27
i JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI RASIMU YA SERA YA ELIMU NA MAFUNZO Novemba, 2012

Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

Embed Size (px)

DESCRIPTION

Mustakabari wa Elimu yetu unahitaji mjadara mpama

Citation preview

Page 1: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

i

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

RASIMU YA SERA YA ELIMU NA MAFUNZO

Novemba, 2012

Page 2: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

i

YALIYOMO

YALIYOMO ............................................................................................... i

FASIRI………………………………………………………………....................iii

DIBAJI ..................................................................................................................... … iv

SURA YA KWANZA ……………………………………………………………….1

1.0 UTANGULIZI ...................................................................................................... 1

1.1. Hali ilivyo………………………………………………………………………1

SURA YA PILI…… ………………………………………………………………. 4

2.0 UMUHIMU WA SERA ..................................................................................... 4

2.1 Dira, Dhima na Malengo ya Sera .................................................................... 4

SURA YA TATU ...... ………..…………………………………………….…………..5

3.0 HOJA NA MATAMKO YA SERA ................................................................... 5

3.1 Mfumo wa Elimu na Mafunzo…….............................................. 5

3.2 Viwango na Ubora wa Elimu na Mafunzo ......................................................... 6

3.3 Fursa za Elimu na Mafunzo .............................................................................. 11

3.4 Rasilimaliwatu ya kulingana na vipaumbele vya Taifa. ................................... 12

3.5 Ugharimiaji wa Elimu na Mafunzo................................................................... 13

3.6 Masuala Mtambuko .......................................................................................... 14

SURA YA NNE………………………………………………………………………20

4.0 .. MUUNDO WA KISHERIA ……………………………………………… 20

SURA YA TANO……………………………………………………………….……21

5.0 MUUNDO WA KITAASISI …….…………………………………………….21

5.1 Ufuatiliaji na Tathmini . …..………………………………………………….21

5.2 HITIMISHO………………................................................................................21

Page 3: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

ii

VIFUPISHO

MKUKUTA

Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini

Tanzania

TEHAMA Teknolojia ya Habari na Mawasiliano

UKIMWI Upungufu wa Kinga Mwilini

UNESCO United Nations Educational Scientific and Cultural

Organisation

VVU Virusi vya Ukimwi

Page 4: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

iii

FASIRI

NENO FASIRI

Mkondo Mchepuo wa elimu na mafunzo

Page 5: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

iv

DIBAJI

Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya

Taifa 2025 imejikita katika kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika

na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya Taifa lipate maendeleo na kuwa taifa lenye

uchumi wa kati na shindani ifikapo mwaka 2025. Dira na mpango huu pia

imebainisha maeneo mbalimbali ambayo elimu au mafunzo hayana budi kuchangia

kwa kiwango cha kutosha kufikia malengo yaliyotarajiwa katika maendeleo ya Taifa.

Kwa mantiki hii elimu na mafunzo bora na endelevu ni muhimu katika kufikia

malengo haya.

Kutokana na umuhimu wa elimu na mafunzo katika maendeleo ya Taifa, Serikali kwa

kushirikiana na wadau imetayarisha Sera mpya ikitilia maanani mafanikio ambayo

yameletwa na Sera zilizotangulia na kulifanya Taifa kupiga hatua katika nyanja za

elimu na mafunzo. Sera kuu zilikuwa ni Sera ya Elimu na Mafunzo 1995, Sera ya

Elimu ya Ufundi na Mafunzo 1996 na Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu 1999 ambazo

zilitekelezwa sambamba na sera nyingine ambazo zinaigusa sekta ya elimu na

mafunzo kama vile Sera ya Sayansi na Tekinolojia 1996, Sera ya Habari na

utangazaji 2003, Sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ya Binafsi 2009, pamoja na

nyingine za aina hiyo.

Sera hii mpya imebainisha maeneo ambayo Serikali kwa kushirikiana na wadau

katika elimu na mafunzo itayawekea mkazo zaidi ili kuweka mazingira mazuri ya

kufikia malengo yetu ya maendeleo. Maeneo haya ni pamoja na kuendelea

kuboresha mfumo wa elimu na mafunzo ili uwe na tija na ufanisi zaidi, kuendelea

kutoa fursa na usawa katika elimu na mafunzo, kuendelea kuboresha mitaala ya

elimu na mafunzo ili iendane na mazingira ya sasa na mahitaji ya maendeleo ya

Taifa, kuendelea kuhuisha masuala ya lugha katika elimu na mafunzo hususan

umahiri na matumizi ya lugha ya kiswahili na alama pamoja na lugha ya kiingereza

na nyingine za kigeni katika kufundishia na kujifunzia, kendelea kuboresha mfumo

na taratibu za upimaji, tathmini na utoaji vyeti katika ngazi zote, kendelea

kuboresha taratibu na uwezo wa uongozi na utawala wa elimu na mafunzo katika

Page 6: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

v

ngazi zote, kuendelea kukuza uwezo katika utoaji wa elimu na mafunzo katika ngazi

zote, kubuni njia mbalimbali na endelevu za ugharimiaji wa elimu na mafunzo, na

kushughulikia masuala mbalimbali mtambuko ili kuleta tija na ufanisi katika sekta ya

elimu na hivyo kuchangia kwa ukamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Kwa sababu hizi Dira ya elimu na mafunzo itakuwa ni “Mtanzania aliyeelimika na

mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitizamo chanya ili kuweza kuchangia

katika kuleta maendeleo ya Taifa” na dhima yetu ni “kuboresha na kuweka mifumo

na taratibu zitakazowezesha kupata idadi ya kutosha ya watanzania walioelimika na

wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya

maendeleo ya Taifa ifikapo 2025”.

Ili kufanikisha Sera hii kwa ukamilifu inahitaji ushirikiano wa wadau wote wa elimu

na mafunzo katika ngazi zote wakiwemo sekta binafsi, Asasi za Kiraia (AZAKI) na

washirika katika maendeleo.

Mwisho, napenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine

katika mchakato mzima wa kukamilisha Sera hii.

Dkt. Shukuru J. Kawambwa (Mb) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi

Page 7: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

1

SURA YA KWANZA

1.0 UTANGULIZI

Utoaji wa elimu na mafunzo nchini Tanzania umekuwa ukiongozwa na sera kubwa tatu ambazo ni: Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996) na Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu (1999). Serikali pia imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba sekta ya elimu na mafunzo inakua na kukidhi mahitaji ya taifa kulingana na uwezo. Kutokana na haya kumekuwa na mafanikio hususan katika ongezeko la shule za msingi, sekondari, vyuo na wigo wa programu za elimu na mafunzo na hivyo kuwa na ongezeko la idadi ya Watanzania walioelimika. Pamoja na mafanikio haya sera hizi zimekuwa zikitumika kwa kipindi kirefu bila marekebisho yanayozingatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, sayansi na teknolojia. Pia, Sera hizi zilitungwa kabla ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, MKUKUTA I na II na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Muda mrefu 2011/12 hadi 2025/26. Tangu Sera hizo kutolewa kumekuwepo na matukio mbalimbali yakiwemo Tanzania kuridhia Maazimio, Itifaki na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa ambayo yanahitaji kuzingatiwa. Hali kadhalika kumekuwa, na baadhi ya masuala Mtambuko ambayo yamejitokeza na hayapo katika Sera za sasa za Elimu na Mafunzo.

