Upload
zanzibari-amani
View
123
Download
2
Embed Size (px)
DESCRIPTION
MWONGOZO NA MAADILI YAWAANGALIZI WA NDANI NA WA NJE WA CHAGUZI ZA ZANZIBAR
Citation preview
TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR
MWONGOZO NA MAADILI YA
WAANGALIZI WA NDANI NA WA NJE WA
CHAGUZI ZA ZANZIBAR
Kimetayarishwa na
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
July, 2015
1
MWONGOZO NA MAADILI YA WAANGALIZI WA NDANI
NA WA NJE WA CHAGUZI ZA ZANZIBAR
DIBAJI
Napenda kuchukuwa fursa hii adhimu kuwakaribisheni nyote, kwa niaba ya Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar na watu wa Zanzibar kwa kukubali mwaliko wa kuwa
Waangalizi wa Uchaguzi katika hali yoyote ile uwe Mwangalizi wa Ndani au
Mwangalizi wa Nje.
Kila Mzanzibari ana haki ya kutumia haki ya kisheria ya kupiga kura kupitia karatasi
ya kura na kuyafanya mawazo au uamuzi wake huo kuheshimiwa. Tume itahakikisha
kila kura iliyo halali inahesabiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Katika
kuhakikisha hilo, Tume imewakaribisha watu wote na wenye nia na lengo jema
wakiwemo Waangalizi wa Uchaguzi.
Tume imefanya matayarisho ya kutosha ili kuhakikisha, Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar
wa 2015, unakuwa ni uchaguzi huru na wa haki na unakidhi matarajio ya wadau,
wakiwemo wapiga kura na wananchi wa Zanzibar. Kila jitihada imefanywa
kuhakikisha watendaji na wasimamizi wa uchaguzi wamepatiwa mafunzo ya kutosha
na wana tabia nzuri. Tume haikusahau suala la uagiziaji wa vifaa ambao umefanywa
kwa wakati ili kuweka mazingira bora ya uchaguzi.
Waangalizi wa Uchaguzi, wana wajibu na wanashauriwa kuweka bayana mafanikio
na kuibuwa changamoto yoyote inayoweza kutokea kupitia Mwngozo huu.
Waangalizi wana umuhimu mkubwa katika kujiridhisha kuwa wapiga kura wanapiga
kura zao katika mazingira ya usalama na amani bila ya vitisho au kulazimishwa
kupiga kura kwa namna fulani na taratibu za upigaji kura zinafuatwa kikamilifu.
Waangalizi, pia watashuhudia iwapo matokeo yaliyotangazwa na Tume yanaendana
na kura zilizohesabiwa. Waangalizi wanapaswa kujua kuwa, ripoti zao za uangalizi
zinatoa taarifa muhimu kwa kuboresha upigaji kura Zanzibar hasa zikizingatia
umuhimu wa ushiriki wa makundi yaliyo katika hatari ya kukandamizwa wakiwemo
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Matayarisho ya kutosha yamefanywa na Tume kwa kufanikisha uangalizi wa
uchaguzi katika hatua zote za uangalizi kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kituo
kinaanzishwa cha kuwasaidia Waangalizi kupata ruhusa zao na pia kuwarahisishia
kazi wao na waandishi wa habari.
Mwongozo huu wa Waangalizi, unaendana na maudhui ya Sheria ya Uchaguzi
Namba 11 ya 1984 na Kanuni zake, Miongozo ya kimataifa ya uangalizi wa uchaguzi,
2
pamoja na Sera ya Tume ya Jinsia na Ushirikishwaji Jamii ya Mwaka 2015 na
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Nawashauri Waangalizi wote watekeleze majukumu yao kwa umakini na weledi na
vile vile kutoa taarifa juu ya mazuri na mabaya yote yanayohusiana na uchaguzi.
Kwa mara nyengine tena nawakaribisha nyote kufanya uangalizi wa uchaguzi wa
mwaka 2015.
