18
Nyaraka ya Kufanyia Kazi 09.1k Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda ya Mwaka 2003 Tony Baker

Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

  • Upload
    others

  • View
    37

  • Download
    0

Embed Size (px)

Citation preview

Page 1: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

Nyaraka ya Kufanyia Kazi

09.1k

Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari:

Kampeni ya Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda ya Mwaka 2003

Tony Baker

Page 2: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye
Page 3: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

1

Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari:

Kampeni ya Mtandao wa Kupambana naRushwa Nchini Uganda ya Mwaka 20031

Tony Baker2

Matatizo ya Bara la Afrika, na hasa nchini Uganda, yanasababishwa na viongozi wanaong’ang’ania madarakani muda mrefu, hali inayowajengea kinga dhidi ya kushitakiwa, rushwa na ulezi.

—Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Hotuba ya Siku ya Kuapishwa kwake, 1986

1. UtanguliziUchunguzi wa kina uliowasilishwa hapa chini unahusu kampeni ya mapambano dhidi ya rushwa iliyofanyika nchini Uganda mwaka 2003. Lengo la kampeni kwa mwaka ule lilikuwa kuhimiza kutungwa sheria itakayohimiza haki ya kupata habari. Haki hii inaonekana kuwa sehemu muhimu sana ya juhudi za mapambano dhidi ya rushwa kwa sababu huwapatia raia, asasi za kiraia na hata wabunge nyenzo ya kufuatilia shughuli za Serikali. Hatimaye, hujenga raia wanaozalisha zaidi, na Serikali iliyo makini zaidi na hivyo kuleta maendeleo nchini kote.

Uchunguzi huu umeandikwa si kwa kueleza harakati za wananchi zilizofanyika nchini Uganda mwaka 2003 tu, bali kupata mafunzo ambayo Tanzania itajifunza na kuyatumia. Hivi sasa nchini Tanzania mtandao wa asasi za kiraia umekabidhi Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari kwa Wizara husika kama ilivyokuwa muswada wa sheria kama huo nchini Uganda. Kwa hiyo, maelezo yatakayofuata yatadokeza njia mbalimbali ambazo Tanzania inaweza kuzitumia ili kuendelea na kampeni zake za kupata habari.

2. MuktadhaBaada ya kupata uhuru kutoka kwa Mwingereza mwaka 1961, Uganda imepitia miongo mingi ya machafuko ya kisiasa mpaka ilipotulia kiasi kuanzia mwaka 1986, na kuendelea na utulivu huo hadi sasa. Japokuwa kumekuwa na azimio hili, “kutokuwapo kwa utulivu wa kisiasa na usimamizi mbaya wa uchumi vimesababisha hali ya kuanguka kwa uchumi kwa mfululizo kulikoifanya Uganda kuwa miongoni mwa nchi masikini na zisizoendelea zaidi duniani” (Taasisi ya Mambo

1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa kama sehemu ya kutimiza masharti ya shahada ya uzamili katika Maende-leo Endelevu - Uchambuzi wa Sera na Utetezi Taasisi ya Masomo ya Uzamili ya SIT Brattleboro, Vermont, Marekani. Shukrani nyingi zimfikie Profesa Jeff Unsicker.2 Ni raia wa Marekani, na baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza, Tony Baker alienda kuishi kwa miaka miwili katika kijiji Mlima Hanang, kaskazini mwa Tanzania. Afanyakazi bega kwa bega na waku-lima wa vijijini, na kupata ujuzi kuhusu harakati za mapambano za wananchi pamoja na hatua za sera zilizorudisha nyuma maendeleo yao na kusababisha umasikini. Kwa imani kwamba mabadiliko ya sera yanaweza kushughulikia sababu za msingi za umasikini na kutotendewa haki, alirudi tena Marekani ku-somea eneo hilo. Kwa sasa Tony ni mwanafunzi wa uzamili akifanya mazoezi kwa vitendo katika idara ya Uchambuzi wa Sera na Utetezi ya HakiElimu.

Page 4: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

2

ya Afrika,3 2008). Kwa mujibu wa Benki ya Dunia4 (2008), Uganda ilikuwa nchi ya 14 masikini zaidi yenye pato ghafi la ndani la dola za Marekani 340 kwa kila mtu, mwaka 2007. Rushwa imetamalaki.

Mamlaka ya Manunuzi na Uuzaji wa Rasilimali za Umma ya Uganda (PPDA) inakadiria kwamba zaidi ya Fedha za Uganda bilioni 330 (dola za Marekani milioni 184) hupotea kila mwaka kutokana na rushwa katika manunuzi, ambayo ni sawa na asilimia 70 ya bajeti ya Serikali ya mwaka. Makadirio ya Mtandao wa Madeni wa Uganda (UDN) yanataja kiasi kinachopotea kwa rushwa kuwa Ush 200 bilioni (dola za Marekani milioni 108) kwa mwaka. Paul Onapa, msemaji mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Uwazi, tawi la Uganda, anaamini kwamba zaidi ya nusu ya fedha za Serikali zinapotea kwa rushwa. Kiasi hicho kitafikia kiasi cha kutisha cha Fedha za Uganda trilioni 1.76 (dola za Marekani 950 milioni). (Biryetega, 2006)

Makala ya hivi karibu yaliyochapwa na The New Vision, shirika la uchapishaji wa aina mbalimbali za habari ambalo ni maarufu nchini Uganda, yameandika kuwa “Uganda inapoteza kiasi cha Ush bilioni 600 kila mwaka kwa udanganyifu katika manunuzi unaofanywa na maofisa wa Serikali” (Businge & Bugembe, 2008). Kusema kweli kuna tofauti kubwa miongoni mwa makadirio ya kiasi cha fedha kinachopotea kwa rushwa nchini Uganda, ingawa ni kweli kwamba tatizo ni kubwa.

Serikali na asasi za kiraia zinaelewa uzito wa suala hili na zimeanza kuchukua hatua. Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda ulianzishwa mwaka 1999 (ACCU, 2008). Mwaka 2000 uliundwa Mtandao wa Wabunge wa Afrika wa Mapambano Dhidi ya Rushwa (APNAC5). Juhudi za kushughulikia rushwa nchini Uganda zinazidi kupamba moto.

3. WateteziMtetezi wa kupambana na rushwa anayezingatiwa na uchunguzi kifani huu ni Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda, au ACCU.6 Mtandao huu ulianzishwa mwaka 1999, ulisajiliwa kama asasi isiyo ya Serikali (NGO) mwaka 2004 na “ni mtandao unaojitegemea, usiofuata upande wowote, usio wa kisiasa, wa kiserikali wala kibiashara” (ACCU, 2008, uk. 2) “unaojumuisha asasi za kiraia 70, watu binafsi, viongozi wa dini, wasomi, waandishi wa habari, vijana, wanawake, wanasiasa na asasi muhimu” (Kisige & Lule, 2008) katika juhudi za “kuhamasisha na kuongeza uwezo wao kuwa sauti moja na yenye nguvu itakayoweka mikakati inayofaa na kubuni ajenda itakayoleta mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa” (ACCU Sekretarieti,7 2007, uk. 3). ACCU huandaa shughuli za “elimu, utetezi na ushawishi” katika ngazi ya taifa, mkoa na wilaya kwa lengo la kupunguza rushwa (MS, 2007).

