheshimiwa Spika kwa kushirikiana na wasaidizi wako
mmeliongoza kwa ufanisi mkubwa tokea lilipozinduliwa mnamo mwezi Novemba 2010.
Mheshimiwa Spika,
Makadirio haya ya Bajeti yaliyowasilishwa na Mhe Waziri wa Mipango na Waziri wa
Fedha juzi siku ya Jumatano ya tarehe 13/05/2015, hivi sasa wananchi kwa hamu kubwa
wanataka kujuwa yanawagusa kwa kiasi gani, kwa kuwa bajeti siku zote huwa ni suala la
wananchi na maisha yao moja kwa moja yanaguswa na mipango inayohusu mahitaji ya
jamii kama vile kilimo, afya, elimu, miundombinu n.k wananchi watataka pia kujuwa
bajeti yao hii imezingatia kiasi gani vipaumbele katika maendeleo ya nchi.
2
Mheshimiwa Spika,
Serikali yoyote duniani lazima iwe na malengo yake na mipango yake sisi kama wajumbe
kuanzia leo hii tutapata nafasi ya kuyachambua malengo na mipango ya Serikali yetu ili
kuweza kuishauri vizuri Serikali yetu kwa faida ya Nchi yetu na Wananchi wetu. Katiba
yetu ya Mwaka 1984 imeweka msingi huo wa lengo kuu la Serikali kama zilivyo serikali
nyengine, ambalo katika Kifungu cha 9 (2) (b) cha Katiba ya Zanzibar imeelezwa kuwa
usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndiyo lengo kubwa la Serikali. Hivyo ni
sawa na kusema kuwa mipango yetu, dira za maendeleo, ilani za vyama vyetu kadiri
zitakavyokuwa na mipango mizuri na mikakati mbali mbali lazima zifuate msingi huu wa
kikatiba wa kuwapa wananchi usalama wao na hali nzuri katika maisha yao.
Mheshimiwa Spika,
Kwa maana hiyo sasa, Kamati yangu imezingatia vizuri Bajeti iliyoletwa na Serikali kwa
mwaka wa Fedha 2015/2016 pamoja na vipaombele vyake. Tutakumbuka kuwa katika
bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika mwezi Juni, 2015 Serikali imejiwekea malengo
makuu ya kujenga jamii iliyoelimika kwa elimu bora na inayotoa wataalamu wenye
hadhi ya Kimataifa, yenye siha, iliyoimarika kiuchumi na inayojali umoja wa kitaifa na
kufuata misingi ya utawala bora.
Mheshimiwa Spika,
Mambo hayo yote kwa pamoja yanajenga falsafa iliyomo katika Dira ya Maendeleo ya
2020 ambayo utekelezaji wake umo katika MKUZA II na Mpango wake wa utekelezaji.
Ukitazama katika bejeti za miaka minne iliyopita ya 2011/2012, bajeti ya mwaka
2012/2013, bajeti ya mwaka 2013/2014, 2014/2015 na hatimaye bajeti ya mwaka
2015/2016 ambapo malengo na vipaombele vyake vinafanana au ni sawa na kusema ni
vile vile.
3
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaona kuwa si vibaya kuwa na malengo yanaofanana wakati tumekusudia
kuwa na muelekeo wa kustawisha jamii yetu kupitia malengo hayo lakini ni vyema basi
katika bajeti zetu tueleze ni kwa kiasi gani tumeweza kutekeleza lengo moja na jengine,
na wapi tumekwama na lengo gani tumeshafikia hatua nzuri ya kulitimiza. Kwa kufanya
hivyo tungelijuwa na wananchi wakaelewa kuwa katika bajeti ya mwaka huu
tumebakisha lengo gani kulitimiza ili tuangalie na mambo mengine.
MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI MWAKA 2015 NA MPANGO WA MAENDELEO
MWAKA 2015/2016.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya utangulizi huo mfupi naomba sasa nielekee katika maoni ya Kamati kuhusu
Mapitio ya Hali ya Uchumi mwaka 2014 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka
2014/15 pamoja na Mwelekeo wa Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2015 na Mpango wa
Maendeleo mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Spika,
Katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2015/16 uliowasilishwa na AR Ikulu na
Utawala Bora, imeripotiwa kukuwa kwa uchumi ambako kumeenda sambamba na
kuimarika kwa ustawi wa wananchi. Kamati yangu katika kuchambua hali ya ukuaji wa
uchumi kwa kuzingatia Mpango wa Utekelezaji wa Mkuza II imeona kuwa taarifa hizi ni
nzuri lakini hazijitoshelezi kuleta tafsiri halisi ya hali za wananchi kuimarika kiuchumi.
Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa mambo yaliyoelezwa ni kuongezeka idadi ya wananchi waliounganishwa
na huduma ya umeme katika gridi ya taifa kutoka watu 8,126 mwaka 2013 hadi kufikia
watu 10,410 mwaka 2014 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 28. Kwa tafsiri ya
kawaida utaona kweli kuwa nambari zimeongezeka lakini tafsiri halisi ya nambari hizo
4
haisemi ni kwa namna gani hali ya uchumi ya mwananchi imekuwa baada ya ongezeko
hilo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imeona kuwa kwa kuwa lengo la Mkuza II ni kustawisha hali za wananchi
na kuimarisha uchumi, tafsiri ya ongezeko hilo halionekani hapa kwa mfano bado
mwananchi wa kawaida aliyeunganishwa na gridi ya taifa, kama ilivyoelezwa hapo juu
analipa kodi ile ile ya 16% ya VAT anayolipa mfanyabiashara ingawa matumizi
yanatofautiana, hali kama hii bado inaonyesha mwananchi huyu analipa gharama kubwa
za maisha na kurejesha nyuma ustawi wa maendeleo yake ambapo siyo lengo la Mkuza
II. Mhe Spika, kamati yangu inaiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapunguzia
wananchi malipo ya V.A.T ili kupunguza makali ya maisha kwa wananchi wetu wengi
ambao hutumia huduma ya umeme kwa matumizi ya kawaida ambayo sio ya biashara,
na kuongeza udhibiti kwa waekezaji wakubwa hasa wenye Viwanda na Mahoteli ambao
Kamati yangu inahisi huko ndiko umeme mwingi unatumika bila ya kulipiwa bili
inayostahili jambo ambalo tunahisi mapato mengi ya Shirika la Umeme yanapotea,
ambapo mzigo huo hubebeshwa wananchi bila ya kujua. Kwa hiyo tunalitaka Shirika la
Umeme kuhakikisha Mahoteli yote ya Kitalii yanaekewa mita za Tukuza ambazo
tunaimani zinasaidia kudhibiti upotevu wa malipo ya Umeme.
Kimsingi ni kweli katika bara la Afrika, Zanzibar ni Nchi pekee iliyoweza kuwafikishia
wananchi huduma muhimu ya umeme kwa asilimia kubwa zaidi hadi vijijini na ni kweli
imeweza kuwasaidia kuinua kipato chao na pia kuibua ajira mpya kupitia matumizi ya
umeme, lakini pia tunalipongeza Shirika la Umeme “ZECO” kwa kukubali ushauri wetu
wa kuwaungia Umeme wananchi kwa njia ya mkopo jambo ambalo limewasaidia
wananchi wengi kuweza kuunga umeme ambao baadhi yao wameanza kwa kuutumia
kwa shughuli mbalimbali za biashara. Kwa hiyo tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kufika vijijini na kuwaelezea wananchi matumizi bora ya
5
huduma ya Umeme kwa ajili ya uzalishaji ili kuwaongezea kipato na isiwe kuwashia taa
tu peke yake.
Mhe Spika, lakini pia kwa Program mpya za Serikali hivi sasa katika PBB je tujiulize katika
Program ya usambazaji wa Umeme mijini na vijini kumepatikana mafanikio
“OUTCOME” gani hadi hivi sasa, kimsingi Kamati yangu imekubali kuwa mafanikio ya
upatikanaji wa huduma ya Umeme imefanikiwa kwa asilimia 80. Kwa hiyo tunaiomba
Serikali kupitia Shirika la Umeme basi kuhakikisha hiyo asilimia 20 ya usambazaji wa
huduma ya umeme iliyobaki ikamilishwe katika Bajet hii inayofuata. Lakini pia
Mtakwimu Mkuu wa Serikali afanye tathmini baada ya wananchi wote kufikiwa na
Umeme katika maeneo yao je umasikini umepungua kwa kiasi gani katika maeneo
mapya yaliyofikiwa na huduma ya umeme.
