22
WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI TAARIFA YA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA KIPINDI CHA MIAKA MINNE KATI YA DESEMBA 2005 HADI DESEMBA 2009: DESEMBA, 2009

WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI · 2014-11-12 · wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya wizara kwa kipindi

  • Upload
    others

  • View
    34

  • Download
    0

Embed Size (px)

Citation preview

WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA

MAENDELEO YA MAKAZI

TAARIFA YA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA KIPINDI CHA MIAKA MINNE KATI YA DESEMBA 2005 HADI

DESEMBA 2009:

DESEMBA, 2009

1

TAARIFA YA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA KIPINDI CHA MIAKA MINNE KATI YA

DESEMBA 2005 HADI DESEMBA 2009 1.0 UTANGULIZI

1.1 Dira/Mwelekeo (Vision) Kuwa mlezi na msimamizi wa uhakika wa Hakimiliki ya ardhi, nyumba bora zenye hadhi na makazi endelevu kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 1.2 Dhima Kuweka mazingira yanayofaa na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za ardhi, nyumba na makazi kwa ajili ya maendeleo ya wateja kijamii na kiuchumi. 1.3 Misingi ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara Wizara iliendelea kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025, Malengo ya Milenia (MDGs), Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA) na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005. Mambo ya Msingi yalioanishwa katika miongozo hiyo yanalenga kuboresha maisha ya wananchi; kudumisha amani, utulivu na umoja; kudumisha utawala bora; kujenga uchumi madhubuti na endelevu; kuboresha afya; mazingira na kuwa na makazi endelevu.

1.4 Majukumu ya Wizara

Wizara katika kipindi hiki iliendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuelekeza nguvu katika maeneo ambayo yanamnufaisha mwananchi ikiwemo kubadilisha ardhi kutoka hali ya Mtaji Mfu na kuwa Mtaji Hai ili iweze kuwasaidia wananchi waondokane na umaskini. Majukumu yanayotekelezwa na Wizara ni yafuatayo: -

• Kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ardhi (1995), Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi (2000) pamoja na

2

Sheria zote zinazohusu Maendeleo ya Ardhi, Mipangomiji, Upimaji wa Ardhi na Ramani;

• Kusimamia na kufanya shughuli za uthamini; • Kusimamia na kufanya shughuli za usajili wa hati za

kumiliki Ardhi, nyaraka mbalimbali, uhamisho wa milki na uwekaji rehani;

• Kufanya utafiti wa nyumba bora; • Kutayarisha Sera na Sheria zinazosimamia ardhi, nyumba

na makazi nchini;

• Kupanga na kusimamia maendeleo ya Miji;

• Kupanga na kusimamia matumizi bora ya ardhi nchini; • Kupima ardhi na kuandaa ramani; • Kufanya shughuli za upimaji majini; • Kusimamia na kuendeleza wafanyakazi wa Wizara na

wale wa Halmashauri, Idara na Mashirika walio katika Sekta ya Ardhi; na

• Kuandaa mipango ya ukuaji wa miji.

2.0 UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA KIPINDI CHA DESEMBA 2005 HADI DESEMBA, 2009:

2.1 Mapato ya Serikali

Serikali kupitia sekta ya ardhi imeweza kuongeza makusanyo ya maduhuli kutoka shilingi bilioni 6 mwaka 2005 na kufikia jumla ya shilingi 14.0 bilioni, Desemba 2009. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 133.3. Ongezeko la ulipaji wa kodi ya pango la ardhi linatokana na: -

(i) Wananchi wengi kuwa na mwamko wa kulipia kodi hiyo.

(ii) Wananchi wengi wamemilikishwa viwanja kwa mujibu wa Sheria za Ardhi kutoka viwanja 5,488 2005 hadi viwanja 14,500 2009.

(iii) Kuongeza hamasa kupitia matangazo kwenye television, redio na magazeti;

3

(iv) Watumishi wamepatiwa mafunzo na zana za kisasa za utunzaji wa kumbukumbu za viwanja na mapato ambayo yanatolewa mara kwa mara katika Jiji la Dar es Salaam na mikoani.

(v) Wizara imeanza kutumia mfumo wa kisasa wa kukadiria kodi (Land Rent Software). Mfumo huu umeanza kutumika katika vituo vya makusanyo katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya na katika Manispaa za Moshi, Arusha, Morogoro.

Kupitia mfumo huu wa kompyuta ni rahisi kuwabaini ambao hawajalipa kodi na kuwafuatilia. Changamoto iliyopo ni kueneza mfumo huu katika Miji na Mikoa yote. Changamoto nyingine ni kuongeza kasi ya kupima viwanja na mashamba ili makusanyo ya kodi yaongezeke.

