18
Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007 Tony Baker Nyaraka ya Kufanyia Kazi 09.2k

Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

  • Upload
    lecong

  • View
    247

  • Download
    0

Embed Size (px)

Citation preview

Page 1: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

Kupambana na Rushwana Haki ya Kupata Habari:

Muswada wa Sheria yaHaki ya Kupata Habari, 2007

Tony Baker

Nyaraka ya Kufanyia Kazi

09.2k

Page 2: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa
Page 3: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

1

Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari:Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 20071

Tony Baker2

Utamaduni wa usiri [ambao] unagubika mfumo wetu wa kikatiba hujenga mazingira ya mienendo mibaya kama vile rushwa, matumizi mabaya ya mamlaka, ubadhirifu, wizi na usimamizi mbaya wa rasilimali za umma, ambayo kwa huunganika na kuzaa ufisadi wa kisiasa unaoonekana katika chaguzi zilizojaa mizengwe na mauaji ya kisiasa.

—Dkt. Sengodo MvungiAliwahi kuwa mwandishi wa habari, mwanasheria na sasa ni mhadhiri

wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(Taasisi ya Habari,3 2008)

1. MuhtasariHivi sasa mlipuko wa rushwa unaendelea kuidhoofisha Tanzania. Kwa mujibu wa Faharasa ya Utambuzi wa Rushwa ya mwaka 2008 (CPI) ya shirika la kimataifa linalopambana na rushwa, Transparency International (TI), Tanzania ni nchi ya 102 kati ya 180 zilizofanyiwa utafiti na kupata alama 3 katika kipimio cha 10, huku alama 10 inaashiria nchi safi—hakuna rushwa—na alama 0 ni ishara ya rushwa iliyokithiri (TI, 2008). Waraka huu wa sera unaeleza hali ya sasa ya rushwa nchini Tanzania, athari zake, vyanzo vyake na ufumbuzi wa kisera. Kwa usahihi zaidi, baada ya kuchambua athari za rushwa kwa taifa la Tanzania, unaonesha namna ambavyo sababu za rushwa za kisheria, kimfumo, kijamii na kiuchumi zinavyoweza kushughulikiwa na kuondolewa kwa sheria inayotafuta haki ya kupata habari.

2. Maana ya RushwaKitabu cha Kudhibiti Rushwa: Mwongozo kwa Mbunge4 kilichotumiwa na Mtandao wa Wabunge wa Afrika wa Kupambana na Rushwa (APNAC) kimeifafanua rushwa kama ni “matumizi mabaya ya wadhifa kwa manufaa binafsi” (Asasi ya Kimataifa ya Wabunge Dhidi ya Rushwa5 (GOPAC), 2005). Rushwa inaweza kugawanywa katika makundi mawili: rushwa ndogo na kubwa. Rushwa ndogo ni ile rushwa ya kiwango kidogo inayotokea kila siku kati ya maofisa wa Serikali wa ngazi ya

1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa kama sehemu ya kutimiza masharti ya shahada ya uzamili katika Maendeleo Endelevu - Uchambuzi wa Sera na Utetezi Taasisi ya Masomo ya Uzamili ya SIT Brattleboro, Vermont, Marekani. Shukrani nyingi ziwafikie Profesa Jeff Unsicker na Nikoi Kote-Nikoi.2 Ni raia wa Marekani, na baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza, Tony Baker alienda kuishi kwa miaka miwili katika kijiji Mlima Hanang, kaskazini mwa Tanzania. Afanyakazi bega kwa bega na wakulima wa vijijini, na kupata ujuzi kuhusu harakati za mapambano za wananchi pamoja na hatua za sera zilizorudisha nyuma maendeleo yao na kusababisha umasikini. Kwa imani kwamba mabadiliko ya sera yanaweza kushughulikia sababu za msingi za umasikini na kutotendewa haki, alirudi tena Marekani kusomea eneo hilo. Kwa sasa Tony ni mwanafunzi wa uzamili akifanya mazoezi kwa vitendo katika idara ya Uchambuzi wa Sera na Utetezi ya HakiElimu.3 Chanzo hiki kinaitwa “Media Institute” kwenye marejeo.4 Kwa kweli, kitabu hicho kinaitwa Controlling Corruption: A Parliamentarian’s Handbook na kilichapishwa na African Parliamentarians Network Against Corruption.5 Chanzo hiki kinaitwa “Global Organization of Parliamentarians Against Corruption” kwenye marejeo.

Page 4: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

2

chini na wananchi, “katika hatua za utekelezaji wa masuala ya siasa” (U4, Faharasa ya Rushwa;6 GOPAC). Hapa ndipo kuna uwezekano mkubwa wa kutoa au kupokea rushwa katika kununua

bidhaa na huduma za serikali—mikataba ya serikali, leseni, huduma za afya, uandikishaji wa wanafunzi, kupunguziwa kodi au jambo lolote la kuharakisha huduma za umma. Kwa sababu hufanyika mahali ambapo umma unakutana na utawala , mara nyingi huitwa rushwa ya urasimu. Kinyume chake, rushwa kubwa hutokea katika ngazi za juu kabisa za serikali, “katika hatua za utungaji wa sera katika siasa” (U4, Faharasa ya Rushwa; GOPAC). Hii hujali zaidi mamlaka kuliko fedha, aina hii ya rushwa inatokea wakati watu waliokabidhiwa mamlaka ya umma ni mafisadi na hutumia nafasi hiyo kudumisha mamlaka yao na utajiri kwa kupuuza au kukiuka sheria, ushawishi wa kibiashara au upendeleo, kubadilisha upangaji wa rasilimali, au kampeni za kuharibu na uchaguzi. Kutokana na hali hii rushwa kubwa aghalabu hufungamana na rushwa ya kisiasa (U4, Faharasa ya Rushwa; GOPAC).

