Upload
others
View
1
Download
0
Embed Size (px)
Citation preview
International
Labour
Organization
INTERNACIONAL
INSTITUT FOR
LABOUR STUDIES
STUDIES ON
GROWTH WITH EQUITY
KUFANYA AJIRA
BORA KUWA KICHOCHEO
CHA MAENDELEO
MUHTASARI WA JUMLA NA
MAPENDEKEZO YA SERA
Ukuaji wa uchumi nchini Kenya umeimarika zaidi katika miaka ya hivi karibuni…
Katika mwaka wa 2003, ukuaji wa uchumi wa Kenya uliimarika: ukuaji halisi wa Jumla ya
Pato la Taifa uliimarika kila mwaka kutoka asilimia 0.3 katika mwaka wa 2002 hadi
takriban asilimia 7 katika mwaka wa 2007 sawa na ukuaji wa mataifa mengine ya Afrika,
Kusini mwa Sahara na hata juu kidogo ikilinganishwa na kiwango cha ukuaji cha
ulimwengu cha asilimia 5.4 kwa wakati huo. Kulikuwepo na ukuaji wakati huu ingawa
kulikuwa na ukame wa mara kwa mara ulioathiri sekta ya kilimo na kusababisha kuibuka
na kufufuka kwa sekta nyingine kama vile sekta ya utalii.
Hata hivyo, mwaka 2008, awamu hii ya upanuzi ilifikia kikomo chake ghafla baada ya
uwekezaji na biasharanje kuporomoka. Ufifiaji huu ulisababishwa kwa kiwango fulani na
vita vya baada ya uchaguzi vilivyozuka mwanzoni mwa mwaka huo, ambao uliathiri sana
sekta nyingi za kiuchumi katika miezi sita ya kwanza ya mwaka wa 2008. Hali hii ya
kuzorota kwa uchumi iliharibiwa zaidi na kudorora kwa hali ya kifedha na kiuchumi
ulimwenguni hasa kufuatia kuongezeka kwa bei za bidhaa. Hata hivyo, baada ya kipindi
cha msukosuko na hali ya kukadiria, uchumi uliimarika kwa kiasi kikubwa katika mwaka
wa 2010 ambapo shughuli za biasharanje na uwekezaji zilirejea kwa ukamilifu. Kufikia
mwishoni mwa mwaka wa 2010, uchumi uliimarika kwa kiwango kikubwa cha asilimia 7.3
sawa na uchumi unaoibuka wa mataifa mengine kwa kipindi hicho. Ukuaji halisi wa Jumla
ya Pato la Taifa katika robo ya tatu ya mwaka wa 2012 ulididimia kidogo hadi asilimia 4.7
na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.7 katika mwaka 2013.
…japo haujakuwa thabiti kutokana na msingi hafifu wa ukuaji na pia ruwaza
legevu ya uwekezaji…
Kwa miongo mitatu iliyopita, ukuaji wa uchumi wa Kenya haujakua kiusawasawa na kwa
miaka 30, kulikuwa tu na kipindi kimoja (ikiwa ni pamoja na kipindi cha hivi majuzi cha
ukuaji) ambapo ukuaji wa uchumi ulikuwa zaidi ya asilimia 5. Ni kweli kuwa Jumla ya
Pato la Taifa la kila mwaka limekuwa asilimia 2 au hata chini ya hii kwa takriban thuluthi
tatu ya kipindi hiki cha miaka 30 na ni la kiwango cha chini sana ikilinganishwa na asilimia
wastani ya mataifa ambayo hayajaendelea sana. Sababu mojawapo inayochangia hali hii
inatokana na kasi ya chini ya mabadiliko yanayolenga mfumo wa uchumi unaotegemea
viwanda.
Ukubwa wa sekta ya viwanda- ikiwa ni pamoja na shughuli za uzalishaji na zisizotegemea
uzalishaji umesalia vivyo hivyo kwa miongo miwili sasa. Utegemeaji wa kilimo –
ambacho ni asilimia 25 ya Jumla ya Pato la Taifa -umeweka uchumi katika hali ya hatari
hasa kutokana na kuongezeka kwa bei ya pembejeo kama vile mafuta na hata hali mbaya
ya anga. Hali hii ni mbaya zaidi kutokana na kwamba majani chai na kahawa pekee
huchangia asilimia 20 ya mapato ya biasharanje.
Kasi ya mabadiliko imeathiriwa pakubwa na kushuka kwa kiwango cha akiba na kukwama
kwa uwekezaji. La mno kabisa ni kuwa, Kenya ilishuhudia udidimiaji mkubwa sana katika
kiwango cha akiba ya jumla ya nchi miongoni mwa mataifa ya ulimwengu yanaoendelea.
Huku mengi ya mataifa ibuka, yale yanayokuwa na yale ambayo hayajaendelea sana
yakiweza kuimarisha kiwango cha akiba yao na kupunguza utegemezi wa ufadhili wa
kutoka nje usiojulikana kama vile ule wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni na ule wa
mikopo ya kigeni. Akiba ya Jumla ya Pato la Taifa la Kenya ilididimia kutoka asilimia 18.6
katika mwaka wa 1990 hadi asilimia 8.9 katika mwaka wa 2010. Kutokana na hali hii,
uundaji wa mtaji maalum wa kijumla haukupiga hatua kama za mataifa mengine
yanayoendelea. Uundaji wa mtaji maalum wa kijumla umekwama kwa asilimia 20 ya Jumla
ya Pato la Taifa kwa mwongo uliopita.