2.2 Kurahisisha Upatikanaji wa Huduma za Ardhi na Hatimiliki

2.2.1 Katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2005, Ibara ya 42 (c) inayoelekeza kuwa Chama kitaielekeza Serikali “kuendelea kurahisisha taratibu za upatikanaji wa hatimiliki za ardhi”, utekelezaji wake ni kama ifuatavyo: -

• Wizara imeanzisha kanda tano za ofisi za Ardhi zinazoongozwa na Makamishna Wasaidizi katika miji ya Dar es Salaam (Kanda ya Mashariki), Mbeya (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini), Mwanza (Kanda ya Ziwa), Moshi (Kanda ya Kaskazini) na Dodoma (Kanda ya Kati). Vile vile, katika mwaka huu wa fedha (2009/10) hatua zimeanza kuchukuliwa kukamilisha uanzishaji wa Kanda ya Kusini itakayokuwa Mjini Mtwara.

4

Ofisi za Kanda zina madaraka ya kusaini hatimiliki na kuratibu shughuli zote za Sekta ya ardhi kwenye Halmashauri za Wilaya na Miji.

• Kutokana na kuanzishwa kwa ofisi hizo kasi ya utayarishaji na usajili wa hati imeongezeka kutoka hati 5,488 ilivyokuwa mwaka 2005 na kufikia hati 14,500 zilizotolewa hadi Novemba 2009. Pia, imewezesha hati milki ya ardhi kupatikana ndani ya siku 180 tofauti na siku za nyuma ambapo ilikuwa inachukua muda wa mwaka mmoja hadi miwili.

• Jumla ya hatimiki za viwanja na mashamba 47,287 zilisajiliwa na kutolewa kwa wananchi kwa kipindi kati ya Desemba 2005 na 2009 kama ifuatavyo, Mwaka 2005/06 hati 5,488; mwaka 2006/07 hati 8,160; mwaka 2007/08 hati 9,733 na Mwaka 2008/09 hati 14,436 na Julai hadi Novemba, 2009 hati 9,470 zimetolewa kwa wananchi. Hati hizi zinatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuweka dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye vyombo vya fedha, dhamana mahakamani na dhamana kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu.

2.2.2 Uanzishaji wa Mabaraza ya Ardhi:

Katika kutekeleza Sheria Na. 2 Mahakama za Ardhi (The Land disputes Courts Act Na. 2 of 2002) katika kipindi hiki yameundwa Mabaraza ya Wilaya 16 na kufanya kuwe na jumla ya Mabaraza 39 yenye Wenyeviti 49 pote nchini. Katika kuundwa kwa Mabaraza haya kigezo kikuu ni wingi wa kesi za ardhi katika Wilaya.

• Katika kipindi hiki jumla ya mashauri 33,163 yalifunguliwa, kati ya hayo mashauri 15,849 sawa na asilimia 48 yamesikilizwa na kutolewa uamuzi. Katika kuongeza kasi ya usikilizaji wa kesi, Mabaraza katika Wilaya 23 yamepatiwa magari mwaka huu wa fedha ili kuwezesha Wenyeviti wa Mabaraza ma

5

Wazee wa Mabaraza kutembelea maeneo yenye mgogogro na kutoa maamuzi.

2.3 Kupima Ardhi na Kuimilikisha kwa Wananchi na

Wawekezaji

2.3.1 Katika kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, Ibara ya 42 (b), inayoelekeza kuwa “Serikali iendeleze kwa nguvu mpya kazi inayofanywa na Halmashauri za Wilaya katika kutambua mipaka ya vijiji na kuvipatia vyeti vya ardhi ya kijiji (Certificate of Village Land) ili matumizi ya ardhi yawe endelevu nchini kote”, Serikali imetekeleza yafuatayo: -

• Kati ya Desemba, 2005 hadi Novemba, 2009 jumla ya vijiji 5,500 vilipimwa na kufikia vijiji 10,100 vilivyopimwa nchini kote. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 92 (92%) ya vijiji vyote vipatavyo 11,000. Vijiji ambavyo mipaka yake bado haijapimwa (936) upimaji utakamilika katika mwaka huu wa fedha.

• Upimaji wa mipaka ya vijiji umewezesha kutayarisha na kutoa vyeti vya ardhi ya vijiji 573 nchini ili kuviwezesha vijiji hivyo kutayarisha na kutoa hati za kumiliki ardhi za kimila (Certificate of Customary Right of Occupancy). Hatimiliki za Kimila zitawawezesha wanavijiji kupata fursa ya kutumia ardhi yao kupata mikopo katika Mabenki kwa ajili ya kujipatia mitaji na kupambana na umaskini.

2.3.2 Kupima Viwanja Mijini

Katika utekelezaji wa IIani ya CCM ya Mwaka 2005, Ibara ya 68 (h), inayoelekeza kuwa “Chama kitaielekeza Serikali kuendeleza miradi ya kupima viwanja katika miji hasa kwenye Makao Makuu ya Mikoa”.

