HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

Embed Size (px)

Citation preview

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    1/24

    1

    SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA

    MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DKT. JAKAYAMRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,

    TAREHE 31 DESEMBA, 2014

    Utangulizi

    Ndugu zangu;

    Watanzania Wenzangu;

    Kama ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga mwaka mmoja nakuukaribisha mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na

    kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Tunamshukuru Muumba wetu

    mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuifikia siku ya

    leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao hawakujaliwa kuiona siku ya leo

    tuzidi kuwaombea mapumziko mema. Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu,

    mwingi wa rehema atujaalie umri mrefu, afya njema na mafanikio tele kwa

    kila tuliombalo katika mwaka 2015 na miaka ijayo.

    Ndugu wananchi;

    Hizi ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais

    wa nchi yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya.

    Mimi wakati huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga

    nikifuatilia kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya

    uongozi wa nchi yetu akitoa salamu zake za kwanza za mwaka mpya,

    itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa kwangu.

    Hali ya Usalama

    Ndugu Wananchi;

    Tunaumaliza mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko

    salama na hakuna tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi

    yetu. Uhusiano wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri.

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    2/24

    2

    Hakuna nchi iliyo adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha

    usalama wa Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na

    viongozi na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea

    kuifanya nchi yetu kuwa salama.Uhalifu Unapungua

    Ndugu Wananchi;

    Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu

    vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya

    uhalifu yaliyoripotiwaPolisi yalikuwa64,088ikilinganishwa na matukio

    66,906katika mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na

    Jeshi la Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja naraia wema. Naomba ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo

    ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

    Ajali za Barabarani

    Ndugu Wananchi;

    Nimefarijika kusikia pia kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini

    nayo yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali14,048

    zilizosababisha vifo vya watu 3,534na wengine16,166kujeruhiwa.

    Mwaka 2013 kulitokea ajali22,383zilizosababisha vifo3,746na majeruhi

    19,433. Hivyo mwaka huu kulikuwa na ajali8,335,vifo212na majeruhi

    3,267pungufu kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia

    moyo ingawa bado ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya

    yaliyotuwezesha kupata unafuu huu mwaka huu yaendelezwe maradufu

    mwaka 2015 na miaka ijayo.

    Ugaidi

    Ndugu Wananchi;

    Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na

    washirika wao wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya

    kigaidi kwa kutumia mabomu na kumwagia watu tindikali Tanzania Bara

    na Zanzibar. Watu112wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    3/24

    3

    wametiwa nguvuni. Tayari watuhumiwa87kati yao wameshafikishwa

    mahakamani na waliosalia watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi

    unaendelea ili kuwatambua wahusika wengine ambao hawajakamatwa.

    Ndugu wananchi;Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa

    vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya

    kutambua mtandao wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za

    kuudhibiti. Hali kadhalika nawashukuru raia wema waliotoa taarifa

    zilizowezesha haya kufanyika. Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa

    mambo yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua tahadhari muda wote

    kwani hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani, lini na wapi.Dawa za Kulevya

    Ndugu Wananchi;

    Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya

    biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu

    watuhumiwa935wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani

    wamekamatwa. Jumla ya kesi19zimefunguliwa Mahakamani. Aidha,

    kiasi chakilo 400za heroine, kilo45za cocaine nakilo81,318za bangi

    zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum

    cha Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea

    kupatikana. Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe

    maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali itaendelea kuwaunga

    mkono.

    Ndugu wananchi;

    Kama nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na

    Kupambana na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza

    katika Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na

    kupendekeza kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za

    kulevya, Muswada huo pia unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye

    nguvu cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    4/24

    4

    ukipitishwa na kuwa Sheria tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano

    dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

    Ujangili wa Wanyamapori

    Ndugu Wananchi;Katika mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi yaujangili na

    biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori

    yameimarishwa. Kwa ujumla kasi ya ujangili imeendelea kupungua.

    Katika mwaka 2014 ndovu114waliuawa ikilinganishwa na ndovu219

    waliouawa mwaka 2013 au ndovu473mwaka 2012. Aidha, majangili

    1,354wamekamatwa na pembe za ndovu542na silaha mbalimbali184

    nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya Idara ya Wanyamaporikatika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaaniTanzania Wildlife

    Agency(TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na

    mapambano dhidi ya ujangili.

    Natoa pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na

    vyombo vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea

    kufanya na mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana

    na ujangili na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori

    zitaendelezwa kwa nguvu zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia.

    Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa

    maendeleo wanaotuunga mkono kwa hali na mali katika mapambano

    haya. Naomba waendelee kutusaidia.