Mheshimiwa Spika,
Kwenye Sekta ya Elimu, Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2015/16, pia kumeelezwa
wastani wa uwiano wa walimu kwa wanafunzi walioorodheshwa katika shule za msingi
za Serikali na binafsi kuwa umeendelea kuwa 1:26 sawa na mwaka 2013. Ukiangalia
wastani huu unaridhisha kwa kuwa hatua hii inasaidia mwalimu mmoja kufanyakazi yake
kwa ufanisi na kuweza kutoa elimu bora.
Lakini kama nilivyotangulia kusema kuwa uwiano huu ni nyenzo ya kufikia kwenye
elimu bora, bado mpango wa maendeleo haujatafsiri kwa uhalisia uwiano huo umeleta
matokeo gani tokea mwaka 2013 hadi mwaka huu wa bajeti, ili tuweze kuona ni kwa
kiasi gani tumepiga hatua katika elimu bora ya msingi. Ninachokusudia kusisitiza hapa ni
kuwa tunapoeleza Mipango yetu tuonyeshe na matokeo yake ambayo yatasaidia
kujitathmini katika kupanga mipango mengine. Lakini pia kamati yangu imeona katika
uwiano wa waalim na wanafunzi umeelezwa kwa ujumla lakini bado kuna baadhi ya
Skuli walimu wanazidiwa sana na idadi ya wanafunzi jambo ambalo huwatwika mzigo
mkubwa walimu lakini pia na kuwanyima fursa nzuri wanafunzi kupata usimamizi mzuri
kutoka kwa walimu wao, tofauti na wanavyopata wanafunzi wenzao.
6
Mheshimiwa Spika,
Sambamba na hilo, Mpango wa Maendeleo pia, umeeleza kuhusu kuongezeka idadi ya
Skuli za Msingi na Sekondari kutoka 392 mwaka 2013 hadi 407 mwaka 2014 kwa Skuli
za Serikali na Skuli 94 mwaka 2013 hadi skuli 99 mwaka 2014 kwa Skuli binafsi. Kamati
yangu ingetaka kujuwa katika ongezeko hilo tumefikiaje malengo ya Dira ya Maendeleo
2020 na Mkuza II, tarakimu za ongezeko hilo hazielezi tulivyofikia malengo kwenye
elimu ya msingi na Sekondari ya kiasi gani elimu yetu imekuwa bora kuanzia ngazi ya
msingi. Hakuna matokeo yaliyoelezwa, kwa mfano, ongezeko hilo limesaidiaje
kuwezesha kila mwanafunzi aliyefikia umri wa kuanza skuli amepata fursa hiyo na
maeneo gani hayajafikia malengo hayo. Kwa hiyo tunaitaka Wizara ya Elimu wakati
watakapokuja kusoma Bajet yao watutolee ufafanuzi kuhusiana na suala hili.
Pia kamati yangu inaishauri Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu
kutokuridhika na idadi ya Skuli na idadi ya wanafunzi walioweza kupata Elimu ya msingi
tu bali kujielekeza sasa na kuandaa mitaala ya kutoa Elimu ya Amali kwa Vyuo vya
Serikali kwa kuvipatia vifaa vya kutosha vya kufundishia kwa kuviimarisha vyuo hivyo
pamoja na Skuli za taaluma ya Ufundi, Afya, Utalii, Kilimo, ili kutoa Elimu bora na
baadae kutoa wahitimu bora katika fani tofati hapo ndio tutakapoona faida ya vijana
wetu wasomi, ambao watakua ndio wataalamu katika mashirika na Makampuni yote
yatakayoamua kufanyakazi Zanzibar. Pia kuimarisha Karakana zetu ili kutoa huduma
bora inayostahiki jambo ambalo litaipunguzia sana mzigo Serikali katika matengenezo ya
magari na zana nyingine za Serikali.
Samba na kuanzisha mitaala ya Elimu ya Kujitegemea katika shule zote za Zanzibar ili kila
mwanafunzi anaemaliza Elimu ya awali basi aweze kua na elimu ya kazi ya mkono
ambapo akiamua kuanzisha shughuli yeyote ya kujiajiri yeye mwenyewe basi dhima yake
kubwa iwe ni kutafuta mtaji wa kuanzisha biashara jambo ambalo vijana wengi watakua
wajasiria mali na kupunguza wimbi la vijana wasiokua na ajira mitaani, na huo umasikini
ndipo tutakapoweza kuupiga vita au kuumaliza kabisa.
7
Mheshimiwa Spika,
Hali ni kama hiyo katika elimu ya juu, ambapo Mpango wa Maendeleo umeeleza idadi
ya wanafunzi waliopata mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka wanafaunzi 881
iliyogharimu Tsh. 5.22 bilioni mwaka 2012/13 hadi wanafunzi 1,467 iliyogharimu Tsh.
6.42 bilioni mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika,
Tarakimu hizo ni nzuri lakini haziotowi picha halisi ya malengo tunayotaka kufikia ya
kusomesha vijana wetu wengi katika elimu ya juu na kuwa na wataalamu wenye uwezo
katika sekta mbali mbali. Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2015/16 haujaeleza wazi
ni idadi ya wanafunzi wangapi wameomba mikopo katika kila kipindi na kati ya hao ni
idadi gani ya wanafunzi wamepata mikopo hiyo, na wangapi walikosa na ni asilimia
ngapi? vile vile kwa kuwa katika kipaumbele chetu cha elimu tunajielekeza kuwa na jamii
iliyoelimika na inayotoa wataalamu wenye hadhi ya kitaifa na kimataifa kama Dira ya
Maendeleo ya 2020 na Mkuza II zinavyoeleza, bado katika mipango yetu hailezi wazi
idadi ya wanafunzi tuliowakopesha miaka ya nyuma ni wangapi wamehitimu na katika
fani zipi, na fani za aina gani bado tuna mapungufu na tunahitaji kuwekeza zaidi, kama
Program mpya ya PBB inavyotaka kuwa tuangalie ( INPUT, ACTIVITIES, OUTPUT na
OUTCOME ). Sasa hapa tunahitaji kuona Outcome ya wasomi wtu katika malengo yetu
ya Milenia.
Lakini isitoshe ni vyema tunahitaji tuone Serikali imeandaa mipango gani ili kuhakikisha
vijana wetu wote wanaohitaji mikopo ya Elimu ya juu wanafanikiwa kupata mikopo
hiyo, kwani lengo la kuboresha huduma za Elimu ni kupata wataalam wanaotosha na
wengine kutoa nje kusaidia wenzetu waliokua na upungufu.
Mhe Spika, tunajua lengo la Serikali la kutoa Mikopo ya Elimu ya juu ni kuhakikisha kila
mwenye uwezo wa kusoma asome bila ya vikwazo, sasa Serikali imejipanga vipi
kushirikisha taasisi binafsi ikiwemo kuzishirikisha Sekta binafsi kushiriki katika kutoa
mikopo hiyo ikiwemo mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Mabenki, na taasisi nyingine za fedha.
8
Mhe Spika, Serikali kila mwaka inatoa fedha kwa ajili ya mfuko wa Elimu ya Juu basi pia
tunaitaka Wizara ya Elimu itueleze mipango yake ni hadi mwaka gani mfuko huu
utaweza kujitegemea kama ulivyokusudiwa kwani Kamati yangu inaamini mfuko huu
umetakiwa kuwa ni ( REVOLVING FUND) sio kila siku kuingizwa fedha bila ya kikomo,
kwa hiyo iko haja ya Bodi ya Miokopo ya Elimu ya juu kuweka utaratibu maalumu wa
usimamizi na ufuatiliaji wa urejeshaji wa mikopo hiyo kwa kuweka (DATABASE) ya
wanafunzi waliopata mikopo ili kufuatilia urejeshaji wake. Mhe Spika kamati yangu
inaamini Bodi ikiweza kuusimamia vizuri mfuko huu basi hapo baadae mfuko huu utakua
na pesa za kutosha na pia kuweza kuziekeza katika mifuko mingine au kuziekeza katika
kununua hisa kwa ajili ya kuzizalisha.