6

• Wizara ilisimamia kutekeleza miradi ya upimaji wa viwanja mijini kwa kushirikiana na Halmashauri za Miji na Wilaya nchini. Kati ya mwaka 2005 na Juni 2009 wizara kupitia Mradi wa Kupima Viwanja 20,000 Jijini Dare s Salaam na Mfuko wa kupima viwanja (PDRF) ilizikopesha Halmashauri 37 jumla ya shilingi billioni 5.8 kwa lengo la kupima viwanja 34,500. Wilaya zilizokopeshwa ni pamoja na Mkuranga kwa ajili ya kupima viwanja 174; Kisarawe (viwanja 103); Magu (viwanja 50); Namtumbo (viwanja 600); Sumbawanga (viwanja 543); Muleba (viwanja 169); Kahama (viwanja 300); Makambako (viwanja 200); Kilolo (viwanja 120); Tandahimba (viwanja 100); Lindi (viwanja 250); Mpanda (viwanja 400); Meatu (viwanja 200); Hanang (viwanja 200); Chato (viwanja 300) na Mbozi walikopeshwa kwa ajili ya kulipa fidia.

• Pia, wizara kwa kushirikiana na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam imefanikiwa kupima viwanja 1,483 katika Mradi wa Kuendeleza Upya Eneo la Kurasini kwa ajili ya kupanua eneo la Bandari, pia Mradi wa kuanzisha Kituo Kipya cha Huduma (Satellite Town) cha Luguruni.

• Kutambua na kupima vipande vya ardhi vitakavyo kabidhiwa Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) kwa ajili ya kuanzisha Hazina ya Ardhi (Land Bank). Utambuzi wa awali wa maeneo yanayofaa kwa ajili ya kuanzisha Hazina ya Ardhi umefanyika katika Wilaya za Ilala, Temeke, Kinondoni, Bagamoyo, Pangani, Kilosa na Kilwa. Lengo la mpango huu ni kupima viwanja kati ya 4,800 hadi 6,000 kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi vinavyofaa kuwekezwa katika sekta za mahoteli, viwanda na kilimo.

7

2.4 Maendeleo ya Makazi na Vijiji, na Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC):

2.4.1 Katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha

Mapinduzi Ibara ya 42 (a) inayoelekeza Serikali “kutekeleza Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kurasimisha ardhi na nyumba zao ili waweze kuzitumia kupata mikopo ya benki na mifuko mingine ya fedha inayokopesha”, Serikali imetekeleza yafuatayo: -

Kurasimisha maeneo yaliyojengwa bila kupimwa:

Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri na Ofisi ya MKURABITA imeendelea kutekeleza mkakati wa kutambua na kurasimisha ardhi na nyumba kupitia utekelezaji wa mpango wa kurasimisha maeneo yaliyojengwa bila kupima. Katika kipindi husika, kati ya mali (ardhi na nyumba zilizo tambuliwa) jumla ya leseni za makazi 90,000 zilitolewa katika Jiji la Dar es salaam. Leseni za makazi (Residential Licence) zina nguvu kisheria sawa na Hatimiliki za Kimila (CCRO) na Hatimiliki zinazotolewa kwa ardhi ya jumla (Certificate of Granted Right of Occupancy). Leseni za makazi zinaweza kutumika kama dhamana ya kupata mikopo katika Mabenki na zinadumu kwa miaka 5. Mpango wa Serikali wa kurasimisha ardhi na nyumba (MKURABITA) ulioanza kutekelezwa Jijini Dar es Salaam pia umeanza kutekelezwa katika Jiji la Mwanza (8,000), Dodoma (6,000), Tanga (4,500), na Moshi (1,500) kati ya miliki hizo zilizokwisha pata leseni za makazi ni 160,500..

8

Uanzishaji wa Miji midogo pembezoni mwa Jiji la Dar es salaam: Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam inatekeleza Mpango wa kuanzisha Miji midogo pembezoni mwa Jiji (Satelite towns). Miji hiyo itakuwa na vituo vya kutoa huduma za kijamii. Madhumuni ya mpango huu ni kudhibiti ukuaji holela wa Jiji la Dar es Salaam na kupunguza msongamano wa watu na magari katikati ya Jiji. Wizara ilikwisha kuanza kutekeleza upangaji wa Kituo kipya cha Luguruni (Kinondoni). Tayari wananchi waliotakiwa kuhama eneo hilo walikwisha kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria za Ardhi. Upimaji wa viwanja 294 kwa ajili ya huduma mbalimbali zikiwemo biashara, Ofisi za Serikali, huduma za kijamii kama vile mabenki, soko, hospitali, maduka makubwa (shopping malls), n.k. ulikwisha kukamilika na uuzaji wa viwanja kwa njia ya zabuni uko katika hatua za mwisho. Pia, kazi ya kuweka miundombinu kama barabara, mifereji ya maji ya mvua, utoaji wa maji taka na maji machafu.