Bw. Salum Kasim Ali
Mkurugenzi wa Uchaguzi
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
3
1.0 UTANGULIZI
Mwongozo huu umekusudiwa kuwasaidia Waangalizi wa Ndani na wa Nje kujua
nidhamu inayotarajiwa kwao watapokuwa Zanzibar, na kuwaongoza katika
utekelezaji wa majukumu yao ya uangalizi wa uchaguzi. Kutokana na sababu
hiyo, Mwongozo huu umejumuisha Maadili ya Waangalizi wa Uchaguzi
wanaoangalia chaguzi za Zanzibar.
Mwongozo pia, una lengo la kusaidia zoezi la uangalizi wa uchaguzi lifanyike bila
ya bughudha kwa mtu ye yote, awe mpiga kura, mtendaji wa uchaguzi,
waangalizi wengine au mdau mwingine yeyote wa uchaguzi.
Uangalizi wa uchaguzi una umuhimu mkubwa kwa vile unasaidia katika kujenga
ukweli, uaminifu na uhalali wa uchaguzi kwa vile unasaidia kujenga mazingira
kwa uchaguzi kuendeshwa kwa uwazi, uhuru na kwa mujibu wa sheria.
Mahususi, uangalizi wa uchaguzi unasaidia kuwaweka watendaji wa uchaguzi
katika hali ya umakini wa kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi na katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kuendesha uchaguzi.
Katika kufanikisha hili, Waangalizi wa uchaguzi wanatakiwa watekeleze wajibu
wao kwa weledi ili kujijengea imani ndani ya mchakato wa uchaguzi na kutoka
kwa wadau wengine.
2.0 UHALALI WA KISHERIA
Mwongozo huu pamoja na Maadili ya Waangalizi wa Uchaguzi kwa ajili ya
Waangalizi wataoangalia chaguzi za Zanzibar, umetolewa chini ya kifungu cha
130 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya 1984, na utawahusu Waangalizi wote
wataoruhusiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
3.0 TAFSIRI
Katika Mwongozo huu, isipokuwa itavyoelezwa vyenginevyo maneno:
a) “Uangalizi wa Ndani” maana yake ni uangalizi wa hatua yoyote ya uchaguzi,
moja au zote zilizomo katika mzunguko wa uchaguzi, unaofanywa na asasi za
ndani na/au mtu ambaye ameruhusiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
kufanya uangalizi.
b) Uangalizi wa Kimataifa” maana yake ni uangalizi wa hatua yoyote ya
uchaguzi, moja au zote zilizomo katika mzunguko wa uchaguzi zikiwemo
tathmini za hali za kabla na baada ya uchaguzi, unaofanywa na asasi za
4
kimataifa na wawakilishi wa serikali za nje walioruhusiwa na Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar kufanya uangalizi.
c) “Waangalizi” maana yake ni waangalizi wa Ndani na wa Nje ya Tanzania, na
inajumuisha wale wanaokuja kutoka nje ya Tanzania kwa ajili ya kutathmini
hali kabla na baada ya uchaguzi.
d) “Kundi la Waangalizi” maana yake ni kundi la Waangalizi walioletwa au
kudhaminiwa na asasi.
e) “Maadili” maana yake ni masharti yaliyomo katika kifungu cha 13 cha
Mwongozo huu.
f) “Tume” maana yake ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
g) “mzunguko wa uchaguzi” maana yake ni mfuatano wa hatua mbali za
uchaguzi toka maandalizi kabla ya uchaguzi, kufanyika kwa uchaguzi
wenyewe hadi tathmini za baada ya kukamilika kwa uchaguzi.
4.0 MUDA WA UANGALIZI:
Muda wa uangalizi wa uchaguzi kuhusiana na Mwangalizi utaanzia tarehe
atayopata ruhusa hadi
a) tarehe iliyowekwa ya kuwasilisha ripoti ya mwisho ya uangalizi, au
b) kufutwa kwa ruhusa ya uangalizi kutokana na kuvunja Maadili, au
c) baada ya kukamilika kipindi cha miezi mitatu baada ya kutangazwa kwa
matokeo ya uchaguzi;
lolote kati ya hayo litalotokea mwanzo.