Mhe Spika, kamati yangu inashauri kua lengo kuu la kutoa mikopo ya Elimu ya juu iwe
ni kupata wataalamu wa kutosha lakini pia iwe na lengo jingine la kuwadhibiti wataalam
(KUMAINTAIN) ili wabakie nchini kuwatumikia wananchi, lakini kuwe na utaratibu
maalum wa kuwalipa maslahi mazuri na kuwapatia vitendea kazi vya kutosha ili waweze
kuzitumia vizuri elimu zao na kuleta tija iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika sekta ya afya nako, Mpango wa Maendeleo haujaeleza matokeo ya ustawi kama
yanavyojieleza katika Mpango wa Utekelezaji wa Mkuza II, katika taarifa yake
Mheshimiwa Waziri ameeleza kuimarika kwa utoaji huduma katika sekta ya afya kwa
kuongezeka madaktari kutoka 40 mwaka 2013 hadi 90 mwaka 2014, na wataalamu wa
Maabara kutoka 212 mwaka 2013 hadi 235 mwaka 2014, vile vile katika Mpango huo
kumeelezwa kuongezeka kwa watabibu kutoka 185 mwaka 2013 hadi 194 mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika,
Katika maelezo hayo yote yanayokusudia kutekeleza hatua za ukuaji uchumi ambao
unakwenda sambamba na ukuaji wa ustawi wa jamii katika eneo hili la afya, ambalo
hakuna atakaebisha kuwa ongezeko hilo lina faida kubwa kiuchumi, lakini Mpango
haujaleza ni kwa kiasi gani ongezeko hilo limesaidia kupunguza vifo vya mama
9
wajawazito, vifo vya watoto wachanga, na watoto wadogo wa chini ya umri wa miaka
mitano ambavyo kama ilivyoelezwa kwenye Mkuza tushuke kutoka vifo 48 vya watoto
wanaozaliwa kati ya 1000 wanaozaliwa. Aidha, ongezeko hilo la madaktari, watabibu
na wataalamu wa maabara halijaeleza ni kwa kiasi gani limeweza kukabiliana na maradhi
na kuweza kuwasaidia wananchi kujua mapema matatizo ya afya yanayowakabili.
Mhe Spika, kamati yangu inaipongeza Serikali kwa kuweka miongoni mwa vipau mbele
vyake kuwa ni suala huduma za Afya na ni kweli tumeona jitihada kubwa zikifanyika,
lakini bado kuna changamoto nyingi katika sekta hii ili kufikia yale malengo ya
Mapinduzi yetu matukufu ya Afro-Shirazi ambayo yamerithiwa na CCM ya kuwapatia
huduma za Afya wananchi wote bila ya malipo, kwa hiyo kamati yangu inaishauri
Serikali kupitia Wizara ya Afya, kuhakikisha lile lengo la kuifanya Hospitali ya Mnazi
Mmoja kuwa Hospitali ya rufaa likamilike ,kwani hivi sasa bado kuna huduma nyingi
hazipatikani ipasavyo hapo Hospitalini, kwa mfano huduma ya X-RAY haiko sawa kwani
ni machine moja tu ndio inayofanya kazi na uwezo wake ni mdogo na wahitaji wako
wengi, kwa hiyo tunaitaka Wizara katika Program ya mwaka huu kuhakikisha ile
Machine kubwa ya X-RAY iliyoharibika itengenezwe kwani inayo uwezo mkubwa mara
mbili ya ili ilikuwepo hivi sasa , na kamati yangu inayo taarifa kua katika nchi za Afrika
machine za aina ile ziko mbili tu Zanzibar na Misri kwa hiyo tunaamini ikitengenezwa
itasaidia kutimiza lengo la kuifanya ni Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa Rufaa kweli, pia
bado katika kitengo cha (EMERGENCY) hakuna madawa va vifaa vya kutosha inabidi
wagonjwa waende wakanunue dawa kwenye Pharmacy sasa tujiulize ikiwa imetokezea
mgonjwa hana jamaa je hizo dawa atanunuliwa na nani? wakati Hospitalini hapo
hazipatikani, kutokana na muda hayo ni baadhi tu ya mambo tu ya kuyashughulikia
miongoni mwa mengi ambayo yanahitaji kuyashughulikia ili kuifanya iwe kweli ni
Hospitali ya Rufaa. Kwa hiyo kamati yangu inataka kwa mipango ya mwaka huu wa
2015/16 tunataka kuona (OUT-COME ) ya Hospitali ya Mnazi Mmoja je tumeweza
kufikia kuiwezesha kuwa ya Rufaa? vinginevyo Manager wa Mradi itambidi aje
kuwajibika pamoja na Waziri muhusika. kwenye mwisho wa mwaka wa bajet ijayo.
Pamoja na hayo lakini tunapongeza kwa jitihada zinazochukuliwa kuongeza na
10
kuboresha huduma za Afya hapa Zanzibar, pia sambamba na hilo kuzingatia maslahi ya
Madaktari wetu pamoja na wauguzi ili wawezekufanya kazi zao kwa utulivu na ufanisi
mkubwa.
Mhe Spika, pamoja na changamoto zilizopo tunaipongeza Serikali kuendelea kuthibiti
ongezeko la maradhi ya Malaria jambo ambalo limewafanya wananchi wengi kuimarika
afya zao, kwa hiyo tunatoa wito kwa wananchi kuimarisha usafi katika makaazi yao ili
kuondoa mazalio ya mbu wanaosababisha homa ya Malaria.
Mhe Spika, pamoja na mafanikio hayo kumejitokeza tatizo jingine la kuongezeka kwa
kasi kubwa kwa Maradhi ya KISUKARI na PREASURE hapa Zanzibar na kupelekea
kusababisha vifo vingi na kuwaacha baadhi ya wananchi na ulemavu wa viungo kwa
kukatwa baadhi ya viungo vyao kutokana na maradhi ya KISUKARI. Kwa hiyo
tunaiomba Serikali kama ilvyochukua jitihada katika kutokomeza maradhi ya Malaria na
tukawatunatolewa mfano Duniani basi sasa nguvu kubwa zaidi ipelekwe katika kudhibiti
maradhi haya ya KISUKARI na PREASURE.
Mheshimiwa Spika,
Mipango yetu ya Maendeleo siku zote inalenga kustawisha hali za wananchi kama
nilivyotangulia kusema. Katika huduma za kijamii bado mwananchi anakwazwa na
gharama kubwa za kupata huduma za lazima kama chakula, maji, afya, umeme,
mawasiliano n.k. Mpango wa Maendeleo umeonesha kuwa Mchango wa sekta ya
huduma katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 41.5 mwaka 2013 hadi kufikia
asilimia 44.7 mwaka 2014 kutokana mchango wa sekta za kifedha, uwekezaji katika
majengo, taaluma, ufundi, habari na mawasiliano. Hata hivyo ukuaji huo bado haujaleta
athari ya moja kwa moja katika pato la mwananchi wa kawaida.
11
Mheshimiwa Spika,
Hilo linakwenda sambamba na mfumko wa bei kwa bidhaa na huduma ambao
umepanda kutoka asilimia 5.0 mwaka 2013 kufikia asilimia 5.6 mwaka 2014 hasa katika
bei za chakula. Hali hiyo bado haijadhibitiwa, kamati yangu inashauri kuwa Serikali
lazima iweke udhibiti wa ukuaji huu kwa kutowaachia wafanyabiashara kuendesha soko
huria wanavyotaka. Tumeona katika sekta ya nishati, bei ya mafuta na upatikanaji wake
imekuwa shida mara kwa mara katika siku za hivi karibuni suala hili nalo pia lipatiwe
ufumbuzi wa kudumu. .hivi sasa kumekua na kupanda na kushuka kwa bei ya matuta
ndani ya kipindi cha miezi miwili tu hili jambo la hatari sana kwa uchumi wa nchi yoyote
haya yanaleta usumbufu katika upatikanaji wa huduma za lazima kwa mwananchi wa
kawaida, na suala hili linaweza pia kuivuruga bajet ya Serikali kwani tunapitisha pesa
nyingi kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya magari na viwanda pia.
Mhe Spika, suala la bidhaa na huduma muhimu ikiwa Serikali haikujitahidi kudhibiti
upandaji wa bei zake basi hata Serikali ikiongeza kiwango cha Mshahara basi itakua ni
bure kwani purchasing power ya fedha hizo zitakua haziendani ya bei za huduma na
bidhaa katika soko kwa hiyo Serikali iangalie uwezekano wa kuboresha, kudhibiti na
kupunguza bei za huduma na bidhaa muhimu kwa maisha ya kila siku, ili kuongeza
perchessing power kwa kipato cha wananchi.