Madhumuni ya ACCU yanatajwa kuwa ni asasi ya kiraia (AZAKI) inayojaribu “kujenga jihadi ya kupambana na rushwa iliyo imara nchini Uganda,” “kuongeza uwezo wa asasi za kiraia kuhimiza uwazi, uwajibikaji na kushiriki katika shughuli nyingine za kupambana na rushwa” na “kuhimiza uelewa zaidi na programu za utetezi wa mapambano dhidi ya rushwa” (ACCU, 2008, uk. 3).

3 Chanzo hiki kinaitwa “Bureau of African Affairs” kwenye marejeo.4 Chanzo hiki kinaitwa “World Bank” kwenye marejeo.5 Chanzo hiki kinaitwa “Afrika Parliamentarians Network Against Corruption” kwenye marejeo.6 Anti Corruption Coalition Uganda7 Chanzo hiki kinaitwa “ACCU Secretariat” kwenye marejeo.

Page 5: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

3

Miongoni mwa vipengele muhimu sana kuhusu mtandao huu ni nguvu iliyoko katika muundo wake. Kuliko kuwa asasi iliyopo mahali pamoja inayojaribu kufanya kazi nchi nzima, ACCU ina mitandao 12 ya mikoa inayopambana na rushwa ambayo kila mtandao unahudumia wilaya nyingi. Kwa mujibu wa tovuti ya ACCU vikundi hivyo vya mikoa vina mitandao ifiatayo:

Mtandao wa Kupambana na Rushwa Koboko (ACCK) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nile Magharibi (MAYANK/MACCO) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Uganda Kaskazini (NUAC) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Karamoja (KAC) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Uganda Mashariki Mtandao wa Kupambana na Rushwa Teso (TAC) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Apac (TAACC) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Magharibi ya Kati (Bunyoro) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Rwenzori (RAC) Mtandao wa Kupambana na Rushwa Uganda Kati Mtandao wa Kupambana na Rushwa Ankole Tokomeza Rushwa Kigezi (KICK) [Zamani ulikuwa Mtandao wa Kupambana Rushwa

Kusini Magharibi Uganda (SWUAC)](ACCU: Mtandao wa Kupambana na Rushwa Uganda,8 2008)

Kutokana na kazi ya wanachama hawa wa mtandao, sehemu yote ya Uganda imefikiwa kijiografia na kuwapo kwao, kama inavyonyeshwa katika ramani:

Imechukuliwa kutoka Wikimedia, 2006

8 Chanzo hiki kinaitwa “ACCU: Anti Corruption Coalition Uganda” kwenye marejeo.

Page 6: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

4

Wanachama hawa wa mtandao wa kupambana na rushwa katika mikoa wana Mkutano Mkuu, ambao ni chombo cha utoaji maamuzi (ACCU, 2008). Ni vigumu kuthibitisha hali halisi ya wanachama hawa wa mikoani, kama kila mtandao unajitegemea kweli au hushiriki kwa kutegemea maagizo ya ACCU au wapo kwa majina tu. lakini kwa kuzingatia kuwapo kwao katika tovuti, inaelekea kwamba baadhi wamekomaa kiasi cha kuwa vyombo vinavyoweza kujiendesha. RAC iko hai kiasi cha kurekebisha taarifa za ukurasa wa tovuti katika Mtandao wa Kituo cha Habari cha Mkoa wa Rwenzori (www.ricnet.info/RAC.HTML). Wakati huohuo inaelekea kuwa SWUAC imekua kiasi cha kustahili kubadili jina kuwa Tokomeza Rushwa Kigezi (KICK) na hivi karibuni imefungua tovuti yake (www.ugandakick.net) yenye katiba, programu, wanachama, picha na habari.

Pamoja na wanachama wa mtandao wa mikoa, ACCU inashirikiana na NGO za kimataifa, zikiwemo Shirika la Kimataifa la Kutetea Uwazi (TI), Action Aid, Oxfam Uingereza, World Vision, FIDA, Mtandao wa Haki za Binadamu (HURINET), na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la MS Denmaki (ACCU: Mtandao wa Kupambana Rushwa Nchini Uganda, 2008). ACCU pia inashirikiana na NGO za kitaifa kama vile Mtandao wa Madeni wa Uganda (UDN), Mkakati wa Madhehebu ya Dini kuhusu Maadili na Uadilifu (INFOC-Uganda) na Mtandao wa Maendeleo wa Vyama vya Kizalendo na vya Hiari (DEVINA) pamoja na watu binafsi (ACCU, Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda, 2008). Asasi hizi hazina uwakilishi katika Mkutano Mkuu wa ACCU kama walivyo wanachama wa mikoa, badala yake, zinachangia ACCU kwa njia ya misaada ya fedha na misaada ya kimikakati.

4. SeraMwaka 2003, Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda (ACCU) ulitilia mkazo zaidi upataji habari. Nchini Uganda, haki ya kisheria ya kupata habari imefafanuliwa wazi katika Ibara ya 41 ya Katiba ya mwaka 1995 inayosema kwamba

(1) Kila raia ana haki ya kupata habari zinazomilikiwa na Serikali au chombo chochote au wakala/shirika la Serikali isipokuwa kama kutolewa kwa habari hizo huenda kutaathiri usalama na uhuru wa Serikali au kuingilia haki ya faragha ya mtu mwingine yeyote.

(2) Bunge litatunga sheria likifafanua daraja za taarifa zilizotajwa katika kifungu cha (1) cha ibara hii na utaratibu wa kupata habari hizo.

(Katiba ya Jamhuri ya Uganda,9 1995)Kama ilivyotajwa hapo juu nyaraka na kumbukumbu za Serikali zinaweza kuangaliwa na umma alimradi kutolewa kwake hakuhatarishi au hakukiuki haki ya faragha ya mtu mwingine.

Ingawa katika vitabu, kupata habari ni haki, lakini kusema kweli Ibara ya 41 inasisitiza kukataliwa kupewa habari. Kukosa kueleweka kwake kunakaribisha maswali mengi yasiyo na majibu. Ni nani anayeamua ni habari zipi zinaweza kuathiri usalama wa taifa au Serikali? Itajulikanaje kama uingiliaji wa faragha ya mtu umetokea? Kutokana na hali hiyo, maofisa fisadi wa Serikali wanaweza kutumia sehemu hii ya sheria kama zana ya kufanyia tabia yoyote ya kihuni (Vyombo vya Habari Uganda–Magazeti, TV na Redio10). Hali hii ilisababisha uzingativu wa ACCU hasa baada ya

9 Chanzo hiki kinaitwa “Constitution of the Republic of Uganda” kwenye marejeo.10 Chanzo hiki kinaitwa “Uganda Press, Media, TV, Radio, Newspapers” kwenye marejeo.

