HISTORIA YANGUMimi naitwa Elimina Rajabu ni mzaliwa wa Tanga wilaya ya Korogwe kijiji cha Kwamkole
kata ya Magunga Msambiazi. Ni mtoto wa nne katika familia yetu. Kuna kaka wawili na dada wawili.
Nilisoma Shule ya Msingi Mlimani katika wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha. Baada ya kumaliza
elimu ya msingi nilichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari ya wasichana Kondoa wilaya ya Kondoa
mkoa wa Dodoma.
Nilihitimu elimu ya sekondari mwaka 2002 na kufanikiwa kujiunga na chuo cha ualimu
Euckenford kilichopo mkoani Tanga. Baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu nilipangiwa mkoa wa
Kilimanjaro wilaya ya Moshi Vijijini, kijiji cha Rauya, Kata ya Marangu Mashariki, Shule ya Msingi
Rauya. Nilianza kufundisha kama mwalimu tarajali kwa mwaka mmoja na kupatiwa ajira rasmi baada
ya kumaliza mwaka wa mafunzo.
Nimebahatika kupata watoto wawili wakiume na wakike.Mtoto wa kiume yupo darasa la pili na
wa kike yupo awali.
Nikiwa kazini niliomba kusoma na nikabahatika kupata kujiendeleza na stashahada ya Elimu ya
kawaida ya Elimu ya Msingi kwa miaka miwili. Nilipangiwa chuo cha ualimu Marangu kilichopo
Moshi Vijijini mkoa wa Kilimanjaro ambapo mpaka sasa nipo chuoni naendelea na masomo.
Maisha ya chuo ni mazuri ila palipo na mazuri hapakosi changamoto mbalimbali. Uzuri wa
maisha ya chuo ni kwamba unakutana na watu kutoka sehemu mbalimbali. Pia watu hawa huwa na
tabia tofauti tofauti zilizo nzuri na mbaya. Tabia nzuri zilizonipendeza ni kushirikiana katika masomo
tukiwa kwenye vikundi na hata ndani ya darasa. Hapa chuoni tunafanya kazi za usafi wa mazingira ya
chuo na mabweni ambapo ndipo tunapolala. Kuna mabweni ya wavulana na wasichana. Mabweni yote
yanamajina, hivyo watu hukaa kwenye mabweni kulingana na jinsi walivyopangiwa. Majina ya
mabweni ya wasichana ni Ukombozi, Mapinduzi, Usalama na Jitegemee. Mabweni ya wavulana ni
Ujamaa, Mwenge, Umoja, Jamhuri, Muungano na Azimio.
Tabia ambazo sikuzipendelea katika chuo ni baadhi ya wanachuo kutoka nje ya chuo bila kuwa
na sare za chuo na pia bila kuomba ruhusa. Kitendo hiki huwafanya wanachuo wanapokutana na
mwalimu wa chuo kuwakimbia au kuwakwepa na kujifanya kama hawajamuona. Tabia hii huwauzi
sana walimu. Pia kuna wanachuo ambao hunywa pombe na kulewa na wanapokuja mabwenini
huongea ovyo. Kitendo hiki huwauzi hata wanachuo wengine. Kuna wanachuo ambao hawapendi
kufanya usafi katika maeneo waliyopangiwa. Hii hupelekea viongozi wa wanachuo kuchukia kwani
hutolea nje kwa ajili ya kufuatilia wale ambao ni wazembe katika kufanya usafi. Tunaosoma wote ni
wanachuo tuliotoka kazini, kuna wanachuo ambao wanajituma kwa kufanya kazi kwa bidii ili
kuondokana na usumbufu wa kutolewa nje ya darasa wakati wa kipindi. Wanachuo wengi kwa sasa
wanafanya kazi wanazopangiwa kwa ushirikiano na kwa kujituma.
Masomo tunayosoma hapa chuoni ni ya kiswahili isipokuwa somo la kiingereza kwa mwaka wa
kwanza tulipoanza. Katika somo la kiingereza tulijifunza literature. Jaribio la kwanza katika somo hilo
lilikuwa la kuongea kiingereza. Kwa kweli ilithihirisha ni kwa jinsi gani wanachuo walivyo waoga
katika kuongea kiingereza. Nasema hivyo nikiwa na maana kwamba wanachuo waliogopa na wengine
walipata mshituko ambao hawakuweza kuongea. Kitendo hiki kiwafurahisha walimu kwani
waligundua kuwa walimu wa shule za msingi hawajui kiingereza na kutathimini kuwa kama walimu
hawa kiingereza kinawatesa je, kufundisha watoto shuleni inakuwaje? Hivyo walibaini kuwa
kiingereza katika shule za msingi ni tatizo.
Katika masomo tunayosoma tunasoma kwa mtindo wa semista. Kusoma kwa semista ni
kwamba kile ulichokisoma semista ya kwanza hutarudia kukisoma katika semista ya pili. Usomaaji huu
ni mzuri kwani hubebi mzigo mkubwa wa masomo katika semista nyingine. Pia ukifaulu mitihani
unaendelea na semista inayofuata na kama ukifeli unapewa mitihani ya marudio ili uweze kuedelea na
semista inayofuata.
Nilichofurahia katika kujifunza kwangu ni katika kujifunza jedwali la kutahini kwani nilikuwa
silijui. Kwa sasa najua kuliandaa jedwali la kutahini na ninaweza kulitumia. Hivyo nikifika shuleni
nitawafundisha walimu wenzangu katika kulitulia jedwali la kutahini kwani litawaonyesha ni nyanja
zipi watapima na idadi ya maswali
Nimatarajio yangu nitasoma kwa bidii ili niweze kufaulu vizuri na kutumia elimu niliyoipata
katika tendo la ufundishaji na ujifunzaji niwapo shuleni. Pia kuwasaidia walimu wenzangu pale
wanapohitaji msaada wa namna ya ufundishaji.