Maeneo mengine yaliyopendekezwa katika mpango huo ni Pugu Kajiungeni (Ilala), Kimbiji, Kongowe na Mjimwema (Temeke) na Bunju (Kinondoni). Mradi wa Kuendelezo upya Eneo la Kurasini: Kazi ya kuendeleza upya eneo la Kurasini ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa. Lengo la mradi huu ni kuwezesha eneo la Kurasini kutumika kikamilifu kwa shughuli za upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ili Tanzania iwe lango kuu la biashara kwa nchi za Maziwa Makuu. Wananchi waliokuwa wakiishi eneo la mradi walifanyiwa uthamini wa ardhi, nyumba na

9

mazao. Wananchi wengi wamekwisha kulipwa fidia na kupatiwa viwanja 463 mbadala eneo la Kibada (Kigamboni). Eneo la Kurasini limepimwa jumla ya viwanja vikubwa 18, kati ya hivyo viwanja 14 tayari vimeuzwa kuuzwa kwa wawekezaji wa huduma zinazoendana na bandari, na viwanja 4 vipo katika mchakato wa kuuzwa. Urasimishaji wa Ardhi Vijijini:

• Katika kipindi hiki mashamba ya wananchi 3,500 yalipimwa katika baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Mbozi, Newala, Mbinga, Njombe, Rungwe, Ileje, Kilombero, Babati, Bariadi, Manyoni na Namtumbo ili kuwezesha kutoa hatimiliki za Kimila. Kutokana na upimaji wa mashamba ya majaribio na utoaji wa hatimiliki za kimila ni mategemeo ya Wizara kuwa wataalam wa sekta ya ardhi katika kila wilaya watajifunza kutoka kwenye Wilaya za mfano ili nao wapime kwenye Wilaya zao.

• Vile vile, Hatimiliki za Kimila (CCRO) 34,529 ziliandaliwa na kutolewa kwa wananchi ndani ya kipindi husika. Aidha, kasi ya uandaaji na utoaji wa hatimiliki za kimila imeongezeka ambapo mwaka 2006 zilitolewa hatimiliki 1,262; mwaka 2007 hati 3,940; mwaka 2008 hati 8,815 na Mwaka 2009 zimetolewa hatimiliki za Kimila 20,512. Utoaji wa Hatimiliki za kimila unategemewa kuongezeka mwaka 2009/10 kutokana na utekelezaji wa mradi wa majaribio katika Wilaya za Babati na Bariadi unofadhiliwa na Benki ya Dunia; na Mradi wa Manyoni na Namtumbo unaotekelezwa na Wizara.

10

Utayarishaji wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi:

• Wizara kupitia Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi inaendelea kuratibu na kuwezesha Halmashauri za Wilaya na Vijiji kutayarisha mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi za wilaya na vijiji. Tayari mpango wa matumizi bora ya ardhi kitaifa (National Land use Plan) umekamilika. Mipango ya matumizi bora ya ardhi kupitia mipangoshirikishi iliandaliwa na kukamilishwa katika Wilaya 20 za Lindi, Kilwa, Nachingwea, Bagamoyo, Mkuranga, Rufiji, Meatu, Kahama, Serengeti, Urambo, Kigoma Vijijini, Morogoro Vijijini, Mkinga, Muheza, Namtumbo, Misungwi, Mpanda, Ileje, Mtwara na Pangani. Katika maeneo hayo jumla ya vijiji 125 viandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Mipango hii inapoandaliwa inaleta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji na hivyo inadumisha amani na utulivu kati ya makundi mbalimbali ya watumiaji wa ardhi.

• Katika kipindi hiki Tume ya Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi imeandaa Programu za Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora (The National Land Use Planning Programmes). Programu hizo ziko 12 ambazo ni Programu ya kuimarisha TUME, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Misitu, Wanyamapori, Madini, Nishati, Miundombinu, Rasimali maji, utalii, viwanda/uoto asili. Madhumuni ya programu hizo ni kuonyesha nafasi ya Wizara ya Ardhi katika kuchangia maendeleo ya Sekta hizo kwa kutenga ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

• Ni muhimu kwa Wizara na taasisi zinazohusika na matumizi ya ardhi zikiwemo Halmashauri za miji na wilaya kutenga bajeti ya utekelezaji wa programu

11

zilizoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi.

2.5 Maendeleo ya Nyumba: Kuundwa kwa Idara ya Nyumba:

2.5.1 Serikali katika nia yake ya kuboresha hali ya maisha ya wananchi na kuchangia kukuza uchumi imeanzisha Idara ya Nyumba. Lengo kuu la kuanzisha Idara hii mpya ni kuongoza na kuratibu usimamizi wa maendeleo ya nyumba nchini.