Page 7: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

5

kuona ugumu unaoyapata mashirika wanachama katika ufuatiliaji wa mafungu na mtiririko wa fedha za Serikali katika ngazi ya Serikali za mitaa ambako matokeo ya utendaji usio na ufanisi ni ya kawaida. Ni kutokana na hali hii ndipo ACCU ilipotangaza kwa dhati mwaka 2003 kuwa “viongozi na watawala mafisadi wanatumia kisingizio cha kutotoa habari ili kutetea maslahi yao ya ubinafsi na uchoyo” (ACCU, 2003).

Mpaka wakati ACCU ilipoanza kulalamika mwaka 2003, Serikali ya Uganda ilikwisha lazimishwa kukubali suala hili lakini ilipiga hatua ndogo katika kukabili tatizo hili. Muswada wa sheria tayari ulishaanza kuandikwa kwanza na Wizara ya Huduma za Umma halafu ikapewa Wizara ya Maadili na Uadilifu. Baada ya hapo, jukumu hilo lilihamishiwa Wizara ya Habari (ACCU, 2003). Kama ucheleweshaji huu wa kiutawala ilikuwa dalili ya udhaifu wa Serikali au kukwepa kwa makusudi kwa suala hili, haiwezi kusemwa kwa uhakika. Kwa hali yoyote ile, ACCU iliona kuwa ni vizuri zaidi kutatua matatizo ya sera ya Ibara ya 41 kwa kuitaka Serikali kuuweka muswada huu wa sheria unaohusu kupata habari katika ajenda ya taifa katika kipindi cha miezi sita na hivyo kuweka lengo kwa “Serikali kuahidi kutunga sheria iliyo wazi kuhusu upataji wa habari bila ya kuwa na masharti mengi” (ACCU, 2003). Katika kipindi cha miezi sita walitaka waone muswada wa sheria unakamilika kuandikwa, kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura na kupitishwa.

5. SiasaIli kuweka katika muktadha wa malengo ya kisiasa ya kampeni hii, itakuwa muhimu kwanza kuangalia muundo wa sekta ya Serikali tunayojadili. Kwa mujibu wa Katiba mpya ya Uganda ya 1995, Rais ndiye Mkuu wa Nchi, Serikali na Majeshi ya Ulinzi na anasaidiwa na Makamu wa Rais na Baraza la Mawaziri. Mawaziri wana mamlaka ya kutayarisha mapendekezo ya sera na kuwasilisha bungeni ambako ndicho chombo chenye mamlaka ya kubadili pendekezo au muswada wa sheria kuwa sheria (Katiba ya Jamhuri ya Uganda, 1995). Pamoja na Rais na Makamu wa Rais, Baraza la Mawaziri lina makundi mawili ya wajumbe: Mawaziri wa Baraza la Mawaziri na Mawaziri wa Nchi, (Baraza la Mawaziri la Serikali ya Uganda11). Ni mjumbe wa kundi hili la pili ndiye aliyepata msisitizo mkubwa wa kampeni ya ACCU.

Kwa kuwa jukumu la kuufikisha bungeni muswada huu wa sheria kwa sasa liko mikononi mwa Wizara ya Habari, imekuwa ndiyo mlengwa mkuu wa ACCU. Kiuhalisia zaidi mamlaka yapo mikononi mwa mtu mmoja, Dkt. Nsaba Buturo, Waziri wa Nchi wa Habari (ACCU, 2003). Kisiasa ni yeye ndiye anayeweza kwa haraka na kwa urahisi na moja kwa moja kuitaka Serikali kuwasilisha muswada wa sheria katika kipindi cha miezi sita.

Wakati huohuo, ACCU imelenga taasisi nyingine za Serikali na maofisa watakaoweza kumshinikiza Waziri wa Nchi wa Habari. La kwanza na muhimu zaidi, kuliona suala hili linahusika sana na ufisadi wa Serikali, ACCU imetafuta rafiki katika ofisi ya Inspekta Jenerali wa Serikali (ACCU, 2003), afisa anayesimamia na kuzingatia utawala wa sheria, anayehimiza utawala bora, anayepeleleza rushwa katika juhudi za kutokomeza na kuongeza uelewa wa umma kuhusu maadili ya Serikali (Katiba ya Jamhuri ya Uganda, 1995). Waziri wa Nchi wa Maadili na Uadilifu ambaye hapo awali alikuwa na jukumu la kuandaa muswada wa sheria kabla ya jukumu hilo kuhamishiwa Wizara ya Habari, na aliyejua kwa kina masuala hayo na taratibu zinazohusika, naye pia alilengwa kuisaidia (ACCU, 2003). Spika wa Bunge ambaye ni mwakilishi mkubwa wa umma bungeni

11 Chanzo hiki kinaitwa “The Cabinet of Uganda Government” kwenye marejeo.

Page 8: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

6

na mwenye kuamua ajenda (Katiba ya Jamhuri ya Uganda, 1995), alikuwa mshirika mwingine muhimu mwenye mamlaka makubwa, kwa kuwa alikuwa alama ya bunge ya kukaribisha muswada wa sheria wa siku zijazo, unaoruhusu upataji habari. Mwisho, ACCU ilitafuta kuungwa mkono na Makamu wa Rais (ACCU, 2003), ambaye, kama mjumbe wa Baraza la Mawaziri, anafanya kazi kwa karibu zaidi na Waziri wa Nchi wa Habari. Walengwa wote hawa wa kisiasa wana nafasi muhimu kwa mada hii, kwa kuwa uandikaji wa muswada wa sheria mwanzoni ulianzishwa na Serikali, kutosimamia hivi sasa kutakuwa kama kudhoofisha juhudi zake.

Pamoja na wanachama wake wa kawaida, ACCU ilitafuta washirika wengine zaidi wa utetezi kwa ajili ya suala hili. Orodha hii ndefu inajumuisha Kikosi cha Wavulana na Wasichana cha Uganda (BGCU), Chama cha Taifa cha Wanafunzi wa Uganda (UNSA), Mshikamano wa Wanawake wa Uganda kwa Maendeleo (UWOTODEV), Jubilee Plus – Uganda, Chama cha Sanaa za Maonesho cha Kimataifa cha Kupambana na Rushwa (IATM), Mtandao wa Asasi za Kitaalamu (NEPRO), Steadfast Peace, Mtandao wa Wabunge wa Afrika wa Mapambano Dhidi ya Rushwa (APNAC) na Chama cha Bunge la Vijana (YPA) (ACCU, 2003).

6. MkakatiKatika ripoti iliyotayarishwa baadaye na kueleza madhumuni na shughuli, Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda (ACCU) ulieleza kwa uwazi mkakati wao kwa kampeni hii ya sera kama ifuatavyo:

Kuweka umuhimu wa umma kupata habari kwenye ajenda ya taifa katika kipindi cha miezi sita hivi inayofuata.

Kujenga uelewa miongoni kwa jamii za vijijini kuhusu haki zao kama zilivyoandikwa katika katiba na kuwahimiza wadai haki hizi na kuzitumia ipasavyo.