5.0 AINA ZA WAANGALIZI
Kutakuwa na Waangalizi wa aina zifuatazo:-
a) Waangalizi wa Ndani ambao wanaweza kutoka katika:
i) Asasi za umma zinazofanyakazi Zanzibar ambazo miongoni mwa
majukumu yake yanahusiana na masuala ya uchaguzi na utawala
bora.
ii) Asasi za kijamii kama vile zisizo za kiserikali (NGO’s) na za wananchi
(CBOs) ambazo zimesajiliwa Zanzibar.
5
iii) Asasi za kidini zilizosajiliwa katika Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania
iv) Wawakilishi wa wagombea na wa vyama vya siasa, vyombo vya
habari na waandishi wa habari wenye vibali vilivyotolewa na
Mamlaka zinazohusika za Zanzibar.
b) Waangalizi wa Nje wanaoweza kutoka katika :-
i) Mashirika au Taasisi za Kimataifa ambazo Tanzania ni mwanachama
au ina uhusiano wa kidiplomasia nazo.
ii) Mashirika au Taasisi za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama au
zina uwakilishi Tanzania.
iii) Ofisi za kibalozi za nchi za nje zinazowakilisha nchi zao Tanzania.
iv) Tume za Uchaguzi kutoka nchi nyengine za Dunia.
v) Asasasi zisizo za kiserikali za kimataifa zinazofanya kazi Tanzania au
iwapo hazifanyi kazi Tanzania, zimepata kibali maalumu cha mamlaka
husika za Zanzibar.
c) Waangalizi wa muda mfupi ambao ni Waangalizi wa Nje wanaokuja
nchini kwa ajili ya kutathmini hali kabla au baada ya uchaguzi na kukaa
kwa muda usiozidi ziku 15.
d) Waangalizi wa muda mrefu ni Waangalizi wa Nje wanaokuja kwa
uangalizi wa hatua zaidi ya moja za uchaguzi na kukaa kwa muda
unaozidi siku 60.
6.0 RUHUSA YA UANGALIZI WA UCHAGUZI:
Kabla ya kuanza majukumu ya uangalizi, Waangalizi lazima wawe wameshapata
ruhusa ya uangalizi ili kuwatofautisha na wadau wengine wa mchakato wa
uchaguzi. Utoaji wa ruhusa kwa Waangalizi ni jukumu la Tume pekee. Ili
Waangalizi waweze kupatiwa ruhusa, utaratibu ufuatao lazima ufuatwe:-
a) Mialiko ya jumla kwa Waangalizi wa Nje hutolewa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
b) Asasi na serikali zinazodhamini Waangalizi zitaijuilisha Tume juu ya dhamira
na mipango yao ya kuleta Vikundi vya Waangalizi, kabla ya siku ya mwisho
itayokuwa imewekwa na Tume.
6
c) Ili mtu atambulike kama Mwangalizi, anatakiwa awe amethibitishwa
kimaandishi na asasi husika au Serikali ya nje kwa Tume kupitia barua
itayotoa taarifa mbali mbali zinazomhusu pamoja na wasifu wake.
d) Japokuwa Waangalizi huweza kuletwa na asasi, ruhusa ya uangalizi
hutolewa kwa Mwangalizi binafsi; kwa hivyo wanawajibika pia kuomba
ruhusa kila mmoja binafsi.
e) Katika maombi yake, kila Mwangalizi atatakiwa kuwasilisha wasifu na taarifa
zake rasmi za utambulisho kwa Tume.
f) Zaidi ya nyaraka za utambulisho wa Mwangalizi zilizowasilishwa na asasi
iliyomdhamini au Serikali yake, kila Mwangalizi atapatiwa na Tume, hati ya
ruhusa pamoja na kitambulisho au vitambulisho vitavyomwezesha
kutambulika kwa urahisi.
g) Mwangalizi atatakiwa muda wote atapokuwa anatekeleza jukumu lake la
uangalizi, kuvaa kwa uwazi kitambulisho atachokuwa amepatiwa na Tume;
atachukua pia nyaraka zake za ruhusa ya uangalizi; na kwa Mwangalizi wa
nje atachukua pamoja na nyaraka hizo, nyaraka zake halali za kusafiria.