…ambayo imeathiri pakubwa uundaji wa nafasi za kazi rasmi na kuzuia uboreshaji
wa hali ya maisha…
Ukuaji wa kiwango cha chini wa kiuchumi umedhihirisha kuwa uboreshaji wa soko la kazi
umekuwa wa kasi ya chini mno. Kati ya mwaka wa 1991 na 2003, kiwango cha ajira
nchini Kenya kilipunguka kwa zaidi ya asilimia 7 kutoka asilimia 67 hadi asilimia 59.7 na
hata katika kipindi cha hivi karibuni cha ukuaji imara na endelezi, ukuaji wa ajira ulienda
sambamba na idadi ya watu wanaofanya kazi. Kwa sababu hiyo, kiwango cha ajira mwaka
wa 2012 - kilichokuwa zaidi ya asilimia 60 – kilisalia katika kiwango cha chini
kikilinganishwa na hali iliyoafikiwa katika miaka ya 1990 na ambayo ni ya chini zaidi ya
wastani ya mataifa ya Afrika, Kusini mwa Sahara (asilimia ya 65.1).
Zaidi ya yote, nafasi nyingi za kazi zimekuwa katika biashara za sekta ya juakali. Katika
mwongo uliopita tu, ajira za sekta ya juakali zisizokuwa za kilimo ziliimarika kwa hadi
takribani ajira milioni 5.1 au asilimia 7.2 kwa mwaka- hiki kikiwa kiwango cha juu zaidi
kuliko kile cha ajira ya mishahara. Kwa sababu hiyo, ajira katika sekta za juakali
zilichangia asilimia 64 ya jumla ya kazi za mwaka wa 2011 – na asilimia 85 wakati ambapo
wakulima waliojiajiri na wanaofanya kazi ndogo ndogo za ukulima wakiwa
wamejumuishwa. Jambo la muhimu ni kuwa, uzalishaji viwandani ulichukua nafasi ya pili
katika kuchangia sana ukuaji wa nafasi za ajira katika sekta ya juakali. Zaidi ya yote,
kiwango kikubwa cha ajira rasmi katika kipindi hiki zilikuwa za kibarua tu: kati ya mwaka
wa 2003 na mwaka wa 2011, nafasi za kawaida za ajira zilikua kwa asilimia 7
ikilinganishwa na asilimia 87 ya ukuaji wa ajira za vibarua.
Kwa sababu hiyo, kumekuwa na mabadiliko madogo na hakuna tofauti katika hali ya
maisha ikiwekwa kwenye mizani ya Jumla ya Pato la Taifa kwa kila mwananchi. Kwa
kweli, mapato ya wastani wa jumla kwa kila mwananchi nchini Kenya yamekuwa asilimia
0.32 kwa wastani kwa mwaka katika miaka 30 iliyopita huku mapato ya wastani wa jumla
kwa kila mwananchi katika nchi ambazo hazijaendelea sana yakiimarika kwa asilimia 1.5
kwa mwaka. Maendeleo ya kadiri katika hali ya maisha yameathiriwa na mwelekeo wa
kuongezeka kwa wafanyikazi katika sekta ya juakali ambao aghalabu hupata mshahara wa
chini sana kwa mwezi ukilinganishwa na kiwango cha umaskini kilichowekwa kimataifa na
kitaifa. Mshahara huo ni kama asilimia ishirini ya ule ambao wafanyikazi wa umma katika
sekta rasmi wanapata (na ulio chini ya nusu ya ule wa wafanyikazi wa sekta za kibinafsi).
…hasa miongoni mwa vijana wa taifa la Kenya...
Vijana hasa wameathiriwa na hali ya kutokuwa na njia thabiti za kuweka misingi ya
kuzalisha nafasi za kazi, huku watu wazima wakifaidi kutokana na ugavi usiokuwa wa
kiusawasawa wa nafasi za kazi zilizozalishwa. Hususan, katika mwaka wa 2012, vijana
wenye umri wa miaka 15 hadi 24 walikuwa chini ya asilimia 19 ya nafasi zote za ajira ilhali
wao ni zaidi ya asilimia 35 ya watu wenye umri wa kufanya kazi. Kwa hivyo sasa, kiwango
cha nafasi za ajira kwa vijana kikiwa asilimia 32.8, ni chini ya nusu ya nafasi ya kiwango
cha watu wazima walioajiriwa. Kiwango hiki ni mojawapo ya viwango vya chini zaidi
katika eneo hili. Vijana wengi wamevunjika moyo na sasa wameanza kuacha soko la kazi
kabisa. Katika mwaka wa 2012, kiwango cha kukaa bila kazi cha watu wenye umri wa kati
ya miaka 15 na 24 nchini Kenya kilifikia asilimia 60.5 – ambapo kilipanda kwa pointi
asilimia 5 tangu mwaka wa 2000 pekee. Tatizo hili ni sugu sana miongoni mwa vijana wa
kike ambao kiwango chao cha kukaa bila kazi ni pointi asilimia 8 zaidi ya vijana wa kiume.
Hata hivyo, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika kiwango cha wanaojua kusoma
na kuandika na kupata masomo ya shule ya msingi kwa jinsia zote. Katika mwaka wa
2009, asilimia 13 pekee ya wakenya wenye umri wa miaka 15 na zaidi hawakujua kusoma
na kuandika. Kiwango hiki ni cha chini kwa pointi asilimia 13 kikilinganishwa na cha
mwaka wa 2000 na chini ya pointi asilimia 24 kikilinganishwa na mataifa ya Afrika, Kusini
mwa Sahara kwa ujumla. Hata hivyo, mabadiliko haya hayajabainika sana katika masomo
ya vyuo ambapo kiwango cha wanafunzi wanaojiunga ni cha chini mno kikilinganishwa
na viwango vya kimataifa. Kwa kweli, katika mwaka 2009, ni asilimia 4 tu ya wakenya
walijiunga na elimu ya vyuo vikuu – ongezeko la pointi asilimia1.3 tangu mwaka 2000.