3. Athari za RushwaWatanzania wote wanakabiliwa na rushwa, hasa rushwa ndogo, katika shughuli mbalimbali za maisha ya kawaida ya kila siku. Mara nyingi haki za msingi na huduma huwa hazipatikani bila ya makubaliano ya rushwa ama hongo—fedha, zawadi za vitu au upendeleo, ngono au aina nyingine. Zaidi ya upungufu uliopo wa huduma za afya, mtu analazimika kulipia zaidi kuonana na muuguzi au daktari, kutibiwa, kupewa kitanda au kupata dawa. Huduma za nyumbani—maji, umeme, simu—zinaweza kupatikana tu baada ya kuwapa rushwa maofisa wanaohusika au wanaotoa huduma. Wakati wa kumpeleka mtoto shule ya sekondari, mtu anatakiwa ampe mkuu wa shule malipo yake maalumu. Kupata nyaraka au vibali vya kawaida kama vile kujenga nyumba ya kuishi, kufungua biashara ndogo au hata kupata cheti halali, maofisa wa serikali ni lazima kwanza walipwe. Wakati wa kushughulika na polisi, mtu anajikuta kuwa yuko tayari kutoa rushwa kupita katika kituo cha ukaguzi wa magari, kukwepa kutozwa faini au kukamatwa kiholela. Ukifika, wakati wa uchaguzi wanasiasa wananunua kura kwa fedha, soda, vyakula au zawadi nyingine. Ni orodha ndefu (REPOA, 2006; U4, Vyanzo na Matokeo ya Rushwa7).

Taasisi ya Kuzuia Rushwa, chombo cha Serikali ya Tanzania, imetaja athari za rushwa ndogo na kubwa kama ifuatavyo:

• Serikali kushindwa kufikia malengo yake • Kuongezeka kwa gharama za kiutawala• Kupungua kwa ukusanyaji wa mapato• Kukosekana kwa ujasiri na kushindwa kufuata kiwango cha juu cha uadilifu• Kupunguza heshima kwa mamlaka• Kupoteza tija kwa sababu muda na nguvu hupotea kwa kuiibia au kuitapeli serikali

kuliko kuimarisha malengo yake• Kupungua kwa uwekezaji wa nchi za nje• Kwa kuwa rushwa inawakilisha kutotenda haki kwa taasisi, bila shaka husababisha

madai na mashtaka ya kusingiziwa ambapo hata ofisa mwaminifu anaweza kutishwa ili kupata fedha, na hivyo hali ya kukosa haki inajitokeza.

(Taasisi ya Kuzuia Rushwa)

6 Chanzo hiki kinaitwa “U4, Corruption Glossary” kwenye marejeo.7 Chanzo hiki kinaitwa “U4, Causes & Consequences of Corruption” kwenye marejeo.

Page 5: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

3

Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Tanzania, au NACSAP, ni mkakati wa kupambana na rushwa, ulioanzishwa mwaka 1999, nao pia unaorodhesha “dhihaka kwa mfumo wa mahakama wa nchi” na “uamuzi unaopimwa kwa fedha kuliko maadili ya binadamu” kama athari zaidi za rushwa (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,8 1999).

Utafiti mkubwa uliofanyika mwaka 2003 na Transparency International kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania unahakiki na kuzidi kufafanua kwa undani zaidi matokeo yaliyotajwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa na NACSAP. Kwa sababu rushwa ni matumizi mabaya ya mamlaka kwa manufaa binafsi, husababisha pengo kubwa la kiuchumi kati ya “walionacho” na “wasionacho” kwa vile wale wenye mamlaka wanajilimbikizia utajiri mwingi zaidi na kuwaachia masikini kiduchu zaidi. Ongezeko hili kubwa la umasikini hupunguza mshikamano wa kijamii na kuongeza ukosefu wa amani na utulivu wa umma. Utafiti huo umeona kuwa “ongezeko la vurugu na wizi wa kutumia silaha mijini, ukiwemo ule wa benki jijini Dar es Salaam na Arusha” (TI, 2003, uk. 13) husababishwa na rushwa. Hawa “walionacho” waliopata utajiri wao kwa njia ya rushwa ndio haohao wanaohonga mahakama kwa kununua uhuru wao toka hatiani na hivyo “kuudhihaki mfumo wa mahakama wa taifa” uliotajwa hapo juu (TI, 2003).

Kwa kuwa maofisa wanatumia muda na nguvu nyingi katika kupata manufaa ya kifisadi, tija ya serikali kwa jumla hushuka kwani uwezo wa kutimiza malengo yake ya kuhudumia wananchi na kupambana na umaskini hupungua. Rushwa ya kisekta inayotolewa kwenye huduma za jamii, husababisha kushindania rasilimali chache ambapo raia wanajihusisha na rushwa kwa kukiuka taratibu sahihi na kuwahonga watoa huduma, “kama ilivyo katika uandikishaji wa wanafunzi na kulazwa katika kliniki na hospitali” (TI, 2003, uk. 13). Hii hugeuka kuwa hali ya kawaida kwa watoa elimu na wafanyakazi wa huduma za afya kuomba rushwa. Na kwa sababu rushwa huchota fedha kutoka katika bajeti za utawala, serikali hulazimika kupandisha kodi, bila kuonesha ufanisi wowote wa huduma (TI, 2003).

Hali kadhalika kuna suala la kimazingira ndani ya rushwa wakati biashara chafu zinaruhusiwa kuanzishwa na kuendelezwa kupitia ukiukaji wa Tathmini za Athari za Mazingira kwa kutumia fedha (TI, 2003).

Kwa ujumla, rushwa huwafanya wananchi “wapoteze imani kwa uongozi wao” (TI, 2003, uk. 13), huathiri mamlaka na uhalali wa serikali yao. Kwa hiyo, wakati serikali inachukua hatua ya kuzuia rushwa, inashindwa muda mfupi tu kwa sababu imetambuliwa kuwa haina mamlaka (TI, 2003). Ni dhahiri kwamba athari za rushwa huongeza madhara kiuchumi, kijamii, kisiasa na kisaikolojia.

