Upload
others
View
15
Download
0
Embed Size (px)
Citation preview
1
RIPOTI YA KAMATI YA BAJETI
YA BARAZA LAWAWAKILISHI ZANZIBAR
KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019
SEHEMU YA KWANZA
UTANGULIZI
Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi ni miongoni mwa Kamati nane (8) za Kudumu za
Baraza, imeundwa chini ya Kanuni ya 106 ya Kanuni za Baraza, Toleo la mwaka 2016.
Aidha, majukumu yake yametajwa katika Jadweli la kwanza la Kanuni hizo.
MAJUKUMU YA KAMATI YA BAJETI YA BARAZA LA WAWAKILISHI
i. Kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu uandaaji wa mwongozo wa kutayarisha
Mpango na Bajeti ya Serikali kwa kila mwaka.
ii. Kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali.
iii. Kufanya utafiti na uchambuzi kuhusu sera za kodi, sera za fedha na sera za kiuhasibu
zilizopendekezwa na Serikali.
iv. Kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu vyanzo vya mapato ya Serikali, na
mapendekezo ya hatua za kupunguza utegemezi wa kibajeti.
v. Kutoa ushauri wa jumla kuhusu Bajeti ya Serikali kwa Baraza na Kamati za Kudumu
za Baraza.
vi. Kuchambua na kutoa maoni na ushauri kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa
unaopendekezwa na Serikali.
vii. Kuchambua hoja zitakazojitokeza kwenye Kamati za Kudumu za Baraza wakati wa
kujadili Bajeti za Wizara kwa ajili ya kuishauri Serikali.
viii. Kuchambua Mapendekezo ya Jumla ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na
Matumizi.
ix. Kufikiria na kuchunguza Mswada wa Makadirio ya Mapato na matumizi ya mwaka.
2
x. Kuchambua mapendekezo ya Serikali endapo itataka kuwasilisha katika Baraza
Mswada wa Matumizi ya Nyongeza kwa mujibu wa Kanuni ya 101 ya Kanuni za
Baraza.
xi. Kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Kamati yaliyotolewa kwenye Ripoti ya Kamati
ya mwaka uliotangulia na kutathmini taarifa ya Wizara juu ya utekelezaji wa maagizo
hayo na kuwasilisha Barazani maoni ya Kamati kuhusu taarifa hiyo.
MUUNDO WA KAMATI:
Kamati ya Bajeti imeundwa na Wajumbe saba na Makatibu wanne (4) kama ifuatavyo:
1. Mhe. Mohamed Said Mohammed Mwenyekiti
2. Mhe. Bahati Khamis Kombo M/Mwenyekiti
3. Mhe. Mohammedraza Hassanali Mjumbe
4. Mhe. Salha Mohamed Mwinjuma Mjumbe
5. Mhe. Abdalla Ali Kombo Mjumbe
6. Mhe. Asha Abdalla Mussa Mjumbe
7. Mhe. Simai Mohammed Said Mjumbe
8. Ndg. Abdalla Ali Shauri Katibu
9. Ndg. Asha Said Mohamed Katibu
10. Ndg. Kassim Tafana Kassim Katibu
11. Ndg. Shaib Fadhil Shaib Katibu
3
SEHEMU YA PILI
UTEKELEZAJI WA KAZI ZA KAMATI
Kwa mwaka wa Fedha 2018/2019, Kamati ya Bajeti imefanya kazi mizunguko mitatu,
mzunguko wa kwanza ulianzia tarehe 20/08/2018 hadi tarehe 31/08/2018 ambapo Kamati
ilifanya kazi Unguja na katika mzunguko wa pili, pia Kamati ilifanya kazi Unguja kuanzia
tarehe 05/11/2018 hadi tarehe 13/11/2018 na kwa Dar es Salaam ilifanya kazi kuanzia tarehe
14/11/2018 hadi tarehe 16/11/2018. Aidha, katika mzunguko wa tatu Kamati ilifanya kazi
Unguja kuanzia tarehe 14/01/2019 hadi tarehe 25/01/2019.