Ni muhimu kutambua kwamba, kiwango cha juu cha watu wasiofanya kazi kinaweza
kukwamiza ukuaji wa kiuchumi wa baadaye kutokana na kuzorota kwa ujuzi na uzalishaji
na pia upungufu wa utendakazi, hasa kwa kuzingatia idadi kubwa ya wasomi nchini
Kenya. Hali ya kutojihusisha na soko la kazi pia inaweza kuwa na madhara makubwa ya
kijamii na inalingana na kutoridhishwa, jambo ambalo linaweza kuleta mvutano wa kijamii
– kama ilivyodhihirika kupitia machafuko ya hivi karibuni ya Kaskazini mwa Afrika na
kwingineko. Kwa kweli, nchini Kenya, vijana wamepoteza matumaini ya kupata nafasi za
ajira na hasa nafasi yao katika jamii kwa jumla. Katika mwaka wa 2011, ni asilimia 15.8 tu
ya idadi ya watu wenye umri wa miaka kati ya 15 na 34 nchini Kenya walioamini kuwa hali
ya uchumi katika maeneo yao ya makaazi ilikuwa inaimarika na ni robo moja tu ndio
walikuwa na imani kwamba ulikuwa wakati mwafaka wa kutafuta kazi. Idadi hii ni
miongoni mwa idadi za chini sana katika bara la Afrika.
…licha ya juhudi kubwa za serikali za kuimarisha soko la kazi.
Katika ngazi ya kitaifa, mipango miwili ya maendeleo iliundwa mwongo mmoja uliopita –
Mkakati wa Kufufua Uchumi kwa Ajili ya Utajiri na Uzalishaji wa Nafasi za Ajira kwa
kipindi cha kati ya mwaka wa 2003 hadi 2007 na ule wa Rajua ya mwaka wa 2030 kwa kati
ya mwaka wa 2008 hadi 2030 (ambao uliupiku ule wa Mkakati wa Kufufua Uchumi kwa
Ajili ya Utajiri na Uzalishaji wa Nafasi za Ajira). Rajua ya mwaka wa 2030 ni mpango wa
muda mrefu wa maendeleo unaolenga kuboresha hali ya maisha ya watu nchini Kenya.
Inajumuisha zaidi ya miradi 120 itakayotekelezwa kwa mipango ya muda wa awamu ya
miaka mitano huku awamu ya kwanza ikikamilika mwaka wa 2012. Kuhusiana na ajira
kama ilivyoratibiwa katika Rajua ya mwaka wa 2030, jumla ya nafasi za kazi zinatarajiwa
kukua kama matokeo ya juhudi za kuimarisha ukuaji wa kiuchumi hivyo basi ndio maana
ya kutokuwepo na juhudi za kipekee au mikakati ya kuzalisha nafasi za kazi.
Rajua hii, hata hivyo, inaonyesha umuhimu wa kuwezesha vijana kupata ujuzi wa hali ya
juu na ustawi. Mipango kwa vijana imependekezwa katika sehemu mbalimbali ikiwemo
kuboresha maarifa ya utendakazi pamoja na kutambua vizuizi katika nafasi ya ajira kwa
vijana. Hii inachangia msururu wa miradi ya serikali, taasisi na mifumo ya sera ambayo
imetekelezwa hivi karibuni kukabiliana na changamoto zinazowakumba vijana, kama vile:
(i) Katika mwaka wa 2005, wizara mpya ya Maswala ya Vijana na Michezo ilibuniwa; (ii)
Katika mwaka wa 2007, serikali ilibuni Sera ya Kitaifa kuhusu Vijana - mifumo ya kisheria
ambayo ililenga kuhakikisha kuwa vijana wanajumuishwa katika maendeleo ya taifa, (iii)
Katika mwaka 2008, Wizara ya Maswala ya Vijana na Michezo ilizindua Mpango wa
Kuwatafutia Vijana Ajira(Youth Employment Marshall Plan) ikiwa na malengo ya
kukabiliana na tatizo la muda mrefu la ajira kwa vijana na (iv) Katika mwaka wa 2010,
Mradi wa Kuwezesha Vijana wa Kenya (Kenya Youth Empowerment Program)
ulibuniwa na serikali ya Kenya kwa ushirikiano na Benki ya Dunia. Mradi huu
ulishughulikia baadhi ya masuala yaliyokuwa yakizingatiwa na mpango wa kutafuta ajira
na pia ukajumuisha shughuli nyingi kama vile utoaji mafunzo na uendelezaji wa sera.
Hata hivyo, miradi ya sera na mikakati ya ukuaji ya hivi karibuni haijafanikiwa ili kuweza
kujumuisha sera za kazi kama sehemu kubwa ya kuimarisha muundo wa sera za mawanda
pana ya kiuchumi. Kwa kweli, kukua kwa Jumla ya Pato la Taifa nchini Kenya
hakujaonyesha kuimarika kwa hali ya soko la kazi hususan kwa vijana. Kwa sasa, mipango
mingi kwa vijana imekosa malengo maalum na vigezo mwafaka vya kupima utendakazi
na hivyo basi si wazi kama kweli mipango hii ni bora na ni kwa kiwango gani inalenga –
au kufaulu katika kukabiliana na changamoto zinazowakumba vijana. Kwa hivyo, ili
kuweza kufaidika na kiwango kikubwa cha ukuaji wa kiuchumi unaotarajiwa, lazima kuwe
na uwiano mkubwa baina ya ukuaji, ajira na usawa. Tunapoendelea, serikali inahitajika
kuangazia mambo matatu muhimu: (i) kuimarisha ukuaji thabiti wa uchumi na faida za
uzalishaji; (ii) kutia bidii katika kuzalisha nafasi za kazi rasmi na (iii) kuhakikisha kuwa
kuna ugavi sawa wa faida zitokanazo na ukuaji hasa za kuhusiana na ajira ya vijana.
Tukiendelea mbele, kutokana na tajriba ya kimataifa, msaada utatolewa kwa
kuzingatia mifumo ya mawanda mapana ya kiuchumi inayolenga ajira...