7.0 VIDOKEZO VYA USHAURI KWA AJILI YA UANGALIZI WENYE UFANISI
Itapendeza kwa Mwangalizi:-
a) Kuwa na kiasi fulani cha uzoefu, sifa ya kutopendelea upande wowote, na
kuonyesha uhuru wa mawazo ili asiburuzwe na vyama vya siasa.
b) Kuweza kuzungumza Kiswahili na/au Kingereza kwa ajili ya mawasiiliano
na wenyeji;
c) Kuwa na uelewa wa Sheria za Uchaguzi za Zanzibar;
d) Kuwa na uelewa na ufahamu wa viwango vya kimataifa vya kuweza
kupambanua hali za mchakato uchaguzi kuwa huru na wa haki ;
e) Kuwa na uwelewa wa historia, jiografia, utamaduni na hali halisi ya
kisiasa ya Zanzibar na;
f) Kuzipa uzito taarifa na ripoti zake za uangalizi kwa kubainisha rejea za
sheria,kanuni, mpango mkakati, na sera zinazoongoza uchaguzi na
kuzioanisha na viwango vya kimataifa vilivyo ridhiwa na Serikali ya
Tanzania juu ya upigaji kura katika vituo vya upigaji kura.
7
8.0 MIONGOZO MAALUMU KWA WAANGALIZI WA NJE
Waangalizi wa Nje zaidi ya masharti ya jumla watawajibika:-
a) Kuwa na hati halali za kusafiria ikiwemo viza pale inapohitajika.
b) Kufuata maelekezo ya kiafya.
c) Kuzingatia vidokezo vya afya vitavyotolewa na Tume na
d) Kufuata tahadhari za kiusalama zitazotolewa na Tume.
9.0 NYARAKA NA TAARIFA ZA MAELEZO YA AWALI
Tume itatoa kwa Waangalizi nyaraka na taarifa juu ya masuala mbali mbali
yanayohusu Zanzibar.
Nyaraka na taarifa hizo zitajumuisha yafuatayo:-
a) Taarifa zinazohusiana na historia (ikiwemo ya uchaguzi), jiografia na hali
halisi ya kisiasa ya Zanzibar.
b) Taarifa kuhusu mchakato wa uchaguzi zikiwemo sheria na kanuni za
uchaguzi.
c) Orodha ya vituo vya kupigia kura anavyotaka kuvifanyia kazi mwangalizi.
d) Orodha ya vyama vya siasa vyenye usajili kamili.
e) Orodha ya wagombea na vyama vyao katika jimbo.
f) Ratiba ya Mikutano ya kampeni za Uchaguzi.
g) Sera ya Tume ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Jamii ya mwaka 2015.
h) Nyaraka nyingine zozote ambazo Tume itaona zitafaa kupatiwa
Waangalizi.
10.0 UPEO WA UANGALIZI :
Upeo wa uangalizi utajumuisha vipindi vyote vya mzunguko wa uchaguzi na
hususan utajumuisha tathmini ya mambo yafuatayo miongoni mwa mengine:-
a) Tume kutopendelea na kufanya kazi kwa uadilifu.
b) Haki na uhalali wa kisheria wa maamuzi yanayofanywa na Tume kuhusiana
na migogoro ya kiuchaguzi.
c) Kutosheleza kwa mfumo wa kisheria unaoongoza masuala ya uchaguzi.
d) Haki katika ukataji wa majimbo ya uchaguzi.
e) Utaratibu wa uandikishaji wa wapiga kura.
f) Mchakato wa uteuzi wa wagombea kuanzia ndani ya vyama vya siasa.
g) Utaratibu wa kuendesha na kusimamia kampeni za uchaguzi.
h) Utaratibu wa kupiga kura na kutangaza matokeo.