Kutungwa Sheria ya Umiliki wa sehemu za Majengo:

• Katika kipindi hiki imetungwa Sheria ya Umiliki wa Sehemu za Majengo Na. 16 ya Mwaka 2008 (The Unit Title Act). Sheria hii inatoa fursa ya wajenzi wakubwa (Estate Developers) kujenga majengo makubwa yakiwemo maghorofa na kuyagawa katika sehemu zinazojitegemea (flats) na kuziuza kwa wananchi. Utaratibu huu utawawezesha wananchi wengi kupata nyumba katika maeneo au majengo ambayo hapo awali haikuwa rahisi. Pia, kupitia sheria hii itawezesha maeneo mapya ya makazi kupangwa na kupata huduma muhimu kama vile maji, barabara, mifereji ya maji ya mvua na majitaka.

2.5.2 Maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya

68 (c) yanatamka kuwa “Serikali itaendelea kuimarisha utafiti kuhusu vifaa vya ujenzi na kufikisha matokeo ya utafiti huo kwa wananchi” ambapo Wizara imetekeleza yafuatayo: -

12

• Katika jukumu hili, Wizara iliwahamasisha wananchi juu ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika Halmashauri za Wilaya 40 na kutoa mafunzo ya vitendo katika Halmashauri za Wilaya 25. Vile vile, jumla ya mashine 350 za kufyatulia matofali ya udongo na saruji yanayofungamana zilitengenezwa na kuuzwa kwa walengwa. Pia, mashine 85 za kutengenezea vigae vya kuezekea na kalibu (Mould) za vigae 820 zilitengenezwa na kuuzwa kwa wananchi. Aidha, kupitia Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi, Wizara ilitekeleza jukumu la kutafiti, kukuza, kushauri na kusambaza matokeo ya utafiti na utaalam wa ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu katika Wilaya mbalimbali nchini. Wilaya hizo ni pamoja na Namtumbo, Temeke, Kinondoni, Ilala, Tabora (Vijijini na Mjini), Iringa vijijini, Dodoma na Tanga. Pia, Wakala ulifanya kazi za kujenga ofisi za Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika ngazi za Wilaya ikiwa ni pamoja na wilaya za Simanjiro, Tarime, Ifakara, Chato na Njombe.

• Wakala kwa kutumia Grassroot Building Brigades (GBB) umefanikiwa kujenga majengo yakujitangaza (Demonstration Houses) na Ofisi za Serikali za mfano kama vile Jengo la Mkuu wa Wilaya na nyumba za wafanyakazi wa Wilaya ya Mvomero.

2.5.3 Katika kipindi hiki Wizara iliendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kujenga nyumba bora kwa kutumia vifaa vya ujenzi vya gharama nafuu kama Ilani ya Uchaguzi ilivyoelekeza katika [kifungu 68 (d)]: Pamoja na kutoa elimu na kuhamasisha wananchi Wakala ulijitangaza kupitia maonyesha mbalimbali kama vile maonyesho ya Nane Nane yaliyofanyika

13

Mjini Mbeya, Morogoro na Dodoma (mara mbili); na kupitia vyombo vya habari kama televisheni na mkutano ya wataalam na uhamasishaji.

2.5.4 Uanzishwaji wa Utaratibu wa Mikopo ya Nyumba:

Katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 Ibara ya 68 (f) inayoelekeza kuwa Serikali itasimamia uanzishwaji wa taasisi za kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa nyumba nchini. Serikali imetunga Sheria ya Mikopo ya Nyumba Na. 17 ya Mwaka 2008 [The Mortgage Financing (Special Provision) Act] iliyotokana na kuzifanyia marekebisho Sheria tatu ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa nyumba nchini. Sheria zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Ardhi (The Land Amendment Act No. 2) ya mwaka 2004, Sheria ya Usajili wa Ardhi (The Land Registration Act Cap.334), na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Madai (The Civil Procedure Act Rivised Edition 2002). Kutokana na kutungwa kwa sheria hii, hivi sasa mabenki 4 yanatoa mikopo kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa nyumba. Benki hizo ni pamoja na Azania Bankcorp, Commercial Bank of Africa, International Commercial Bank na Stanbic Bank. Benki zingine zinajiandaa kufungua dirisha la kutoa mikopo ya nyumba. Watanzania wanatakiwa kuzitumia kikamilifu fursa zinazotokana na kuwepo kwa mikopo ya nyumba, na pia kutimiza wajibu wao wa kulipa mikopo kwa mujibu wa mikataba wanayoingia. Aidha, Serikali kwa kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia inawezesha kuanzishwa kwa chombo cha fedha cha kukopesha mabenki kwa ajili ya kutoa mikopo ya nyumba ambayo kwa kawaida ni ya muda mrefu wa hadi miaka 30. Chombo hicho ambacho

14

kitajulikana kama Tanzania Mortgage Refinancing Company kitaendeshwa kibiashara na kumilikiwa na mabenki yatakayonunua hisa kwenye chombo hicho na hivyo kufaidika na mikopo ya muda mrefu kwa riba nafuu. Mabenki hayo yatakopesha wananchi kwa muda mrefu kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa nyumba.

Upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mikopo ya muda mrefu kutachangia wananchi wengi kupata mikopo na kupungua kwa riba kubwa inayotozwa na mabenki kwa sasa. Aidha mikopo hiyo itakuwa ni kichocheo kwa maendeleo ya kiuchumi kufuatia kuongezeka kwa ajira na kipato moja kwa moja kutokana na shughuli za ujenzi au kutokana na matumizi yanayofuatia baada ya nyumba kukamilika. Mapato ya kodi ya serikali yanatarajiwa kuongezeka kutokana na matumizi ya mikopo hii. Mkopo wa Benki ya Dunia utatumika pia kuweka na kuendeleza utaratibu wa mikopo midogo ya nyumba (Housing Microfinance). Mikopo hiyo inatarajiwa kuwasadia watu wenye kipato kidogo ambao hawana uwezo wa kupata mkopo mkubwa kwa wakati mmoja. Utaratibu huu utawapa fursa wasio na uwezo kujenga nyumba kwa awamu, kumalizia au kukarabati nyumba zao. Baada ya kuweka mazingira ya upatikananji wa mikopo ya nyumba, Serikali inahakikisha upatikanaji wa nyumba bora nchi nzima kulingana na mahitaji hasa mijini kwa kuhamasisha makampuni binafsi ya uendelezaji milki (real estate developers) kujenga nyumba za bei nafuu. Aidha, Shirika la Nyumba la Taifa linafanyiwa mabadiliko ili liweze kuwa mwendelezaji mkubwa wa nyumba za bei nafuu nchi nzima( master real estate developer).

15

2.5.5 Shirika la Nyumba la Taifa:

Katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005, kuhusu “Shirika la Nyumba la Taifa kuendelea kujenga nyumba za makazi na za biashara kwa ajili ya kuuza na kupangisha nyumba zilizo chini yake [kifungu 68 (g)], Wizara imetekeleza yafuatayo:-

• Shirika la Nyumba la Taifa limeendelea kujenga nyumba za biashara na makazi, ushauri wa kitaalam (consultancy) katika sekta ya ujenzi na kuzifanyia matengenezo nyumba zilizo chini yake. Hivyo, katika kipindi husika, Shirika lilikamilisha ujenzi wa nyumba za makazi 271 katika maeneo ya Dar es Salaam, Chato, Ruangwa na Chalinze kwa gharama ya shilingi bilioni 7.4. Vile vile Shirika linaendelea na ujenzi wa nyumba nyingine 124 katika miji ya Arusha, Dodoma na Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi bilioni 10.3.

• Kwa upande wa majengo ya vitega uchumi Shirika lilikamilisha ujenzi wa majengo matatu kwa gharama ya shilingi bilioni 2.9 katika miji ya Iringa, Kigoma na Arusha. Majengo mengine mawili yanaendelea kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 42 katika miji ya Dar es Salaam na Shinyanga.

• Kuhusu miradi ya ubia inayoshirikisha sekta binafsi, Shirika limekamilisha ujenzi wa majengo 25 kwa gharama ya shilingi bilioni 41 na ujenzi wa majengo mengine 48 unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 90 katika miji ya Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza na Arusha.

• Baada ya kuanza kutumika Sheria ya mikopo ya nyumba utaratibu wa Ubia umesitishwa badala yake NHC watakopa kujenga wenyewe bila ubia. Aidha, Shirika linaendelea kutenga fedha kiwango cha kati ya asilimia 20 hadi 25 ya mapato yake yatokanayo na

16

kodi za pango kila mwaka kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya nyumba zake 16,021. Lengo kuu ni kupendezesha miji yetu. Changamoto iliyopo ni kuligeuza Shirika hili

kutoka katika shughuli za kupangisha nyumba na kukusanya kodi ili liingie katika biashara ya kujenga nyumba kwa wananchi wa kipato cha chini na kati na kuziuza.

2.6 Utekelezaji wa Mkakati wa Kutoa Elimu Kwa Umma

• Elimu kwa umma kuhusu Sera ya Taifa ya Ardhi, Sheria za ardhi, Sheria ya Matumizi ya Ardhi, Sheria ya Mipangomiji na Sheria ya Mahakama za Ardhi imeendelea kutolewa nchini kote.

• Jumla ya nakala 40,000 za Sheria ya Mahakama za Ardhi na Kanuni zake zilichapishwa na kuasambazwa nchini kote.

• Jumla ya nakala 20,000 za Sheria ya Ardhi ya Vijiji pamoja na Kanuni zake zilichapishwa na kusambazwa nchini kote.

2.7 Kuanzishwa kwa Hazina ya Ardhi (Land Bank)

Katika kutekeleza kauli mbiu ya kitaifa ya “Kilimo Kwanza”, Wizara imepewa jukumu la kuratibu uanzishwaji wa Hazina ya Ardhi (Land Bank) kwa ajili ya kutenga ardhi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika kilimo cha mashamba makubwa nay a kati. Hivyo, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka za Mikoa na Wilaya inaendelea kubaini mashamba makubwa yasiyoendelezwa kwa muda mrefu ili taratibu za kubatilisha milki zifanyike kwa ajili ya kupata ardhi huru itakayomilikishwa kwa wawekezaji. Hata hivyo Serikali itahakikisha kuwa, ardhi itakayotengwa kwa ajili hii haitahusisha mashamba ya wanavijiji wala haitoathiri mahitaji ya baadae ya wanakijij husika.