Kenya itahitaji kiwango cha ukuaji wa kiuchumi kwa mwaka cha asilimia 5 ambacho
ndicho kinalengwa kuwa cha mwaka 2013 ili kuweza kuchukua idadi kubwa ya watu
wenye umri wa kufanya kazi; na ya karibu asilimia 10 ili kuhakikisha faida ya ajira hasa
kwa vijana. Hivyo basi, mkakati thabiti wa mawanda mapana ya kiuchumi ambao
unakabiliana na hali mbaya iliyopo sasa utakuwa muhimu sana kuwezesha Kenya kuafikia
kiwango cha ukuaji ambacho kitapelekea kuzalisha nafasi za kutosha za ajira. Ingawa
kumekuwa na maendeleo katika nyanja fulani, maendeleo zaidi yatategemea nyanja
nyinginezo.
• Kuhakikisha kwamba kuna mazingira mwafaka ya uwekezaji: Ingawa sera za mawanda
mapana ya kiuchumi za kupunguza gharama ya kukopa na kuongeza uwezekano
wa kupata mikopo ni muhimu, sera hizi pekee hazitoshi kuhakikisha kuwa
mazingira mwafaka ya uwezekaji yameafikiwa.. Sera nyinginezo na bora za
mawanda mapana ya kiuchumi zinaweza kufikiriwa. Hii itapelekea kuwepo kwa
mazingira bora ya uwekezaji ambayo yanahitaji kuimarishwa na sera faafu za sekta.
Kwa mfano;
o Kuboresha kiwango cha kuweka akiba: Serikali inaweza kufikiria mbinu mpya
na bora ili kupunguza matumizi ya kinyumbani na kuhimiza uwekaji wa
akiba nchini kwa mfano kwa kutoa ishara ya mfumko wa bei na pia ile
bondi inayohusiana na Jumla ya Pato la Taifa. Bondi za ishara ya mfumko
wa bei huenda zikawashawishi watu kuweka akiba zaidi huku bondi
inayohusiana na Jumla ya Pato la Taifa ikisaidia taifa kulipa kiwango cha
deni ambacho kinaoana na kiwango cha ukuaji wa Jumla ya Pato la Taifa.
Mataifa mengi kama vile Ajentina, Meksiko, Nijeria na Jamhuri ya Bolivia
ya Venezuela yalitoa rasimu tofauti za bondi zinazohusishwa na Jumla ya
Pato la Taifa kwa miongo mitatu iliyopita hali ambayo ilisaidia sana katika
kupunguza gharama ya kukopa na ikaimarisha uwezo wa kupata mitaji
nchini na kimataifa. Utoaji wa bondi zinazohusishwa na Pato la Jumla la
Taifa inaweza hususan kusaidia katika kuhakikisha kuwa matumizi muhimu
yanayohitajika katika sekta za kijamii kama vile za afya, elimu na ile ya
usalama wa kijamii hazipati pigo pindi kunapotokea matatizo ya kiuchumi.
o Ukopeshaji kwa sekta muhimu: Wafadhili wanaweza kutumia hitaji la kuwa na
akiba ya rasilimali ili kuzifanya benki kutoa mkopo kwa sekta muhimu za
uchumi. Mbinu hii itawezesha benki kurekebisha viwango vya hifadhi zao
za fedha kulingana na sekta wanazohitaji kukopesha. Kwa mfano, Reserve
Bank of India imeanzisha mpango wa kutoa Mkopo kwa Sekta Muhimu
(Priority Sector Lending) ili kulenga sekta ambazo ziko tayari kutoa nafasi
zaidi za ajira rasmi kwa muda mfupi na ule wa kadiri. Zaidi ya yote, benki
za kibiashara zinaweza kupewa jukumu la kukidhi malengo maalum ya
kutoa mkopo kwa sekta muhimu na kunaweza kuwepo na adhabu kali
ikiwemo kupoteza akiba ya ziada na hata utoaji huduma ya mikopo ya
kulipiwa kwa mishahara ikiwa benki haitaafikia malengo muhimu ya
ukopeshaji kwa sekta muhimu.
• Mikakati ya kuboresha uzalishaji: Kenya inahitaji kuweka mikakati mwafaka ili
kusisimua utendakazi na uzalishaji kwa jumla ili kuhakikisha kuwa uchumi na
wafanyikazi wake umesalia kuwa wenye ushindani mkubwa ulimwenguni. Hii
inaweza kuafikiwa kutokana na kuondoa motisha ya ushuru kwa biashara zilizo na
mbinu bora za kutoa maarifa na zenye kuendeleza uzalishaji katika uwekezaji wao.
Serikali pia inaweza kuanzisha “Hazina ya Uzalishaji” ambayo itatoa misaada na
hata mikopo kwa mashirika ili kuwekeza katika utoaji wa mafunzo kwa wafanyi
kazi wao na kuboresha kiwango chao cha uzalishaji. Zaidi ya yote, sehemu kubwa
ya sera ya kiviwanda ambayo inalenga kupunguza kuwepo kwa idadi kubwa ya
wafanyikazi wa maarifa fulani na kuendeleza sekta ambazo zinazalisha kwa
kiwango kikubwa inaweza kuwa mkakati wa jumla wa kuendeleza uzalishaji. Sera
hizi zitahitaji kuhakikisha mfungamano na utaratibu uliowekwa kuonyesha
mfumko na sera za kiwango cha ubadilishanaji wa sarafu kwa upande mmoja na
sera za ajira na elimu kwa upande mwingine. Kwa sababu hii, ni muhimu
kutambua kuwa maendeleo katika uzalishaji wa ajira kwa kawaida hayapunguzi
mahitaji ya kazi. Kwa hakika, tajriba ya uchumi wa mataifa ya Asia Mashariki
unaonyesha kuwa nafasi ya ajira na ukuaji wa uzalishaji wa kazi haufai kuwa
mchezo wa patapotea.