4. Vyanzo vya RushwaKutambua vyanzo vya rushwa ni suala tata kama ilivyo kuzielezea athari zake, kama siyo zaidi. Taasisi ya Kuzuia Rushwa na NACSAP hutoa tathmini ya kwa nini rushwa ipo nchini Tanzania. Taasisi ya Kuzuia Rushwa imebainisha vyanzo vya rushwa kubwa na ndogo kama ifuatavyo:

• Udhaifu na kukosa ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi• Miundo ya kisheria, kiutawala na kisiasa inatoa mazingira muafaka ya kutoa au

kupokea rushwa

8 Chanzo hiki kinaitwa “United Republic of Tanzania” kwenye marejeo.

Page 6: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

4

• Hali ngumu ya uchumi inayowalazimisha watu kutafuta namna ya kujikimu: Hii inachangiwa na mishahara midogo kwa watumishi wa umma na kuongezeka kwa

kasi kwa gharama za maisha.• Taratibu zinazochukua mlolongo mrefu na mgumu (urasimu)• Kutokuwa na uhakika wa kipindi cha ajira• Kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza maamuzi• Kukosekana kwa utashi wa kisiasa• Kumomonyoka kwa maadili ya uongozi• Kuibuka kwa matumizi ya kifahari

(Taasisi ya Kuzuia Rushwa)

Vyanzo hivi na vile vya NACSAP vinajadiliwa kwa kirefu hapa chini. NACSAP inawasilisha mchoro ufuatao ili kuonyesha kile kinachoitwa “mtazamo wa kiuchanganuzi” wa vyanzo vya rushwa:

Kasoro za mfumo - Mifumo - Taratibu - Miongozo

Uelewamdogo wa wananchi

Uingiliaji wakisiasa

Muundo wa sheriaSheria zinazopinganaSheria zilizopitwa na wakatiKukosekana kwa sheria

Uwezo mdogowa kiasasi

Uroho na matumizi mabaya ya mamlaka

Ukosefu wa nidhamu

Kutomudu

Rushwa

(Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1999)

Tunaweza kuvipanga vyanzo hivi vingi vilivyotolewa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa na NACSAP katika makundi manne: muundo wa sheria, masuala ya mfumo, mazingira ya jamii na hali ya uchumi. Tukianza na muundo wa sheria, mapambano yanayoendeshwa dhidi ya rushwa ni dhaifu mno na kwa hiyo, husababisha kuwapo na mazingira mazuri zaidi ya kuendeleza rushwa. Utafiti wa mwaka 2003 wa Mifumo ya Uadilifu ya Taifa uliyofanywa na Transparency International kuhusu Tanzania unasisitiza kwamba sheria zilizopo zinahitaji ushahidi mwingi ili kuweka na kufanya mashtaka dhidi ya maofisa wanaotuhumiwa kula rushwa kuwa na uwezekano mdogo wa kufanikiwa. Katika tabia inayozidi kuwa na ujanja, utata na usiri zaidi, rushwa inazidi kuwa vigumu kuikabili kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Page 7: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

5

Masuala ya mfumo yanajumuisha mambo mengi yanayochochea rushwa. Mifumo ya kisheria, kisiasa na kiutawala kuwa chini ya serikali kuu ina maana kwamba upangaji wa rasilimali unadhibitiwa na viongozi wachache wenye mamlaka makubwa. Uhuru wa kiutawala wa mamlaka yao unaongezwa zaidi na maofisa wasiofaa na hata wala rushwa katika ufuatiliaji na ukaguzi (TI, 2003). Kwa uwazi na uwajibikaji mdogo katika mfumo, matumizi mabaya haya ya madaraka hayaepukiki mbele ya uroho na umaskini. Taratibu na miongozo katika mifumo hii huchukua muda mrefu, huchosha na si wa kifanisi. Pamoja na ushawishi wa fedha wa kukubali kupokea rushwa kutoka kwa mtu au kikundi kinachotafuta kukiuka sheria, kuachana na urasimu na kanuni huwashawishi maofisa wa serikali na kuiharibu zaidi (TI, 2003).

Aidha, baadhi ya vipengele vya mazingira ya kijamii ya Tanzania vinachochea rushwa. Uhusiano wa familia pana au makabila huzaa upendeleo kwa misingi hiyo. Dhana ya mafanikio inayozidi kutafsiriwa na mali na matumizi kuliko huduma bora kwa manufaa ya wananchi inapesababisha maafisa wengi wa serikali katika harakati za kujitafutia wao wenyewe mamlaka, fedha na hadhi. Wakati rushwa inaweza kuchangia katika utafutaji huo, vitendo vingi zaidi vya rushwa hujitokeza; uadilifu wa uongozi huzidiwa na uroho wa binadamu. Viwango vidogo vya uelewa wa wananchi na udhaifu wa jamii za kiraia katika uwanja wa siasa-jamii pia unawezesha rushwa kushamiri bila kipingamizi. Ni siku za hivi karibu tu ndipo vikundi vya asasi za kiraia vilipoanza kuzungumzia rushwa (TI, 2003).

Mwisho, kutokana na hali ya uchumi, Taasisi ya Kuzuia Rushwa inazungumzia kuhusu kutokuwa na uhakika wa ajira na mishahara midogo. Kutokuwa na uhakika wa muda wa ajira huwasababisha viongozi kujinufaisha zaidi na mamlaka waliyonayo kazini kwa kuendeleza rushwa. Mishahara midogo inayotokana na uwepo wa sekta kubwa ya umma wakati rasilimali za kuhudumia ni chache mno, huwalazimisha watumishi wa umma kutafuta mapato ya ziada kwa njia nyingine, hasa kupitia hongo (U4, Vyanzo na Matokeo ya Rushwa).

5. Sera ya Kupambana na RushwaTanzania imepambana na rushwa kwa muda mrefu. Tangu mwaka 1966, Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (Mchunguzi Maalum) hufuatilia matumizi mabaya ya mamlaka ya serikali yanayofanywa na maofisa na idara za serikali. Ili kuimarisha uwezo huu, Sheria ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1971 ilitungwa na kupitishwa na hatimaye kusababisha kuanzishwa kwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (wakati ule ilijulikana kuwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa) mwaka 1975 (REPOA, 2006). Mwaka 1983, Sheria ya Uhujumu Uchumi ilipitishwa, na kutaja rushwa kuwa ni kosa la kiuchumi, lakini baadaye mwaka 1984 ilibadilishwa na Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi. Sheria hii ya pili iliipa uwezo zaidi Sheria ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1971 kwa kutaja makosa yaliyoelezwa kama makosa ya jinai ya kiuchumi yanayostahili adhabu (TI, 2003).