Kutumia vyombo vya habari vyote na kuwahamasisha matabaka yote ya kijamii nchini Uganda kuhusu umuhimu wa sheria yenye uwazi. Hatimaye hii itafungua njia ya kuwahusisha wadau wote kuanzia watunga sera hadi wa wananchi vijijini kuzungumza kwa sauti moja na kudai kuhusishwa katika mchakato unaofuata wa kutayarisha sheria kuhusu upataji wa habari.

Kukusanya habari na uchunguzi kifani kuhusu matatizo yaliyokabiliwa na asasi za kiraia katika kupata habari katika Serikali za Mitaa.

Kujenga uelewa na ushiriki kuhusu rushwa miongoni mwa watoto na vijana pamoja na kuongeza matumizi ya maigizo shirikishi katika shughuli za kupambana na rushwa.

Kutangaza ACCU na kuiwezesha ionekane zaidi. (ACCU, 2003)

Ingawa ilikuwa ni njia yenye sura nyingi, kiini cha mkakati huu kimelenga zaidi kuongeza uelewa wa umma kuliingiza suala hili katika ajenda ya taifa.

7. MbinuIli kutekeleza mkakati wao, ACCU imetumia mbinu mbalimbali. Mbinu zote zilikuwa chini ya

Page 9: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

7

mwamvuli mmoja wa tukio lililojulikana kuwa Wiki ya Kupambana na Rushwa iliyofanyika kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi tarehe 2 Novemba, 2003 katika wilaya za mikoa wanachama wa mtandao nchini kote. Fedha zilichangishwa na ACCU na kusambazwa kwa wanachama wa mtandao kupitia sekretarieti. Baadaye zilifanyika shughuli mbalimbali za kupambana na rushwa katika maeneo husika, wanachama wa ACCU na wabia wao walishiriki kwa ukamilifu katika wiki yote ili kuhakikisha sauti zao zinasikika (ACCU, 2003).

Kwanza, katika matayarisho ya Wiki ya Kupambana na Rushwa, kamati ya vyombo vya habari ya ACCU ilifanya kazi ya kuwaalika wananchi washiriki katika shughuli mbalimbali zinazotarajia kufanyika. Makala ya matoleo maalumu yalichapishwa kwenye magazeti mbalimbali ya kitaifa na ya mikoani. Mkutano na vyombo vya habari ulitangazwa kwenye vipindi 27 vya mazungumzo katika redio na vipindi viwili vya televisheni nchini kote. Muda wa matangazo ulilipiwa na Inspekta Jenerali wa Serikali na kutangaza mazungumzo yaliyorekodiwa, maigizo ya kuchekesha na ujumbe kuhusu uhuru wa kupata habari (ACCU, 2003).

Katika uzinduzi rasmi wa wiki hiyo, kulikuwa na maandamano yaliyoandaliwa na Jubilee Plus pamoja na mabango, vipeperushi na magari ya wazi yenye wasanii wanaofanya maonyesho, yaliyopita katika Uwanja wa Katiba wa Kampala ambako wawakilishi wa Serikali kuu na Serikali za mitaa walikuwepo pamoja na wajumbe wa asasi za kiraia. Sherehe zote ziliongozwa na Inspekta Jenerali kwa maombi ya ACCU. Katika wilaya nyingine IATM iliongoza maandamano na Spika wa Bunge alikuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi. Wilaya nyingine zilifanya maandamano yao katika miji mikuu ya mikoa (ACCU, 2003).

Hali kadhalika mjini Kampala, INFOC-Uganda iliandaa mkutano wa taifa uliyofunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi wa Maadili na Uadilifu. Mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe 200 kutoka Serikalini, bunge na asasi za kiraia walioeleza uzoefu wao kuhusu ugumu wa kupata habari na kusisitiza umuhimu wa watungasheria (wabunge) kushughulikia jambo hili muhimu. Katika siku nyingine mjini Kampala, NEPRO iliandaa mkutano wa asasi za kitaaluma kujadili mada hiyo. Katika wilaya nyingine zote, mikutano ya aina hiyo ilifanywa (ACCU, 2003).

Wilaya za nchini Uganda zilifanya mazungumzo ya hadhara na majopo ya majadiliano kuhusu rushwa na upataji habari. Jubilee Plus, IATM, Shirika la Kimataifa la Kutetea Uwazi – Uganda, DENIVA au mitandao ya ACCU mikoani iliandaa na kuliwezesha kila tukio (ACCU, 2003).

Katika wilaya 12, UNSA iliendesha mashindano ya midahalo shuleni ambapo mada ilikuwa umuhimu wa kupata habari na umuhimu wake kama zana ya kupambana na rushwa. Wana mjadala bora waliendelea kushindana kimkoa na halafu kitaifa, yote hayo ndani ya wiki ya kupambana na rushwa. Hali kadhalika midahalo mingine ya shule na ya wazi ilifanywa (ACCU, 2003).

Baadhi ya wilaya ziliendesha mashindano ya kuimba yenye mada maalumu na kuongeza uelewa wa kampeni. Katika mashindano hayo yote, wasanii 29 wa wilayani, shule za sekondari 25, na vikundi mbalimbali vya kwaya, walitunga nyimbo za kupambana na rushwa na kushiriki katika mashindano ya kuimba. Nyimbo zinazoelimisha na zenye ujumbe kulingana na mada zilitengenezwa kitaalamu na kusambazwa katika CD kwenye vituo vya redio vilivyozipiga wakati wa vipindi vyao vya muziki vya kila siku (ACCU, 2003).

Page 10: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

8

Maigizo na tamthilia navyo vilitumiwa. Tamthilia 18 za jukwaani zilionyeshwa katika maeneo mbalimbali ya soko. IATM ilifanya tamthilia shirikishi katika wilaya zote tisa (ACCU, 2003).

Katika wilaya nyingine kulitayarishwa vyanzo vya taarifa na makala katika kipindi cha wiki hiyo. Utafiti wa wananchi kuhusu uzoefu wao wa kupata habari ulifanywa. Wanachama wa ACCU walizindua kwa mara ya kwanza vitabu vitatu vidogo kuhusu kupambana na rushwa kwa asasi za kiraia. Brosha na vijitabu vinavyolenga bunge kuhusu suala la kupata habari vilitayarishwa. Mwishoni, muswada wa igizo lililokuwa na jina la Pazia uliandikwa (ACCU, 2003).

Hatimaye, mbinu nyingine kadhaa zilitumika. Maeneo na mikusanyiko ya kidini yalitumika wakati mahubiri kuhusu uovu wa maofisa fisadi yalifanywa. Wanachama wa mtandao wa mikoani pamoja na INFOC-Uganda walisambaza waraka wao. Hata mashindano ya mpira yaliyojulikana kwa jina la Kombe la Kupambana na Rushwa yalifanyika ambapo wanachama wa asasi za kiraia walicheza dhidi ya maofisa wa Serikali za mitaa (ACCU, 2003).