Kutokana na sera kupitwa na wakati, mfumo wa elimu na mafunzo umekuwa hauendani kikamilifu na mahitaji ya maendeleo ya Taifa na wakati mwingine kushindwa kumwezesha Mtanzania kuchagua kujiendeleza kutoka katika mikondo ya kitaaluma au kitaalamu na kinyume chake. Aidha mfumo huu haujafaulu kutoa wahitimu wanaotosheleza mahitaji ya wataalamu katika nyanja muhimu za maendeleo ya Taifa kwa kadri ya uwezo wake. Aidha, idadi ya wahitimu kutokana na mfumo huu, hawatoshelezi hususan katika nyanja za Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na nyingine ambazo ni vipaumbele vya taifa na wengine kukosa umahiri unaotakiwa na sehemu mbalimbali ikiwemo soko la ajira. Vilevile, fursa za elimu na mafunzo haziwiani na mahitaji halisi ya makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo walemavu, wanawake na wale wenye kasi tofauti katika elimu au mafunzo yao. Mfumo huu pia una uwigo finyu wa kugharimia elimu na mafunzo na hauzingatii kikamilifu masuala mtambuko ambayo yameendelea kujitokeza kadri taifa linavyopiga hatua katika maendeleo.

Changamoto za kisera zilizojitokeza zinatoa msukumo wa kuwa na Sera mpya inayozingatia mahitaji ya maendeleo ya taifa na masuala mengine ambayo yamejitoeza tangu sera za sasa zipitishwe.

1.1. Hali ilivyo

Tanzania imejiwekea malengo ya kufikia kiwango cha Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia uchumi wa kati Taifa halina budi kuwa na jamii ilyoelimika na inayopenda kujielimisha zaidi. Takwimu za URT (2012) zinaonyesha kuwa kiwango cha uandikishaji kwa rika lengwa katika elimu ya Msingi ni asilimia 92. Aidha, asilimia ya wanaoendelea katika elimu ya Sekondari ngazi ya kawaida ni wastani wa asilimia 50 URT (2012). Vilevile, wastani wa karibia asilimia 10 tu ya wahitimu wa elimu ya msingi wamekuwa wakipata fursa ya kujiunga na Mafunzo ya Ufundi Stadi na wanaobaki hujiunga na ulimwengu wa kazi bila kuwa na stadi stahiki. Asilimia ya wanaojiunga na Elimu ya Sekondari ngazi ya Juu ni wastani wa asilimia 12.1 URT (2011). Idadi hii ya ushiriki katika elimu ya sekondari ngazi ya juu hautaliwezesha Taifa kufikia malengo yake ya Maendeleo katika elimu, maarifa na ujuzi kama

Page 8: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

2

Mpango wa Maendeleo wa Taifa unavyotarajia. Kiwango cha udahili wa jumla katika elimu ya Juu Tanzania ni asilimia 1.5 wakati takwimu katika eneo hilo kwa nchi za uchumi wa kati ni karibu asilimia 13 UNESCO (2009). Aidha, kiwango hicho kwa Tanzania ni cha chini kabisa kulinganisha na nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mwenendo huu, umelifanya Taifa kuwa na upungufu wa Watanzania wenye Elimu, stadi, Ujuzi katika maeneo mbalimbali ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Hali hii inatoa changamoto kwa wadau wa elimu na mafunzo kuboresha mfumo na miundo iliyopo ili kukidhi mahitaji ya Taifa na kuhimili ushindani wa Kikanda na Kimataifa.

Kumekuwa na mafanikio katika elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali hususan ongezeko la shule za msingi kutoka 14, 257 mwaka 2005 hadi shule 16,331 mwaka 2012. Idadi hii imeongeza uandikishaji wa wanafunzi wa shule za msingi kutoka 7,541,208 (Wavulana 3,855,712 na wasichana 3,685,496) mwaka 2005 hadi 8,247,172 (wavulana 4,086,280 na wasichana 4,160,892) mwaka 2012. Kwa upande wa Elimu ya sekondari inaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la shule za sekondari kutoka shule1,745 mwaka 2005 hadi shule 4,528 kwa mwaka 2012 na kuwezesha ongezeko la wanafunzi wa elimu ya sekondari ngazi ya kawaida kutoka 489,942 (wavulana 258,134 na wasichana 231,808) mwaka 2005 hadi wanafunzi1,802,810 (wavulana 954,961 na wasichana 447,849) mwaka 2012. Aidha, Idadi ya wanafunzi katika elimu ya sekondari ngazi ya juu imeongezeka kutoka 34,383 (wavulana 21,620 na wasichana 12,763) mwaka 2005 hadi wanafunzi 81,462 wavulana 55,512 na wasichana 25,950) mwaka 2012. Katika Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kumekuwa na ongezeko la vyuo kutoka 695 mwaka 2005 hadi 750 mwaka 2011 na kuwezesha ongezeko la wanachuo kutoka 78,586 (wanaume 43,022 na wanawake 35,564) mwaka 2005 hadi wanachuo 104,840 (Wanaume 54,350 wanawake 50,190) mwaka 2011.

Katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo viliongezeka kutoka Vyuo 195 mwaka 2005 hadi kufikia vyuo 260 mwaka 2011 na kuongeza udahili wa wanachuo kutoka 40,059 (Wanaume 30,123 na wanawake 9,636) mwaka 2005 hadi 85,040 (wanaume 46,342 na wanawake 38,698) mwaka 2011. Hali kadhalika katika vyuo vya ualimu kumekuwa na ongezeko la vyuo kutoka 52 mwaka 2005 hadi vyuo 103 mwaka 2011 na kuwezesha ongezeko la wanachuo kutoka 26,224 (Wanaume 13,484 na wanawake 12,740) mwaka 2005 hadi 43,258 (wanaume 24,360 na wanawake 18,898) mwaka 2012. Upande wa Vyuo vya Elimu ya juu kumekuwa na ongezeko la vyuo vikuu na Vyuo vikuu vishiriki kutoka 23 mwaka 2005 hadi Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu vishiriki 46 mwaka 2011 na kuongeza udahili wa wanachuo kutoka 37,667 (Wanaume 25,061na wanawake 12,606) mwaka 2005 hadi 166,484 (wanaume 105,892 na wanawake 60,592) mwaka 2012.

Kutokana na tathmini hii ambayo inaonyesha kwamba maboresho mbalimbali yanayofanywa na kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau yamekuwepo mafanikio katika Sekta ya elimu na mafunzo, bado kumeendelea kuwepo na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kurekebishwa. Mfumo uliopo si nyumbufu kuruhusu elimu na mafunzo kupatikana na kutambulika kwa njia mbalimbali na mbadala kufanya elimu na mafunzo kuwa na mwendelezo ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa. Kumekuwa pia na changamoto katika mitaala hususan inapolinganishwa na mahitaji halisi katika maendeleo ya Taifa. Aidha, kuna upungufu wa vifaa na nyenzo za kufundishia na kujifunzia na baadhi na vilivyopo vimepitwa na wakati ama kutokuendana na mahitaji ya sayansi na teknolojia ya