    Hali ya Uchumi Jumla

    Ndugu wananchi;

    Mwaka 2014 ulikuwa mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika

    sekta nyingi ulikuwa ni mzuri. Ndiyo maana tunategemea kuwa tutafikia

    au hata kuvuka lengo tulilojiwekea la pato la taifa kukua kwaasilimia 7.4

    mwaka huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwaasilimia 7.3. Mfumuko

    wa bei uliendelea kushuka na kufikiaasilimia 5.8Novemba, 2014

    ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwaasilimia 6.0. Hali nzuri ya

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    5/24

    5

    upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya mfumuko wa bei

    kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa bei

    utaendelea kushuka na kufikiaasilimia 5ifikapo Juni, 2015.

    Mauzo NjeNdugu Wananchi;

    Mauzo nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia

    Oktoba 31, 2014, Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya

    dola za Marekanimilioni 8,503.9ukilinganisha na mauzo ya dolamilioni

    8,332.5katika kipindi kama hicho mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa

    makubwa zaidi kama bei za kahawa, chai, korosho na pamba

    zisingeanguka au bei ya dhahabu nayo isingepada.

    Akiba ya Fedha za Kigeni

    Ndugu Wananchi;

    Akiba yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekanimilioni

    4,251.8 kwa kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014. Kiasi hicho

    kinatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje kwa miezi4.1.Hii ni chini ya lengo

    letu la kuwa na akiba ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi

    minne na nusu. Hata hivyo,sina wasiwasi kabisa kwamba tofauti hii

    ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.

    Mapato ya Serikali

    Ndugu Wananchi;

    Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi

    Novemba, 2014 yaliongezeka kutoka shilingibilioni 3,555.5kipindi kama

    hicho mwaka 2013 hadi shilingibilioni3,924.1mwaka huu. Hata hivyo,

    makusanyo hayo yalikuwaasilimia 90ya lengo tulilojiwekea la kukusanya

    shilingibilioni 4,459.7. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu

    mbalimbali zilizosababisha lengo lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya

    mwaka wa fedha wa 2014/2015. Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa

    kurekebisha mambo hayo ili katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    6/24

    6

    makusanyo yafikie lengo na ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la nusu ya

    kwanza.

    Takwimu Mpya za Pato la Taifa

    Ndugu wananchi,Ni utaratibu wa kawaida wa nchi zote duniani kuwa na mwaka

    unaotumika kuwa kizio (base year) cha kukokotoa takwimu za Pato la

    Taifa. Ni utaratibu wa kawaida pia kwa kila baada ya muda fulani mwaka

    wa kizio hubadilishwa. Lengo ni kuboresha takwimu husika. Katika

    marekebisho hayo pia huingizwa thamani ya bidhaa na huduma mpya

    katika pato la taifa na kuziondoa zilizotoweka ili kutoa picha halisi ya

    ukuaji wa shughuli za kiuchumi.Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria

    (mwaka 2013) na Kenya (mwaka 2014) wamefanya marekebisho ya

    takwimu zao za pato la taifa. Na sisi Tanzania tumefanya hivyo mwaka huu

    (2014). Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu kurekebisha takwimu za pato la

    taifa. Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka 1966, 1976, 1992 na 2001.

    Ndugu wananchi;

    Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za

    pato la taifa na kukokotoa takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama

    mwaka wa kizio. Kutokana na marekebisho yaliyofanyika, pato la taifa

    kwa mwaka 2013 nishilingi trilioni70kwa kutumia bei za mwaka 2007.

    Ukitumia bei za mwaka 2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 nishilingi

    trilioni 53.17.Kuongezeka kwa pato la taifa kumeongeza pia pato la

    wastani la kila Mtanzania kutokashilingi 1,186,200(sawa naUS$ 742) kwa

    bei za mwaka 2001 hadishilingi 1,560,050(sawa naUS$ 977) kwa bei za

    mwaka 2007.

    Kilimo na Chakula

    Ndugu Wananchi;

    Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya

    chakula nchini. Uzalishaji ulikuwa tanimilioni 16.02ukilinganisha na

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    7/24

    7

    uzalishaji wa tanimilioni 14.38mwaka wa jana 2013.Hili ni ongezeko la

    tanimilioni 1.64. Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna

    ziada yatani milioni 3.25.Katika ziada hiyo, mahindi yanachangia tani

    milioni 1.55,mchele tani794,000na kiasi kinachobakia kinachangiwa namazao mengine ya chakula.