8. TathminiKwa kuangalia mchakato wa kampeni hii ya utetezi, Wiki ya Kupambana na Rushwa imekuwa na matokeo mazuri. Nadharia ya hoja kumi za Veneklasen na Miller (2002) kwa ajili ya utayarishaji wa ujumbe itatumika kama mfumo wa uchambuzi wa kufaa kwa ujumbe huo. Hoja hizo ni pamoja na:

1. Ijue hadhira yako. 7. Tayarisha ujumbe kulingana na njia2. Elewa mazingira yako ya kisiasa na wakati. ya kuufikisha.3. Hakikisha kuwa ujumbe ni rahisi na mfupi. 8. Iruhusu hadhira ifikie uelewa wao.4. Tumia matukio halisi ya maisha na madondoo. 9. Ihimize hadhira ichukue hatua.5. Tumia lugha fupi, yenye nguvu na vitenzi 10. Wasilisha ufumbuzi unaoweza

tendaji. kupatikana.6. Tumia hoja zinazoeleweka na namba kwa ubunifu. (kur. 232-234)

Hoja hizo zinajadiliwa kama ifuatavyo.

Kwanza ACCU walijua hadhira yao na waliikabili katika viwango mbalimbali. Maofisa wa Serikali walishirikishwa moja kwa moja, mtandao wa AZAKI uliundwa, NGO za kitaifa na kimataifa zilihusishwa, na juhudi zilifanywa kuwaelimisha, kuwashirikisha na kuwahamasisha wananchi kwa kutumia mbinu zenye mielekeo mbalimbali. ACCU walijua ipasavyo mazingira ya kisiasa. Badala ya kuikabili Serikali kuhusu ufisadi wake, ACCU walijitokeza katika siasa kama marafiki wanaojaribu kuisaidia Serikali kukamilisha jambo ambalo tayari imekusudia kulifanya. Maofisa wa Serikali walikuwa washiriki wenza katika Wiki ya Kupambana na Rushwa na kugharimia hata baadhi ya shughuli. Mbinu hizi si kama zilihusu suala hili tu, bali zilikusudia kujenga urafiki na mshikamano binafsi, kama ilivyo katika mashindano ya mpira ya kirafiki. Mtazamo chanya wa ACCU umefanikisha sana ajenda yao katika uwanja huu wa siasa katika mazingira ya kisiasa ambayo huenda yasilete matokeo mazuri wakati wa mashambulizi.

Page 11: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

9

Matukio halisi ya maisha ya kutoruhusiwa kupata habari yametolewa na washiriki wa mazungumzo ya wazi, majopo ya majadiliano na utafiti uliofanywa nchini kote na halafu vilitayarishiwa makala na nyenzo. Hatimaye ujumbe, ulitumiwa katika njia mbalimbali za kupasha habari zikiwemo redio, televisheni, vitabu, mchezo wa kuigiza, nyimbo, mikutano, tamthilia za mitaani, mahubiri na hata michezo. Kila moja ya vyombo hivi vya kupitishia ujumbe kiliwafikia watu kwa njia mbalimbali na bila shaka ilionyesha matumizi ya ubunifu wa hoja na habari. Msisitizo wa mbinu wa ACCU umekuwa katika kuongeza uelewa na kuwahimiza wachangie katika mchakato wa kisiasa kwa kufanya shughuli mbalimbali wakati wa Wiki ya Kupambana na Rushwa ili kila mmoja aweze kushiriki kwa njia atakayoona inafaa zaidi. Mwisho, ufumbuzi ulitolewa, ambao ni muswada mpya wa sheria utakaofafanua na kuipa mamlaka Ibara ya 41 ya Katiba uwasilishwe kwenye ajenda ya bunge na kupitishwa.

Hata hivyo, haielekei kwamba ACCU itatayarisha ujumbe mmoja mahususi na mfupi, na pengine ingewasaidia kuunganisha juhudi zao nchini kote kwa ujumbe mmoja kama njia ya dhahiri. Hali kadhalika, mbinu za Wiki ya Kupambana Rushwa 2003 zilikuwa zikishawishi kwa kiwango cha juu, kwa upande wa mahubiri, ambayo yanaweza kuonekana kuwa ni kutumia nguvu. Bila shaka hali hii imeongeza shaka kuhusu mafanikio yake kwa kipengele cha kuiachia hadhira ifikie hitimisho lake. Ukiacha mifano hii miwili ya kipekee, ACCU imeonesha mfano wa kampeni inayofaa kwa mujibu wa VeneKlasen na Miller (2002).

Katika kutathmini mafanikio kwa msingi wa matokeo, Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003 ilielekea kuwa na mafanikio makubwa. Katika “Masomo ya Ulinganifu kutoka Visa Mkasa vya Utetezi wa Haki za Jamii,”12 Gabrielle Watson (2001) ametaja baadhi ya viashirio vya mafanikio ya utetezi wa haki za jamii (uk. 238) vinavyoweza kutumika kuamua athari ya kampeni ya ACCU.

Kwanza inatokana na mtazamo wa sera—“Sera, sheria, programu, mfano wa jambo lililowahi kutokea, n.k., ilianzishwa na kutekelezwa” (Watson, 2001, uk. 238). Wakati wa sherehe za kufunga, tarehe 2 Novemba, Waziri wa Nchi wa Habari, Dkt. Nsaba Buturo, aliyekuwa mlengwa mkuu wa kampeni ya sera, alitoa tamko la ahadi kwamba Wizara ya Habari itawasilisha kanuni za muswada wa sheria kwenye Baraza la Mawaziri ifikapo Desemba 2003 na kuwa na muswada utakaokuwa tayari kuwasilishwa bungeni mwezi Machi 2004 (ACCU, 2003). Ahadi hii ilikuwa hatua kubwa na matokeo ya moja kwa moja ya Wiki ya Kupambana na Rushwa. Baadaye Sheria ya Kupata Habari ya 2005 ilipitishwa na bunge mwaka 2005, iliridhiwa na Rais tarehe 7 Julai, 2005 na kuanza kutumika tarehe 20 Aprili, 2006. Kwa muhtasari,

Sheria hiyo inahimiza Serikali yenye ufanisi, inayofanyakazi, yenye uwazi na uwajibikaji, huwezesha Ibara ya 41 ya Katiba, huwalinda wapasha habari, inahimiza uwazi na uwajibikaji katika vyombo vyote vya Serikali pamoja na kuwawezesha wananchi kuchambua ipasavyo na kushiriki kwenye mamuzi ya Serikali yanayowaathiri. (Babalanda 2006)

Kutokana na haya, ni dhahiri kwamba kwa matokeo ya sera, Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003 ilikuwa na mafanikio makubwa.