• Kufanya biasharanje kuwa anuwai: Kupanua aina za bidhaa za biasharanje
kunakoandama pamoja na kutunga sera za kiviwanda kutaifanya Kenya kudhibiti
mapato ya nje, kupunguza hatari ya kuanguka kwa bei za bidhaa na kupunguza
madhara yanayotokana na kuanguka ghafla kwa uzalishaji wa bidhaa za kilimo
kutokana na hali mbaya ya hewa. Sera hii, mwanzo kabisa, itapelekea ukuaji thabiti
wa kiuchumi hali ambayo itaongeza nafasi za ajira. Zaidi ya yote, uzalishaji anuwai
na bidhaa za biasharanje utakuwa na uwezo wa kuboresha ajira hasa katika sekta
zenye kuleta faida. Ili kuafikia hili, ukopeshaji kwa sekta muhimu (kama
ilivyoelezwa hapo juu) unaweza kuwa suluhu. Hata hivyo, sera ya kiviwanda
inayolenga mbele itakuwa muhimu katika kuhakikisha kuwa taasisi za elimu
zinatoa elimu, mafunzo maarifa mwafaka ili kufanikisha sekta za biasharanje zenye
uwezo.
Ingawa mfumo thabiti wa mawanda mapana ya kiuchumi na kuimarika kwa ukuaji wa
uchumi ni muhimu, bado hautoshelezi. Kwa kweli, mwelekeo wa ukuaji wa uchumi wa
sasa hautaweza kuleta mabadiliko katika sekta ya ajira. Kwa hivyo, kunahitajika juhudi za
kipekee ili kukabiliana na changamoto za suala la ajira linalokumba Kenya hasa kwa
kuzingatia mwelekeo wa kuongezeka kwa kutoajiriwa kirasmina vilevile ongezeko la
ukosefu wa ajira na hali ya kutoridhika miongoni mwa vijana.
… pili, ili kuchangia urasimishaji wa miradi ya sekta rasmi na kuboresha
mazingira ya wafanyikazi katika sekta ya jua kali...
Juhudi za kubadili ongezeko la sekta za nafasi za kazi za juakali na kuendeleza
urasimishaji wa kampuni utapelekea maendeleo katika ukuaji wa nafasi za ajira na kutia
nguvu juhudi za uzalishaji na uwekezaji. Kusisimua uzalishaji wa nafasi za ajira rasmi
kutasaidia kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kupunguza hali ya uchumi
kuyumbayumba. Ili kuafikia hili, tunaweza kuzifikiria mbinu zifuatazo:
• Kuimarisha maendeleo ya sekta za kibinafsi na urasimishaji wa biashara za sekta ya juakali
na kazi: Mojawapo ya vikwazo vya uzalishaji wa nafasi za kazi rasmi ni kuwepo
kwa vizuizi vya kujiunga na uchumi rasmi. Hii inajumuisha mifumo ya sheria na
kanuni zinazomuumiza mfanyibiashara katika shughuli zake, sera dhalimu katika
utozaji ushuru na taratibu za kuchosha za kusajilisha biashara. Japo Kenya imepiga
hatua katika siku za hivi karibuni, bado kampuni za Kenya zinahitaji kukabiliana
na asasi za serikali kuu pamoja na za serikali za mashinani ili kupata leseni ya
biashara. Hii hulifanya zoezi hili kuwa refu (data za hivi karibuni zinaonyesha
kuwa huchukua siku 32 kuanzisha biashara hapa Kenya) na la gharama kubwa.
Ingawa hatua thabiti zimechukuliwa katika miaka ya hivi karibuni katika uwanja
huu, juhudi za ziada zinahitajika katika kupunguza vikwazo vya kufanya biashara
na vile vya ushuru (hasa kwa biashara ndogondogo) ili kuwapa moyo wajasiriamali
kurasimisha biashara zao. Kwa kuongezea, hali ya kutokuwa na haki za umiliki
thabiti ni kikwazo kingine kinachozuia urasimishaji wa biashara. Mifano kutoka
mataifa mengine katika mambo haya yaweza kuwa muhimu:
o Brazili imechangia urasimishaji kwa kuwapa mikopo wenye biashara
ndogondogo, vyama vya ushirika, miradi yenye juhudi za uzalishaji katika
sekta rasmi. Brazili pia imepunguza hatua zinazohitajika katika kurasimisha
biashara kutoka hatua 41 hadi hatua 7 na pia kupunguza mzigo wa ushuru
kwa wenye biashara ndogondogo zilizoajiri mtu mmoja. Pia serikali ya
Tanzania imechukua hatua za kupunguza vizuizi vya kurasimisha biashara
kupitia njia tatu za kuboresha usajili wa biashara, kanuni za biashara (kama
vile utoaji leseni) na utengenezaji wa mapato ya serikali (kama vile utozaji
ushuru, ukusanyaji wa kodi n.k).
o Peru imechukua hatua mwafaka ya kukabiliana na hali ya ukosefu wa haki
za umiliki wa mali kwa kubuni Mfumo wa Usajili wa Praedial ambao
uliwapa familia zaidi ya milioni 1.2 hati miliki na ikasaidia zaidi ya biashara
380,000 kujiunga na uchumi rasmi.
o Mataifa kama vile Urugwai na Liberia yamepunguza sana muda wa
kuanzisha biashara kwa kuanzisha mfumo wa ‘one stop shop’ ambao
unaleta shughuli zote za vyeti, habari na fomu zinazohitajika kuanzisha
biashara mahali pamoja panapoweza kufikika wa urahisi. Shughuli kama
hizi pia zinaweza kuchangia ujasiriamali wa vijana (Tazama hapo chini).
o China imeimarisha maendeleo ya kuondoa shughuli za uzalishaji wa
mashinani zisizokuwa za kilimo ili kuweka mwingiliano thabiti baina ya
sekta ya kilimo na uchumi, huku ikizalisha nafasi ya ajira rasmi. Kwa kweli,
ukuaji mkubwa wa sekta ya shughuli zisizo za kilimo mashinani
umechangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa hina huku ikiimarisha
pato la kaya za mashambani na hivyo kuchangia maendeleo ya mashinani.