Page 9: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

3

sasa. Vilevile kuna changamoto katika mfumo wa ajira hivyo kusababisha uhaba wa wataalam mbalimbali wanaoweza kushiriki katika kutoa na kusimamia elimu na mafunzo nchini. Hili linakwenda sambamba na changamoto wa upatikanaji wa walimu/wahadhiri wenye sifa stahiki kuwa ni mgumu katika baadhi ya taaluma na fani. Pamoja na jitihada mbalimbali zilizowekwa kitaifa ili kuleta fursa sawa kwa watanzania wenye mahitaji muhimu au mafunzo katika maeneo mbalimbali bado kumekuwa na changamoto katika kumfikia kila mlengwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukubwa wa nchi na vikwazo vya kijiografia. Kumekuwepo pia changamoto katika mfumo wa ugharamiaji wa elimu na mafunzo kuwa na wigo finyu ambao umesababisha kutokuwepo na uwiano stahiki na endelevu. Changamoto nyingine zipo katika ushirikiano na ubia katika elimu na mafunzo baina ya taasisi za elimu na mafunzo na sekta binafsi na sera zilizopita baadhi ya masuala mtambuka hayakuzingatiwa kikamilifu na hivyo kusababisha kutotekelezwa kikamilifu

Changamoto katika sekta ya elimu na mafunzo nchini

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa sera za Elimu na Mafunzo, zimekuwepo changamoto mbalimbali zikiwemo kuwa na :

a) Mfumo nyumbufu unaoruhusu elimu na mafunzo kupatikana na kutambulika kwa njia mbalimbali mbadala.

b) Mitaala inayokidhi mahitaji halisi ya rasilimaliwatu katika kuleta maendeleo ya Taifa.

c) Vifaa na nyenzo bora na za kutosha kwa ajili ya kufundishia, utafiti na kujifunzia kwa kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

d) Mfumo wa ajira unaowezesha upatikanaji wa wataalam wa kada mbalimbali wanaohitajika katika sekta elimu na mafunzo nchini.

e) Uwezo wa kuhakikisha fursa kwa usawa inatolewa kwa kila Mtanzania kulingana na mahitaji yake na sehemu na mazingira aliyopo.

f) Mfumo wa ugharamiaji wa elimu na mafunzo wenye wigo mpana na endelevu.

g) Masuala mtambuko yanayozingatiwa kikamilifu katika elimu na mafunzo.

h) Ushirikiano na ubia katika elimu na mafunzo baina ya taasisi na sekta binafsi

Page 10: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

4

SURA YA PILI

2.0 UMUHIMU WA SERA

Kutokana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Tanzania inategemewa kuwa Taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na hivyo matarajio ni kwamba tutakuwa na jamii iliyoelimika na inayopenda kujielimisha na kujenga uchumi imara na shindani unaoongozwa na elimu na ujuzi. Kwa matarajio haya elimu na mafunzo vimepewa kipaumbele na kwamba: elimu na mafunzo ndio tegemeo la nchi katika kuleta mitizamo ya kimaendeleo na hatimaye kulifanya taifa kuwa shindani, kusonga mbele na kuwa moja ya nchi yenye uchumi wa kati. Sekta ya elimu na mafunzo haina budi kujikita katika idadi ya kutosha ya wahitimu wenye sifa, mitizamo na ujuzi stahiki ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali za Taifa na kufanikisha maendeleo yanayotarajiwa na taifa ifikapo 2025. Mambo haya yamebainishwa katika MKUKUTA pamoja na mpango wa maendeleo wa taifa. Kwa sababu hii, Sera ya Elimu na Mafunzo imeandaliwa ili ielekeze kujibu malengo na matarajio ya maendeleo ya Taifa.

2.1 DIRA, DHIMA NA MALENGO YA SERA

Dira

Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mtizamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Dhima

Kuweka na Kuboresha mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha ili waweze kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Malengo ya Sera

Lengo la Jumla:

Watanzania walioelimika na wenye maarifa na ujuzi kuweza kuchangia kwa haraka katika maendeleo ya taifa na kuhimili ushindani.

Malengo Mahsusi

Malengo mahsusi ya Sera ni kuwa na:

(a) Mfumo, miundo na taratibu nyumbufu kumwezesha Mtanzania kujiendeleza kwa njia mbalimbali katika mikondo ya kitaaluma na kitaalamu.

(b) Elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora unaotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.

(c) Upatikanaji wa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo nchini.

(d) Ongezeko la rasilimaliwatu kulingana na vipaumbele vya Taifa.

(e) Mfumo endelevu wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo nchini.

(f) Mfumo wa elimu na mafunzo unaozingatia masuala mtambuko .

Page 11: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

5

SURA YA TATU

3.0 HOJA ZA SERA NA MATAMKO

3.1. Mfumo, miundo na taratibu nyumbufu kumwezesha Mtanzania kujiendeleza kwa njia mbalimbali katika mikondo ya kitaaluma na kitaalamu.

Suala

Miundo na taratibu za elimu na mafunzo

Maelezo

Pamoja na kwamba taifa limeendelea kutekeleza muundo wa kitaaluma wa 2-7-4-2-3+, na muundo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi wa 2-7-4-1+. Hata hivyo miundo hii bado haiingiliani kwa urahisi. Aidha wapo wahitimu wa darasa la saba wanaojiunga na mafunzo ya ufundi stadi lakini mwendelezo wao haupo kwenye miundo iliyopo. Hali hii imesababisha kutokuwa na muunganiko, ulinganifu na mtiririko mzuri katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo na hivyo kusababisha wahitimu kukosa mwendelezo katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo na wengine kutokuwa na mwelekeo.

Lengo

Kuwa na mfumo, miundo na taratibu nyumbufu za elimu na mafunzo na kuleta tija na ufanisi.

Tamko

3.1.1. Serikali itaweka mfumo, miundo na taratibu nyumbufu katika elimu na mafunzo ili kuleta ulinganifu, muunganiko na ufanisi wa ngazi na fani mbalimbali za kitaaluma na kitaalamu kumwezesha mwanafunzi kutoka mkondo mmoja kwenda mwingine.

Suala:

Umri na muda wa elimu na mafunzo

Maelezo:

Muundo wa elimu na mafunzo uliopo unatoa fursa ya mtoto mwenye umri wa miaka mitano kujiunga na elimu ya awali kwa muda wa miaka miwili. Mtaala wa elimu ya awali umetengenezwa kwa namna ambayo unatakiwa ufundishwe kwa miaka 2 lakini utafiti unaonyesha mtaala huo huo unaweza pia kufundishwa kwa mwaka mmoja. Aidha, elimu ya awali haizingatii mahitaji maalumu ya baadhi ya watoto. Pia itifaki ya Dakar ya mwaka 1999 ambayo ilitakiwa itekelezwe hadi ifikapo mwaka 2015 ambayo Tanzania imeridhia, elimu ya awali inatakiwa kuwa kati ya umri wa miaka mitatu hadi sita. Aidha, elimu ya lazima kwa sasa ni darasa la saba. Wahitimu wa elimu ya lazima katika mfumo wa sasa wanakuwa na umri wa miaka 13. Wahitimu hawa wanakuwa na umri mdogo na pia hawana maarifa na ujuzi unaotosheleza kujiunga na ulimwengu wa kazi au kukabiliana na changamoto za maendeleo iwapo watakosa fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari ngazi ya kawaida. Pia muda wa kusoma katika ngazi nyingine umeendelea kutokuwa na

Page 12: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

6

falsafa ya kuongoza suala hili na hivyo kutokuwa na ulinganifu na mwingiliano fanisi.

Lengo

Kurekebisha muda wa elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali ili kuleta tija, ufanisi na matumizi bora ya rasilimali.

Tamko

3.1.2. Serikali itaweka utaratibu wa Elimu ya Awali kuwa ya lazima na kutolewa kwa watoto wenye umri kati ya miaka mitatu hadi mitano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja

3.1.3. Elimu –Msingi kuwa ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne; na kutolewa kwa miaka kumi na umri wa kuanza darasa la kwanza kuwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na maendeleo na uwezo wa mtoto kumudu masomo katika ngazi husika.