17

2.8 Kumbukumbu za ardhi na Mawasiliano Katika kuboresha kiwango cha utoaji wa huduma za sekta ya ardhi kwa wateja; tangu Desemba, 2005 hadi Oktoba 2009, huduma nyingi za ardhi zinatolewa kwa kutumia mifumo ya kompyuta. Mpango wa muda mrefu wa mafunzo ya kompyuta kwa watumishi wa wizara na ofisi za ardhi katika Halmashauri unatekelezwa kwa awamu. Vilevile imebuniwa mifumo inayotumia teknologia ya kisasa na imeanza kutumika kuboresha kumbukumbu na huduma za ardhi kwa wananchi. Baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja na:

• Mfumo wa Kumbukumbu za Ardhi (Management of Land Information Systems);

• Mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu za upimaji (Surveys Regstration System); na

• Mfumo wa kukadiria kodi za ardhi (Land Rent Management System).

2.9 Uboreshaji wa Sheria na Kutunga Sheria Mpya

Serikali inaendelea na mchakato wa kuziboresha sheria zinazoonekana kuwa ni kikwazo kwa utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi. Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Sheria ya Usajili wa Hati Sura ya 334. Sheria hii itafanyiwa marekebisho ili kuboresha kazi za usajili wa hati na nyaraka za kisheria. Pia, Sheria zingine muhimu zitatungwa ili kuondoa urasimu na vikwazo katika kuwahudumia watanzania na kuharakisha upatikanaji wa maisha bora kwa kila mtanzania. Sheria Mpya zitakazotungwa ni pamoja na Sheria ya Kusimamia kazi za Uthamini (The Valuation Act) na Sheria ya Wakala wa Majengo (The Estate Agency Act).

3.0 CHANGAMOTO ZILIZOPO NA JINSI

TUNAVYOZIKABILI

3.1 Kupima Ardhi yote nchini na Kutayarisha Ramani

18

• Ardhi ya Tanzania ina ukubwa wa kilomita za mraba 942,600 kati yake kilomita za mraba 888,200 ni eneo la nchi kavu. Ardhi hii ndiyo rasilimali ya msingi inayowezesha kutumika kuleta maendeleo kupitia sekta zote. Hata hivyo ili ardhi iweze kutumika kuleta maendeleo ni lazima kila kipande kitambuliwe kipimwe kimilikishwe na kipangiwe matumizi. Changamoto inayotukabili ni kuwa mpaka sasa ardhi iliyopimwa na kumilikishwa inakadiriwa kuwa asilimia moja tu ya ardhi yote. Matokeo ya hali hii ni kutokutumia ardhi iliyopo kikamilifu na kuongezeka kwa migogoro baina ya watumiaji mbalimbali.

• Wizara kwa kutumia Mkopo wa Benki ya Dunia imeanza kuweka mfumo wa alama za msingi wa upimaji ardhi na utayarishaji wa ramani (Geodetic Reference Frame) ambao utawezesha kuharakisha upimaji ardhi kwa gharama nafuu na utayarishaji wa ramani. Pamoja na mkopo wa Benki ya Dunia, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya upimaji wa ardhi, utayarishaji ramani, upangaji wa matumizi ya ardhi na umilikishaji kwa wananchi wa mijini na vijijini.

3.2 Umilikishaji Ardhi

Kutokana na kuwa sehemu kubwa ya nchi haijapimwa wananchi wengi wana ardhi (Land lords) lakini hawana hati miliki, leseni za makazi wala hatimiliki za kimila. Hivyo hawanufaiki na mikopo kwa kukosa dhamana. Changamoto iliyopo ni kupima ardhi na kuimilikisha kwa wananchi. Kwa sasa wananchi wanashindwa kutumia rasilimali ardhi kujiletea maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii jambo hili linachelewesha juhudi za serikali za kuondoa umaskini. Hivyo, jitihada zinaendelea kuchukuliwa za kusogeza huduma za upangaji wa ardhi, uthamini, upimaji na umilikishaji karibu zaidi na wananchi kwa kukasimu mamlaka katika ngazi za Kanda, Mikoa na Wilaya.

19

Halmashauri za Wilaya zina changamoto ya kuondoa upungufu uliopo wa Wataalam wa Sekta ya ardhi wa 74% kwa kuajiri wataalam wa kutosha, pia wanunue zana za kupima ardhi.