12 Chanzo hiki kinaitwa “Comparative Lessons from Social Justice Advocacy Case Studies” kwenye marejeo.

Page 12: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

10

Jambo la pili linahusu miundo ya utawala—“Nafasi ya kidemokrasia ilipanuliwa; Njia mpya za ushiriki; Uhuru wa kutenda, kuhusika; Wadhifa, uaminifu na mamlaka ya washiriki wa kampeni kuimarika” (Watson, 2001, uk. 238). Kwa upande wa Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003 inaelekea kuwa na mafanikio makubwa. Uaminifu wa washiriki wengi katika kampeni hii uliimarishwa kwa mafanikio ya wiki hiyo; hata hivyo, mafanikio ya aina hii yalipatikana miaka kadha baadaye baada ya kupitishwa na kutekelezwa kwa Sheria ya Kupata Habari ya 2005 ambayo imefungua njia mpya zaidi za ushiriki wa kidemokrasia na uhuru wa uhusika wa Serikali.

Tatu ni kiashirio kinachohusu asasi za kiraia:

Asasi za vijijini zilizo imara na NGO zenye miundo ya kiukamilishi na uwajibikaji; Uwezo wa kueleza haki (kisiasa, kiraia, kijamii na kiuchumi) na kuandaa mapendekezo kudai haki hizi; Kuongezeka kwa uelewa wa wanachama na sekta nyingine za jamii ya kiraia na umma kuhusu masuala yaliyopo. (Watson, 2001, uk. 238)

Mwitikio, juhudi na uimarishaji wa AZAKI wakati wa Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003 ulikuwa mkubwa. Haki ya kupata habari ilitangazwa sana kiasi kwamba raia wote wa Uganda nchini kote walielewa na kujadili kwa uwazi katika vikao mbalimbali, kwa hiyo kampeni hii ya ACCU ilionyesha mafanikio makubwa.

9. Mafunzo YaliyopatikanaMatendo na matukio katika uchunguzi kifani wa Uganda yaliyoelezwa hapo juu yanatoa mafunzo kwa utetezi wa sera nchini Tanzania kuhusu kampeni yake kwa ajili ya kupata habari. Mafunzo haya yanahamishika kutokana na kufanana kwa mazingira ya masuala yote kama ilivyo Uganda. Rushwa nchini Tanzania ni kikwazo kikubwa cha muda mrefu na imekuwa ikitangazwa sana katika vyombo vya habari, bungeni na kwa wananchi kwa ujumla. Hali kadhalika asasi za kiraia nchini Tanzania zinaanza kuvutiwa. Mwezi Agosti 2007, mtandao wa AZAKI uliandika na kuwasilisha Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari mwitikio wao kwa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Kupata Habari ambao asasi za kiraia zimeuona kuwa ni sheria katili yenye uonevu ambayo itakandamiza haki ya kupata habari kuliko kuimarisha. Kama ilivyokuwa kwa muswada wa sheria ya kupata habari uliobaki katika Wizara ya Habari nchini Uganda, Muswada wa Haki ya Kupata Habari wa Tanzania umefikia hatua ileile ya kutoenda popote ndani ya Wizara ya Habari, ingawa kumekuwa na ahadi za mara kwa mara za kuwasilisha muswada huo bungeni (Moshiro, 2008).

Sasa, kwa kuwa juhudi za utetezi zimetulia kwa muda nchini Tanzania, kampeni ya kupata habari, iliyoongozwa na Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda, unatoa mafunzo muhimu kwa asasi za kiraia nchini Tanzania kuhusu namna ya kusonga mbele na kampeni kutoka hali yake ya ufungwa. Mikakati mitano muhimu ya utetezi iliyoko katika kampeni ya ACCU inaelekea ni muhimu sana kwa hali ya sasa ya Tanzania.

Jambo la kwanza na muhimu kabisa, wakati watetezi wa Kitanzania wamefanikiwa kuunda Mtandao wa Uhuru wa Habari na Kujieleza—mtandao wa wanachama 11 zikiwemo AZAKI za ndani ya nchi na za kimataifa—kama ilivyofanya ACCU kwa wabia wake, muundo wa kitaasisi wa ACCU ni tofauti kabisa kwa siasa kali na imechangia sana ushindi wao. Kwa kawaida NGO na

Page 13: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

11

AZAKI zina ofisi makao makuu na pengine ofisi chache za mikoa, na hujaribu kufanya miradi na kampeni nchini kote. Kwa upande wa Tanzania shughuli nyingi za AZAKI zipo Dar es Salaam. Hali kadhalika kwa Mtandao wa Uhuru wa Kupata Habari na Kujieleza ambapo wanachama wake wote nchini wako Dar es Salaam. Ingawa hali hiyo bila shaka inapata mafanikio ya kiasi fulani, baadhi ya kampeni pengine kama hii kwa ajili ya haki ya kupata habari, inahitaji kuungwa mkono na wananchi wote nchini ili kukabili upinzani. Kwa maneno mengine, kwa kuwa sauti zote zinatoka Dar es Salaam tu, Waziri wa Habari hana sababu ya kutosha ya kuwasilisha muswada huu wa sheria bungeni. Hali ya kuweko mikoani na wilayani kwa ACCU kumetanzua mtanziko huu. Kama inavyoonekana katika ramani hapo juu, maeneo ambayo wanachama wa mikoa 12 wa mtandao wanaendesha shughuli zao, yanahusisha takribani nchi yote. Wakati Wiki ya Kupambana na Rushwa ilipokuja mwaka 2003, haikuwa tukio moja kubwa linalotokea katika mji mkuu tu, bali ni shughuli nyingi za kupambana na rushwa zilizoratibiwa na zinazofanyika wakati mmoja nchini kote Uganda. Kuwapo kwake hakukuweza kupingwa.

Ni uwezo wa kupanua uhusiano kuwa matawi imara nchini kote ndiyo unaohitajika katika kampeni ya Tanzania. AZAKI nyingi, kama vile zile za mtandao, zina mwelekeo huo, lakini hazifiki mbali. Vikundi mara nyingi huwa na asasi wabia nchini kote lakini wabia hao huwa watu binafsi ambao wanawasiliana nao mara chache au kuonana nao katika mikutano kuliko kuwasiliana kila wiki ili kuhakikisha kuwa utekelezaji unaendana na mkakati wa kampeni. Hali kadhalika, AZAKI zina wanachama nchini kote, lakini hawajikusanyi kuunda chombo cha Mkoa. Mifano hii yote inaonyesha uwezekano wa kuunda matawi ya mikoa kama yale ya ACCU yanayoweza kuhamasishwa kwa urahisi ili kupata chombo cha kitaifa.

Pili, kama ilivyodokezwa hapo juu, mtazamo chanya na wenye manufaa ambao ACCU imetumia kwa Serikali umeleta mafanikio makubwa. Katikati ya suala linalohusu rushwa ambapo Serikali na maofisa wake wangeweza kulengwa kwa urahisi kama wapinzani katika mapambano dhidi ya asasi za kiraia, ACCU imegeuza kuwa ushirikiano wa pamoja wa Serikali na asasi za kiraia katika mapambano dhidi ya suala fulani ambalo pande zote zinataka kuboresha. Hii imesababisha kampeni yenye mafanikio makubwa kuliko ambavyo mapambano hasi dhidi ya Serikali yangefanya.