8
i) Ujumuishaji wa kura katika hatua zote na kutangaza matokeo ya uchaguzi.
j) Hali ya kisiasa baada ya kukamilika kwa uchaguzi.
k) Katika tathmini yake ya kila moja ya hatua hizi na masuala mengine ya
mzunguko wa uchaguzi, Mwangalizi atatarajiwa kukusanya taarifa sahihi
kwa kuzingatia yafuatayo:-
i) Uelewa wa kutosha wa Sheria, Kanuni, Mpango Mkakati na Sera
zinazoongoza chaguzi na taratibu za utendaji kazi wa Tume.
ii) Hali halisi ya kisiasa ya nchi, kabla, wakati na baada ya uchaguzi,
hususan taswira za wananchi kuhusiana na maisha yao ya kawaida,
usawa wa kijinsia na ushiriki wa makundi mbalimbali ya kijamii,
harakati za vyama vya siasa, wagombea, wapambe na wengineo.
iii) Ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hususan
mazingatio maalumu watakayokuwa wamewekewa kurahisisha
ushiriki wao katika uchaguzi.
iv) Mchanganuo wa takwimu kijinsia.
v) Hali ya utayari wa uchaguzi kama vile uandikishaji wa wapiga kura,
utoaji wa elimu ya uraia na ya wapiga kura, uteuzi wa wagombea,
ukataji wa majimbo ya uchaguzi, kampeni za uchaguzi n.k.
vi) Uelewa juu ya wajibu wa kila mdau wa uchaguzi na wananchi kwa
jumla katika shughuli za uchaguzi.
vii) Namna haki za msingi za watu zinavyoheshimiwa kwa mnasaba wa
uchaguzi.
viii) Kama vyombo vya habari vya umma vinatumiwa kwa usawa na
vyama vya siasa wakati wa kampeni.
ix) Kama fursa ya matumizi ya vyombo vya habari vya binafsi
inatolewa kwa usawa kwa vyama vya siasa pamoja na kuzingatia
maslahi yaliyotangazwa navyo.
x) Uheshimu wa jumla wa Maadili ya Vyama vya Siasa na wadau
wengine.
xi) Uwakilishi wa vyama vya siasa na/au wagombea katika maeneo na
vituo vya uandikishaji na kupigia kura.
9
xii) Ushirikishwaji wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi
katika harakati za Tume ya uchaguzi.
xiii) Uzowefu na uwezo wa watendaji wa uchaguzi katika kupanga na
kuendesha uchaguzi.
xiv) Maoni ya jumla juu ya uchaguzi ulivyokwenda hususan kuhusu
kujitokeza kwa wapiga kura; urahisi wa mchakato wa upigaji kura,
uhesabuji wa kura, ujumuishaji wa kura na utangazaji wa matokeo.
xv) Aina ya migogoro iliyojitokeza na namna ilivyoshughulikiwa na
wahusika wa shughuli za uchaguzi.
xvi) Kutathmini taarifa zote bila ya jazba za aina yoyote, wala upendeleo
kwa mwelekeo wa kuweka wazi mambo yaliyokwenda vyema;
mambo yaliyokwenda kombo kutokana na kuvunjwa kwa sheria na
kanuni na kupuuzwa kwa viwango vya kimataifa vya uendeshaji wa
uchaguzi; na hatimaye masuala yatayopaswa kushughulikiwa katika
chaguzi za siku za mbele.
xvii) Kuwasilisha ripoti za uangalizi wa uchaguzi kwa Tume na wadau
wengine wanaohusika.