• Kubuni mikakati ya usalama wa kijamii kama chombo cha kuboresha hali ya utendakazi wa
wafanyikazi wa sekta za juakali: Wafanyakazi wengi wa sekta ya juakali hapa Kenya
hukosa huduma za kimsingi za usalama wa kijamii huku wakiwa katika hali hatari
bila kinga yoyote ya afya ya kikazi pamoja na hatari za kiusalama na kukosa kinga
katika maswala ya kukosa ajira, ajali, ugonjwa au hata uzee. Huduma nzuri za
kijamii zinaweza kuimarisha hali ya afya ya mtu pamoja na ile ya wafanyikazi wa
sekta za juakali na kuimarisha uwezo wao wa kujipanga na kudai mazingira bora ya
kikazi. Baadhi ya mifano ni pamoja na mpango wa UMASIDA huko Tanzania.
Huu ni mfumo wa kijamii wa bima ambao unalenga kupunguza matatizo ya
wafanyikazi wa sekta za juakali kupata matibabu. Pia, kuna Chama cha Muungano
wa Wanawake Waliojiajiri ambacho kilibuniwa kukabiliana na matatizo ya
wanawake wa Kihindi. Wanawake hao ambao hufanya kazi zisizo rasmi
walichukua jukumu la kuhakikisha kuwa wanapata matibabu, usalama wa mapato
na kujiimarisha. Kijumla, watengenezaji wa sera wanafaa kutilia maanani kuwa
matumizi katika shughuli hizi za kijamii ni jambo la uwekezaji wa muda mrefu na
wala si chombo cha kukabiliana na majanga tu.
...na tatu, kubuni mkakati wa ajira ya kitaifa kwa lengo haswa la kuzalisha nafasi
za ajira kwa vijana.
Serikali ya Kenya imepiga hatua katika kukabiliana na changamoto za ajira kupitia
mipango maalum, sera na asasi ya soko la kazi. Hata hivyo, mkakati wa pamoja wa kitaifa
wa ajira ambapo sera za ajira hujumuishwa katika mikakati ya maendeleo na mipango ya
ukuaji huenda ikaleta mchango zaidi. Kwa kweli, kuna utambuzi mpya kuhusu umuhimu
wa ajira kama jambo la msingi katika ukuaji wa uchumi na ufanisi. Kiungo muhimu cha
mkakati huu kitakuwa ni kuwahusisha vijana katika utaratibu wa kufanya maamuzi.
Mataifa mengi yameweka mikakati ya kitaifa ya ajira ikiwemo juhudi zinazolenga miaka
mingi ya utekelezi kama vile ‘Action Plan for Jobs’ iliyotekelezwa huko Ireland na
ambayo inatunga sera nzuri za ajira ambazo ni hatua ya kuimarisha sekta hii. Wenye
kubuni sera nchini Kenya wanaweza kujifunza kutokana na ubora na udhaifu wa juhudi
hizi katika kutayarisha mikakati yao ya maendeleo. Hii haitasaidia tu kuboresha
utayarishaji wa yale yaliyomo na vielelezo katika miradi ya vijana bali pia itasaidia
kutayarisha mchakato jumlishi ambao utawaona vijana kuwa muhimu katika kuleta suluhu
kinyume na kuwaona kuwa vyanzo vya matatizo. Juhudi za aina mbalimbali zinaweza
kuwa mojawapo ya mikakati hiyo kama vile:
• Kubadilisha mipango iliyopo sasa ili iweze kuafikia changamoto za ajira kwa vijana: Ingawa
juhudi za hadi sasa za kukabiliana na hali ya ukosefu wa ajira kwa vijana
zinasherehekewa, bado zimesalia kuwa za kijumla katika utekelezaji wake. Hii ina
maana kuwa, zinawalenga vijana kwa jumla lakini zinakosa kutambua vijana walio
na uhitaji zaidi na kukabiliana na changamoto maalum za vijana nchini Kenya
kama vile; (i) Ukosefu wa nafasi za kazi kwa vijana na (ii) uwezo wao wa chini wa
kupata nafasi hizo za kazi zilizo chache. Sera na miradi inayolenga changamoto
maalum – kama vile kuwa na ujuzi ufaao – zinafaa zaidi kuliko kulenga tu kiwango
fulani cha umri. Ili kuimarisha umuhimu wa mipango iliyopo sasa kwa vijana,
masuala yafuatayo yanahitaji kushughulikiwa:
o Kuanzisha ujuzi na soko la kazi, kuwezesha mabadiliko ya kutoka shule na kuingia
katika ajira inayojumuisha vipengele vya ujuzi wa mahusian: Kuna mawazo
yanayofanana miongoni mwa washikadau mbalimbali hapa Kenya kuwa
mojawapo ya sababu za kuwa na kiwango kikubwa cha vijana wasio na ajira
ni kutowiana kwa ujuzi wao na ule unaohitajika katika soko la kazi. Ripoti
hii inatilia mkazo umuhimu wa sera za elimu za utoaji mafunzo lakini
muhimu zaidi zinapochukuliwa kwa ajili ya mahitaji ya ajira. Kwa mfano,
Jamhuri ya Korea na Singapore hazikuzingatia tu suala la elimu bora
(ikiwemo ya shule za upili na vyuo) bali pia ujuzi wa kiufundi ulio bora,
mambo ambayo waliamini yalikuwa mihimili katika kuboresha utendakazi
na ushindani. Mataifa haya mawili yalianzisha malipo ya mafunzo ili
kuwashawishi wajasiriamali kushiriki katika kuwapa wafanyikazi wao
mafunzo. Zaidi ya yote kuoanisha elimu na mafunzo kungeweza
kuimarishwa na sera ambazo zinawasaidia vijana kupata tajriba ya kazi ili
kuwawezesha kujumuishwa katika ajira kwa muda mrefu. Miradi ya Joven
huko Chile na Juventud y Empleo huko Jamhuri ya Dominika ililenga sio
tu kutoa ujuzi wa kitaaluma kwa vijana bali pia ujuzi wa kukabiliana na
maisha katika soko la ajira.