    Ndugu wananchi;

    Kuna jambo moja muhimu kuhusu ununuzi wa nafaka ambalo

    ningependa kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi

    ya Chakula (NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama

    wote unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo tu

    ya nafaka ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka akiba yataifa ya chakula cha kutumika wakati wa dharura ya watu kupata tatizo la

    njaa. Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana na uwezo wa maghala

    yake kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni kuhifadhitani 246,000

    ingawaje tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa

    kuhifadhitani 400,000ifikapo 2015.Hivyo basi kwa Wakala kununuatani

    292,415.41mwaka huu ina maana kwamba kiasi cha kaributani 50,000

    zinahifadhiwa nje ya maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo utaratibu

    mzuri na haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka hiyo kuharibika na

    kuzua mgogoro mkubwa siku moja.

    Ndugu wananchi;

    Baada ya NFRA kununuatani 292,415.41kuna takribanitanimilioni

    2.96za nafaka ya ziada ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima.

    Mategemeo yetu ni kuwa wafanyabiashara wetu watanunua nafaka hiyo kwa

    ajili ya kuuza mijini na kwingineko inakohitajika. Bahati mbaya mwaka huu

    kama ilivyokuwa mwaka wa jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza

    kununua nafaka yote ya ziada ambayo Serikali haikuweza kununua kupitia

    Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hali hii imezua tatizo ambalo Serikali

    kwa kushirikiana na wafanyabiashara nchini hatuna budi kulitafutia

    majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine ndani na hata nje ya nchi

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    8/24

    8

    ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada. Nimeagiza Wizara ya Kilimo,

    Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa chini na

    kushirikiana na wafanyabiashara kulitafutia ufumbuzi suala hili lenye maslahi

    makubwa kwa wakulima na nchi yetu kwa jumla.Ndugu Wananchi;

    Katika mazingira haya, ninapopata taarifa ya kuwepo watu wanaotaka

    kuuza mahindi nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo na maafisa wa Serikali

    inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya hivyo

    waache mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao

    kufanikisha azma yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao

    wajitokeze kufanya biashara hiyo. Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza nikwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia

    njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna

    sababu ya kufanya hivyo.

    Miradi ya Kimkakati

    Ndugu wananchi;

    Katika mwaka 2014 utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa

    mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 2015/16)

    umeendelea vizuri. Tunayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka

    2015 miradi mingi itakamilika.

    Tuanze na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na

    Songosongo hadi Dar es Salaam. Mradi huu unategemewa kukamilika

    Januari, 2015. Utakapokamilika utatuwezesha kutimiza lengo letu la

    kuzalishaMW 2,780zaumeme ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya

    ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili

    iweze kusafirishwa kwenda kwenye masoko, inakwenda vizuri.

    Ndugu Wananchi;

    Utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme

    vijijini umeendelea vizuri na tumepata mafanikio makubwa yasiyokuwa

    na mfano wake katika historia ya nchi yetu. Hadi kufikia Novemba, 2014,

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    9/24

    9

    jumla ya vijiji3,836vimepatiwa umeme na vingine1,500vinategemewa

    kupatiwa umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji5,336kati ya vijiji

    12,423vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na

    asilimia 43ya vijiji vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasawananchi milioni 17.3nchi nzima sawaasilimia 36 wamefikiwa na

    huduma ya umeme ikilinganishwa na watumilioni 8.1sawa naasilimia

    18.4waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015

    tunatarajia watumilioni 18.2sawa naasilimia 38watafikiwa na umeme.

    Kwa upande wa vijijini mwaka 2012 watumilioni 2.3sawa naasilimia 7

    walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo itaongezeka na kuwa

    milioni 7.4sawa naasilimia 21. Haya ni mafanikio makubwa kwawananchi wengi vijijini na mijini kupata umeme katika kipindi kifupi kiasi

    hiki. Ni mageuzi ya aina yake yatokayotoa mchango muhimu katika

    kuinua hali za maisha ya Watanzania.

    Ndugu Wananchi;

    Tunaanza kuiona nuru ya matumaini kwamba siku si nyingi kutoka

    sasa, makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma ya Liganga

    yataweza kutumika kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wa Ludewa.

    Maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015 kuanza

    ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua

    umeme, ujenzi wa mgodi wa chuma kisichoyeyushwa pale Liganga na

    ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha chuma.

    Natoa pongezi maalum kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na

    wabia wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya China kwa hatua

    iliyofikiwa. Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika itatoa ajira33,000za

    moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja.

    Ndugu Wananchi;

    Mradi mwingine mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo

    Maalumu la Kiuchumi (Special Economic Zone) la Mbegani, Bagamoyo.

    Kwa mujibu wa mpango kazi wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka ya

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    10/24

    10

    Kuendeleza Maeneo huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni yaChina

    Merchants Holdings Internationalna Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali

    za Serikali ya Oman (Oman State General Reserve Fund), ujenzi wa bandari

    na miundombinu mingine itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwakuanza Julai 2015.