11.0 UTARATIBU WA KURIPOTI:
Ni matarajio ya kawaida kwamba Kundi la Waangalizi litabainisha miongozo yake
kwa Waangalizi wake kabla ya kuanza majukumu yake. Hata hivyo, Waangalizi
Zanzibar wanatarajiwa kutoa taarifa/ripoti za wanayoyaona katika hatua tatu
kama ifuatavyo:-
a) Wakati wa Uangalizi Wenyewe:
Mwangalizi ataripoti bila ya kuingilia kati kwa aina yoyote mchakato wa
uchaguzi unaoendelea, changamoto yoyote ya kiutekelezaji wa sheria
atayoibaini wakati wowote wa uandikishaji wapiga kura au upigaji kura, kwa
Tume au Msimamizi wa Uchaguzi au Msaidizi wake ambaye ataifanyia kazi
kasoro hiyo na kuirekebisha ipasavyo.
b) Mara Baada ya Uchaguzi:
Mwangalizi au Kundi la Waangalizi, kwa kadiri itavyokuwa, litawajibika
kutoa taarifa ya awali ya uangalizi itayoelezea tathmini yake ya ujumla juu
ya uchaguzi ulivyoendeshwa.
10
c) Katika kipindi cha siku 90 baada ya kutangazwa kwa matokeo
Waangalizi au makundi ya Waangalizi, kwa kadiri itavyokuwa, watawajibika
kuwasilisha ripoti zao za mwisho za uangalizi kwa Tume.
Katika utayarishaji wa ripoti zao, Waangalizi au makundi ya Waangalizi
watapaswa kuzingatia yafuatayo:-
i) Upekee na uhalisia wa Zanzibar, kuhusiana na historia yake,
maendeleo ya kikatiba, shughuli za kisiasa, utamaduni na mfumo wa
uchaguzi.
ii) Kila uchaguzi una mambo yanayoutofautisha na mwingine kulingana
na sehemu unapofanyika na sheria zinazouongoza.
iii) Uchambuzi wenye kuheshimika wa mambo yaliyoonekana katika
uangalizi wa uchaguzi hutokana na taarifa za kweli, zilizo sahihi na
zenye kuthibitika. Uchambuzi unaotokana na hisia, utashi, uvumi au
mtazamo aliokuja nao Mwangalizi hupelekea ripoti zisiso sahihi.
iv) Kutumia lugha ambayo haitokuwa chanzo cha mtafaruku na mgogoro
usiokuwa wa lazima.
v) Ripoti zisielezee tu mambo yaliyokwenda kombo, bali pia mambo
yaliyokwenda vyema na kutoa mapendekezo juu ya mambo ya
kufanya yatayosaidia kufanya chaguzi za siku za mbele kuwa bora
zaidi.
vi) Katika ripoti zao, Waangalizi wanapaswa kujiepusha kuingiza maneno
ya uvumi kutoka watu wengine, bali wajikite katika mambo
waliyoyaona wenyewe, wakizingatia vidokezo mbalimbali vya ushauri
vilivyomo katika Mwongozo huu.
12.0 HAKI ZA WAANGALIZI:
Waangalizi Zanzibar watakuwa na haki zifuatazo:-
a) Kuomba na kupatiwa kwa wakati muafaka taarifa stahiki juu ya kila hatua
ya mchakato wa uchaguzi.
b) Kupata wepesi wa kuingia katika maeneo ya uchaguzi kama vile vituo vya
uandikishaji au vya kupigia kura wakati na baada ya shughuli husika; na
kuomba na kupatiwa taarifa kutoka kwa wahusika walioruhusika wa
11
uendeshaji wa uchaguzi, watendaji wa vyombo vya kutunga sheria,
maofisa husika wa serikali, waandishi wa habari, asasi nyengine yoyote
husika na wadau wataofikiriwa kuwa na taarifa zitazoweza kusaidia
uangalizi.
c) Kuwa na uhuru wa kutembea Zanzibar yote isipokuwa maeneo ya kijeshi
na maeneo mengine yaliyokatazwa kisheria.
d) Bila ya kuathiri Maadili yaliyotajwa katika kifungu cha 13 cha Mwongozo
huu, kuwasiliana kwa uhuru na wawakilishi wa vyama vya siasa.
e) Kuhakikisha usalama wao pahali popote wanapokwenda wakitekeleza
majukumu yao.