3.1.4. Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha muda wa kukamilisha elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali za elimu baada ya Elimu-Msingi unakuwa na tija na ufanisi.

3.2. Elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora unaotambulika kikanda na kimataifa.

Suala

Udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo

Maelezo

Serikali katika kuhakikisha kwamba elimu na mafunzo nchini yanakuwa na viwango na ubora unaostahili imeweka mamlaka na taasisi mbalimbali katika kusimamia hili. Mamlaka na taasisi hizi zimekuwa zikipata changamoto mbalimbli hususani katika maeneo ya mwingiliano wake, utendaji wake, na mawasiliano baina ya mamlaka na taasisi hizo. Vile vile kumekuwa na changamoto zinazojitokeza kutokana na kukua kwa sekta ya elimu na mafunzo na hivyo kupelekea umuhimu wa kuwa na mamlaka na taasisi za usimamizi, udhibiti na uthibiti wa elimu na mafunzo ambazo zinaendeshwa na mfumo mahususi wa kutengeneza, kutoa na kutambua tuzo kitaifa.

Lengo

Kuwa na ufanisi katika usimamizi, udhibiti na uthibiti wa ubora na utoaji wa elimu na mafunzo.

Tamko

3.2.1 Serikali itaimarisha ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote ikiwemo masuala ya ushauri.

Suala

Mitaala ya elimu na mafunzo

Page 13: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

7

Maelezo

Utandawazi na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa sasa vinahitaji wataalamu wenye uwezo wa kuhimili hali hiyo. Kuna umuhimu wa kuangalia upya ubora wa elimu na mafunzo yanayotolewa katika ngazi zote. Elimu na mafunzo bora hayana budi kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko hayo. Kumekuwa na changamoto pia katika mitaala hususan inapolinganishwa na mahitaji halisi katika maendeleo ya Taifa.

Mitaala ya elimu na mafunzo inatarajiwa kumpa mwanafunzi hamasa ya kujielimisha, maarifa, stadi na mwelekeo stahiki, hivyo haina budi kuzingatia maeneo ya utafiti, sayansi na teknolojia, stadi za teknolojia asili, TEHAMA na stadi za maisha pamoja na njia mbalimbali na mbadala za kufundishia ili kumwezesha mlengwa kukabiliana kikamilifu na changamoto za maendeleo na ujuzi unaojitokeza kutokana na sayansi na teknolojia. Vile vile programu katika vyuo ziwe na muunganiko na mlinganisho wa kimaudhui katika ngazi za elimu na mafunzo ili kutoa wataalamu wenye viwango bora kwa lengo la kuhimili ushindani katika utandawazi.

Kuna hitaji la kupitia upya mitaala ya elimu na mafunzo katika ngazi zote ili kuendana na maendeleo na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kitaifa, kikanda na kimataifa.

Lengo

Kuwa na mitaala inayokidhi mahitaji katika kuleta maendeleo ya Taifa na kuhimili ushindani.

Tamko

3.2.2 Serikali itaimarisha ukuzaji, uboreshaji na utekelezaji wa mitaala kwa kuzingatia mahitaji ya taifa na ya walengwa katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

3.2.3 Serikali itaimarisha usimamiaji na upimaji wa utekelezaji wa mitaala katika taasisi za elimu na mafunzo katika ngazi zote ili kuleta ufanisi wa elimu na mafunzo yatolewayo.

Suala

Nyenzo, vifaa na zana za kufundishia na kujifunzia

Maelezo

Utekelezaji fanisi wa mitaala unategemea upatikanaji wa nyenzo, vifaa na zana nyingine stahiki za kufundishia na kujifunzia. Kumekuwa na upungufu wa nyenzo, vifaa na zana bora za kufundishia na kujifunzia na baadhi ya vilivyopo vimepitwa na wakati ama kutokuendana na mahitaji ya sayansi na teknolojia ya sasa. Hali hii imechangia kutoa wahitimu wasio na umahiri wa kutosha kukabiliana na changamoto za kimaendeleo.

Lengo

Kuwa na nyenzo, vifaa na zana stahiki zinazokidhi mahitaji ya kufundishia na kujifunzia.

Page 14: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

8

Tamko

3.2.4 Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha vifaa, nyenzo na zana stahiki za kufundishia na kujifunzia katika elimu na mafunzo zinatosheleza kulingana na mahitaji na maendeleo ya sayansi, teknolojia na mbinu za kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote.

Suala

Miundombinu katika elimu na mafunzo.

Maelezo

Uwepo wa miundombinu ya kutosha na yenye viwango vya ubora stahiki ni muhimu katika kuinua ubora wa Elimu na Mafunzo katika ngazi zote. Miundombinu iliyopo katika shule, vyuo na taasisi nyingine za elimu na mafunzo ikiwemo majengo, mifumo ya maji, umeme na barabara imechakaa na haitoshelezi mahitaji ya makundi yote. Mipango ya maendeleo ya elimu na mafunzo iliyopo haitoshelezi mahitaji ya miundombinu kulingana na ongezeko la watumiaji. Aidha, hakuna utamaduni wa utunzaji na uhifadhi na matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu ya shule, vyuo na taasisi za elimu na mafunzo.

Lengo

Kuwa na miundombinu bora na stahiki inayokidhi mahitaji katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Tamko

3.2.5 Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha uwepo wa miundombinu bora na stahiki ya kutosheleza mahitaji ya elimu na mafunzo katika ngazi zote.

Suala

Mazingira na huduma muhimu shuleni na vyuoni.

Maelezo

Utoaji wa elimu na mafunzo unahitaji mazingira yenye utulivu, usalama na kumvutia mwanafunzi na mwalimu kuwa sehemu ya mazingira hayo. Shule na vyuo vinapaswa kuwa kwenye mazingira stahiki na yenye huduma muhimu ili kuwezesha utoaji wa elimu kwa ufanisi . Mazingira katika baadhi ya shule na vyuo nchini ni duni na hayana usalama wa kutosha. Aidha, kuna changamoto nyingi katika upatikanaji wa huduma muhimu kama chakula, maji safi na salama, afya, umeme, mawasiliano na usafiri. Huduma hizi huongeza ushiriki katika elimu na mafunzo. Kuna umuhimu wa kuwa na mazingira yanayokidhi mahitaji na huduma muhimu shuleni na vyuoni ili kuinua ubora wa elimu na mafunzo.

Lengo

Kuwa na mazingira salama na huduma muhimu na endelevu shuleni na vyuoni.

Tamko

3.2.6 Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa huduma muhimu

Page 15: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

9

zikiwemo za chakula bora, mawasiliano, umeme, maji safi na salama, na afya zinapatikana katika shule na vyuo.

3.2.7 Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha kuwepo kwa mazingira bora na yenye usalama katika utoaji wa elimu na mafunzo nchini.

Suala

Matumizi ya Kiswahili, Kiingereza, lugha ya alama na lugha nyingine za kigeni katika mawasiliano.

Maelezo

Lugha za Kiswahili, Kiingereza, na lugha nyingine za kigeni pamoja na za alama zinafundishwa kama masomo katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo. Pamoja na juhudi za kufundisha lugha hizo, bado kuna udhaifu wa kumudu lugha sanifu katika mawasiliano. Sehemu kubwa ya udhaifu huo inatokana na miundombinu na mbinu duni za kufundishia, umahiri mdogo na matumizi madogo ya lugha sanifu katika mazingira ya kawaida.