Mhe Spika, pamoja na hayo kwa kulinganisha maisha ya kawaida ya wananchi katika
bara la Afrika Zanzibar wananchi wanaishi maisha mazuri hadi vijijini kuliko nchi nyingi
za Afrika kwani huduma muhimu ikiwemo barabara, Shule za msingi na Sekondari,
umeme, maji, vituo vya Afya, huduma za fedha, ikiwemo Mabenki Tigo pesa, Easypesa,
M-pesa. Airtel Money n.k. hizi zote ni huduma ambazo katika nchi nyingi za Kiafrika
hazipatikani kwa karibu vijijini, ila ni mijini tu, Mhe Spika, tatizo ambalo wananchi wengi
wanafikiria kuwa ukuaji wa uchumi kua haulingani na kipato cha mwananchi wa
kawaida, ni kwa sababu wanapenda kulinganisha maisha baina yao kwa kipato na
jingine ni kwamba pesa haikai mifukoni kwani kila kitu au bidhaa unayoihitaji
inapatikana katika soko, na kwa kuwa watu wengi hupenda kuboresha maisha yao basi
12
akipata pesa huimarisha aidha makaazi yao, kununua usafiri wao binafsi, kununua mavazi
mazuri, haya ndiyo yanayosababisha kuona pesa haitoshi lakini wanashindwa
kulinganisha maisha walioshi wazee wao huko miaka ya nyuma kulingana na wanayoishi
wao hivi sasa, ukiangalia kiasi miaka kumi nyuma vijijini katika kijiji unaweza kumkuta
mtu mmoja tu ndie anaemiliki simu ya mkononi, lakini leo hii karibu kila nyumba tatu
basi lazima utawakuta watu wanaomiliki simu za mkononi, pia vijiji vingi hapa Zanzibar
kulikuwa hakuna watu wanaomiliki Gari za kwao wenyewe labda Gari za Ushirika
walizopewa na Serikali, lakini leo hii vijiji zaidi ya asilimia 80 wamo watu wanaomiliki
Gari zao wenyewe, hiyo ni baadhi ya mifano kuwa Pato la Taifa linapokua basi
linachangia kukua kipato cha wananchi wa kawaida na kuimarika kwa maisha yao.
Mheshimiwa Spika,
Umefika wakati Serikali iwezeshe Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati (ZURA), ambao sheria
yake imepitishwa hivi karibuni na Baraza hili tukufu, kufanyakazi yake kudhibiti mtindo
huu wa wafanyabiashara wa mafuta kuhodhi soko la mafuta kwa kuwa wao peke yao
ndiyo waagizaji, wasambazaji na wauzaji reja reja, kamati inashauri mtindo huu
ukiachwa kama ulivyo tatizo la upatikanaji wa nishati ya mafuta litaendelea na kuathiri
upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi. Aidha, kamati inaishauri Serikali kuwa na
miundombinu yake ya akiba ya mafuta (GOVERNMENT DEPORT) pindi inapotekea
upungufu kwa namna yoyote ile basi iweze kuingiza mafuta kwenye soko ili kusaidia na
kuepusha usumbufu kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Jambo jengine muhimu kamati yangu inataka kulisema kwa msisitizo ni bajeti yetu katika
kuhudumia mahitaji ya lazima kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Waziri. Katika hili
kamati yangu imetambuwa kuwa Malengo ya Mkuza II yameweka wazi namna Serikali
13
inavyoweza kujitoa katika kufanya kila jambo na kuziacha Serikali za Mitaa kufanya
majukumu hayo.
Mheshimiwa Spika,
Mpango mzuri uliowekwa katika Mkuza II wa kukasimisha (ugatuzi) madaraka katika
Serikali za Mitaa, kama ungefanyika mapema, ungesaidia sana kuipunguzia Serikali mzigo
mzito wa kupanga bajeti kwa kila jambo katika ngazi ya Serikali kuu.
Mheshimiwa Spika,
Katika Mpango wa Utekelezaji wa Maendeleo wa Mkuza II imewekwa vizuri dhana
kukasimu (ugatuzi) madaraka kwa serikali za mitaa (D by D) yaani (Decentralization by
Devolution). Mpango huu umo kwenye Mkuza lakini utekelezaji wake unahitaji
kusimamiwa na hivi sasa sheria zimeshatungwa kwa ajili ya kushurutisha utekeleza wa
Sera na malengo hayo.
Kamati yangu inaomba Serikali kuzingatia kwa makini na kuziwezesha Serikali za mitaa
zikafanyakazi kwa uhuru lakini kwa mujibu wa Sheria kwa lengo la kuisaidia Serikali kuu
katika kuteleza vipaumbele vyake vya afya, elimu, maji, miundombinu, biashara na
uwekezaji wenye tija.
Mhe Spika, suala la utawala wa Serikali la Mitaa ni jipya ingawa sehemu kubwa ya
watendaji ni walewale kwa hiyo yatahitajika mafunzo ya kutosha katika kuibua,
kutekeleza na kusimamia mipango na miradi yote iliyopangwa na itakayoibuliwa na
wadau mbali mbali katika kila halmashauri na Mabaraza ya Miji. Kwa hiyo kwa kua
Serikali kwa makusudi imeamua kukasimu madaraka kwa Serikali za mitaa basi itoe uhuru
wa kutosha kwa wakurugenzi wa Halmashauri na mabaraza ya miji kuonyesha uwezo
wao katika kuibua na kuisimamia miradi hiyo kikamilifu bila ya usumbufu kwa mujibu
wa Sheria na Kanuni kama zitakavyoeleza, kamati yangu inawataka viongozi wote wa
Halmashauri na Mabaraza ya Miji kuwa waadilifu na fedha watakazotengewa pamoja na
kua na uadilifu katika kuingia mikataba kwa miradi yote mikubwa na midogo
14
watakayoiibua kwatika maeneo yao, hili likifanyika tunaamini litaharakisha maendeleo
kwa haraka hapa Zanzibar na kuongeza kipato kwa wananchi wetu na kupata huduma
bora kwa unafuu na kwa urahisi.
Mhe Spika, kamati yangu inaiomba Tume ya Mipango kusimamia kikamilifu miradi yote
itakayoibuliwa na Halmashauri na Mabaraza ya Miji hasa katika matumizi bora ya ardhi
kwa kuzigatia ardhi ya Zanzibar ni ndogo kwa hiyo kuhakikisha hakutotokea migongano
kwa matumizi ya ardhi na mipango ya maendeleo ya kitaifa na ile ya Halmashauri, kwa
hiyo ni vyema kuyatangaza maeneo yote ya hifadhi ya Taifa, maeneo ya vianzio vya
maji, lakini pia maeneo ya Kilimo ili shughuli za maendeleo zisijekutuletea changamoto
nyingine katika matumizi ya ardhi.
MAONI YA KAMATI KUHUSU MAKADIRIO YAMAPATO NA MATUMZI YA SERIKALI
KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016
Mheshimiwa Spika,
Naomba sasa nielekeze maoni ya Kamati yangu katika Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016, bajeti ambayo imewasilishwa
mbele ya Baraza lako na Mheshimiwa Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya mwaka huu ni tofauti sana na bajeti zilizotanguliwa kujadiliwa nakupitishwa na
Baraza hili. Bajeti hii imekuja katika Mtindo mpya kwa kuwa ni bajeti inayozingatia
Programu za Maendeleo. Itakumbukwa kuwa kuanzia mwaka 2011/12 Serikali ilianza
matayarisho ya maandalizi ya mfumo wa mageuzi ya bajeti yenye lengo la kuimarisha
uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa bajeti, ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa bajeti.
Lengo kubwa ambalo kamati yetu tunakubaliana nalo katika mpango huu mpya ni
kuhakikisha kuwa kila shilingi inayoidhinishwa na Baraza na kutumiwa na Serikali iwe
inaleta manufaa kwa walengwa na wananchi kwa ujumla. Tena kwa kuzingatia Program
iliyokubaliwa na Baraza la Wawakilishi.
15
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kuwa na mfumo mpya wa bajeti ambayo inazingatia programu, lakini bado
bajeti yetu inaendelea kuwa ya makusanyo kwanza na kutumia baadaye (cash budget).
Katika mtindo huu wa bajeti inailazimu Serikali kuwa na vyanzo vya uhakika vya
kukusanya kodi na mpango madhubuti wa kudhibiti uvujaji wa makusanyo hayo. Mara
nyingi katika bajeti zetu kinachokadiriwa kukusanywa sicho kinachopatikana, aidha,
kinachotumika huwa ni kikubwa zaidi kutoka na sababu mbali mbali.
Mhe Spika, kama alivyotoa ufafanuzi Waziri wa Fedha kuhusu hali ya Uchumi wetu
katika kipindi kinachoishia june 2015, kwamba uchumi wetu kwa mwaka 2014
umeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 7.0 kulinganisha asilimia 7.2 ya mwaka 2013,
ambapo pato la Taifa la kila mtu limeongezeka kufikia wastan wa 1,552,000 sawa na
USD 939, 2014 kulingana na 1,384,000 sawa na 866 mwaka 2013.
Mhe Spika, kwa kuangalia kijumla kwa miaka 5 ya Serikali hii ya awamu ya saba
inayoongozwa na D.k A.M. Shein uchumi wetu umeendelea kukua kwa wastan wa
asilimia 6.3 kwa mwaka ambapo pato la Taifa limekua kwa wastan kutoka 848.2 Bil.
hadi kufikia 1,115.4 Bil. Sawa ma kasi ya 31.5 kwa mwaka, ambapo pato la mtu
mmojammoja, pia limekua kutoka 856,000 mwaka 2010 hadi kufikia 1,552 (939) kwa
mwaka 2014 .