    Miundombinu ya Usafiri na Uchukuzi

    Ndugu Wananchi;

    Katika mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na

    kuimarisha barabara za udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea

    kote nchini. Huu nao ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami19

    zenye urefu wakilometa1,459zimekamilika kujengwa mwaka huu katikaMikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga,

    Morogoro, Arusha, Tabora na Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara

    nyingine24katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa,

    Simiyu, Katavi, Tabora, Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo

    wakati wo wote mwaka 2015 zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa

    barabara nyinginenaneyanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.

    Kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya

    kazi ya ujenzi na ukarabati wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka

    huu Mfuko huo umetengewashilingi bilioni 751.7ukilinganisha na

    shilingi bilioni 504.4mwaka jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la

    msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero. Matumini yetu ni kuwa

    ujenzi wa daraja hilo na Daraja la Kigamboni utakamilika mwaka 2015.

    Ujenzi wa Daraja la Malagarasi ulishakamilika mwaka jana,

    kinachosubiriwa ni sherehe ya uzinduzi.

    Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha

    ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni

    matarajio yetu pia kwamba mabasi yataanza kusafirisha abiria katika

    kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Halikadhalika, tunategemea

    katika mwaka 2015 ujenzi utaanza wa barabara zinazozunguka jiji la Dar es

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    11/24

    11

    Salaam (ring roads), barabara ya Mwenge - Morocco na ile ipitayo juu ya

    nyingine (flyovers) eneo la TAZARA. Vile vile, daraja jipya la Salenda

    litaanza kujengwa. Aidha, kivuko cha abiria300cha MV Dar es Salaam

    kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam Kaskazini na Ferrymapema mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza msongamano wa

    magari katika jiji la Dar es Salaam.

    Usafiri wa Anga na Reli

    Ndugu wananchi;

    Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati

    zimeendelea kwa mafanikio. Mwaka huu vichwavinanevya treni

    vimekarabatiwa, mabehewa mapya22ya abiria na mabehewa274ya mzigoyamenunuliwa. Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini kati ya

    Novemba na Desemba mwaka huu. Kati ya Januari na Mei, 2015

    tunatarajia kupokea vichwa vipya vya treni13. Uboreshaji huu wa huduma

    za treni unakwenda sambamba na ukarabati wa reli yenyewe, ujenzi wa

    madaraja na kuimarisha maeneo yaliyo korofi katika reli hiyo.

    Kuhusu ujenzi wa reli iliyo pana zaidi (standard guage), yenye

    uwezo wa kubeba mabehewa mengi na kuwezesha treni kwenda kwa

    mwendo wa kasi zaidi, juhudi za kutafuta fedha za ujenzi au wabia wa

    kushirikiana nasi kujenga zinaendelea. Wakati huo huo, tunaendelea na

    juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya TAZARA ili mambo

    yaende vizuri. Tutashirikiana kwa karibu na wabia wenzetu wa Zambia.

    Bahati nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga mkono juhudi zetu za

    kufufua reli ya TAZARA.

    Usafiri wa Anga

    Ndugu Wananchi;

    Sekta ya usafiri wa anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi

    ya abiria wanaowasili na kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini

    imeongezeka kutoka abiriamilioni 2.5mwaka 2013 hadi abiriamilioni3.5

    kufikia Septemba, 2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za nje

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    12/24

    12

    zimeongezeka kutoka274Januari, 2013 hadi295kufikia Septemba, 2014.

    Hili ni ongezeko laasilimia 8. Safari za ndege ndani ya nchi nazo

    zimeongezeka kutoka safari230,458mwaka 2013 hadi safari241,922mwaka

    2014. Hii ni sawa na ongezeko laasilimia 39. Maongezeko haya nikielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii na biashara nchini

    zimeendelea kukua.

    Ndugu Wananchi;

    Ujenzi wa Jengo la3 (Terminal3)la Abiriakatika Uwanja wa Ndege

    wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri. Jengo hilo

    litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa

    abiriamilioni 8kwa mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la2(Terminal2)

    utafanyika ili liweze kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi

    huo, Wakala wa Viwanja vya Ndege wameendelea kukarabati na

    kuboresha viwanja vya ndege vyaKIA, Mwanza, Songwe, Bukoba,

    TaboranaKigoma. Tunatarajia ukarabati wa viwanja vya ndege vya

    ShinyanganaSumbawangakuanzamapema mwaka 2015.

    Elimu

    Ndugu wananchi;

    Tumeendelea kupiga hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu

    nchini. Tumefanikiwa kupunguza tatizo la upungufu wa maabara, vitabu

    na walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu

    36,339kati ya81,562wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu

    45,223yaani26,946wa shule za msingi na18,277wa shule zasekondari

    hususan wa masomo ya sayansi.Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa

    masomo ya sanaa katika shule za sekondari.