o Kuhakikisha usawa katika kushiriki kwenye mipango hasa kwa wanawake na vijana
wa mashinani: Ili kuhakikisha usawa katika kushiriki kwenye mipango na
kuzuia ubaguzi, Mradi wa Kuimarisha Watoto na Vijana (Programme for
the Promotion of Children and Youth) ulitekelezwa nchini Uganda kati ya
mwaka wa 2003 na 2006. Mpango huu ulitekelezwa kwa ushirikiano wa
serikali ya Uganda na Ujerumani na ulikuwa na mbinu ya kuendeleza
matakwa ya wale vijana wasiojiweza wanaoishi mashinani, ambao walikuwa
wakiteseka kutokana na aidha ukosefu wa ajira au kuwepo kwa nafasi
chache za ajira.
o Kuwasaidia wasiojiweza: Sera za zamani za ajira zinaweza kuwa zimepitwa na
wakati kwa nia ya kutaka kuwachochea vijana ambao wamekufa moyo na
ambao hawajakuwa na ajira kwa kipindi kirefu. Kwa mfano, nchini Misri
juhudi za kutaka kuwajumuisha tena vijana katika ajira na kwa ujumla katika
jamii, mradi uliofadhiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la
Umoja wa Mataifa (UNESCO) unatoa mafunzo ya kusoma na kuandika,
elimu ya kiufundi, mbinu za kukabiliana na maisha na vilevile mafunzo ya
tarakilishi na ujuzi wa lugha za kigeni.
• Kuboresha hali ya uchumi ili kuwezesha ajira: Kuimarisha ukuaji wa kiuchumi na
kuhakikisha uthabiti ni muhimu lakini hakutoshi katika kukabiliana na changamoto
za vijana. Huku kutahitaji juhudi zaidi ambazo zitabuniwa ili kuboresha hali ya
uchumi kuweza kuajiri na kuchochea mahitaji ya ajira kwa vijana. Kwa kweli,
katika juhudi za kuhakikisha ugavi sawa wa faida kutokana na ukuaji, mataifa
mengi yametilia mkazo shughuli za kutoa motisha kwa wajasiriamali ili kuwaajiri
vijana kama wafanyikazi wao huku wengine wakiendeleza ujasiriamali miongoni
mwa vijana. Baadhi ya juhudi hizi zimeainishwa hapa chini:
o Kulenga ruzuku na mbinu nyingine zitakazochangia kuajiriwa kwa vijana: Serikali
zinaweza kuchangia mahitaji ya vijana ya ajira kwa kutoa motisha kwa
wajasiriamali watakaowaajiri vijana kama wafanyikazi wa kupitia kwa malipo
ya ruzuku au kuondolewa ushuru. Mradi wa ajira wa The First
Employment Programme ulioanzishwa Brazili, Kolumbia, Paragwai na hivi
karibuni Meksiko na Mradi wa Mshahara wa Vijana kupitia Ruzuku
(Youth Wage Subsidy Programme) huko Uturuki ni mfano wa mipango
ambayo inayalipa makampuni ruzuku ili kuyafanya yawaajiri vijana wengi.
Ili miradi hii ifanikiwe ni muhimu ihakikishwe kuwa imelengwa kwa idadi
ya watu walioathiriwa kama vile kwa kutoa msaada wa mafunzo ya gharama
ya chini kwa wenye kampuni zinazowaajiri vijana ambao wanatarajia
kukamilisha masomo ya shule ya upili au kutoa malipo ya gharama ya chini
kwa vijana ambao hawajaajiriwa kwa muda. Hili ndilo lengo la mradi wa
‘First Employment Programme’ unaolenga vijana ambao hawana tajriba ya
ajira.
o Kuhimiza ujasiriamali miongoni mwa vijana: Mbinu nyingine ambayo inaweza
kusaidia katika kuongeza kiwango cha ajira miongoni mwa vijana ni ile ya
kuhimiza ujasiriamali miongoni mwa vijana. Miradi iliyofanikiwa ya
ujasiriamali haijumuishi tu msaada wa kuanzisha pekee bali pia maarifa ya
jinsi ya kukuza na kuimarisha shughuli za biashara. Kwa mfano, Mradi wa
Nafasi za Vijana wa Kaskazini mwa Uganda unawapa vijana wenye umri wa
kati ya miaka 16 na 35 pesa taslimu za kushughulikia mipango ya mafunzo
na vyombo vya kimsingi vinavyohitajika kuanzisha biashara.
o Kuhimiza uhusiano baina ya vijana na wazee: Ni muhimu kukumbuka kuwa
vijana na wazee si vibadala katika sekta ya ajira na kwamba kumkweza au
kumuumbua mmoja wao si hasara wala faida kwa mwingine. Mara kwa
mara inawaziwa kimakosa kuwa kustaafu mapema kwa wazee kutatoa
nafasi ya ajira kwa vijana – wazo ambalo limepelekea kuwepo kwa uhusiano
mbaya baina ya makundi haya mawili. Makundi yote mawili ya vijana na
wazee ni muhimu katika uzalishaji hasa katika sekta ya ajira. Zaidi ya yote,
kutokana na mwingiliano na wafanyikazi wenye tajriba kupitia ushauri,
wafanyikazi wachanga wanaweza kudumisha maadili katika sehemu zao za
kazi na kuchangia katika kuzitupilia mbali imani potovu za vijana. Juhudi
za hivi majuzi za serikali ya Kenya za kuzindua mpango wa ukufunzi
nyanjani ni wazo zuri lakini litahitaji kufuatiliwa kwa makini ili kuhakikisha
kuwa sera za vigezo na kanuni zilizotajwa zinahusishwa na kutiliwa
maanani.