Lugha ya Kiswahili ni lugha ya Taifa na inatumika kama lugha ya kwanza au ya pili miongoni mwa wananchi wengi. Lugha ya Kiswahili imekua kwa kiwango cha kimataifa ambapo inaweza kutumiwa na wananchi wengi kupata maarifa katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sayansi na teknolojia. Lugha ya Kiingereza inatumika kama lugha ya pili kwa baadhi ya wananchi. Kiswahili na Kiingereza ni lugha rasmi za kiofisi. Ufahamu mzuri wa Kiingereza na lugha nyingine za kigeni pia unamwezesha mtanzania kuwa na mawasiliano na watu wa mataifa mengine na kupata elimu na maarifa. Aidha lugha ya alama hutumika kufanya mawasiliano baina ya viziwi na watu wengine. Wanafunzi hawa wanashindwa kupata elimu na mafunzo kwa ufanisi kutokana na kutokuwepo na utaratibu mahsusi wa kufundisha na kutumia lugha ya alama kwa jamii nyingine ambayo siyo viziwi.

Lengo

Kujenga uwezo wa kutumia lugha mbalimbali katika mawasiliano .

Tamko

3.2.8 Serikali itaweka utaratibu wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ili kuwa na wanafunzi mahiri wenye uwezo wa kuwasiliana kwa Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za kigeni katika mfumo wa elimu na mafunzo.

3.2.9 Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha Lugha ya alama kutumika katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

3.2.10 Serikali itahakikisha lugha ya kiingereza na nyingine za kigeni zinafundishwa kwa ufasaha na ufanisi katika ngazi zote za elimu na mafunzo nchini ili kuleta ufahamu na umahiri kutokana na umuhimu wa lugha hizo katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Suala

Lugha ya kufundishia na kujifunzia

Maelezo

Page 16: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

10

Kwa sasa, lugha za kufundishia na kujifunzia katika elimu na mafunzo ni Kiswahili na Kiingereza. Lugha ya kufundishia elimu ya awali na msingi ni Kiswahili. Aidha, lugha ya Kiingereza inatumika kufundishia katika baadhi ya shule.

Lugha ya Kiingereza hutumika kufundishia katika shule za sekondari, vyuo vya ualimu ngazi ya stashahada, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu. Aidha, lugha ya Kiswahili hutumika kufundishia katika vyuo vya mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti na vyuo vya ufundi stadi. Matumizi ya lugha ya Kiingereza yanazidi kupanuka ulimwenguni kutokana na utandawazi. Hali kadhalika, matumizi ya Kiswahili nchini na katika mabara mengine yameongezeka. Pia Tanzania imeridhia itifaki ya Jumuia ya Afrika Mashariki kuhusiana na maendeleo na matumizi ya Kiswahili na Tanzania kuchaguliwa kuwa makao makuu ya Taasisi ya Kuendeleza Kiswahili katika Jumuia.

Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuimarisha matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza kwa kuzifanya kuwa lugha za kufundishia katika ngazi mbalimbali.

Lengo

Kuimarisha ufundishaji kwa kutumia lugha stahiki

Tamko

3.2.11 Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha lugha ya Kiswahili na Kiingereza kuwa lugha za kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Suala

Upimaji na tathmini katika Elimu na Mafunzo.

Maelezo

Upimaji na tathmini katika elimu na mafunzo unatumia njia mbalimbali ambazo hutofautiana kulingana na ngazi, fani na aina ya kozi. Uhalali wa matokeo ya upimaji na tathmini unategemea uthabiti na ukamilifu wa kila hatua ya mchakato wa upimaji. Upimaji na tathmini hufanywa na shule na vyuo na kuratibiwa na taasisi zilizopewa dhamana hiyo.

Kumekuwepo na malalamiko kuhusu matokeo ya wanafunzi wengi kutofaulu mitihani yao katika ngazi mbalimbali. Aidha, baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuendelea kutoka ngazi moja hadi nyingine kutokana na dosari katika upimaji na tathmini. Pia vyuo na taasisi mbalimbali wakati mwingine, hutoa programu zinazofanana lakini baadhi ya vigezo vya upimaji na tathmini ya programu hizo havilingani. Hali hii inasababisha baadhi ya wahitimu kutofikia viwango stahiki vya umahiri vinavyotakikwa katika sehemu mbalimbali ikiwemo ulimwengu wa kazi.

Kutokana na umuhimu wa upimaji na tathmini katika elimu na mafunzo, hakuna budi kuwa na utaratibu wa kitaifa wa kudhibiti upimaji na tathmini katika ngazi na programu mbalimbali za elimu na mafunzo.

Lengo

Kuimarisha upimaji na tathmni katika elimu na mafunzo.

Page 17: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

11

Tamko

3.2.12 Serikali itaweka utaratibu na kuimarisha upimaji na tathmini katika elimu na mafunzo kwa ngazi zote.

3.2.13 Serikali itaweka na kusimamia mfumo wa kitaifa wa sifa linganifu wa tuzo kwa ngazi zote za elimu na mafunzo ili kurahisisha wahitimu kuweza kujiendeleza kielimu na mafunzo.

Suala

Uratibu,udhibiti na uthibiti wa programu, mitihani na tuzo za nje zinazotolewa nchini.

Maelezo

Mitihani ya bodi mbalimbali za mitihani ya nje katika ngazi za taaluma na utaalamu huratibiwa na Baraza la Mitihani Tanzania, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania kulingana na ngazi husika. Aidha, baadhi ya shule na vyuo visivyo vya serikali hutumia mitihani ya nje kwa baadhi ya wanafunzi wake. Kutokana na kupanuka kwa teknolojia, baadhi ya watu wamekuwa wakifanya mitihani ya nje kupitia mitandao. Vile vile, kuna shule, vyuo na vituo ambavyo vinaendesha masomo na mitihani ya nje bila kutambuliwa rasmi. Hali hii inafanya udhibiti wa uendeshaji wa masomo na mitihani ya aina hiyo kuwa mgumu. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kudhibiti masomo, mitihani na tuzo za nje.

Lengo

Kuwa na udhibiti wa masomo, mitihani na tuzo za nje.

Tamko

3.2.14 Serikali itaweka utaratibu na kuimarisha uthibiti wa programu, mitihani na tuzo za nje zinazotolewa nchini katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

3.3. Upatikanaji wa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo nchini

Suala

Fursa kwa usawa katika elimu na mafunzo

Maelezo

Fursa za elimu na mafunzo zinapatikana kwa kila Mtanzania bila ubaguzi wa jinsi, rangi, kabila, dini, hali ya kijamii au kipato ili kufikia malengo ya elimu na mafunzo kwa wote. Pamoja na juhudi za Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutoa fursa za elimu kwa makundi yote, baadhi ya makundi bado hayajafikiwa kikamilifu kutokana na sababu za kijamii, kiuchumi na kijiografia. Aidha, Kuna mdondoko wa wasichana na wavulana katika mfumo wa elimu kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za ujauzito, ndoa za utotoni, ajira za watoto na utoro. Hata hivyo, ushiriki wa wasichana katika elimu unapungua kadiri wanavyoendelea katika ngazi za juu za elimu na mafunzo ukilinganishwa na ushiriki wa wavulana. Kuna umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kupata elimu na mafunzo kwa wote.

Page 18: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

12

Lengo

Kuwa na fursa na usawa katika elimu na mafunzo

Tamko

3.3.1 Serikali itaongeza fursa anuai za elimu na mafunzo kwa usawa kwa makundi yote ya kijamii kwa ngazi zote.

3.3.2 Serikali itaondoa vikwazo vinavyozuia fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo na kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika.