Mhe Spika, kutoka mwaka 2010/11 hadi 2014/15 mapato ya ndani yamongezeka kutoka
181.4 Bil. Kufikia 360.4,Bil mwaka 2014/15 sawa na ukaji wa asilimia 98.7 kwa miaka 5
ambapo ni sawa 19,7 kwa kila mwaka, Mhe ongezeko hili ni kubwa na linatia moyo na
mafanikio haya yasingeliweza kufikiwa bila ya kelele na makaripio mbali mbali kutoka
kwa wajumbe wako wazito wa Baraza la Wawakilishi walipoamua kikamilifu bila ya
kujali tofauti zao za kisiasa na KUISIMAMIA Serikali kikamilifu katika kuonyesha maeneo
yaliyokua pesa za Serikali zilimokua zikivuja, ingawa kuna baadhi ya watu wakiwemo
baadhi ya viongozi wasiojua nini wajibu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walikua
wakinuna na kutuona wabaya lakini faida yake leo hii ndio tunaiona kuwa mapato
16
yameongezeka maradufu na udokozi umepungua kwa asilimia kubwa, Mhe Spika, katika
kipindi chote hicho tunamshukuru sana Rais wetu alitulia kimya na wala hakutuingilia
wakati tulipokua tukipiga kelele kuisema ,tukiikosoa na tukiisimamia Serikali yake katika
kupiga vita ubadhirifu wa mali na fedha za umma usatahamilivu wake kwetu leo yeye
mwenyewe anaweza kupanda majukwaani akijinasibu kuwa Serikali yake ndani ya
kipindi alichokabidhiwa kuiongoza Zanzibar Serikali yake imeweza kuongeza ukusanyaji
wa mapato kwa karibu asilimia 98 lutoka kiasi cha Bilioni 181. hadi Bilioni 360 ,hii ni
hatua kubwa ya mafanikio kwa uongozi wake na uadilifu wake kwa Taifa letu kwa hiyo
hatunabudi sote wananchi wa Zanzibar tumpongeze kwa kazi kubwa aliyoifanya na
inafaa tuendelee kumuunga mkono ili atuletee matunda mengi zaidi katika miaka ijayo.
Mhe Spika, mafanikio hayo lazima tujiulize yametokana na nini? Hili ni suala kila mmoja
wetu anapaswa ajiulize na tutafute jawabu ya pamoja ili tuendelee na ukuaji wa mapato
na Uchumi wa Nchi yetu, Mhe Spika, bila shaka mafanikio hayo yametokana hali ya
Amani na utulivu uliopo hapa nchini kwetu, Mhe Spika, lakini mimi nimeanza kua na
wasiwasi kua hali hiyo ya Amani imeanza kuingia mashaka hasa katika kipindi hiki
tunachoelekea kwenye uchaguzi mkuu kwani tumeanza kuona viashiria vya uvunjifu wa
Amani kuanzia humu ndani ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi ikiwa ndio kioo cha
jamii kwani kulianza kujitokeza vurugu wakati Serikali ilipoleta hoja ya taarifa ya sheria
ya kura ya maoni iliyopitishwa na Bunge ifanyekazi na hapa Zanzibar tulianza kuona
mpasuko mkubwa wa Serikali yetu kwani kulitokea zomea zomea kutoka baadhi ya
Mawaziri na Wajumbe kutoka kambi ya Upinzani kuonyesha kua hawaiungi mkono, sasa
suala la kujiuliza kwani mawaziri hawana vikao vyao vya BLM ambapo kama
wanatofautiana kimawazo watofautiane hukohuko lakini cha kushangaza walikuja
kupingana ndani ya ukumbi wa Baraza ambapo ni kinyume na Katiba ya Zanzibar ibara
ya 43(5) inawataka Mawaziri wote kuwajibika kwa pamoja ndani ya Baraza la
Wawakilishi, laikni isitoshe na katika kikao hicho hicho cha Mwezi wa April tulishuhudia
kwa mara nyingine tena Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikatika pande mbili ndani ya
Baraza la Wawakilishi pale ilipowasilishwa hoja ya Mhe Hamaad Masoud kuhusu
vitambulisho vya Uzanzibari pamoja na Kauli ya Serikali iliyotolewa na Mnadhim wa
17
Serikali Mhe Waziri katika afisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kua hoja ile
haina msingi na wananchi wanatakiwa wafuate taratibu za kisheria katika kutafuta haki
zao bila ya kutumia shindikizo la Baraza la Wawakilishi tuliona tena Mawaziri wa pande
zote walitofautiana tena ndani ya Baraza la Wawakilishi ambapo kifungu kilekile cha
43(5) cha Katiba ya Zanzibar kilikiukwa tena hii ni ishara mbaya kwa Serikali hii ya
Umoja wa kitaifa na inaweza kuashiria kua viongozi ambao wao ndio walitunga Katiba
hii ndio hao hao wanaanza kuikiuka Katiba hiyo hiyo.
Mhe Spika, kwa maana hiyo kama anavyotuasa Rais wetu pamoja na Makamo wa Pili
wa Rais kuendelea kuwa wamoja tueke mbali tofauti zetu hasa katika mambo ya msingi
lakini kubwa ni kufuata Katiba na Sheria za Nchi katika kutekeleza majukumu yetu kwani
ikiwa Serikali wenyewe hawaonyeshi Umoja ndaNI YA Baraza kama Katiba inavyoeleza
basi tusitegemee na waliobaki kuwa wataweza kuvumiliana, sasa naomba sisi wenyewe
tuwe mfano kwani isijekua anachelewa Ng’ombe wa mbele akapata bakora Ng’ombe
wa nyuma ambao ni Wawananchi.
Mhe Spika, kama Waziri wa Fedha alivyotuomba mwaka uliopita tumruhusu Serikali
itumie kiasi cha 707.8 Bil.kwa ajili ya kuendeshea Serikali kwa mwaka 2014/15 ambapo
kwa kazi za kawaida T/sh 376.5 na kazi za Maendeleo 331.3 hapa ametuelezea hadi
kufikia March makusanyo halisi yamefikia karibu Bil 275 sawa na asilimia 92.1 kati ya
298.7 Bil zilizotarajiwa matarajio hadi kufikia june yatafikia 375.4 ambapo itafikia kiasi
cha asilimia 93.1 ya makadirio ya mwaka huu.
Mhe Spika, kama alivyoelezea Waziri wa Fedha kuwa matumizi halisi hadi kufikia March,
mwaka huu karibu 369,Bil zimetumika sawa na 52 asilimia ya malengo ya mwaka
ambapo kati ya hizo kiasi 261.2 zimetumika kwa kazi wa kawaida sawa na 96 ya
matarajio. Mhe Spika kama mchanganuo kwenye hotuba ya Waziri inavyoonesha kuwa
Mishahara 74% ,OC 61%, Mfuko Mkuu 69.3% na Ruzuku 65%.
Mhe Spika, kamati yangu haijaridhika kwa kuona kua kwa upande wa OC 61% tu ndizo
zilizoingizwa wakati pesa hizo ndio pesa za kuendeshea shughuli muhimu za mawizara
18
wakati katika mfuko mkuu wa Serikali zimetumika karibu 69.3% hali hii hairidhishi hata
kidogo kwa hiyo kamati yangu inaitaka Serikali kupunguza matumizi yasiyokua ya lazima
na pesa zaidi zielekezwe kwenye OC ili malengo ya mawizara yaweze kufanikiwa kama
wanavyotuomba kila mwaka hapa Barazani, kwa hiyo safari za viongozi zisizokua za
lazima zipungue ili pesa nyingi ziende kuendeshea Serikali. Mhe Spika, kamati yangu
inaitaka Serikali katika Bajeti hii asilimia ya OC iwe ya pili kiasilimia baada ya mishahara
ambayo haiwezi kuepukika.
Mhe Spika, kwa upande wa shughuli za Maendeleo, kwa miezi tisa ni Bil. 108.5 tu ndizo
zilizotumika ikiwa ni 32.7 tu ya lengo hii imetokana na kuendelea kusua sua kwa miradi
ya TERMINAL BUILDING Karume Air-port Zanzibar, BARABARA ZA KATI na Mradi wa
ZUSP, na uzembe huu umesababisha hata kupungua kwa mchango wa Washirika wa
Maendeleo kuchangia miradi hiyo.
Mhe Spika, kwakweli kamati yangu haijaridhika kabisa na kusua sua kwa miradi hii
wakati tunaambiwa ilifanyiwa uchambuzi yakinifu kabla lakini hadi leo miradi
imombioni na haijulikani itakamilika lini ingawa kila mwaka tunaambiwa itamaliza kabla
ya mwaka husika na tunaridhia kwa hiyo tunaitaka Serikali.