Hata hivyo, Taasisi ya Kuzuia Rushwa imeshindwa kufanya kazi bila utashi wa kisiasa unaotakiwa kuipa nguvu zaidi sheria, na rushwa imeendelea kushamiri kwa kasi. Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitungwa na kupitishwa mwaka 1995 (TI, 2003), na Januari 1996, iliundwa Tume ya Rais ya Kuchunguza Mianya ya Rushwa. Ripoti ya Warioba (iliyopewa jina la J.S. Warioba, mwenyekiti wa Tume hiyo ya Rais) iliwasilishwa mwezi Desemba 1996, na kueleza kwa kina aina, sababu na vyanzo vya rushwa nchini Tanzania na mapendekezo ya njia za kupambana na rushwa. Ripoti ya Warioba iliyopata sifa sana (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,9 1996), “ilikuwa ni

9 Chanzo hiki kinaitwa “United Republic of Tanzania” kwenye marejeo.

Page 8: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

6

miongoni mwa uchambuzi ulioheshimiwa zaidi kuhusu rushwa kuliko nchi nyingine yoyote ya kiafrika” (TI, 2003, uk. 32), imefanya kazi nzuri ya kushughulikia suala la rushwa kwa ukamilifu na bila ya kumwonea mtu haya, kwa kutaja moja kwa moja majina ya ofisi, idara na mashirika yaliyoenea rushwa na mbinu zinazotumika kuiruhusu rushwa kuwapo (Doig na Riley, 1998).

Katika kuunga mkono ripoti hiyo, Rais aliunda na kuiweka chini yake nafasi ya ya Waziri wa Nchi Utawala Bora mwaka 1997 (TI, 2003), na mwaka 1999 Serikali iliendelea kuunda Mfumo wa Taifa wa Utawala Bora na Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (NACSAP). Hadi mwaka 2001, mpango huo mpya umesababisha kuondolewa kwa maofisa fisadi, kuimarishwa kwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa, kuundwa kwa Kitengo cha Kuratibu Utawala Bora, kutungwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1999) na kubadilishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) (REPOA, 2006).

Wakati wa kukamilishwa kwa awamu ya kwanza ya NACSAP wa mwaka 2000-2005, ushahidi kwamba rushwa, matumizi mabaya ya mamlaka na ukiukwaji wa haki za binadamu vilikuwa vimekithiri katika ngazi ya serikali za mitaa na hivyo kuhitaji kuzinduliwa NACSAP II mwaka 2006. Awamu hii ya pili ya NACSAP iliyoanza mwaka 2006 hadi 2010 inaendeleza utekelezaji wake katika zaidi ya wizara, idara na mashirika na kujumuisha mipango ya kupambana na rushwa na utekelezaji katika mamlaka za serikali za mitaa (Fieldstad, Ngalewa, na Katera, 2008).

Wakati Tanzania inaelekea kutimiza malengo ya NACSAP, Programu ya Ushirikiano wa Pande Tatu (NATPP), ulioanzishwa mwaka 2005, unaratibu juhudi za asasi za kiraia, sekta binafsi na Serikali kufikia malengo ya NACSAP na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TUKUKURU), iliyoanzishwa mwaka 2007 kwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, imeongeza nguvu zaidi kazi ya Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Mtandao wa Ushauri Ulimwenguni10).

Mwisho, mwezi Desemba mwaka 2006, Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ilichapisha Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Kupata Habari. Ingawa mwanzoni ulipokewa kwa shauku kubwa kutokana na kwamba kupata habari kwa umma limekuwa suala kubwa, Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Kupata Habari, ukiuchunguza kwa karibu, umekosolewa sana na wasomi, wamiliki wa vyombo vya habari na wanaharakati wa asasi za kiraia kwa sababu una vifungu vinayokataza kuliko kuongeza kiasi cha habari zinazoweza kufikiwa na umma na kuweka kikomo cha kisheria kwa wale wanaojulikana kisheria kuwa ni waandishi wa habari. Baadaye mtandao wa vyombo vya habari na asasi za kiraia uliitikia na kufanikiwa haraka kushirikiana na serikali na kufikia makubaliano kuwa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Kupata Habari usiwasilishwe bungeni kama ilivyopangwa na kwamba mtandao huo uruhusiwe kutoa mapendekezo katika muswada wa sheria ya kupata habari (Baraza la Habari la Tanzania,11 2007).

6. Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007Mwezi Agosti 2007, Mtandao wa Uhuru wa Kupata Habari na Kujieleza ulitimiza wajibu wake kwa kuikabidhi Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari ambao ni jibu la Mtandao kwa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Kupata Habari. Mtandao huo, ambao ni uleule uliokuwa na jukumu la kuzuia Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Kupata Habari wa Serikali, ina washiriki wafuatao:

10 Chanzo hiki kinaitwa “Global Advice Network” kwenye marejeo.11 Chanzo hiki kinaitwa “Media Council of Tanzania” kwenye marejeo.

Page 9: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

7

Baraza la Habari Tanzania (MCT) Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-Tan) Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)Chama cha Sheria Tanganyika (TLS) Asasi ya Taifa ya Msaada wa Sheria (NOLA)Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT)Asasi ya Elimu ya Sheria Tanzania (TANLET)Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)Ibara ya 19—UingerezaChama cha Vyombo ya Habari Vya Jumuiya ya Madola—India

(Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari,12 2007)

Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, Waziri wa Habari ameendelea kutoa ahadi za kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari. Mpaka sasa hajafanya hivyo (Moshiro, 2008).

Kupata habari maana yake ni “upataji wa habari rasmi kwa umma” (Fahamu na Ibara ya 19,13 uk. 29) ambapo vyombo vya umma vinatakiwa kuchapisha makundi muhimu ya habari pamoja na kutoa njia zinazofaa kwa raia kupata habari mahususi baada ya kuziomba (Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa14). Ikiwa imeelezwa maana yake katika Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, upataji wa habari ni “ukaguzi wa kazi na habari, kuandika dondoo na muhtasari na kupata nakala za habari zilizoidhinishwa au kuchukua sampuli za habari” (Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007).

Kama ilivyoelezwa na shirika la Transparency International,

Kupata habari inahusiana na sera, mienendo, sheria na taratibu zinazohakikisha uwazi katika kushughulikia masuala ya umma. Kwa maana pana ni suala la kupata kwa kiasi gani habari zilizozuiliwa ndani ambazo watu wa nje wanastahiki kupata, na wanachoweza kufanya watu wa nje iwapo watu wa ndani hawako tayari sana kuruhusu upatikanaji huo.