13.0 MAADILI YA WAANGALIZI :
Ingawa Waangalizi hutekeleza majukumu yao kwa uhuru, kuna sheria, kanuni na
maadili wanayotarajiwa kama sharti la msingi na wajibu, kuyaheshimu na
kuyafuata ili wadhihirike kuwa ni watu wenye hadhi stahiki ya kuaminika na
kuheshimika; na vitendo vyao vyenye faida katika kukuza demokrasia ya
uchaguzi
Kwa kuzingatia misingi ya sheria za uchaguzi, kanuni na viwango vya kimataifa
vya uendeshaji uchaguzi, Waangalizi watawajibika kutekeleza masharti yafuatayo
ambayo kwa pamoja yanafanya Maadili ya Waangalizi:-
a) Kuruhusiwa kwa ukamilifu na Tume kabla ya kuanza harakati za uangalizi.
b) Kuzielewa na kuziheshimu sheria za Tanzania kwa jumla na hususan za
Zanzibar.
c) Kutopendelea kabisa kwa namna yoyote vyama vya siasa, wagombea na
mchakato wote wa uchaguzi kwa jumla.
d) Kuwa watu wenye tabia za kujiheshimu na kuheshimu wengine.
e) Kuheshimu majukumu, hadhi na madaraka ya maafisa wa uchaguzi.
f) Kutoingilia kwa namna yoyote, kazi za maofisa wa uchaguzi wala uendeshaji
wa uchaguzi kwa ujumla.
12
g) Kuepuka malumbano na maofisa wa uchaguzi, mawakala wa vyama vya
siasa na wa wagombea, Waangalizi wengine, wadau wengine ndani ya
vituo vya kuandikishia wapiga kura na vya kupigia kura ambayo yanaweza
kusitisha mwenendo wa uandikishaji, upigaji kura na kuhesabu kura.
h) Asifanye kazi za utendaji (kama vile kutoa maagizo au amri kwa watendaji
wa shughuli za uchaguzi), wala asifanye kazi za tume ya uchunguzi au za
ushauri elekezi.
i) Kujizuia kutoa taarifa kwa umma ambazo zinaweza kusababisha mtafaruku
au migongano wakati wa mchakato wa uchaguzi.
j) Kujiepusha kutoa maelezo na taarifa zisizo sahihi.
k) Kujiepusha na matumizi ya lugha au vitendo vinavyoweza kusababisha
uvunjifu wa amani wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea.
l) Kutowatumia kisiasa wasaidizi wao kama vile wakalimani na madereva.
m) Kuheshimu utamaduni wa nchi.
n) Kutotangaza au kutochapisha kabisa matokeo ya uchaguzi kabla
hayajatangazwa na Tume.
o) Kurudisha kitu chochote ambacho ametakiwa na tume kurejesha baada ya
matumizi yake.
p) Kuwasilisha ripoti kamili ya uangalizi kwa Tume katika kipindi kisichozidi siku
90 baada ya kutangazwa kwa matokeo kwa kuzingatia maelekezo ya
kifungu cha 11(c) cha Mwongozo huu.
14.0 KUONDOLEWA HADHI YA UANGALIZI
Mwangalizi yeyote anaweza kuzuiliwa uangalizi wake katika mazingira
yafuatayo:-
a) Ikiwa atakiuka kipengele chochote cha Maadili, ruhusa yake ya uangalizi
itaweza kufutwa (baada ya mashauriano na uongozi wa Kundi lake la
Waangalizi au asasi iliyomdhamini); hivyo kusababisha kuzuiliwa kwa
harakati zake za uangalizi.
b) Ikiwa atamfanyia kampeni mgombea au chama cha siasa au kuonesha
upendeleo kwao, siyo tu ruhusa yake ya uangalizi itafutwa, bali pia atakuwa
13
ameathiri uwezekano wa kuruhusiwa tena kushiriki uangalizi wa chaguzi za
siku za mbele za Zanzibar.
c) Ikiwa Mwangalizi au Kundi la Waangalizi limekiuka matakwa ya kifungu cha
13(p) cha Mwongozo huu watakuwa wameathiri sana uwezekano wa
kuruhusiwa tena kushiriki uangalizi wa chaguzi za siku za mbele za Zanzibar.