Hii ni changamoto mahususi nchini Tanzania ambapo AZAKI zimekuwa mara kwa mara zikionekana kwa Serikali kama wachochezi wenye fujo ambao mara nyingi hutumia muda wao “kwa kutoa shutuma zisizostahili” na “kudharau juhudi” za Serilaki (Mwakalebela, 2009). Angalia kauli ifuatayo kuhusu uhusiano kati ya AZAKI na Serikali iliyotolewa na Mbunge wakati wa maonesho ya hivi karibu ya asasi za kiraia kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma: “Pande mbili hizi zina uadui ingawa zote zinatimiza malengo yanayofafana—kuwahudumia watu. Asasi za kiraia huwafanya wabunge kama maadui” (Mwakalebela). Hali hii ni hatari kwa juhudi za kampeni kwa sababu hatimaye wabunge hawa wana mamlaka ya kuupa mtandao kile wanachotaka. Kwa Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari kupitishwa kuwa sheria kunahitajika kazi kubwa ya kurekebisha uhusiano huu kuwa ni wa ushirikiano na Serikali kufikia lengo moja, kama ilivyokamilishwa na ACCU.

Tatu, kiwango cha mbinu zilizofanywa na ACCU wakati wa Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003 kimeonesha kujitolea kwa dhati na ubunifu vilivyoleta matokeo makubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi. Kwa kuangalia kwa jumla, wananchi ndio wapokeaji wa nguvu ya matukio na shughuli vilivyowaarifu kuhusu haki ya kupata habari. Hii pia imetokana na hali ya ACCU

Page 14: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

12

kuwa hadi mikoani na wilayani kuwezesha kupata hali halisi ya mtu, mawazo yaliyochochewa na michango ya wajumbe wote wa mikoa. Hatimaye, wakati wa Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003, Mganda atakuwa ameangalia maigizo ya mitaani, kushuhudia jopo la majadiliano ya wazi, kushiriki katika maandamano, kufungua televisheni na kuangalia mazungumzo na kusikiliza wimbo mpya redioni, vyote vinahusu kupambana na rushwa na haki ya kupata habari.

Vipengele hivi vinasababisha funzo la nne kutoka kampeni ya ACCU kuhusu haki ya kupata habari kwa ujumla. Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003 inatoa onyo la namna ya kutetea haki kati ya vyombo vyenye mamlaka visivyoonekana. Kama ilivyofafanuliwa na Veneklasen na Miller (2002), mamlaka yasiyoonekana imeelezwa kuwa ni “mchakato, mienendo, kanuni za utamaduni na mila na desturi (ambazo) hujenga uelewa wa watu kuhusu mahitaji yao, majukumu, mambo yanayowezekana na matendo yanayozuia hatua zinazofaa kuleta mabadiliko” (uk. 50). Kudhibiti kupata habari kwa aina hii ya mamlaka na “inaweza kuongeza hisia za kutokuwa na mamlaka, ujinga na kujilaumu” (uk. 49). Wanyime watu kupata habari kwa muda mrefu, na wataamini kuwa kanuni kwamba hawana haki ya kupata, na kwamba wamekosea kudai haki hiyo. Hii ina ukweli kwa Tanzania, ambako mamlaka na maarifa huwatenganisha wananachi na Serikali kwa kiwango kikubwa. Athari hizi zinapanua kazi ya utetezi kuanzia kutanzua tatizo hadi mahali pa kuanzia pa ngazi ya chini pa kuliona tatizo. Utetezi si kama unatoa ufumbuzi tu, bali huinua uelewa wa watu ili wafahamu kuwa tatizo lipo hasa. Kwa hiyo katika muundo wa mamlaka yasiyoonekana, Veneklasen na Miller wanaeleza elimu, ushirikiano, uelewa wa siasa, kubadilishana matukio na kusema kuwa ni zana za utetezi zinazofaa (uk. 50), zana ambazo ACCU imezitumia ipasavyo katika kampeni yao ya kudai haki ya kupata habari na hiyo itasaidia sana katika kampeni za Tanzania.

Mwisho, wakati kujenga uelewa kwa wananchi wote ni muhimu, ndivyo ilivyo pia kuzingatia walengwa sahihi wa kampeni. Kwa lugha rahisi ni kwamba walengwa ni wale wenye mamlaka ya kuwapa watetezi kile wanachotaka. Kwa hali ya Uganda na Tanzania, walengwa ni wa aina moja—Waziri wa Habari ana mamlaka ya kupeleka muswada wa sheria ya kupata habari bungeni na wabunge nao wana mamlaka ya kutunga sheria. Hawa ni watu mahsusi na wakati juhudi kubwa zinatakiwa kufanywa kuwahamasisha wananchi kwa ujumla, isisahauliwe kwamba hatimaye kampeni hii itawategemea maofisa wachache wa Serikali. ACCU ilifanya urafiki na Inspekta Jenerali, Waziri wa Nchi wa Maadili na Uadilifu na Spika wa Bunge na kufikia hadi kuwafanya wageni rasmi wa baadhi ya matukio ya Wiki ya Kupambana na Rushwa. Hali kadhalika ni muhimu kwamba mtandao wa uhuru wa kupata habari na kujieleza unajitambulisha na kujihusisha karibu zaidi na wanasiasa wanaoelekea kuwaunga mkono kama vile Waziri wa Nchi wa Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na wakuu wa baadhi ya asasi za Serikali kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (CHRAGG).

Kusema kweli, kutangaza kampeni ya haki ya kupata habari si jambo rahisi. Inahitaji ujanja na kutoyumba. Wakati msisitizo lazima uwekwe kwa baadhi ya maofisa wa Serikali, kuongeza uelewa wa wananchi wote ni muhimu pia. Wakati kukata tamaa hutokea unapofanya kazi na Serikali isiyokubaliana, hata hivyo kunahitajika uangalifu katika kulinda uhusiano uliopo. Haya yote ni maeneo ambayo waendesha kampeni wa Tanzania kutetea haki ya kupata habari wanaweza kujifunza kutoka kwa wenzao wa Uganda.

Page 15: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

13

10. HitimishoUganda inaendelea kupambana na rushwa kwa njia mbalimbali. Vita havijaisha, lakini harakati za asasi za kiraia zinaongezeka kila siku. Mafanikio ya Wiki ya Kupambana na Rushwa 2003 yamechochea ACCU kuendelea kutumia mbinu hii katika miaka yote ya karibuni ili kuongeza uelewa wa rushwa katika nyanja za manunuzi ya umma, elimu ya msingi na huduma za afya. Kutokana na kazi ya asasi kama vile Mtandao wa Kupambana na Rushwa Nchini Uganda, kuna matumaini kwamba wananchi na Serikali wataendelea na juhudi zao za kujenga maisha bora kwa pamoja na kwamba Tanzania inaweza kuiga toka kwao.