(TI, Upataji wa Habari – Majadiliano15)

Uhimizaji wa kupata habari unatokana na msingi wa wazo “kwamba habari zinazodhibitiwa na mamlaka ya umma ni rasilimali muhimu kwa umma na kwamba upatikanaji wa habari hiyo kwa umma unahimiza uwazi na uwajibikaji mkubwa wa mamlaka hizo za umma, na kwamba taarifa hiyo ni muhimu kwa mchakato wa kidemokrasia” (Kocaoglu, Figari na Darbishire, 2006, uk. 5).

Sheria ya Haki ya Kupata Habari inahakikisha upatikanaji wa habari kwa namna nyingi. Kwanza, inaeleza maana ya haki ya kupata habari na kusisistiza kwamba upatikanaji huo ni bure. Halafu, inavitaka vyombo vya umma na vya binafsi kuchapisha kila baada ya muda fulani habari muhimu kupitia njia zinazoeleweka kwa ajili ya kukidhi maombi ya kupata habari. Kushindwa kufanya

12 Chanzo hiki kinaitwa “Stakeholder’s Proposal for the Right to Information Act” kwenye marejeo.13 Chanzo hiki kinaitwa “Fahamu & Article 19” kwenye marejeo.14 Chanzo hiki kinaitwa “United Nations Development Programme (UNDP)” kwenye marejeo.15 Chanzo hiki kinaitwa “Transparency International (TI), Access to information – Discussion” kwenye marejeo.

Page 10: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

8

hivyo kwa upande wowote kutaadhibiwa kisheria. Sheria hiyo imekuwa na uangalifu wa kuwalinda wapasha habari wanapotoa taarifa ya matukio ya rushwa na ukiukaji wa utaratibu. Mwisho, Sheria ya Haki ya Kupata Habari inaunda vyombo viwili vipya. Kwanza ni “Tume ya Habari,” chombo cha serikali kitakachohakikisha upataji wa habari na kusimamia malalamiko pale itokeapo kukataliwa kupata habari. Pili, “ Jukwaa la Wadau wa Habari,” ni mkutano wa asasi za kiraia unaoshauri na kufuatilia Tume ya Habari (Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007).

Sheria ya Haki ya Kupata Habari ina nafasi kubwa katika kupambana na rushwa kwa kushughulikia sababu nyingi zilizotajwa hapo juu. Kusema kweli, sheria hii inaimarisha muundo wa sheria wa Tanzania. Pale ambapo ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka maofisa fisadi, ukusanyaji ushahidi unawezeshwa na Sheria ya Haki ya Kupata Habari kwa namna mbili. Kwanza inatoa ushahidi zaidi kwa kutaka utayarishaji wa nyaraka na uchapishaji wake, ambapo kwa sasa hakuna hata moja kati ya hayo. Pili inaimarisha uwezo wa kukusanya ushahidi kwa kuharamisha uzuiaji wa baadhi ya habari.

Aidha, Sheria ya Haki ya Kupata Habari inaipa nguvu Katiba ya Tanzania, hasa Ibara ya 18(1) na 18(2) zinazosema kuwa

Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

(Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 2000)

Tanzania pia imeridhia sheria nyingi za kimataifa, kwa mfano Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (Ibara ya 19), Makubaliano ya Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa ya Umoja wa Mataifa (Ibara ya 19 (2)) na Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu (Ibara ya 9 (1)), zinazoeleza uhuru wa kujieleza zikiwemo haki za kupokea na kutoa habari (Chachage, Kyando na Rajani, 2005). Zaidi ya kutoa ushahidi kwa ajili ya mapambano dhidi ya rushwa na kuwezesha katiba yake, Sheria ya Haki ya Kupata Habari inaimarisha sheria hizo za kimataifa na pia kuimarisha muundo wa sheria wa Tanzania unaozihusu.

Kuhusiana na sababu za kimfumo, Sheria ya Haki ya Kupata Habari inaziba mianya ambayo zamani ilikuwa ikiwawezesha viongozi wa umma kutumia madaraka yao vibaya kwa kuanzisha njia kwa raia kufuatilia utendaji wao. Wito wa wananchi wa kutaka kutolewa kwa habari za sheria, siasa na utawala huleta uwazi na uwajibikaji. Hii huanza kudhoofisha matendo vya ufisadi kwa kuyafafanya yawe magumu kuendelea nayo kwa kuyafanya yawe magumu kuyaficha. “Rushwa hushamri zaidi gizani,” kwa hiyo maendeleo yoyote yanayotoa mwanga kwa serikali na michakato yake kwa kuyafichua yaonekane kwa umma yanapunguza rushwa (Kocaoglu et al., 2006, uk. 5). Kwa kuhakikishiwa kupata habari rasmi kwa umma, vyombo vya habari na asasi za kiraia, si kama tu kutawafichua wale ambao sasa wanajishughulisha na rushwa na matumizi mabaya ya mamlaka, bali pengine lililo muhimu zaidi, wengine hawatathubutu kushawishika na hongo kwa kukiuka taratibu sahihi wakati ujao. Kwa hiyo, uwazi uliopatikana sasa unazuia rushwa ya siku zijazo na

Page 11: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

9

kusababisha mfumo wa kutoa huduma za umma uwe wa ufanisi na uwezo (TI, Upataji wa Habari – Majadiliano).

Hata hivyo, maeneo ambako pengine athari za Sheria ya Haki ya Kupata Habari zitaonekana zaidi ni katika mazingira ya jamii. Kupata habari kunaongeza uelewa wa umma na matendo ya asasi za kiraia kwa kuwapa raia elimu itakayowasaidia kuwajibisha asasi na kufanya uamuzi wa busara. Kutokana na habari ya uwazi na ufuatiliaji wa umma, maofisa wanakabiliwa na matokeo yanayowakataza wasiingie kwa urahisi katika choyo au upendeleo wa ndugu katika ajira na hivyo kulazimika kurudisha uaminifu wa uongozi unaoharibika ndani ya hali ya sasa ya rushwa. Uwezeshaji huu wa raia kudai habari kutoka kwa asasi, kutafuta marekebisho na mamlaka na kushinikiza kuwaadhibu wahalifu unarudisha uwiano wa mkataba wa jamii kati ya raia wote na taifa, mfumo uliokusudiwa kuwa kama utaratibu wa kuwajali kwa manufaa ya wananchi. Lakini katika rushwa unaharibiwa na choyo ili badala yake uwe mfumo wa manufaa binafsi. Kwa kuwa rushwa na kunyimwa habari kunadhoofisha na kukatisha tamaa raia, haki ya kupata habari kimsingi hujenga uaminifu kati ya watu na taifa kwa kuondoa usiri na kujenga upya imani (TI, Upataji wa Habari16).