3.3.3 Serikali itahakikisha kuwa wanafunzi wanaokatisha masomo kutokana na ujauzito au sababu nyingine wanapata fursa ya kuendelea na masomo na kukamilisha mzunguko wa elimu na mafunzo katika ngazi husika.

Suala

Elimu na mafunzo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo masafa.

Maelezo

Serikali imeweka utaratibu wa elimu au mafunzo kwa ajili ya watoto, vijana na watu wazima, waliokosa fursa katika mfumo wa kawaida ili kujiendeleza kielimu na kumudu changamoto za maisha au kuhitimu katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo. Fursa za aina hii zinaweza kutolewa kwa ufanisi kwa kuweka miundo stahiki katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo nchini.

Elimu hii inaweza kutolewa vizuri zaidi endapo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na rasilimaliwatu wenye ujuzi stahiki vitatumika. Kuna upungufu wa rasilimaliwatu wa kutoa elimu hiyo na pia vifaa vya TEHAMA ni vichache na havikidhi mahitaji ya utandawazi na ushindani pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo, wakati mwingine kusababisha changamoto za ufanisi na viwango duni vya ubora wa elimu itolewayo.

Lengo

Kuimarisha elimu na mafunzo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo masafa.

Tamko

3.3.4 Serikali itaweka utaratibu na mazingira wezeshi ya kuhakikisha elimu na mafunzo inatolewa kwa ufanisi katika ngazi zote kwa njia huria na masafa.

3.4. Ongezeko la rasilimaliwatu kulingana na vipaumbele vya Taifa

Suala

Upatikanaji wa rasilimaliwatu mahiri na wa kutosha.

Maelezo

Kupanuka kwa sekta rasmi na isiyo rasmi kumeongeza fursa za kiuchumi ambazo

Page 19: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

13

zimeleta msukumo kwa taifa kuwa na rasilimaliwatu iliyoelimika na inayopenda kujielimisha kwa kiwango cha juu ili kuweza kuhimili ushindani na changamoto za utandawazi, soko la pamoja la Afrika Mashariki, mtangamano wa kikanda na kimataifa, kupanuka kwa sayansi na teknolojia, uwekezaji, fursa za kitaalamu zinazoibuka na uhamaji wa watu katika kutafuta ajira na fursa nyinginezo. Utoaji wa elimu na mafunzo hauna budi kukidhi mahitaji haya na hivyo kuhitaji rasilimaliwatu stahiki.

Uwezo wa utoaji wa elimu na mafunzo unaathiriwa na upungufu wa rasilimaliwatu katika sekta ya elimu na mafunzo. Hali hii inasababishwa na changamoto katika mfumo wa ajira katika sekta ya elimu na mafunzo hususan kwa walimu, watendaji, wasaidizi na wasimamizi wa elimu katika baadhi ya maeneo ikiwemo miundo ya kuwatambua na kuwatayarisha, ajira, usimamizi, kuwavutia na kuwabakisha kazini, kuwaendeleza katika fani husika, kurithishana na kuondoka kwenye ajira pamoja na uwiano wa jinsia katika masuala hayo.

Lengo

Kuwa na rasilimaliwatu mahiri na wa kutosha ili kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali kwa maendeleo ya Taifa.

Tamko

3.4.1 Serikali itaboresha mfumo wa ajira katika sekta ya elimu na mafunzo ili uwe mahususi na kukidhi mahitaji, upatikanaji na usimamizi wa rasilimaliwatu kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu na mafunzo.

3.4.2 Serikali itaweka mazingira bora na kuhakikisha kuwa sekta ya elimu na mafunzo inatoa rasilimaliwatu wa kutosha na mahiri kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali kwa maendeleo ya Taifa.

3.5. Mfumo endelevu wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo nchini

Suala

Ugharimiaji wa elimu na mafunzo.

Maelezo

Kazi kubwa ya serikali ni kuweka mfumo endelevu wa ugharamiaji wa elimu na mafunzo nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Katika miaka ya hivi karibuni suala la ugharamiaji wa elimu na mafunzo limeendelea kuwa tete hususan katika kujua gharama halisi za kumsomesha mwanafunzi, vyanzo vya fedha kwa ajili ya kugharamia elimu au mafunzo, walengwa halisi wanaohitaji kugharamiwa elimu au mafunzo yao, aina ya ugharamiaji ambayo mlengwa anahitaji na jinsi ya kuifikisha katika eneo linalohusika. Eneo hili linahitaji kutizamwa kwa ukaribu ili kuweza kuweka mfumo na miundo ambayo itatupatia suluhisho.

Lengo

Page 20: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

14

Kuimarisha mfumo wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo na kufanya uwe endelevu.

Tamko

3.5.1 Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa elimu na mafunzo kwa ngazi zote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu na mafunzo.

3.6. Mfumo wa elimu na mafunzo unaozingatia masuala mtambuko.

Suala

Elimu ya mazingira na Afya ya Jamii

Maelezo

Ongezeko la idadi ya watu na shughuli mbalimbali za huduma ya kijamii na za uchumi zisizozingatia taratibu zinazofaa zimesababisha uharibifu wa mazingira nchini. Afya ya jamii inakabiliwa na matatizo na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazingira hatarishi, mitindo duni ya maisha na ukosefu wa maadili yanayosababisha matatizo mbalimbali ya afya. Matatizo hayo ni pamoja na saratani, shinikizo la damu, kiharusi, kisukari, VVU/UKIMWI, kifua kikuu, malaria,minyoo, kichocho, matumizi mabaya ya dawa za kulevya na lishe duni. Elimu itolewayo shuleni na vyuoni haina budi kumjengea mwanafunzi na jamii inayoizunguka tabia na utamaduni stahiki kuhusu utunzaji wa mazingira na afya ya jamii.

Lengo

Kuwa na sekta ya elimu na mafunzo yenye ufahamu, maarifa, stadi na utamaduni wa kutunza mazingira na afya ya jamii.

Tamko

3.6.1 Elimu na Mafunzo yenye maudhui ya masuala mtambuka kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa.

Suala

Ushauri na unasihi katika elimu na mafunzo na masuala ya kazi na kujiendeleza.

Maelezo

Huduma ya ushauri na unasihi inalenga kumwezesha mwanafunzi na jumuiya ya shule kwa ujumla kukabiliana na changamoto za maisha ili kujenga mwelekeo, tabia na kuendeleza mila, desturi na maadili mema katika jamii. Kutokana na kukosekana kwa huduma hii wakati mwingine kumesababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii. Pia huduma hii inahitajika katika kumsaidia mwanafunzi kujua mustakabali wa masomo atakayoyachagua au aliyoyachagua na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa na mwanafunzi mwenyewe. Huduma za ushauri na unasihi pia zinahitajika kwa wafanyakazi katika ngazi zote za elimu ili waweze kupata stadi za maisha za kujitambua na kufanya maamuzi sahihi katika kutekeleza wajibu wao kikamilifu.

Lengo

Kuwa na huduma ya ushauri na unasihi inayokidhi mahitaji katika elimu na mafunzo.