Kamati katika kutekeleza majukumu yake ilikutana na Wizara na Taasisi mbali mbali za
Serikali, Wadau na kufanya vikao na Wawekezaji wa Sekta ya Utalii na Hoteli, wazalishaji
wa vinywaji visivyo na kilevi na baadhi ya wafanyabiashara. Lengo la vikao hivyo ni kujadili
mambo yanayohusiana na uwekezaji, biashara, mfumo wa kodi na kupata maoni yao katika
kuimarisha maeneo hayo na hata kusaidia kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Afisi kwa kushirikiana na Kamati, ilizingatia suala la kuwapatia mafunzo wajumbe kwa
lengo la kuwajengea uwezo na kukuza uelewa mpana wa mambo mbali mbali. Hivyo, Kamati
pamoja na mambo mengine, ilipata fursa ya mafunzo yanayohusiana na uchambuzi wa Deni
la Taifa, uchambuzi wa mswada wa fedha na kodi na Mafunzo kuhusiana na Uandaaji,
Uchambuzi na Usimamizi wa Bajeti kwa Mfumo wa Programu (PBB).
MAENEO YALIYOFANYIWA KAZI NA KAMATI YA BAJETI
1. Kupokea taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha Januari –
Februari 2017/2018, Aprili – Juni 2017/2018, Julai – Septemba, 2018/2019 na
Octoba – Disemba, 2018/2019.
2. Mamlaka ya Kuendeleza Viwanda vidogo vidogo na vya kati (Small and Medium
Industrial Development Authority – SMIDA)
3. Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amaan Karume ( Terminal III)
4. Kiwanda cha Sukari – Mahonda
5. Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar
(ZPRA)
6. Mahkama Kuu – Zanzibar
4
7. Mradi wa Mahkama Kuu - Tunguu
8. Eneo la Kuhifadhia Mafuta na Gesi na Ujenzi wa Bandari ukanda wa Mangapwani –
Bumbwini
9. Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri
10. Mradi wa Kiwanda cha Kuzalisha Maziwa – Fumba
11. Ziara ya Kamati ya Bajeti Tanzania bara
12. Shirika la Bima - Zanzibar
13. Shirika la Umeme - Zanzibar
14. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF)
15. Kikao cha Pamoja Baina ya Kamati na Wafanyabiashara
16. Kikao cha Pamoja Baina ya Kamati na Wawekezaji wa Sekta ya Utalii na Mahoteli
17. Kikao cha Pamoja Baina ya Kamati na Wawekezaji wa Viwanda vya Vinywaji
Visivyo na Kilevi.
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI ROBO YA TATU
(JANUARI – FEBRUARI 2017/2018)
Mapato
Kwa kipindi cha Januari - Februari, 2017/2018, Serikali ilipanga kukusanya jumla ya TZS
122.351 bilioni kutokana na vianzio vya ndani ambapo ZRB ilikadiriwa kukusanya TZS
64.980 bilioni, TRA TZS 42.803 bilioni, mapato yasiyo ya kodi TZS 11.068 bilioni na PAYE
TZS 3.3 bilioni. Aidha, Serikali ilikadiria kupokea jumla ya TZS 13.005 bilioni kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo.
Katika kipindi hichi, utekelezaji halisi kwa Januari – Febuari, 2017/2018, kwa upande wa
mapato ya ndani yalifikia TZS 125.930 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 103 ya makadirio
yaliyopangwa. Jumla ya TZS 30.121 bilioni zilipokelewa kutoka kwa washirika wa
maendeleo.
Matumizi
Kwa upande wa matumizi katika kipindi cha Januari - Febuari, 2017/2018, Serikali ilikadiria
TZS 133.328 bilioni, ambapo TZS 117.114 bilioni ni matumizi ya kawaida na TZS 16.214
bilioni ni matumizi kwa kazi za maendeleo. Aidha, fedha kwa miradi iliyochangiwa na
washirika wa maendeleo ilikadiriwa kuwa TZS 28.208 bilioni.