3.3 Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Serikali ilianzisha mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi na nyumba kwa kuanzisha Mabaraza ya Ardhi kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi Taifa. Chamamoto iliyopo ni kuwa mfumo huu bado haufanyi kazi kwa ufanisi. Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Kata hayajaimarika ipasavyo kuweza kufanya kazi kwa ufanisi. Elimu zaidi inahitajika kwa wanaoyaendesha Mabaraza hayo pamoja na kuwapatia vitendea kazi kutoka Halmashauri za Wilaya. Vile vile ipo changamoto ya kuanzisha Mabaraza haya katika kila Wilaya na hili litawezekana kwa kuongeza bajeti ya uendeshaji wa Mabaraza hayo.

3.4 Viwango vya fidia Gharama za fidia kwa wananchi zinalipwa kwa kuzingatia mahali ardhi ilipo, maendeleo na gharama zinginezo kulingana na uthamani uliofanyika kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999. Changamoto iliyopo ni wananchi kulalamikia viwango vya malipo ya fidia. Kutokana na changamoto hiyo, Wizara chini ya ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali inahuisha viwango vya fidia mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya bei za soko.

3.5 Uendelezaji wa Miji

• Katika miji yetu kuna kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu wanaohamia mijini kutoka vijijini ikilinganishwa na

20

uwezo wa kukidhi mahitaji ya miundombinu na upimaji wa viwanja. Hivi sasa 30% ya Watanzania wanaishi mijini na ifikapo 2050 inakadiriwa zaidi ya 50% ya Watanzania watakuwa wanaishi mijini. Changamoto iliyopo ni kuwepo kwa ongezeko la ujenzi holela mijini ambapo asilimia zaidi ya sabini ya makazi mijini wanaishi katika maeneo yasiyopimwa. Aidha kuna vijiji vinavyokuwa haraka na kuchukua sura ya kimji.

• Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kurasimisha makazi yasiyopangwa na pia Serikali inaboresha miundombinu ya msingi katika maeneo hayo. Katika baadhi ya miji, Serikali inaendelea kuandaa mipango ya muda mrefu (Masterplans), na kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja ili kuondoa tatizo la ujenzi holela.

3.6 Mabadiliko katika Shirika la Nyumba la Taifa Shirika la Nyumba la Taifa linao uwezo wa rasimali ya majengo yenye thamani kubwa. Lakini halijaweza kutoa mchango unaotarajiwa kwenye sekta ya makazi na uchumi wa Taifa. Changamoto iliyopo ni kulibadilisha Shirika hili kutoka katika hali yake ya sasa ya mpangishaji wa nyumba na kukusanya kodi, na kulifanya liingie katika biashara ya kujenga na kuuza nyumba ili kukuza mtaji wake na hivyo kupata uwezo wa kuwekeza zaidi katika maendeleo ya makazi nchini.

3.7 Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi umekuwa ukifanya juhudi kubwa za kiutafiti na kusambaza matokeo ya tafiti zinazofanywa kwa wananchi. Changamoto iliyopo ni kuwa baada ya kukamilisha utafiti hakuna mfumo wa kupokea na kusambaza matokeo ya tafiti hizi kwenye viwanda vya uzalishaji au wajasiliamali ili teknolojia hii iwafikie wananchi. Kwa

21

mfano kwa sasa mahitaji ya mashine za kutengeneza matofali yanayofungamana ni makubwa kuliko uwezo wa Wakala lakini hakuna kiwanda kilicho tayari kupokea teknolojia hiyo ya kuzalisha mashine za kutosha kukidhi mahitaji ya soko. Jitihada zinaendelea kuhamasisha wajasiriamali kusambaza zana zinazotokana na utafiti.

4.0 HITIMISHO

Kufuatia mwelekeo wa Serikali wa kuelekeza nguvu zake katika kuimarisha kilimo kupitia kauli Mbiu ya Kilimo Kwanza Wizara ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa ardhi inamilikishwa kwa wakulima wadogo; kwa kutoa hatimiliki za kimila kwa mashamba yao. Pia kutenga maeneo (Land Bank) kwa ajili ya mashamba makubwa na viwanda vya mazao yatokanayo na kilimo (Agro Industries). Aidha matumizi mengine makubwa ya ardhi yakiwemo ya uendelezaji wa nyumba (Real Estate Development), Mahoteli, Viwanda n.k. yanatengewa maeneo. Vilevile baada ya kukamilika kwa mpango wa Taifa na Matumizi Bora ya Ardhi, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau wengine inajukumu la kuhakikisha kuwa maeneo yenye migogoro na migogoro sugu ya matumizi ya ardhi yanapatiwa ufumbuzi. Kufuatia hili Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri kuhakiki, kupima, kupanga matumizi ya ardhi, kusajili na kutoa hati katika maeneo hayo ili kuwezesha kuwepo kwa usalama wa milki na hivyo kuondoa migogoro kati ya watumiaji mbalimbali wa ardhi. Natoa rai kwa Mamlaka na Taasisi mbalimbali kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha kuwa ardhi inaziwezesha sekta zote kutoa mchango katika vita vya kuwaondolea wananchi umasikini.