Page 21: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

15

Tamko

3.6.2 Serikali itaweka utaratibu wa kuimarisha utoaji wa huduma ya ushauri na unasihi katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Suala

Haki za mtoto na adhabu za kutesa na kudhalilisha

Maelezo

Watoto ni kundi kubwa katika jamii ambalo halina uwezo wa kujilinda dhidi ya uonevu wa aina mbalimbali. Haki za mtoto ni stahili maalumu ambazo mtoto anazaliwa nazo na anapaswa kufurahia kwa sababu tu yeye ni binadamu. Haki hizi zinahusisha maeneo makuu matatu yaani; haki za kupatiwa mahitaji muhimu ya kimaisha kama vile chakula, mavazi, malazi, elimu na fursa nyingine; haki za kulindwa dhidi ya maradhi, uonevu, udhalilishwaji, ubaguzi, ukatili wa aina yoyote na haki ya kushirikishwa kwenye masuala mbalimbali yanayowahusu. Baadhi ya adhabu ambazo zimekuwa zikitumika kwa ajili ya kuwarekebisha wanafunzi zimekuwa zikikinzana na dhana hii ya kumlinda na kumwendeleza mtoto. Hivyo, kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa elimu unaozingatia haki ya mtoto hususan unaoweka bayana wajibu wa jamii katika kumwendeleza mtoto na kuondokana na adhabu za kumtesa au kumdhalilisha.

Lengo

Kuwa na mfumo unaozingatia haki na wajibu wa mtoto katika utoaji wa elimu na mafunzo na kuzuia adhabu za kutesa na kudhalilishwa .

Tamko

3.6.3 Serikali itaweka utaratibu utakao hakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa na hapewi adhabu za kutesa au kudhalilisha wakati akipatiwa elimu au mafunzo katika ngazi

mbalimbali.

Suala

Nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika elimu na mafunzo.

Maelezo

Utawala bora unajumuisha uongozi, usimamizi na uendeshaji unaozingatia utawala wa sheria, uadilifu, nidhamu, uwajibikaji, uwazi, ushirikishwaji na usawa ili kufikia malengo mbalimbali ya maendeleo ya taifa. Utawala bora unapatikana kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria mbalimbali katika uongozi na utawala. Mmomonyoko katika sehemu yoyote ya utawala bora husababisha viongozi, watendaji na wanafunzi kutofikia malengo waliyokusudia na wakati mwingine kusababisha migomo, udanganyifu, matumizi mabaya ya rasilimali, uharibifu wa miundombinu pamoja na mambo mengine ambayo hayana manufaa kwa maendeleo ya Taifa.

Lengo

Page 22: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

16

Kuwa na nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika elimu na mafunzo

Tamko

3.6.4 Serikali itaongeza ufanisi, tija, uwajibikaji na uongozi bora katika usimamizi na uendeshaji wa elimu na mafunzo nchini

3.6.5 Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha maadili ya walimu na watumishi wengine yanazingatiwa katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Suala

Menejimenti ya data za Elimu na Mafunzo.

Maelezo

Menejimenti ya data inahusisha uratibu wa ukusanyaji, uchambuzi, uhifadhi na usambazaji wa data na taarifa. Hifadhi-data inawezesha uwepo wa data unganifu kutoka taasisi na asasi za elimu na mafunzo katika ngazi zote. Uwepo wa mfumo madhubuti wa menejimenti ya data unachangia kwa kiasi kikubwa kuleta ufanisi katika uendeshaji wa elimu na mafunzo. Kuna vyanzo vingi vya data za elimu na mafunzo ambavyo data zake hazina uhakiki na uratibu madhubuti. Hali hii inapunguza usahihi, uhakika na ufananivu wa data kwa wakati. Ni muhimu data na taarifa mbalimbali za Elimu na Mafunzo kukusanywa, kuchambuliwa na kuhifadhiwa vizuri ili ziweze kupatikana na kutumiwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Lengo

Kuimarisha mfumo wa menejimenti ya data za Elimu na Mafunzo.

Tamko

3.6.6 Serikali itaimarisha mfumo wa menejimenti ya data na taarifa za elimu na mafunzo kwa ngazi zote.

Suala

Ushirikiano wa elimu na mafunzo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Maelezo

Elimu ya Juu ni suala la muungano, wakati ngazi nyingine za elimu sio za muungano. Hata hivyo sekta za Elimu Tanzania Bara na Tanzania Visiwani zina uhusiano na ushirikiano katika maeneo ya mitaala na upimaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Hali kadhalika, katika ngazi ya elimu ya sekondari na vyuo vya ualimu kuna uhusiano katika maeneo ya mitaala, upimaji na utoaji vyeti. Kwa kuzingatia hali hiyo, kuna umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Lengo

Kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kielimu kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Page 23: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

17

Tamko

3.6.7 Ushirikiano katika Elimu na Mafunzo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utaimarishwa.

Suala

Ushirikiano katika elimu na mafunzo kikanda na kimataifa.

Maelezo

Tanzania imeridhia mikataba, itifaki na maazimio mbalimbali ya elimu na mafunzo kikanda na kimataifa. Mafanikio yaliyopatikana nchini katika sekta ya elimu na mafunzo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na utangamano na ushirikiano kikanda na kimataifa Pamoja na mafanikio, zipo changamoto mbalimbali hususan katika kuyatafsiri na kutekeleza kitaifa maazimio mbalimbali ya elimu na mafunzo yanayotokana na utangamano na ushirikiano huo.

Lengo

Kuweka utaratibu wa kutekeleza kitaifa maazimio ya kikanda na kimataifa katika elimu na mafunzo.

Tamko

3.6.8 Serikali itaweka muundo wa kutekeleza maazimio na itifaki za ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine, kikanda na kimataifa katika elimu na mafunzo.

Suala

Ardhi kwa asasi za elimu na mafunzo.

Maelezo

Asasi za elimu na mafunzo zinahitaji kuwa na ardhi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na maendeleo ya baadaye. Maeneo ya asasi hizo yanatakiwa kuwa ya amani, tulivu na salama ili kuhakikisha utoaji wa elimu bora. Asasi nyingi za elimu na mafunzo ziko kwenye ardhi ambayo haijamilikishwa kwao kisheria. Aidha, kumekuwepo na tabia ya uvamizi wa ardhi iliyotengwa kwa ajili ya asasi za elimu na mafunzo za Serikali na zisizo za Serikali. Ili kulinda ardhi za asasi za elimu na mafunzo nchini zisivamiwe, kuna umuhimu kwa asasi zote za elimu na mafunzo kuwa na umiliki wa ardhi kisheria.

Lengo

Kuwa na asasi za elimu na mafunzo zenye hatimiliki za ardhi kisheria.

Tamko

3.6.9 Serikali itahakikisha kila taasisi ya elimu na mafunzo inakuwa na hatimiliki ya ardhi mahali ilipo taasisi hiyo kwa ngazi zote.

Suala

Kutambua na kuendeleza vipaji na vipawa

Page 24: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

18

Maelezo

Mitaala kwa sasa haitoi fursa ya kutosha kubaini na kukuza vipaji na vipawa na haizingatii mahitaji ya wanafunzi wenye kasi ndogo au kubwa ya kujifunza katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Lengo

Kuwa na mfumo wa elimu na mafunzo unaotoa fursa ya kuendeleza vipaji na vipawa na kuzingatia uwezo wa mwanafunzi.

Tamko

3.6.10 Serikali itaweka utaratibu utakaowezesha maendeleo ya wanafunzi wenye vipaji, vipawa na kasi tofauti katika kujifunza kwa ngazi zote za elimu na mafunzo.