• Mkakati wa utatu wenye mshikamano unahitajika ili kuinua vijalizo vilivyotajwa: Kushiriki
katika mazungumzo ya pamoja na washikadau wafaao hasa wakati wa kuzingatia
juhudi za sera kwa vijana ni muhimu kuhakikisha kuwa hatua hizo zinakabiliana na
mahitaji ya sekta ya ajira. Ni kweli kuwa mazungumzo ya pamoja na washikadau
husika yanaweza kusaidia katika kuleta uwiano wa habari kati ya serikali, waajiri na
vijana, kukabiliana na mahitaji maalum ya wafanyikazi na waajiri na pia kuanzisha
uhusiano wa kimikakati kwa lengo la kuafikia matokeo thabiti kwa muda mrefu.
Baadhi ya mifano ambayo Kenya inaweza kujifunza siku za baadaye imeainishwa
hapa chini:
o Kujenga ushirikiano na sekta za kibinafsi na mashirika ya kimataifa: Kukuza
ushirikiano na mashirika haya ni muhimu sana sio tu katika kufanikisha
kujumuishwa kwa mahitaji ya wabia katika sera za kitaifa ya ajira lakini pia
kuwaruhusu washirika wa kibinafsi kujumuishwa katika utayarishaji wa
bajeti na mipangilio ya mikakati ya ajira. Afrika Kusini, kwa mfano, iliasisi
ushuru wa kisheria mnamo Aprili mwaka wa 2000 ambao ulihitajika
kuwekezwa na waajiri kugharamia mafunzo na maendeleo kama mkakati wa
ujuzi wa serikali. Kwa upande mwingine, ushirikiano na mashirika ya
kimataifa unaweza pia kuchangia pakubwa. Mradi wa Shirika la Leba
Ulimwenguni wa Ajira kwa Vijana, (Youth Employment Programme)
huzingatia mtazamo jumlishi unaohusisha sera za mawanda mapana za
kiuchumi na malengo maalum ya kukabiliana na matakwa na ugavi pamoja
na kiwango na ubora wa ajira.
o Kuhimiza ushirikishi wa vijana katika mchakato mzima: Vijana wenyewe ni
washikadau muhimu katika mjadala, uundaji na utekelezaji wa sera na
miradi ya ajira kwa vijana. Vijana ni wafanyikazi wa siku za usoni na kwa
hivyo wana fursa nzuri na uwezekano kwa maendeleo yajayo ya taifa.
Mfano moja wa nchi iliyojizatiti kuwashirikisha vijana au makundi ya vijana
katika sera na mipango yake ya ajira kwa vijana ni Sri Lanka. Mpango
Tekelezi wa Kitaifa wa Ajira kwa Vijana wa Sri Lanka (The National Action
Plan for Youth Employment) ulihusisha vijana kote nchini katika mfumo
na uendelezaji wa mchakato wa mashauriano. Matokeo ya mashauriano
haya yalikuwa kwamba hoja muhimu ziliafikiwa, kama vile mapendekezo ya
marekebisho kumi na -tano ambayo yalitiliwa maanani katika kuchapisha
mswada wa mwisho wa Mpango Tekelezi wa Kitaifa.
o Kuboresha ufuatilizi na utathmini wa miradi: Uwezo wa waundaji sera wa
kuboresha ufaafu wa miradi iliyopo na ile mipya unategemea muundo bora
wa utathmini. Kijumla, hata hivyo, kuna machache zaidi yanayojulikana
kuhusiana na juhudi zilizopo sasa. Kwanza kabisa, ni muhimu kukusanya
na kuchunguza habari na matokeo ya kabla na baada ya mradi wowote.
Kwa kiasi kinachowezekana, habari ya kutosha inatakiwa kukusanywa:
gharama, hali ya ajira, malipo, habari za idadi ya watu, kiwango cha elimu
n.k. Pili, ni muhimu kuwafuatilia washiriki kwa muda mrefu. Kwa kuwa
katika hali nyingi, mafanikio ya miradi, hasa katika kuwapa vijana mafunzo,
hukua kwa kipindi fulani cha muda. Kufuatilia washiriki na matokeo hata
baada ya mradi kukamilika kwa mfano baada ya miaka 3-5 kunafaa kuwa
sehemu ya mkakati wa ufuatilizi na utathmini. Kwa kuhitimisha, serikali
inafaa kuanzisha, tokea mwanzo, malengo yaliyo wazi na yenye kupimika
kwa mujibu wa matokeo yanayotarajiwa katika kipindi kifupi au kirefu.
Kazi hii si nyepesi lakini inawezekana muradi malengo ya ajira yajumuishwe
katika mkakati wa sasa wa mpango wa maendeleo.
Uchaguzi uliofanyika mwanzoni mwa mwezi Machi 2013 ulitoa mwanya wa nafasi ya
kutekeleza mabadiliko yaliyopendekezwa Kenya kujumuisha ajira katika shughuli nzima
ya ukuaji na maendeleo. Hususan, awamu ya kwanza ya mpango wa muda wa miaka tano
(Medium-Term Plan) wa Rajua ya Mwaka wa 2030 ulikamilika mwaka wa 2012 na awamu
ya pili ya utaratibu huu inaanza mwaka wa 2013 hadi 2017. Awamu hii itatoa nafasi bora
zaidi katika kuingiza sera za sekta ya ajira katika mipango ya maendeleo.
Serikali mpya, hata hivyo, itahitajika kushirikiana na waajiriwa na waajiri. Kwa kweli,
mazungumzo faafu ya pamoja yanaweza kutoa mwelekeo bora zaidi wa mabadiliko na
kuleta sera zenye usawa na uthabiti za kutekelezwa. Kwa sababu hii, Shirika la Leba
ulimwenguni (ILO) kupitia ujuzi wake wa kitafiti na kitaaluma na ambao unawezesha
mazungumzo yanayohusu pande hizi tatu lina jukumu muhimu la kutekeleza pamoja na
serikali na washikadau wengine wa kijamii ili kuhakikisha kuwa kuna ukuaji na usawa.