    Mwaka huu tumeanza mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya

    Diploma ya Ualimu kwa masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu

    cha Dodoma ambapo jumla ya wanafunzi5,602wa masomo hayo

    wamedahiliwa. Mpango huu utatuwezesha kupunguza pengo kubwa

    tulilonalo la walimu wa sayansi katika muda mfupi zaidi.

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    13/24

    13

    Ujenzi wa Maabara

    Ndugu wananchi;

    Ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za

    sekondari za Kata3,463umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shuleinatakiwa zijengwe maabara10,389ilipofika Novemba, 2014. Taarifa

    kutoka TAMISEMI zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 29, 2014,

    maabara 4,207sawa naasilimia40.5zilikuwa zimekamilika, maabara5,688

    sawa naasilimia 54.8zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji,

    na maabara494sawa naasilimia 4.zilikuwa katika hatua za awali za

    ujenzi.

    Ndugu Wananchi;Natoa pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya,

    Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji

    nchini pamoja na wananchi, kwa jitihada kubwa iliyofanyika. Kwa

    kutambua jitihada hizo, nimeongezamiezi sitazaidi kwa wale ambao

    hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo wafanye hivyo. Sikusudii

    kuongeza tena muda baada ya hapo. Naomba watumie kipindi hicho

    kitumike kutafuta vifaa vya maabara. Serikali itasaidia upatikanaji wa

    watunza maabara (laboratory technicians) ambao tumeanza programu

    kubwa ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya maabara.

    Ununuzi wa Vitabu

    Ndugu Wananchi;

    Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya

    kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa tunanunua

    vitabu kwa kutumia Bajeti ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki zetu

    wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali ya Marekani imetupatia vitabu

    milioni 2.5vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari.

    Ongezeko hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wakitabu kimoja

    kwawanafunzi wannena kufikiakitabu kimojakwawanafunzi wawili.

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    14/24

    14

    Lengo letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo ifikapo

    mwaka 2016.

    Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo

    Ndugu wananchi;Mafanikio mengine tuliyopata mwaka huu ni kukamilika kwa Sera ya

    Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua muhimu sana katika

    maendeleo ya elimu nchini hakuna badala yake. Sera mpya inalenga

    kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu

    zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa za elimu iliyo bora

    na inayolinga na wakati tulionao. Jambo jipya sana na la kihistoria katika

    Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu yasekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za

    msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari.

    Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa maagizo kwa

    Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na

    Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango kuanza kutafakari

    namna jambo hilo litakavyotekelezwa.

    Afya

    Ndugu Wananchi;

    Katika mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa

    Watanzania ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa

    ya dengue iliyowapata watu1,039na kusababisha vifo vya watu3kati yao.

    Kwa upande wa maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua

    watu wenye maradhi hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege

    vya kimataifa na vituo vyote vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema

    kuwahudumia wagonjwa wa maradhi hayo iwapo watatokea.

    Mwaka huu pia, Madaktari wetuwatanowamekwenda Liberia

    kusaidiana na ndugu zetu wa huko katika kukabiliana na ugonjwa wa

    ebola. Madaktari wetu hao wako salama na wanaendelea vizuri kutoa

    huduma. Madaktari hao watakaporejea nchini watakuwa hazina kubwa ya

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    15/24

    15

    taifa katika kupanga mipango ya kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hali

    kadhalika, watakuwa viongozi wa wengine katika kutibu wagonjwa wa

    maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.

    Ndugu Wananchi;Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri

    watumishi wa sekta ya afya8,345ambao kati yao kuna madaktari244,

    madaktari bingwa75, wauguzi2,555na wataalamu wa kada nyingine za

    afya5,471. Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi

    kutoka wanafunzi7,956katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi9,730.

    Kwa ongezeko hilo, sasa tumefikiaasilimia 97ya lengo letu la kudahili

    wanafunzi10,000ifikapo mwaka 2017.Jitihada zetu za kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari,

    Wauguzi na wataalamu wengine wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa

    hospitali ya kufundishia pale Mloganzila unaendelea vizuri na hospitali ya

    kufundishia ya Chuo Kikuu cha Dodoma umekamilika. Ni matarajio

    yangu kuwa wakati wo wote mwakani ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo

    Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila utaanza. Ujenzi huo ukikamilika

    Chuo kikuu cha Muhimbili kitaweza kudahiliwanafunzi 12,000kutoka

    wanafunzi 2,500wa sasa jambo ambalo litafanya upungufu wa Madaktari,

    Wauguzi na Wataalamu wa Afya kupata jawabu la uhakika. Tumeendelea

    kufanya mambo mengine ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za ubongo na

    mishipa ambalo limekamilika pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata

    vifaa.