Mwisho, Sheria ya Haki ya Kupata Habari inashughulikia sababu za rushwa za kiuchumi pia. Katika mfumo ambao mafisadi watakamatwa, watumishi wa umma kamwe hawatatumia vibaya mamlaka yao hata kama hawana uhakika wa ajira. Hali kadhalika, mishahara midogo haitachochea kupokea hongo iwapo kufanya hivyo uwezekano wa kupoteza kazi unaongezeka sana. Kwa upande mwingine, kupata habari kunaweza kuongeza mishahara, na hivyo kupunguza rushwa; kwa kuwa ulinzi wa umma unapunguza “kuvuja” kwa fedha za kodi kwa rushwa bado fedha nyingi zitabaki kuwalipa watumishi wa umma. Kurudisha imani na uaminifu vilivyotajwa katika aya iliyopita hutokea pia kwa mawakala wa uchumi wa ndani ya serikali na wasio wa serikali. Kwa kutoa fursa kubwa kwa habari ya ndani, asasi kama vile NGO za kimataifa, mabenki ya maendeleo ya mataifa mbalimbali, na wahisani wakubwa huongeza imani zaidi kwa serikali ya Tanzania, kuangilia kwa uhalali zaidi na kuipatia vyanzo vya kupata fedha vya kuendelea, uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja na msaada (TI, Upataji wa Habari – Majadiliano).

Kwa muhtasari, Sheria ya Haki ya Kupata Habari inapambana na rushwa kwa kuwapatia wananchi habari ambayo wanaweza kujitathimini, kugundua matukio ya matumizi mabaya ya mamlaka na kulindwa kama wapasha habari. “Kupata habari ni kama kuzuia rushwa kwa kufungulia vyombo vya habari kutekeleza kazi zao za uchunguzi, kupasha habari upande wa upinzani wa siasa, kuchochea mdahalo wa wazi na kuwapa uwezo asasi za kiraia na watu binafsi kufuatilia bajeti, matumizi na miradi” (U4, Rushwa na Ufumbuzi Wake17). Kuhakikisha haki hii ni hatua nyingine ya busara katika mapambano yanayoendelea dhidi ya rushwa.

7. UtekelezajiHata hivyo kama inavyoonekana kupitia hatua iliyopita ya utungaji sheria za Tanzania, kutunga sera hakutoshi mbele ya rushwa. Kutokana na hali ilivyo, rushwa kubwa ni kupuuza au kukiuka sheria. Ikitokea hivyo, msisitizo haugeukii utungaji sera tu bali utekelezaji. Ni kutokana na sababu hii ndiyo maana Sheria ya Haki ya Kupata Habari inaanzisha Tume ya Habari na Jukwaa la Wadau wa Habari.

16 Chanzo hiki kinaitwa “Transparency International (TI), Access to information” kwenye marejeo.17 Chanzo hiki kinaitwa “U4, Corruption and Possible Cures” kwenye marejeo.

Page 12: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

10

Kama ilivyotajwa hapo juu, Tume ya Habari ni asasi iliyoundwa kuhakikisha kuwa habari zinapatikana. Huratibu vyombo vya umma na binafsi katika uchapishaji wao wa habari, huunda na kusimamia masijala kuu—Masijala ya Habari ya Taifa—kwa habari ile na huwapatia wananchi. Kwa matukio ya kukataliwa kupata habari, Tume ya Habari hupokea malalamiko na kuchunguza sababu. Aidha, huchapisha miongozo na kanuni ili vyombo vya habari, asasi za kiraia na wananchi waelewe Sheria ya Haki ya Kupata Habari na namna ya kuitumia (Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007).

Tume ya Habari inaundwa ili kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, lakini tume yenyewe inalindwaje dhidi ya rushwa? Hili hufanyika kupitia mchakato wa uteuzi wa wajumbe wake. Kwanza,

Tume ya Habari itakuwa na wajumbe tisa, ambao wote watakuwa na utaalamu fulani, kulingana na elimu au uzoefu wao katika habari, sheria, jinsia, vyombo vya habari na maeneo mengine yanayohusika yanayofahamika kwa viwango vya uadilifu, uaminifu, kutopendelea na uwezo.

(Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007, Ibara ya 23 (1))

Mchakato wa uchaguzi wa wajumbe hawa tisa wa Tume, watakaotumikia vipindi viwili vya miaka mitano, hufanywa na Kamati ya Uteuzi, yenye wajumbe wanane mashuhuri wenye uzoefu wa kutetea habari huru na utawala bora. Wajumbe wa Kamati ya Uteuzi ni wateule wanaotoka kila mmoja katika sekta zifuatazo.

1) Wizara yenye dhamana ya sheria na mambo ya katiba2) Baraza la huru la habari lililoanzishwa kibinafsi, la kitaalamu na linalo jitegemea3) Chama cha wamiliki wa vyombo vya habari4) Chama cha waandishi wa habari wataalamu5) Chama cha Wanasheria Tanganyika6) Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG)7) Asasi ya elimu ya juu ya vyombo vya habari8) Asasi ya taifa ya haki za binadamu isiyo ya serikali

(Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007)

Kwa sababu wanatoka kwenye baadhi ya vikundi na asasi zilizochangia katika kuandika Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari na kampeni ya kuridhiwa kwake, wajumbe wa Kamati ya Uteuzi wana shauku na maslahi ya kuijaza Tume ya Habari kwa kuingiza wajumbe watakaotekeleza Sheria ya Haki ya Kupata Habari kwa ukamilifu na bila rushwa.