Mhe Spika, hali hii ya uzorotaji wa baadhi ya miradi mikubwa hapa Zanzibar
inazorotesha uchumi wa Zanzibar, lakini kuna kila dalili ya kua kuna baadhi ya watu
aidha kwa tama au kwa kutokujua kile wanachokifanya, basi hutafuta Wakandarasi
wabovu au wasiokua na uwezo wa kufanya miradi mikubwa makampuni ya mifukoni
ambayo hushindwa kazi njiani au kujenga chini ya kiwango, na kwa kutahadharisha
Serikali kwa mambo kama haya, kunafunu kua katika mradi wa ZANZIBAR GROUND-
HANDLING katika Uwanja wa ndege wa ABEID AMAAN KARUME kuna taarifa ya kua
tayari makosa kama hayo yameanza kwa kazi hiyo kupewa Kampuni FEKI ambayo kwa
taarifa inasemekana haikushinda Tender, haina uwezo , haina uzoefu, haijawahi
kufanyakazi hata pahala popote Duniani haina kigezo chochote,baya zaidi pia
inavyosemekana hata usajili wake kwa msajili wa Makampuni unautata, baya zaidi
inasemekana kua hata zana walizoleta hapa nchini kwa ajili ya kufanyia ni mitumba
19
ambayo imeshafanyiwa kazi na kampuni nyingine huko falme za Kiarabu, eti kampuni
hiyo ndio inakuja kuanzia kazi kwenye Uwanja wa Ndege mpya wac Kimataifa wa
ABEID AMAAN KARUME ZANZIBAR, kwa kweli ni jambo la kusikitisha sana wakati
kuna makampuni mengi ambayo yaliomba kazi hiyo ambayo yanasifa, uzoefu , ubora na
tungelitarajia zingeliweza kuleta zana mpya zinazolingana na hadhi ya Uwanja wetu
mpya wa kimataifa wa Zanzibar hii ni aibu kwetu Uwanja mpya zana za kufanyia kazi
mitumba, Mhe Spika, tunaitaka Serikali kutupatia maelezo kamili ya mradi huu na uhalali
wa Kapuni hii na kwa hivi sasa kuna tatizo gani katika usajili wa Kampuni hii, Nadhani
wakati umefika kwa Serikali yetu iwaonee huruma wananchi wetu kwa kuwafanyia
mambo mazuri kwani pesa haitoshi hata tukipata ngapi basi tutaona hazitoshi kwani
tunapenda kujitajirisha japo wananchi wakiumia.
Mhe Spika, kamati yanguinaitaka Serikali kuhakikisha katika kipindi kijacho kuifanyia
tathmini miradi yote na kutafuta makampuni yenye ubora na uwezo , pia kuweza
kusimamia na kujua ni kwa muda gani itakamilika, kwani kuchelewa kumalizika kwa
miradi hiyo au kukosa ubora kwa miradi hiyo kunaibebesha Serikali gharama za ziada ili
kukamilisha miradi hiyo na kuubebesha mzigo wa madeni wananchi.
Mhe Spika, kamati imeridhika na hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya
Fedha, za kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa upande wa TRA na ZRB ya usimamizi
wa kimaeneo ( BLOCK MANAGEMENT SYSTEM) kwa kutumia Technologia ya GPS,
uimarishaji wa Uthamini katika maeneo ya Forodha, (VALUATION) ili kujua thamani
halisi ya bidhaa zinazoingizwa nchini. ingawa hapa bado kuna bandari bubu nyingi
ambazo huingiza bidhaa bila ya kulipiwa kodi. Hasa katika kisiwa cha Pemba. Hatua
nyingine Marekebisho ya ada za Bandari ambayo imesaidi kutatua tatizo la madawati
hapa Zanzibar ingawa kamati yangu haijaridhika na usimamizi wa matumizi wa fedha
hizi tunaitaka kamati husika kufuatilia hilo. Na katika hili tunaungana mkono na
mapendekezo mapya ya Waziri kutoza ada hii kuanzia mwaka huu kwa wasafiri
wanaoenda Pemba kwani matunda yake tumeanza kuyaona. Pia hatua kupunguza
misamaha ya kodi ambapo kamati yangu inaitaka Serikali kupitia Wizara ya Fedha,
20
kuangalia misamaha ile tu ambayo itazalisha ajira au kutoa huduma za nafuu kwa jamii.
Mhe Spika, kamati yangu pia inaitaka Serikali kutokuridhika tu na kutoa misamaha ya
kodi lakini ifuatilie matumizi ya misamaha hiyo je inatumika kwa asilimia 100% kama
ilivyokusudiwa? Kwani tunawasiwasi kua kuna baadhi ya bidhaa zinazosamehewa kodi
kwa ajili ya miradi ya uekezaji sehemu Fulani huingia mitaani kwa kuingizwa kwenye
soko kwa kuuzwa jambo ambalo huikosesha Serikali mapato.
Mhe Spika, ili kuweza kuitekeleza kwa ufanisi Bajet inayotumia Program, tunaiomba
Serikali kupitia Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuanza kuweka
utaratibu wa kufungua Account Maalum na kuweka fedha, ili kuweka akiba ya kuanzia
Bajeti ya mwaka unaofuata, ili kufikia lengo la kuwa na akiba ya fedha ya mwaka mzima
wakati wa kupitisha Bajet ya Serikali, na mapato yanayopatikana kwa mwaka ule iwe
kujazia tu bajet hiyo ya mwaka husika hapo ndipo tutakapoweza kuitekeleza vizuri
BAJET INAYOTUMIA PROGRAM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Makadirio ya bajeti ya mwaka 2015/16, Serikali inakusudia kuifanya iwe bajeti
inayotegemea vyanzo vya ndani zaidi kwa vile vyanzo vyengine vya mapato kama vile
misaada ya kibajeti havina uhakika kupatikana kwake na kunaleta athari katika
utekelezaji wa bajeti. Kamati yangu imeliona hili na ingawa Serikali itaweka namna ya
kuzipokea fedha za misaada ya kibajeti zitakapopatikana, lakini utaratibu huu uwe wa
wazi ambao utawezesha ufuatiliaji na kujua kiasi gani kimepatikana na kimetumika katika
mipango ipi. Mhe Spika, katika utaratibu huu kamati yangu inamuomba waziri wa
Mipango pamoja na Fedha, kuweka utaratibu maalum wa kila robo ya Mwaka kukutana
na Kamati ya Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi ili kutoa taarifa ya upatikanaji wa hizo
fedha za GBS au kutokupatikanwa, na kuweza kupatiwa taarifa ya mgawanyo wa fedha
21
hizo katika miradi mbali mbali, kwani tumepitisha Bajeti ambayo inaruhusu mapato
ambayo hayakulengwa MOJA MOJA.
Mheshimiwa Spika,
Changamoto kubwa ya bajeti yetu ni namna ya kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya
ndani na kudhibiti matumizi yasiyozingatia sheria. Kamati yangu imeona kuwa kuna
udhibiti hafifu wa makusanyo sambamba na njia za ukusanyaji wa mapato hayo
zilizopitwa na wakati ambazo makusanyo hufanyika mkono kwa mkono.
Mheshimiwa Sipika,
Makadario ya Bajeti ya mwaka 2014/15 yalilenga katika ukusanyaji mapato katika
vyanzo ambavyo vimezoeleka, ingawa kila bajeti vyanzo hivyo huwa havifikii makadirio
halisi, mfano mapato yasiyokuwa ya kodi, yalikadiriwa kuwa jumla ya Tsh.16.4 bilioni
ambapo hadi mwezi Machi 2015 ni Shilingi Bilioni 12.8 zimekusanywa. Mara nyingi
kamati yangu imeshauri kuwa uwezekano wa kufikia na kuvuka lengo la ukusanyaji wa
mapato hayo upo endapo tutaachana na mtindo wa kukuanya kwa njia za mikoba na
vikapu (CASH COLLECTION) badala yake kutumia mfumo wa kibenki (E-CARD), bado
Kamati yangu inasisitiza kuwa malipo ya ada zote katika huduma zinazotolewa na
Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali, yalipwe kupitia benki ili kudhibiti uvujaji wa
mapato hayo na kuongeza mapato ya Serikali.
Mhe Spika, suala hili linawezekana kwani kuna baadhi ya maeneo kwa mfano, hivi sasa
Air-port kwenye malipo ya VISA na Uhamiaji kupitia malipo ya huduma za Pas-port , pia
baadhi ya malipo kupitia ZRB. Kwa mifano hiyo hili linawezekana.