    Maji

    Ndugu Wananchi;

    Katika mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi

    mbalimbali ya kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini.

    Kwa ajili hiyo miradi498ya maji vijijini imekamilika na miradi740ipo

    katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine378ipo katika

    maandalizi ya ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba katika mwaka

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    16/24

    16

    ujao wa 2015, miradi mingine731itatekelezwa na vituo25,790vya kuchota

    maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza kuwafikiaasilimia 71ya

    wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutokaasilimia 58ya sasa.

    Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la kuwapatia watumajiasilimia 65ya Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi langu

    kwa ndugu zetu wa Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa ukaribu zaidi

    na wawapatie fedha kwa wakati.

    Ndugu Wananchi;

    Utekelezaji wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga Same

    Mkomazipamoja na miji na vijiji vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015.

    Fedha zimekwishapatikana na Mkandarasi wa Awamu ya Kwanzaameshapatikana. Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana

    muda si mrefu kutoka sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi

    wa maji wa mji wa Orkesment.

    Ndugu Wananchi;

    Mwaka huu miradi ya kuipatia maji miji kadhaa nchini ilikamilika na

    tatizo la upungufu wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji

    kadhaa ambayo miradi imefikia hatua ya juu na kwamba wakati wowote

    mwakani itakamilika. Jiji la Dar es Salaam lipo katika kundi hili. Kazi ya

    upanuzi wa miradi ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa msaada wa

    Serikali ya Marekani na mkopo kutoka Serikali ya India imefikia hatua

    nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

    Mwaka ujao pia visima virefu vya Kimbiji na Kipera vitachimbwa na

    Bwawa la Kidunda litaanza kujengwa.

    Serikali ya India pia imekubali kutupatia mkopo waDola za

    Marekani milioni 268.2kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji

    miji ya Tabora, Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa

    kujumuisha miji ya Sikonge na Urambo katika mradi huo utaangaliwa.

    Bunge na Mahakama

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    17/24

    17

    Ndugu Wananchi;

    Katika mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea

    kutekeleza vyema majukumu yao. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa

    Tanzania limeweza kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa pamojana kulazimika kugawana Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la

    Katiba. Bunge limefanya mikutanomitatu,Miswada17ya Sheria ilisomwa

    kwa mara ya kwanza, Sheriatanona maazimiosabayalipitishwa. Maswali

    ya msingi569na ya nyongeza1,541yaliulizwa na kujibiwa. Aidha, sakata la

    Akaunti ya Tegeta Escrow nalo lilijadiliwa na kutolewa maazimio.

    Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu maazimio hayo na bado

    tunaendelea.Napenda kuitumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge

    wetu kwa kutekeleza vizuri wajibu wao wa Kutunga Sheria na kusimamia

    Serikali. Nawasihi waendelee na msimamo huo mwema na chanya kwa

    maslahi ya nchi yetu na watu wake.

    Ndugu Wananchi;

    Kwa upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri

    inayofanywa ya kupunguza mrundikano wa mashauri katika Mahakama

    za ngazi zote. Wahenga wamesemamcheza kwao hutunzwa. Hatuna

    budi kutoa pongezi maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed

    Chande Othman kwa uongozi wake mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji

    wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi

    na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wamejiwekea malengo ya

    kusikiliza na kutoa hukumu kwa mashauri yasiyopungua200kwa mwaka

    kila mmoja wao.

    Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea

    vizuri. Mashauri870yalisikilizwa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya

    Rufani, mashauri11,334kwenye Mahakama Kuu, mashauri8,715kwenye

    Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri25,683katika Mahakama za

    Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa Mahakama Kuu

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    18/24

    18

    kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama

    ilivyofanyika Kigoma, Shinyanga na Tabora umesaidia sana kupunguza

    mrundikano wa mashauri ya siku nyingi. Haijawahi kutokea mashauri

    mengi kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika historia ya Mahakamanchini.

    Ndugu Wananchi;

    Mkakati huu mpya umeleta matumaini mapya kwamba tatizo la

    kuchelewesha kwa mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa

    limeanza kupatiwa ufumbuzi. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote

    natoa shukrani na pongezi nyingi kwa Jaji Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji

    Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa ngazi zote kwa kazinzuri waifanyayo.

    Hali kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama na

    watendaji wote wa Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya kuwawezesha

    Majaji na Mahakimu kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika utendaji

    Mahakamani umebadilika na kuwa bora zaidi. Mimi naahidi kuendelea

    kusaidia Mahakama kwa kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina kutoa kwa

    wakati pesa zilizotengwa katika bajeti.