Kama hatua ya ziada ya usalama, Sheria ya Haki ya Kupata Habari inaanzisha Jukwaa la Wadau wa Habari, kikundi cha asasi za kiraia kinachoangalia mwenendo wa Tume ya Habari. Jukwaa la Wadau wa Habari ni asasi ya kiraia iliyo huru inayojitegemea na iliyoanzishwa binafsi, inajumuisha hasa “baraza la habari lililoanzishwa binafsi la kitaalamu na linalojitegemea na Chama Cha Wamiliki wa vyombo vya habari” lakini liko wazi kwa vikundi vyote vya asasi za kiraia (Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007, Ibara ya 42 (2)). Kwa hiyo, inashauri na kufuatilia Tume ya Habari na kulipatia bunge ripoti kivuli ya mwaka kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari (Pendekezo la Wadau kwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007). Kwa namna hii, uhusiano wa moja kwa moja kati ya watu na Serikali unakuwapo kuhakikisha kwamba Sheria ya Haki ya Kupata Habari inatekelezwa vya kutosha na kwa usahihi.

Page 13: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

11

8. HitimishoKwa kuwa waraka huu ulianza na kunukuu maneno ya Dkt. Sengodo Mvungi akizungumzia “utamaduni wa usiri” unaojenga mazingira mazuri ya rushwa, unamalizia na dondoo la kukumbusha kutoka kwake kuhusu jukumu la kupata habari:

Ni muhimu kujitahadharisha dhidi ya shauku kubwa kuhusu kupitishwa kwa Sheria za Uhuru wa Kupata Habari. Sheria hizi si suluhisho kwa ajili ya mfumo wa utawala wa sheria wenye kuamrisha. Demokrasia ni utamaduni wa kisiasa unaoweka msingi wa namna watu wanavyoishi na kwa hali hiyo haiwezi kushindwa na sheria moja tu. Sheria ya haki ya kupata habari inaweka nguzo moja tu. Bali lazima ivuke mipaka kwa kubatilisha na kurekebisha mamia ya sheria za kimamlaka zinazozuia utolewaji wa habari wakati wa kulinda utamaduni wa usiri wa utawala. (Taasisi ya Habari, 2008)

Usikosee; haki ya kupata habari kwa vyovyote vile siyo “silaha pekee” dhidi ya rushwa. Miswada mingine mingi ya sheria na marekebisho ya sheria zilizopo hivi sasa inapendekezwa kushughulikia suala hili pia (Taasisi ya Habari). Hata hivyo, Sheria ya Haki ya Kupata Habari itaanzisha “nguzo moja” katika mapambano dhidi ya rushwa, na ni kutokana na sababu hii ndiyo maana muswada huu wa sheria ni lazima upitishwe.

Kwa miaka ya hivi karibu, asasi za kiraia kama HakiElimu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umasikini (REPOA) na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) zimefanya utafiti wa kina na kutayarisha ripoti nyingi kuhusu mapambano ya kuendelea wanayoyakabili Watanzania katika kupata habari (Chachage, Kyando na Rajani, 2005; Kirei na Rajani, 2006; Ally, 2007). Waandishi wa NACSAP wanaelewa upungufu huu na wametaja maeneo kama vile uchapishaji wa habari, manunuzi ya umma na kuwalinda wapasha habari kama vipaumbele katika mkakati wao wa kuzuia rushwa (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1999). Pamoja na haya yote, ni wazi kwamba uwezo wa kupata habari hizo unahimizwa na watu katika matabaka yote ya jamii ya Tanzania kuanzia sekta ya kiraia hadi serikali. Kazi iliyo mbele yetu hivi sasa ni kufanikisha malengo kupitia Sheria ya Haki ya Kupata Habari.

Page 14: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

12

MarejeoAlly, B.(2007,Agosti). More access to information in Tanzania? A follow-up study. Dar es Salaam:

HakiElimu. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.hakielimu.org/hakielimu/documents/document93more_access_to_info_en.pdf

Chachage, C., Kyando, N., & Rajani, R. (2005, Agosti). Access to information in Tanzania: Still a challenge: A research report. Dar es Salaam: HakiElimu, LHRC, & REPOA. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.hakielimu.org/hakielimu/documents/document87report_access_info_tz_challenge_en.pdf

Doig, A., & Riley, S. (1998). Corruption and anti-corruption strategies: Issues and case studies from developing countries. Katika G.S. Cheema & J. Bonvin (Eds.), Corruption and Integrity Improvement Initiatives in Developing Countries (kur. 45-62). Paris: OECD. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www .integridadepublica.org.mz/tools/Corrupção%20e%20Estratégias%20Anti-Corrupção.pdf

Fahamu & Article 19. Campaigning for access to information. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.article19.org/pdfs/tools/foi-training-course.pdf

Fjeldstad, O., Ngalewa, E., & Katera, L. (2008, Aprili). Citizens demand tougher action on corruption in Tanzania. Research on Poverty Alleviation, Brief 11. Dar es Salaam: REPOA. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.repoa.or.tz/documents_storage/Publications/Repoa%20Brief%2011%20April%202008.pdf

Freedom House. (2008, Aprili 29). Freedom of the press 2008 – Tanzania. UNHCR Refworld. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.unhcr.org/refworld/docid/4871f63728.html

Global Advice Network. Public anti-corruption initiatives. Business Anti-Corruption Portal. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.business-anti-corruption.com/country-profiles/sub-saharan-africa/tanzania/initiatives/public-anti-corruption-initiatives/

Global Organization of Parliamentarians Against Corruption (GOPAC). (2005, Agosti). Controlling corruption: A parliamentarian’s handbook. World Bank Institute. Ilipatikana Mei 16, 2009, kutoka http://www.gopacnetwork.org/Docs/CCH%20FINAL%20Aug%2005%20ENG.pdf

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (2000). Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977. Dar es Salaam. Ilipatikana Septemba 3, 2009, kutoka http://www.tanzania.go.tz/images/katibamuungano.pdf

Kirei, A., & Rajani, R. (2006, Mei). What can people know? Access to information in Tanzania: Findings of a nationwide opinion poll. Dar es Salaam: HakiElimu & REDET. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.hakielimu.org/hakielimu/documents/document90report_what_can_people_know_en.pdf

Kocaoglu, N., Figari, A., & Darbishire, H. (Eds.). (2006). Using the right to information as an anti-corruption tool. Berlin: Transparency International (TI). Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.transparency.org/content/download/9633/66877/file/TI2006_europe_access_information.pdf

Media Council of Tanzania. (2007). Annual report. Ilipatikana Mei 16, 2009, kutoka http://www.mct.or.tz/PDFFiles/Annual%20Report%202007.pdf