Mhe Spika, Sasa kwa mifano hiyo tunaishauri Serikali, kuanzisha ada mpya ya malipo ya
ada ya Utalii kwa kutoza ada moja tu ya USD 100 kwa kila mtalii anaeingia Nchini na
baadae igawanywe katika yale maeneo ambayo watakayo amua kutembelea. Hii pia
itasaidia kukusanya mapato katika ada ya vivutio vya utalii kwa mfano kwenye Spice
Tour’s Farms, Baet-El –Jaib, Kanisa la Mkunazini, Minara miwili, kwenye magofu ya
22
Serikali, na maeneo mengine, lakini ada hii pia itasaidia kujua wale watalii waliongia
Nchini wametembelea maeneo gani na pia kujua ni maeneo gani hutembelewa na
wageni wengi zaidi kuliko pengine, ili kuweza kuboresha miundombinu kwa maeneo
hayo.
Mhe Spika, eneo jingine tunaloshauri Serikali kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya
Serikali ni katika malipo ya wageni kwenye Mahoteli ya kitalii, eneo hili kamati yangu
imegundua Mahoteli mengi ya Kitalii yamekua na utamaduni wa wageni wao kulipia
vyumba nje ya Nchi (malazi) wakati walipaswa malipo hayo kulipiwa hapa Zanzibar,
jambo hili linasababisha udanganyifu mkubwa wa kujua ni wageni wangapi wamelala
katika Mahoteli hayo , ili kuweza kupata kodi ya Serikali, kwa hiyo pia eneo hili Serikali
kuanzisha utaratibu wa kuanzisha kadi maalum ya Utalii ambayo atapewa pale uwanja
wa ndege baada ya kulipia ada ya VISA na mtalii atai-(SWAAP) hiyo card wakati wa
kuingia Nchini na atai-(SWAAP TENA) wakati wa kuondoka Nchini ili kujua alipoingia
nchini alikaa kwa muda gani hapa Zanzibar. Tukiweza kutumia utaratibu huu basi
utaweza kusaidia kukusanya pesa nyingi na mapato hayo yataweza kuziba lile pengo la
Serikali kutaka kukopa karibu 30 Bil. ili kufidia pengo la Bajeti yetu.
Mheshimiwa Spika,
Katika mapato yasiyokuwa ya kodi, zipo fedha za gawio kutoka Mashirika
yanayomilikiwa na Serikali. Katika gawio hilo Serikali iliongeza kutoka asilimia 10 kwa
mwaka wa fedha 2014/2015 hadi asilimia 20 ambapo jumla ya Tsh. 727 milioni
zimekusanywa. Kamati yangu ingependa kujuwa ni Mashirika yepi yameweza kumudu
kulipa gawio kwa asilimia hiyo 20 iliyoongezwa na Mashirika yepi hayajaweza kumudu
kulipa na kwa sababu gani. Nasema hivyo, kwasababu Mashirika haya huwa
hatuidhinishi fedha zao za makusanyo na matumizi, isipokuwa ruzuku tu kwa yale
yanayopata ruzuku, na ingawa Sheria ya Mitaji ya Umma namba 4 ya mwaka 2002,
inataka taarifa za mwaka na fedha za mashirika ya Umma ziwasilishwe katika Baraza la
Wawakilishi na Waziri husika.
23
Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka huu wa bajeti 2015/2016, Mapato ya ndani yaliyokadiriwa kukusanywa ni
Tsh.450.5 bilioni, ambayo ni ongezeko la asilimia 25 ya matarajio ya mapato ya mwaka
2014/15 ya Tsh. 360.4 bilioni. Katika matarajio ya mwaka huu ambayo Serikali
imeshaeleza kuwa itategemea zaidi makusanyo ya ndani kuendesha bajeti, bado Kamati
yangu ina wasiwasi wa kufikia malengo ya ukusanyaji kwa vile vyanzo vya mapato ni
vile vile na mfumo wa ukusanyaji wa mapato hayo una mianya mingi na kuvuja.
Mheshimiwa Spika,
Katika eneo la Uwanja wa ndege ambapo malipo ya viza za watalii yanafanyika
kumekuwa na changamoto kubwa ya ukusanyaji. Utaratibu uliokuwapo awali
umeonesha kuwa mapato yamekuwa yakivuja kwa kiwango kikubwa kutoka na mapato
hayo kukusanywa kwa njia ya mkono (cash). Imedhihirika kuwa baada ya mpango wa
majaribio wa kukusanya mapato hayo kwa njiaya kieletroniki kupitia benki ya CRDB
mapato hayo yameongezeka mara tatu zaidi ya yale yaliyokuwa yakikusanywa kwa
mkono. Mfumo huu wa ukusanyaji wa fedha kwa njia za kibenki umeonesha ni kwa kiasi
gani tunaweza kuongeza makusanyo na kudhibiti uvujaji wa mapato hayo.
Mheshimiwa Spika,
Kama nilivyoelezea hapo awali Katika maeneo mengi ambayo watalii wanatembelea
Serikali imekua haipati fedha inayotokana na utalii huo, maana yake ni kusema kwamba
mtalii anapokuja nchini kile kitendo cha yeye kuja hakiongezi fedha yoyote katika mfuko
wa Serikali, mtalii huyo akishalipa malazi hakuna na pahala anapotembea hakuna
sehemu ya malipo hayo yanayoingia Serikalini. Kamati yangu inaona kuwa ili utalii uwe
na faida maeneo yote yanayotembelewa na watalii lazima yawe na mfumo wa malipo
ambao kasma fulani ya kodi itakwenda Serikalini, kamati yangu imepata taarifa na kujua
24
kuwa maeno ya Msikiti wa Kizimkazi, kanisa la Mkunazini na Minara Miwili, Mashamba
ya Viungo (spice farms) na Fukwe za Bahari nyingi watalii wanakwenda kwenye maeneo
hayo wanalipa na hakuna fedha inayoingia Serikalini.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu tumependekeza kuwa ili Serikali iweze kupata fedha zinazotokana na utalii
lazima iweke miundombinu ya kisasa ya ya mashine za kieletroniki za ukusanyaji
mapato, ambayo ipo, na wataalamu wake wapo na imeshafanyiwa majaribio pale
uwanja wa ndege na kuleta matokeo mazuri. Miundombinu hiyo iwekwe kwenye
maeneo yote ambayo watalii wanatembelea na kila senti itakayolipwa Serikali itapata
kodi yake.
Mheshimiwa Spika,
Utalii imekuwa ni miongoni mwa sekta kiongozi katika kuchangia mapato ya Serikali,
tukiacha iendeshwe tu na Wawekezaji, kama tunavyoacha sekta ya nishati ya mafuta,
basi wananchi hawataona umuhimu wake, na ile sera ya utalii kwa wote itaonekana
kama imeshindwa kufanya kazi, hivyo basi, Kamati yangu inaitaka Serikali kuwatambuwa
waendesha biashara ya utalii wote (tour operators) kwa kuwaweka chini ya mwamvuli
mmoja kama nilivyoseama awali na kuwatoza kodi kwa mujibu wa sheria. Kamati yangu
imepata taarifa kuwa kuna waendesha biashara ya utalii wengi ambao hawalipi kodi na
wanaendelea kufanya shughuli hizo kinyume na sheria na kuikosesha mapato Serikali.
Endapo watawekwa kwenye mwamvuli mmoja kupitia taasisi za waendesha biashara ya
utalii mfano ZATI au ZATO na kila anayefanya biashara hii akalazimika kutambuliwa na
taasisi hizi, italeta urahisi kuwatambua na kupata kodi ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
Imefika wakati sasa Serikali itoe tamko rasmi kwa waendesha biashara ya utalii
kuhakikisha kuwa malipo yote ya fedha za viza kwa wageni, yanalipwa kwa njia ya kadi
(e-card) badala ya njia ya mkono (cash). Kamati imepata taarifa kuwa wapo baadhi ya
25
waendesha biashara ya utalii wanaowashawishi watalii kulipa fedha za viza kwa njia ya
mkono (cash) ingawa watalii wenyewe wapo tayari kufanya malipo hayo kwa njia ya
kadi. Sambamba na tamko hilo, Serikali isisite kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria
wale wote watakaokiuka tamko hilo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inasisitia kuwa katika sekta ya utalii, Serikali imekuwa ikipoteza mapato ya
malazi ya wageni katika hoteli, moja ya sababu kubwa ya kukosekana kwa mapato hayo
ni kukosekana kwa takwimu sahihi za malazi ya wageni pamoja na wenye mahoteli
kupokea malipo hayo kupitia akaunti za benki za nje ya nchi. Utaratibu huu unaifanya
ZRB kushindwa kujuwa ni kiasi gani kimelipwa na kinachostahiki kukatwa kodi kwa vile
hawana uwezo wa kufikia akaunti za benki za nje za mahoteli hayo.