Utekelezaji halisi kwa upande wa matumizi kwa kipindi Januari – Febuari, 2017/2018 ulifikia
TZS 141.685 bilioni ya makadirio yaliyopangwa.
5
Deni la Taifa
Kuhusiana na deni la taifa, hadi kufikia Febuari, 2019 deni lilifikia TZS 444.480 bilioni
lilojumuisha deni la ndani TZS 162.870 bilioni na deni la nje ni TZS 281.610 bilioni. Sababu
za kuongezeka kwa deni la ndani ni pamoja na kuongezeka kwa madeni ya wazabuni, mkopo
wa hati fungani na kuongezeka kwa madeni ya kiinua mgongo. Kwa upande wa deni la nje,
miongoni mwa sababu za kuongezeka kwake ni kutokana na kushuka kwa thamani ya
shilingi ya Tanzania.
TATHMINI YA KAMATI JUU YA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA
SERIKALI KWA KIPINDI CHA (JANUARI-FEBRUARI) 2017/2018)
1. Kwa kipindi cha Januari – Febuari 2017/2018, mapato ya Serikali yameongezeka na
kupindukia lengo la makadirio na kufikia TZS 125.930 bilioni ambazo ni sawa na
asilimia 103 ya makadirio yaliyopangwa. Hali hii inaonesha ishara nzuri katika
jitihada za kukuza mapato ya Serikali na kupunguza utegemezi wa Bajeti kutoka kwa
washirika wa maendeleo.
2. Deni la taifa limeendelea kukua siku hadi siku licha ya Kamati kuarifiwa kuwa Deni
hilo ni himilivu. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa Febuari 2018 deni
liliongezeka hadi kufikia jumla ya TZS 444.5 bilioni ikilinganishwa na deni la TZS
374.6 bilioni la mwezi wa Februari mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 18.
3. Kwa kipindi cha miezi miwili Januari – Febuari, 2017/2018, jumla ya TZS 141.68
zimetumika. Matumizi haya ni makubwa ukilinganisha na mapato halisi
yaliyokusanywa katika kipindi hicho ambayo ni TZS 125.93 bilioni.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa Serikali ina vyanzo mbali mbali vya mapato na ina uwezo wa kufanya
matumizi kwa mujibu wa programu na miradi iliyojipangia kwa kipindi husika cha
mwaka wa fedha, Kamati inaishauri Serikali iweke mkazo zaidi katika kudhibiti
uvujaji wa mapato kwa kuzingatia kuwa, matumizi yanayofanyika ni kwa mujibu wa
malengo na mapato yaliyopo.
2. Pamoja na uhimilivu wa Deni la Taifa kama Kamati ilivyoelezwa, Kamati inaishauri
Serikali ihakikishe deni hilo haliongezeki kwa kasi na kuathiri mwenendo wa uchumi.
Aidha, taarifa za deni la taifa zipatikane kwa wakati kwa vyombo husika ikiwemo
Benki Kuu ya Tanzania tawi Zanzibar ili vyombo hivyo viwe na taarifa sawa.
6
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI ROBO YA NNE
(APRILI – JUNI 2017/2018)
Kamati ya Bajeti ilipokea taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha Aprili –
Juni 2017/2018, ambapo kwa kipindi hicho Kamati iliarifiwa kwamba Serikali ilikadiria
kukusanya jumla ya TZS 183.9 bilioni ikijumuisha TZS 160.8 bilioni kutoka vyanzo vya
ndani, TZS 9.6 bilioni mapato kutoka nje na 13.5 bilioni ni gawio la faida kutoka Benki Kuu
ya Tanzania. Makusanyo halisi kwa kipindi cha miezi mitatu (Aprili – Juni ) ni TZS 224.5
bilioni ambazo ni sawa na asilimia 122 ya matarajio, ikijumuisha makusanyo ya ndani
yaliyofikia Tsh 167.6 bilioni na mapato mengineyo TZS 56.9 bilioni ikiwemo gawio la faida
kutoka Benki Kuu TZS 13.5 bilioni na mapato kutoka nje Tsh 43.4 bilioni.
Kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2017/18, matumizi halisi yalifikia jumla ya
TZS 222.6 bilioni, yakijumuisha matumizi ya vyanzo vya ndani ya jumla ya TZS 186.8
bilioni na TZS 35.8 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo. Ikilinganishwa na kipindi
kama hicho mwaka 2016/17 kumejitokeza ongezeko la matumizi la asilimia 36 kutoka TZS
164.3 bilioni. Kati ya matumizi hayo, TZS 153.2 bilioni zimetumika kwa matumizi ya
kawaida sawa na asilimia 93 ya lengo.
Deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 26 kutoka TZS 405.5 bilioni kwa kipindi cha Aprili
Juni 2016/2017 hadi kufikia TZS 512.5 Aprili –Juni 2017/2018.
Mfumko wa Bei kwa nchi za Afrika Mashariki.
Kasi ya mfumko wa bei kwa nchi za kwa nchi za Afrika Mashariki ulipungua na kufikia
wastani wa asilimia 2.2 kwa kipindi cha Aprili – Juni, 2018 ikilinganishwa na kipindi kama
hicho kwa mwaka 2017 ambapo kasi ya mfumko wa bei ilikuwa 9.1. Kwa mujibu wa
takwimu, nchi iliyoripotiwa kuwa na kasi ndogo ya mfumko wa bei ni Rwanda ambapo
ulifikia wastani wa asilimia 1.4 mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa 9.4 kwa kipindi
2017.
Utalii
Katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2018, idadi ya watalii imeongezeka kwa wastani
wa asilimia 26.8 na kufikia watalii 76,304 ikilinganishwa na watalii 60,158 kwa kipindi cha
April – Juni, 2017.
7
TATHMINI YA KAMATI JUU YA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA
SERIKALI ROBO YA NNE (APRIL – JUNI 2017/2018)
Kamati ilichambua na kutathmini taarifa ya Bajeti kwa kipindi cha Aprili – Juni 2017/2018
na miongoni mwa mambo ya msingi ambayo Kamati imeyabaini katika taarifa hiyo ni kama
ifuatavyo:
1. Katika robo ya nne ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, upatikanaji wa fedha za
misaada ya kibajeti pamoja na mikopo kutoka kwa wafadhili uliridhisha na hivyo
kusaidia sana utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambazo ni msingi muhimu katika
ukuaji wa Uchumi.
2. Baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Rwanda zimeweza kudhibiti kwa kiasi
kikubwa mfumko wa bei kutokana na kuimarisha uzalishaji wake wa ndani.
3. Kamati imepata changamoto ya kutojua taarifa za fedha halisi zinazotokana na
shughuli za Utalii, ambapo licha ya idadi ya watalii kuongezeka, Kamati hukosa
taarifa za fedha zinazoongezeka katika sekta ya utalii kutokana na ongezeko la idadi
ya watalii hao.
4. Deni la Taifa limeendelea kuongezeka kwa kasi licha ya Kamati kuarifiwa kwamba
deni hilo ni himilivu. Kamati imegundua ongezeko la deni la taifa haliendi sambamba
na ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Ili kukabiliana na tatizo la kupanda kwa mfumko wa bei hususan wa bidhaa za
chakula na athari zake kiuchumi, Kamati inaishauri Serikali kuongeza juhudi katika
kuimarisha uzalishaji wa ndani ili kudhibiti kasi ya mfumko huo.
2. Kutokana na kutofahamika thamani halisi ya fedha zinazotokana na ongezeko la
watalii, Kamati inaishauri Serikali kutafuta mfumo utakaowezesha kujua thamani
halisi ya fedha inayotokana na sekta ya utalii ili kusaidia katika kutathmini na kuweka
mikakati ya kuikuza zaidi sekta hiyo pamoja na kutoa taswira halisi ya mchango wa
sekta hiyo katika uchumi wa Zanzibar.