    Mapambano Dhidi ya Rushwa

    Ndugu Wananchi;

    Mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka

    yameendelea bila ya ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU

    wamepokea taarifa237na wamekamilisha uchunguzi wa mashauri545.

    Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni428. Mashauri yaliyomalizika

    ni205, kati ya hayo125watuhumiwa waliachiliwa na80walipatikana na

    hatia na kuhukumiwa. Mwaka huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye

    thamani yashilingi bilioni 38.96zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi

    hiyo kiutendaji, maafisa wapya394wameajiriwa.

    Sherehe za Miaka 50 ya Muungano

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    19/24

    19

    Ndugu Wananchi;

    Mwaka huu wa 2014 tuliadhimisha miaka 50 ya Muungano wa nchi

    zetu mbili yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika

    kwa heshima inayostahili. Maadhimisho yalifikia kilele tarehe 26 Aprili,2014 na zilifanyika sherehe nchini kote na sherehe hizo zilifana sana. Ni

    ukweli usiopingika kuwa kwa Muungano wetu kuweza kudumu kwa nusu

    karne ukiwa bado imara na unazidi kustawi ni mafanikio makubwa.

    Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri. Naamini Muungano wetu

    utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwani yale

    mambo yenye kuleta matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.

    Miaka 50 ya JWTZ

    Ndugu Wananchi;

    Wakati nchi inasherehekea miaka 50 ya Muungano, baadhi ya

    vyombo na taasisi muhimu kitaifa zilifanya hivyo hivyo. Miongoni mwa

    walioadhimisha nusu karne ya kuundwa kwake ni Jeshi la Ulinzi la

    Wananchi wa Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1 Septemba,

    1964. Jeshi letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa la

    kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli Mkoani

    Arusha.

    Nilibahatika kushuhudia siku ya mwisho ya zoezi hilo.

    Nilifurahishwa sana na kiwango cha utayari kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi

    wetu walionesha weledi wa hali ya juu, umahiri mkubwa, ujasiri,

    ukakamavu na uvumilivu wa aina yake wakati wa kutekeleza majukumu

    yao katika mazingira magumu ya uwanja wa medani za vita.

    Niliwapongeza siku ile na narudia tena leo kuwapongeza. Niliyoyaona

    yamenihakikishia mimi na Watanzania wote kuwa Jeshi letu la Ulinzi la

    Wananchi wa Tanzania liko imara kulinda mipaka ya nchi yetu na

    kuhakikisha usalama wa taifa letu na watu wake. Jeshi letu bado ni lile

    tunalolijua sisi sote, lakini limezidi lile lililomngoa mvamizi Dikteta Iddi

    Amin wa Uganda, tena limezidi kwa mbali.

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    20/24

    20

    Mchakato wa Katiba Mpya

    Ndugu Wananchi;

    Mwaka huu pia tumeshuhudia kukamilika kwa zoezi muhimu la

    kuandika Katiba Inayopendekezwa. Kama tujuavyo sote, mchakato uliozaaKatiba Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi ndani na nje ya

    Bunge Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo lilikamilisha kazi

    yake kwa salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014 ambayo ndiyo

    ilikuwa siku ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali

    Mohamed Shein tulikabidhiwa nakala za Katiba Inayopendekezwa tarehe 8

    Oktoba, 2014. Nimeshatimiza wajibu wangu wa kuchapisha katika Gazeti

    la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni kuwa tarehe 30Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya Uchaguzi kufanya

    matayarisho husika ya kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika.

    Ndugu Wananchi;

    Moja ya mambo muhimu ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa

    sasa ni kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Mpiga Kura. Tume

    imeamua kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Register.

    Uandikishaji wa majaribio umefanyika katika baadhi ya Kata katika

    Majimbo ya Mlele, Kawe na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza yatasaidia

    kuboresha mfumo huo kabla ya uandikishaji wa watu wote wenye sifa

    stahiki kuanza.

    Ndugu Wananchi;

    Napenda kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu

    wote kuwa mfumo mpya unatengeneza Daftari Jipya la Mpiga Kura

    ingawaje lugha inayotumika ni uboreshaji wa Daftari la sasa. Uboreshaji

    huu wa Daftari la Mpiga Kura ni tofauti na ule tuliouzoea ambapo

    walikuwa wanaandikishwa wapiga kura wapya na wale waliopoteza

    vitambulisho vyao. Safari hii wanaandikishwa wote wapya na wa zamani

    na wote watapata vitambulisho vipya. Hivyo basi, sisi wenye vitambulisho

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    21/24

    21

    vya kupiga kura vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze kujiandikisha wakati

    ukifika.