Page 16: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

14

MarejeoACCU. (2003). Anti Corruption Week 2003 Report. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka

http://www.anticorruption.or.ug/index.php?option=com_docman&task=doc_download&gid=4&Itemid=

ACCU. (2008). Articles and Memoranda of Association of Anti Corruption Coalition Uganda. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.anticorruption.or.ug /index.php?option =com_docman&task=doc_download&gid=6&Itemid=

ACCU: Anti Corruption Coalition Uganda. (2008). ACCU Members & Partners List. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.anticorruption.or.ug/index.php ?option =com _content&view=article&id=18&Itemid=9

ACCU Secretariat. (2007). Annual report January-December 2007. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.anticorruption.or.ug/index.php?option=com_docman &task=doc_download&gid=3&Itemid=

APNAC. Uganda Report. Ilipatikana January 18, 2009, kutoka http://www.apnacafrica.org/uganda_report_e.htm

Babalanda, V. (2006, Oktoba 18). Uganda: It’s your right to get information. The Monitor. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka www.humanrightsinitiative.org /programs/ai/rti/international/laws_papers/uganda /its_ur_rt_to_get_info_vincent _babalanda.pdf

Biryetega, S. (2006). Reporter’s notebook: Uganda. Global Integrity. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.globalintegrity.org/reports/2006/UGANDA/notebook.cfm

Bureau of African Affairs. (2008, Novemba). Background note: Uganda. U.S. Department of State. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.state.gov/r /pa/ei / bgn/2963.htm

Businge, C., & Bugembe, A. (2008, Desemba 18). Uganda: Country Loses Sh600 Billion Annually Due to Corruption. The New Vision. Ilipatikana January 18, 2009, kutoka http://allafrica.com/stories/200812190054.html

Constitution of the Republic of Uganda. (1995). Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.ugandaonlinelawlibrary.com/files/constitution/constitution_1995.pdf

KICK. (2006). KICK Kick Corruption Out of Kigezi. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.ugandakick.net/

Kisige, A., & Lule, J. (2008, Mei 24). Anti-corruption war boosted. Sunday Vision, Uganda. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.assetrecovery.org/kc /node/0a45a4fc-29f7-11dd-846b-9d0d584fafe2.html.0;jsessionid=C21543031D240CD9A1FECFF9CF41F49E

Moshiro, G. (2008, Oktoba). Mkuchika and the specter of the past. Media Watch, 103, 7, 11. Ilipatikana May 16, 2009, kutoka http://www.mct.or.tz/images/stories/MediaWatch/media%20watch%20october%202008.pdf

MS Danish Association for International Co-operation (2007, Mei 7). Anti Corruption Coalition Uganda (ACCU). Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.ms.dk/sw19200.asp?cardId=113

Page 17: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

Mwakalebela, L. (2009, Juni 29). Civic societies blamed for delaying CDF. Daily News, p. 3.

Rwenzori Anti Corruption Coalition (RAC). Rwenzori Region Information Center Network. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.ricnet.info/RAC.HTML

The Cabinet of Uganda Government. My Uganda. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.myuganda.co.ug/govt/cabinet.php

Uganda Press, Media, TV, Radio, Newspapers. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://www.pressreference.com/Sw-Ur/Uganda.html

VeneKlasen, L., & Miller, V. (2002). A new weave of power, people, & politics: The action guide for advocacy and citizen participation. Oklahoma City, OK: World Neighbors.

Watson, G. (2001). Comparative lessons from social justice advocacy case studies. In Cohen, D. et al (Eds.), Advocacy for social justice: A global action and reflection guide. Bloomfield, CT: Kumarian Press.

Wikimedia. (2006, Julai 20). Image: Kalangala district Uganda.png. Wikimedia Commons. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://commons.wikimedia.org/wiki/Image:Kalangala_District_Uganda.png

World Bank. (2008, Oktoba 17). Gross national income per capita 2007, Atlas method and PPP. World Development Indicators Database. Ilipatikana Desemba 8, 2008, kutoka http://siteresources.worldbank.org/DATASTATISTICS/Resources/GNIPC. pdf

Page 18: Mafunzo kwa Tanzania Kuhusu Kufanikisha Haki ya Kupata Habari: Kampeni ya Mtandao wa ...hakielimu.org/files/publications/Lessons for Tanzania... · 2014-05-04 · ya 1995, Rais ndiye

Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi

HakiElimu imeanzisha Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi (Working Paper Series) kwa lengola kuchapisha upya makala mbalimbali za uchambuzi katika muundo ambao ni rahisi kuwafikia nakusomwa na watu wengi. Mlolongo wa nyaraka hizi unatarajiwa kuchangia katika kujengaufahamu wa jamii na katika mdahalo kuhusu masuala ya elimu na demokrasia.

Mlolongo huu unajumuisha taarifa na makala mbalimbali zilizoandikwa na wafanyakazi na wanachama wa HakiElimu, mashirika na watu binafsi waliokuwa na ubia nasi. Baadhi ya nyaraka hizi zimeandikwa mahsusi kwa ajili ya mlolongo huu, wakati nyingine zinatokana na kazizilizokwisha chapishwa hapo awali. Nyaraka nyingi zilizochapishwa katika mlolongo huu nimakala ambazo uandishi wake bado unaendelea, hivyo hazikukusudiwa kuwa ni nyarakazilizokamilika kabisa.

Maoni yanayotolewa humu ni ya mwandishi (waandishi) mwenyewe na si lazima yaweyanawasilisha maoni ya HakiElimu au taasisi nyingine yoyote. Mawasiliano yote kuhusu makalamahsusi katika mlolongo huu yafanywe moja kwa moja kwa waandishi wake; kwa kadiriinavyowezekana, anuani zao zimeonyeshwa katika tanbihi/rejea chini ya ukurasa wa 1 wa makalahusika.

Nyaraka hizi zinaweza pia kupatikana katika tovuti ya HakiElimu: www.hakielimu.org. Nyarakazote zinaweza kuchapishwa kwa minajili isiyo ya kibiashara baada ya kupata idhini ya maandishi kutoka kwa HakiElimu na mwandishi husika.

Lengo letu ni kuchapisha makala fupi zilizo wazi na bayana na tungependelea zaidi ziwe na urefuwa kati ya kurasa sita hadi kumi na mbili. Hata hivyo, makala zenye urefu wa hadi kurasa ishirinizinaweza kufikiriwa. Tunakaribisha sana makala zenu. Makala hizo ziwasilishwe kwetu zikiwakatika mfumo wa kielektroniki kwa kutumia anuani inayoonyeshwa hapo chini:

HakiElimu

HakiElimu inafanya kazi kuleta usawa, ubora, haki za binadamu na demokrasia katika Elimu, kwakuziwezesha jamii kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa shule, kuwa na ushawishi katika utayarishaji wa sera,

kuhamasisha majadiliano ya kibunifu ya umma kwa lengo la kujiunga pamoja kuleta mabadiliko,kuendesha tafiti zinazohoji na kuchambua mambo kwa kina, kuendesha kampeni za utetezi na

kushirikiana na wabia wengine ili kufikia malengo ya pamoja na kupigania haki ya jamii.

HakiElimu Nyaraka za Kufanyia KaziSLP 79401 • Dar es Salaam • TanzaniaSimu (255 22) 2151852 / 3 • Faksi (255 22) [email protected] • www.hakielimu.org