Suala

Elimu na mafunzo yasiyo na mwisho

Maelezo

Utoaji wa elimu na mafunzo endelevu kwa maana ya elimu na mafunzo yasiyo na mwisho ni jambo ambalo Taifa halina budi kulitilia maanani hususan kwa sababu ya maendeleo ambayo yameshafikiwa kwa sasa katika taaluma ya tathmini ya elimu na mafunzo. Hili ni muhimu katika kuwatambua na kuwapa fursa ya kujiendeleza katika ngazi mbalimbali hususan wale ambao wamepata elimu, maarifa, ujuzi au stadi mbalimbali bila kuwa darasani au sehemu zilizotengwa kwa ajili hiyo kwa sababu mbalimbali. Hii pia ni katika kutambua mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na taifa kubuni njia mbalimbali za elimu ikiwemo elimu kwa njia ya posta, elimu kwa njia ya redio, maktaba za taifa na kisomo cha watu wazima. Maeneo haya budi yazidi kuendelezwa ili kumfikia kila mtanzania katika elimu na mafunzo.

Lengo

Kutambua jitihada za Mtanzania kujiendeleza kielimu, kupata maarifa, ujuzi na stadi za kazi.

Tamko

3.6.11 Serikali itaweka utaratibu na kuimarisha utambuzi wa viwango vya Elimu na mafunzo ili kutoa fursa ya kila Mtanzania kujiendeleza kielimu, kupata maarifa na stadi za kazi kwa kuzingatia kwamba elimu au mafunzo hayana mwisho.

Suala

Utoaji wa elimu ya sayansi na teknolojia

Maelezo

Sayansi na teknolojia ni nyenzo muhimu katika kumwezesha binadamu kumudu mazingira yake na kumwezesha kuwa na maendeleo. Shule na vyuo vina majukumu muhimu ya kukuza elimu ya sayansi na teknolojia. Mitaala ya shule na vyuo inatakiwa kuwekea mkazo ufundishaji wa masomo ya hisabati, sayansi na teknolojia. Pia kuna umuhimu wa kuweka mkazo katika matumizi ya sayansi na teknolojia katika

Page 25: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

19

kufundishia na kujifunzia

Lengo

Kuwa na jamii inayotumia sayansi na teknolojia kwa ufanisi.

Tamko

3.6.12 Serikali itaboresha utaratibu wa ufundishaji wa masomo ya hisabati, sayansi na teknolojia katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

3.6.13 Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha matumizi zaidi ya sayansi na teknolojia katika utoaji wa elimu na mafunzo katika ngazi zote.

Suala

Ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika elimu na mafunzo

Maelezo

Serikali imetoa fursa kwa wadau mbalimbali kushiriki katika kuleta maendeleo ya Taifa na hivyo kubuni njia na mikakati mbalimbali kulifanikisha hili. Tayari, kwa mfano sera na sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ile ya binafsi zimeshapitishwa mwaka 2009 na kuanza kutumika. Katika sekta ya elimu na mafunzo ushiriki wa sekta ya binafsi umekuwa na tija katika kusaidia jitihada za serikali kutoa elimu na mafunzo kwa Mtanzania. Ushiriki huu hauna budi kuendelezwa ili kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

Lengo

Kuendelea kuboresha ushiriki wa wadau mbalimbali katika sekta ya elimu na mafunzo.

Tamko

3.6.14 Serikali itaweka utaratibu na kuimarisha ushiriki fanisi wa wadau mbalimbali katika sekta ya elimu na mafunzo katika ngazi zote.

Page 26: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

20

SURA YA NNE

4.0. MUUNDO WA KISHERIA

4.1 Sheria ya Elimu na Mafunzo

Utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo utakuwa na muundo wa kisheria utakaowawezesha wahusika kutekeleza majukumu yao. Sheria mbalimbali zinazohusu elimu na mafunzo nchini zitapitiwa upya na kufanyiwa marekebisho au kufutwa. Mapitio ya sheria hizo yatazingatia muundo wa kitaasisi ulioainishwa katika sera hii, vyombo vitakavyoanzishwa na makubaliano yaliyopo kwenye mikataba na maazimio mbalimbali ya kikanda na kimataifa kuhusu elimu na mafunzo.

4.2 Vyombo vya Kisheria vya Kusimamia Elimu na Mafunzo

Kutakuwepo na vyombo vya kisheria katika ngazi zote ili kusimamia utekelezaji wa elimu na mafunzo katika maeneo hayo kwa mujibu wa sheria. Vyombo hivyo vitasimamia: uanzishaji wa shule na vyuo, uanzishaji na utekelezaji wa programu za elimu na mafunzo, maendeleo ya taaluma na utaalamu, nidhamu, uwajibikaji na maadili katika elimu na mafunzo, utoaji wa huduma za maktaba kwa wananchi, udhibiti na uthibiti wa ubora wa elimu na mafunzo; ulinganifu wa sifa za kitaalamu na kitaaluma; usimamizi wa rasilimali na ushauri wa elimu na mafunzo.

4.3 Sheria za Kusimamia Shule na Vyuo vya Elimu na Mafunzo

Shule na vyuo vitatambuliwa kisheria na kuundiwa vyombo vya usimamizi.

Page 27: Rasimu ya Sera ya Elimu Tanzania

21

SURA YA TANO

5.0 MUUNDO WA KITAASISI

Sera ya Elimu na Mafunzo itatekelezwa katika ngazi zote za elimu na mafunzo. Ili kufikia azma hiyo, Wizara yenye dhamana ya Elimu na Mafunzo itashirikiana na wizara nyingine, mashirika na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, washirika wa maendeleo wa ndani na nje, jamii na wadau wengine wa elimu na mafunzo. Aidha, Sera ya Elimu na Mafunzo itatekelezwa kiutawala na kiutendaji katika ngazi za; Taifa, Serikali za mitaa, shule na vyuo na kwamba Serikali itaweka muundo wa kitaasisi katika ngazi zote utakaofanikisha utekelezaji wake.

5.1. UFUATILIAJI NA TATHMINI

Ufuatiliaji na Tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ni jukumu la Wizara yenye dhamana ya Elimu na mafunzo. Hata hivyo, ufuatiliaji na tathmini utategemea juhudi za pamoja na ushiriki wa karibu baina ya wizara nyingine, mashirika na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, washirika wa maendeleo wa ndani na nje, jamii na wadau wengine wa elimu na mafunzo.

Utekelezaji wa matamko yaliyo ainishwa katika sera utaenda sambamba na mkakati wa utekelezaji wa sera. Wizara yenye dhamana ya elimu na mafunzo ya ufundi itakusanya, itaunganisha na kuchambua taarifa za utekelezaji wa programu mbalimbali. Wadau wote wanategemewa kutoa taarifa stahiki kwa wizara yenye dhamana ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Wizara yenye dhamana ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na wadau wengine watakuwa na majukumu yafuatayo katika ufuatiliaji na tathmini ikiwemo kuweka viashiria, vigezo na muda wa tathmini.

5.2. HITIMISHO

Sera hii ya Elimu na Mafunzo imeandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Madhumuni ya sera hii ni kutoa mwongozo wa jumla wa uendeshaji wa elimu na mafunzo kwa mtazamo wa dira ya maendeleo ya Taifa 2025, mipango na mikakati ya maendeleo ya Taifa, na mabadiliko ya ulimwengu hususan katika uchumi, sayansi na kiteknolojia ili tuweze kufikia lengo la kuwa na uchumi unaoendeshwa na elimu na ujuzi na kulifanya Taifa liwe moja ya mataifa yaliyo na kipato cha kati.

Sera hii pia imezingatia masuala mtambuko ili kufanikisha kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.