    Jambo la pili ni kwamba, Daftari la Mpiga Kura linalotayarishwa siyo

    kwa ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa peke yake, daftarihilo hilo litatumika pia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo

    basi, kujiandikisha ni jambo muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu

    utajinyima fursa ya kushiriki kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa

    bali pia utakosa fursa ya kuchagua Rais wako, Mbunge wako na Diwani

    wako. Katu usikubali yakukose hayo.

    Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

    Ndugu Wananchi;Kama mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014

    ulifanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji,

    vijiji na mitaa. Uchaguzi umekwisha na viongozi wamekwishapatikana.

    Sasa ni wajibu wa viongozi hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa

    walioendesha uchaguzi ni wakati mzuri wa kufanya tathmini ili wapate

    mafunzo yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa TAMISEMI na Wakurugenzi

    Watendaji wa Halmashauri, lengo liwe ni kuona namna ya kuimarisha

    mazuri na kusahihisha makosa na matatizo yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa

    amani watambue matatizo ya kiusalama yaliyotokea na kuona namna ya

    kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya namna hiyo yasijitokeze tena.

    Hatma ya yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya vizuri zaidi katika chaguzi

    zijazo za Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu

    wa mwaka 2015.

    Jumuiya ya Afrika Mashariki

    Ndugu Wananchi;

    Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya

    ya Afrika Mashariki. Ni zamu yetu kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi

    wa Jumuiya yetu kati ya nchi wanachama. Ni dhamana kubwa na kwamba

    wenzetu wa Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze katika

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    22/24

    22

    kutekeleza malengo na madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa

    katika Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika,

    tunategemewa kuongoza katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya

    vikao vya Jumuiya. Hii inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetuambayo utekelezaji wake unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa

    katika kipindi cha uongozi wetu.

    Kwa niaba ya Watanzania wote napenda kuwashukuru ndugu zetu

    wa Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda kwa kutuamini. Napenda kuahidi

    kuwa hatutawaangusha. Sisi Watanzania tutafanya kila tuwezalo

    kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya Jumuiya

    yenyewe, nchi zetu na wananchi wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi kuwawabunifu kwa nia ya kuona utangamano unakua na kustawi kwa kasi na

    kuzaa matunda ya maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda

    tuliyoyatarajia tulipoamua kuanzisha Jumuiya hii na matunda tuliyoyapata

    tulipoamua kwa hiari yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.

    SADC, AU NA UN

    Ndugu Wananchi;

    Kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, tunaahidi kuendelea kuwa

    wanachama waaminifu na kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wa

    shughuli mbalimbali za mashirika haya ya kikanda na kimataifa. Kwa

    upande wa SADC tutaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mikakati na

    mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ile ya kisiasa na

    kiusalama kama ilivyoainishwa katika RISDP (Regional Indicative Strategic

    Development Plan) na SIPO (SADC Strategic Indicative Plan for the Organ).

    Kwa ajili hiyo Tanzania, itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza

    utangamano wa kiuchumi katika SADC na kusaidia kuimarisha uhusiano

    mwema na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa SADC. Hii ni

    pamoja na kusaidia katika kutatua migogoro ya kisiasa na kusalama kati ya

    nchi wanachama.

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    23/24

    23

    Kwa upande wa Umoja wa Afrika tutaendelea kutekeleza maamuzi

    ya vikao na taasisi mbalimbali za Umoja huo. Daima tutakuwa

    wanachama waaminifu wa Umoja wa Afrika na kuchangia katika

    uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa Mataifa tutaendelea kutimiza wajibuwetu kama wanachama wa Umoja huo wa kimataifa ulio adhimu na

    muhimu kwetu na dunia nzima. Tutaendelea kushiriki katika shughuli za

    ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao wanajeshi

    wetu katika majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi za

    Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari wakati

    wote kuchangia zaidi iwapo Umoja wa Mataifa watatutaka tufanye hivyo.

    Hitimisho

    Ndugu Wananchi;

    Namaliza hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania

    wote kwa kuiunga mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu

    uliowezesha nchi yetu kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia

    katika mwaka 2014. Tumeweza kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu

    mengi. Umoja wetu na mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika

    hapa. Tunauanza mwaka 2015 kwa matumaini makubwa. Mwaka 2015

    unatupa fursa kubwa ya kuendelea kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka

    ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo huenda ukawa na changamoto

    na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu. Uelewa wetu, umoja wetu,

    mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo ndivyo vitakavyotuvusha

    kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina imani kubwa kwa

    uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri ya nchi

    yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu.

    Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na

    miaka ijayo. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka

    mpya.

    Mungu Ibariki Afrika!

    Mungu Ibariki Tanzania!

  • 8/10/2019 HOTUBA YA MWAKA 2015 - FINAL.doc

    24/24

    24

    Asanteni kwa kunisikiliza.