Page 15: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

13

Media Institute. (2008). Are editors doing enough for press freedom? Ilipatikana Mei 16, 2009, kutoka http://eastafricapress.net/index2.php?option=com_content&do_pdf=1&id=209

Moshiro, Gervas. (2008, Oktoba). Mkuchika and the specter of the past. Media Watch, 103, 7, 11. Ilipatikana May 16, 2009, kutoka http://www.mct.or.tz/images/stories/MediaWatch/media%20watch%20october%202008.pdf

Research on Poverty Alleviation (REPOA). (2006, Aprili). Combating corruption in Tanzania: Perception and experience. Afrobarometer, Briefing Paper 33. Cape Town, South Africa: The Institute for Democracy in South Africa. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.repoa.or.tz/documents_storage/Research_Activities/AfrobriefNo33.pdf

Stakeholder’s Proposal for the Right to Information Act, 2007. (2007). Ilipatikana Mei 16, 2009, kutoka http://www.mct.or.tz/images/stories/stakeholders%20proposals%20for%20the%20right%20to%20information%20act%202007.pdf

Taasisi ya Kuzuia Rushwa. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.tanzania.go.tz/pcb

Transparency International (TI). Access to information. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.transparency.org/global_priorities/access_information

Transparency International (TI). Access to information – discussion. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.transparency.org/policy_research/ach/strategies_policies/access_to_information_discussion

Transparency International (TI). (2003). National integrity systems TI country study report Tanzania 2003. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.transparency.org/content/download/7395/45985/file/Tanzania_NIS_Study.pdf

Transparency International (TI). (2008). 2008 corruption perceptions index. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.transparency.org/content/download/36589/575262

U4. Causes & consequences of corruption. U4 Anti-Corruption Resource Centre. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.u4.no/helpdesk/faq/faqs1.cfm

U4. Corruption glossary. U4 Anti-Corruption Resource Centre. Ilipatikana Mei 16, 2009, kutoka http://www.u4.no/document/faqs5.cfm#pettycorruption

U4. Corruption and possible cures: National (local) anti-corruption strategies and policies. U4 Anti-Corruption Resource Centre. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.u4.no/helpdesk/faq/faqs2a.cfm

United Nations Development Programme (UNDP). Frequently asked questions. Asia-Pacific Human Development Report: Tackling Corruption, Transforming Lives: Accelerating Human Development in Asia and the Pacific. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.undprcc.lk/ext/crhdr/FAQ.html

United Republic of Tanzania. (1996, Desemba). Executive Summary Commission Report on the State of Corruption in the Country. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.ipocafrica.org/pdfuploads/EXECUTIVE%20SUMMARY%20COMMISSION%20REPORT%20ON%20THE%20STATE%20OF%20CORRUPTI.pdf

Page 16: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

14

United Republic of Tanzania. (1999, Novemba). The national anti-corruption strategy and action plan for Tanzania. Ilipatikana Aprili 21, 2009, kutoka http://www.ipocafrica.org/pdfuploads/THE%20UNITED%20REPUBLIC%20ANTI-CORRUPTION%20OF%20TANZANIA%20THE%20NATI_003.pdf

Page 17: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa
Page 18: Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa …hakielimu.org/files/publications/Anti-Corruption and... · 2014-05-04 · 1 Toleo la awali la makala haya liliwasilishwa

Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi

HakiElimu imeanzisha Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi (Working Paper Series) kwa lengola kuchapisha upya makala mbalimbali za uchambuzi katika muundo ambao ni rahisi kuwafikia nakusomwa na watu wengi. Mlolongo wa nyaraka hizi unatarajiwa kuchangia katika kujengaufahamu wa jamii na katika mdahalo kuhusu masuala ya elimu na demokrasia.

Mlolongo huu unajumuisha taarifa na makala mbalimbali zilizoandikwa na wafanyakazi na wanachama wa HakiElimu, mashirika na watu binafsi waliokuwa na ubia nasi. Baadhi ya nyaraka hizi zimeandikwa mahsusi kwa ajili ya mlolongo huu, wakati nyingine zinatokana na kazizilizokwisha chapishwa hapo awali. Nyaraka nyingi zilizochapishwa katika mlolongo huu nimakala ambazo uandishi wake bado unaendelea, hivyo hazikukusudiwa kuwa ni nyarakazilizokamilika kabisa.

Maoni yanayotolewa humu ni ya mwandishi (waandishi) mwenyewe na si lazima yaweyanawasilisha maoni ya HakiElimu au taasisi nyingine yoyote. Mawasiliano yote kuhusu makalamahsusi katika mlolongo huu yafanywe moja kwa moja kwa waandishi wake; kwa kadiriinavyowezekana, anuani zao zimeonyeshwa katika tanbihi/rejea chini ya ukurasa wa 1 wa makalahusika.

Nyaraka hizi zinaweza pia kupatikana katika tovuti ya HakiElimu: www.hakielimu.org. Nyarakazote zinaweza kuchapishwa kwa minajili isiyo ya kibiashara baada ya kupata idhini ya maandishi kutoka kwa HakiElimu na mwandishi husika.

Lengo letu ni kuchapisha makala fupi zilizo wazi na bayana na tungependelea zaidi ziwe na urefuwa kati ya kurasa sita hadi kumi na mbili. Hata hivyo, makala zenye urefu wa hadi kurasa ishirinizinaweza kufikiriwa. Tunakaribisha sana makala zenu. Makala hizo ziwasilishwe kwetu zikiwakatika mfumo wa kielektroniki kwa kutumia anuani inayoonyeshwa hapo chini:

HakiElimu

HakiElimu inafanya kazi kuleta usawa, ubora, haki za binadamu na demokrasia katika Elimu, kwakuziwezesha jamii kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa shule, kuwa na ushawishi katika utayarishaji wa sera,

kuhamasisha majadiliano ya kibunifu ya umma kwa lengo la kujiunga pamoja kuleta mabadiliko,kuendesha tafiti zinazohoji na kuchambua mambo kwa kina, kuendesha kampeni za utetezi na

kushirikiana na wabia wengine ili kufikia malengo ya pamoja na kupigania haki ya jamii.

HakiElimu Nyaraka za Kufanyia KaziSLP 79401 • Dar es Salaam • TanzaniaSimu (255 22) 2151852 / 3 • Faksi (255 22) [email protected] • www.hakielimu.org