Kamati imeona kuwa huu ni ujanja unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wenye
mahoteli kukwepa kulipa kodi. Kisingizio kinachotumika ni kuwa hakuna mfumo wa
kulipa fedha wa kielekroniki ambao wageni wakiwa nje wanalipa, jambo ambalo kamati
imebaini siyo la kweli, Kamati imekaa na wataalamu wa fedha na kutambua kuwa
mifumo ya malipo ya fedha ya aina yoyote ipo nchini kwetu, ikiwemo mfumo wa
malipo kwa njia za kieletroniki.
Mheshimiwa Spika,
Kamati inapendekeza kuwepo na mfumo huu wa ukusanyaji kwa vile kwanza kama
nilivyoeleza hauna gharama kwa Serikali, wataalamu wapo, teknolojia ipo, mfumo huu
unarahisisha huduma, unaongeza mapato ya Serikali na kupunguza kuvuja kwa mapato
hayo, lakni la muhimu zaidi hata utitiri wa kodi unaepukwa na kuondoa urasimu, kwani
kama kodi italipwa kwa njia ya mashine kila eneo ambalo huduma inatolewa litapata
fedha yake Serikalini ambayo itakuwa imeshalipwa kwa njia ya pamoja (Centralized
system).
26
Mheshimiwa Spika,
Eneo jengine ambalo Kamati inapendekeza kwa Serikali kulifanyia kazi ili iongeze
mapato yake ni fedha za Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), bado Serikali
haijalifanyiakazi ipasavyo eneo hili, Kamati imefanya utafiti na kuona kuwa Wafanyakazi
wa kigeni waliopo hapa nchini wanalipa fedha zao za hifadhi ya jamii kupitia kwenye
mifuko ya hifadhi ya nchi zao huku wao wakiwa hapa hapa, matokeo yake ni kuwa
fedha hizo zinafaidisha nchi zao. Kamati inaona kuwa na sisi tungeweka utaratibu
mwepesi kuwezesha wananchi wetu wanaofanyakazi nchi za nje waweze kuleta fedha
zao za hifadhi ya jamii kwa ZSSF, ambazo zingesaidia kujenga nchi yao na kuongeza
mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, eneo jingine mapato ya Serikali yanapotea kwa wingi ni magendo ya
mafuta, kumekua na ujanja mwingi unaofanywa na waingizaji mafuta kwa kushirikiana
na baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu katika kupima kiwango halisi cha
mafuta yanayoingizwa Nchini, lakini pia mashirikiano ya baadhi ya wafanyabiashara ya
Magendo ya Mafuta wanaotumia meli ndogo kupakua mafuta Baharini
(TRANSHIPMENT) kabla ya kuletwa kwenye (DEPORT) Maeneo haya mawili ndio hasa
njia kuu za uvujaji wa mapato ya Magendo ya mafuta hapa Nchini, kwa hiyo kamati
yangu ili kupunguza wizi huu basi tunaitaka Serikali kuleta Sheria itakayozuia Makampuni
yanayoingiza Mafuta Nchini kumiliki vituo vyao vya Mafuta na kuuza rejareja kwani
hapo nyuma miaka ya 90 ulikuwepo utaratibu huu na ulisaidia sana udhibiti wa mapato
ya serikali na magendo ya mafuta.
Mheshimiwa Spika,
Kamati kwa kirefu imejeribu kushauri njia mbali mbali za kusaidia Serikali kuongeza
makusanyo ya bajeti yake, bila shaka kama ushauri wa kamati utafanyiwa kazi huenda
tukaondokana na utegemezi wa bajeti kwa kiasi kikubwa pamoja na kupungua nakisi ya
bajeti ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2015/16, Serikali imepanga kukopa Tsh. bilioni
27
30 kufidia upungufu huo wa bajeti. Pamoja na hivyo, bado tunaamini kuwa vyanzo
vyetu vya mapato tukivisimamia na kuviendesha kitaalamu tunaweza kupanuwa wigo
wa makusanyo kutoka hapa tulipo.
Mheshimiwa Spika,
Katika kuimarisha mapato lazima na kwenye matumizi kuwe na udhibiti, tumeona katika
Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuna mapungufu mengi ya udhibiti
wa matumizi yasiyozingatia taratibu za fedha katika taasisi mbali mbali za Serikali. Ripoti
za Mdhibiti zilizowasilishwa katika Baraza hili zimebainisha mapungufu hayo kwa kirefu.
Kamati yangu inaamini kuwa endapo tutaendelea na kufumbiana macho katika kudhibiti
matumizi yasiyozingatia sheria basi hata tuimarishe vipi vyanzo vya mapato bado
tutakuwa na tatizo la kufikia malengo ya utekelezaji wa bajeti zetu.
Mheshimiwa Spika.
Kamati yangu inaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa mikikati yake katika
hatua zake za kuimarisha mapato ya ndani kwa mashirikiani ya TRA,ZRB na Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu kwa kuanzisha mfumo wa walipa kodi kwa maeneo maalum (BLOCK
MANAGEMENT SYSTEM) kwa kutumia System ya Technologia ya (GPS) ,kuimarisha
UTHAMINI wa Forodha, kupunguza misamaha ya kodi ,n.k kamati yangu iaitaka Serikali
kwa upande wa Forodha bidhaa zote zinazoingia N chini basi zilipiwe kupitia mfumo wa
kibenki kwav kufungwa machine za kukusanya fedha kama ilivyofanyika katika Uwanja
wa Ndege wa A.A.Karume Zanzibar ambao umeonyesha mafanikio makubwa.,
Pia kwa upande wa misamaha ya kodi kamati yangu inaitaka Serikali kutokuridhika na
utoaji wa misamaha tu bali kufuatilia hizo bidhaa zinazosamehewa ushuru je zinatumika
katika maeneo yaliyokusudiwa? Kwani kunataarifa kua baadhi ya vifaa hivyo huingizwa
madukani na kuuzwa na kuikosesha pesa Serikali yetu, lakini pia kufuatilia je ni kweli
28
bidhaa zinazosamehewa ushuru je zinatumika kwa kutoa unafuu wa huduma kwa
wananchi wetu? Ili msamaha huo uwe na tija kwa jamii yetu.
Mhe Spika, katika kuimarisha mapato kwa mwaka huu unaonzia July 2015/16 kamati
yangu imeridhika na hatua zinazotaka kuchukuliwa katika kuongeza mapato ikiwemo
kuanzisha matumizi ya Machuine za Electrical Fiscal Devices FEDs kamati yangu inaomba
kabla ya kuanza kutumika Machine hizi basi ni vyema kukatolewa semina maalum kwa
wafanya biashara wetu wa Zanziba ili kuepuka matatizo yaliyojitokeza kwa upande wa
TZ,bara ambapo ulileta usumbufu mkubwa kwa wananchi watumiaji wa bidhaa.
Mhe Spika, pia kamati yangu inaomba kutoa angalizo kwa Serikali katika mapitio hayo
ya ada yafanywe kwa uangalifu mkubwa vinginevyo mzigo huo utarudi kwa wananchi
na kupunguza uwezo wao matumizi sambamba na mfumko wa bei.
Mhe Spika, katika marekebisho ya kodi ambapo mswaada wake utakuja baadae
ningelitaka kujua hiyo tozo ya asilimia 2 ya ununuzi wa Umeme imekusudiwa nini kwani
hofu yangu itakua ni kumuongezea mwananchi bei ya Umeme jambo ambalo kamati
yangu haikubaliani nalo kwani litamuongezea mwnanchi ugumu wa maisha, kwani
umeme kwa sasa sio anasa bali ni sehemu ya maisha yetu.
Mhe Spika, kamati yangu inapongeza hatua ya Serikali kuanzisha mifuko mbali mbali ili
kukidhi baadhi ya mahitaji ya lazima kwa wakati muafaka kwani mifuko hiyo tayari
itakua na fedha za kuanzia.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia naomba kutoa pongezi kwa wajumbe wenzangu wote
wa Kamati ya Wenyeviti kwa mashirikiano makubwa walionipa kwa kipindi chote cha
miaka mitano nikiiongoza kamati hii kwa ruksa yako naomba niwatambue wajumbe hao
kama hivi ifuatavyo.
1) Mhe. Hamza Hassan Juma ====Mwenyekiti,
2) Mhe. Mgeni Hassan Juma === Mjumbe,
29
3) Mhe. Mahmood Mohd Mussa ==== Mjumbe,
4) Mhe. Mlinde Nassor Juma === Mjumbe,
5) Mhe. Omar Ali Shehe ==== Mjumbe,
6) Mhe. Hija Hassan Hija === Mjumbe,
7) Mhe. Ussi Jecha Simai == Mjumbe,
8) Ndg. Nasra Awadh Salmin === Katibu
9) Ndg. Khamis Hamad Haji ===Katibu
Mhe Spika baada ya hayo naomba kuwasilisha.
Ahsante,
……………………………….
Hamza Hassan Juma,
Mwenyekiti,
Kamati ya Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.