15.0 KUTUMIKA NA KUMALIZIKA MATUMIZI YA MWONGOZO HUU:
Mwongozo huu utaanza kutumika pale Mwangalizi au Kundi la Waangalizi
watapokubali mwaliko waliopewa na Tume, na utakoma pale Mwangalizi au
Kundi hilo litapowasilisha ripoti yake ya mwisho, au vinginevyo
atapokuwa/litapokuwa limeondolewa hadhi ya uangalizi.
Jecha S. Jecha
Mwenyekiti
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
Zanzibar, 2015
14
TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR
Ahadi ya Waangalizi wa Uchaguzi Kutekeleza Mwongozo na Maadili
Nathibitisha kuwa, nimeusoma na kuuelewa Mwongozo huu na Maadili ya Wangalizi
wa Uchaguzi kwa Waangalizi wa Ndani na wa Nje.
Sasa naahidi kuwa nitautekeleza na kuufuata Mwongozo huu na kwamba utekelezaji
wa majukumu yangu utafuata Mwongozo huu. Sina mgongano wa maslahi ya
kisiasa, kiuchumi au mengineyo yoyote, ambao unaweza kuathiri uwezo wangu wa
utendaji kazi wa kuwa Mwangalizi asiyekuwa na upande fulani na kufuata kikamilifu
Maadili ya uangalizi yaliyomo katika Mwongozo huu.
Naahidi kuwa nitahakikisha kuwa nitafanya kazi zangu bila ya kuwa na upendeleo wa
kisiasa. Nitatoa maamuzi kufuatana na taarifa sahihi na kufanya uchambuzi
usioegemea popote wakati wote. Nitatoa uamuzi kufuatana na ushahidi ulio wazi na
uliofanyiwa utafiti.
Kwa hali na namna yoyote ile sitoingilia kati wala kuzuwia mchakato wa uchaguzi.
Nitaheshimu sheria za Zanzibar na Tanzania na mamlaka ya watendaji wa uchaguzi
na kuendeleza heshima juu ya mamlaka za uchaguzi na nyenginezo. Nitaheshimu
haki za msingi na uhuru wa watu wa Zanzibar. Nitadumisha tabia njema na heshima
kwa wengine, nitaheshimu tamaduni, mila na silka za Zanzibar na nitafanya
maamuzi muafaka katika kujitathmini na kuhakikisha nafanya kazi zangu kwa weledi
wa hali ya juu wakati wote, ikiwemo wakati wa faragha.
Naahidi kulinda heshima ya asasi za uangalizi za ndani, Makundi ya Waangalizi wa
Nje ambayo ninayafanyia kazi na kufuata maelekezo yao. Nitahudhuria mikutano ya
kupata taarifa, mafunzo na kutoa taarifa inayotakiwa. Nitashirikiana katika kuandaa
maelezo au taarifa kadiri itavyohitajika kwangu. Sitatoa taarifa, maelezo au
majumuisho yangu binafsi kwa vyombo vya habari au kwa umma kabla ya asasi
yangu ya uangalizi ya ndani au Kundi langu la Waangalizi wa Nje kutoa taarifa yake,
isipokuwa kama nitaruhusiwa au nitaelekezwa hivyo.
15
Jina : ______________________Wadhifa : ____________________
Taasisi ya Uangalizi : ______________________________________
Uraia: __________________________________________________
Saini: ________________________
Tarehe:_____________________