3. Kutokana na kasi kubwa ya kuongezeka deni la taifa, Kamati inaishauri Serikali
iweke mikakati ya kupunguza kasi ya ukuaji wa deni hilo kwa kuimarisha mapato ya
8
ndani na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo uliotokana na fedha
za mikopo unakwenda kwa mujibu wa malengo na muda uliokusudiwa.
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA KIPINDI CHA
ROBO YA KWANZA (JULAI –SEPTEMBA 2018/2019)
Kamati ya Bajeti ilipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi
cha robo ya kwanza (Julai – Septemba 2018/2019) ambayo ilijumuisha taarifa ya mwenendo
wa Uchumi wa Zanzibar, mwenendo wa uchumi wa dunia na kanda, ukusanyaji wa mapato
ya Serikali na matumizi pamoja na taarifa kuhusu deni la taifa.
Mapato
Serikali ilipanga kukusanya jumla ya TZS 222.5 bilioni, TZS 189.5 bilioni kutokana na
mapato ya ndani na TZS 33.0 bilioni kutokana na mapato ya nje. Aidha katika ukusanyaji
halisi Serikali ilifanikiwa kukusanya jumla ya TZS 196.1 bilioni sawa na asilimia 88 ya
matarajio ya kukusanya TZS 222.5 bilioni. Makusanyo hayo yalijumuisha fedha kutoka
makusanyo ya ndani ya TZS 176.6 bilioni, mapato mengineyo ya TZS 19.5 bilioni na
mapato kutoka nje TZS 19.5 bilioni. Kwa ujumla mapato yameonekana kukuwa kwa asilimia
13 kwa kulinganisha na TZS 173 bilioni zilizokusanywa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka
2017/2018.
Matumizi
Serikali ilitumia jumla ya TZS 222.5 bilioni zilizojumuisha matumizi ya vianzio vya ndani
yaliyofikia TZS 199.6 bilioni na TZS 22.8 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Matumizi hayo yote ni sawa na ongezeko la asilimia 25 ya matumizi halisi ya TZS 177.5
bilioni katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2017/2018.
Mfumko wa Bei
Mfumko wa bei kwa nchi washirika wa biashara na Zanzibar kama China, India na UAE
katika kipindi cha Julai – Septemba, 2017 umepanda kutoka asilimia 2 hadi kufikia wastani
wa asilimia 3.3 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2018. Kwa upande wa Zanzibar
mfumko wa bei za chakula ulishuka hadi kufikia asilimia 3.5 kulinganisha na mfumko wa bei
wa asilimia 5.9 kwa mwezi Septemba kwa mwaka 2017. Hali hii ilitokana na kushuka kwa
bidhaa za chakula kama vile unga wa mahindi, samaki, ndizi mbichi na sukari. Aidha kwa
upande wa bidhaa zisizo za chakula mfumko wa bei umepanda hadi kufikia asilimia 6.1
kulikotokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa za nishati ya mafuta na saruji.
9
Deni la Taifa
Deni la taifa hadi kufikia mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2018/2019 limerikodiwa
kuwa ni TZS 469.6 bilioni ambazo ni sawa na ongezeo la asilimia 17 ikilinganishwa na deni
la TZS 401.6 bilioni lililoripotiwa katika kipindi kama hicho katika mwaka 2017/18.
TATHMINI YA KAMATI JUU YA TAARIFA YA UTEKELZAJI WA BAJETI YA
SERIKALI KWA KIPINDI CHA ROBO YA KWANZA (JULAI –SEPTEMBA
2018/2019)
1. Pamoja na kuimarika kwa uchumi wa dunia na Afrika ya Mashariki kwa sababu mbali
mbali ikiwa ni pamoja na ukuaji wa viwanda na usarifu wa mazao. Kwa upande wa
Zanzibar pamoja na kuripotiwa kuimarika kwa shughuli za uchumi na kupelekea
kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kwa robo ya kwanza na ya pili
kulinganisha na ukuaji wa robo kama hiyo kwa mwaka 2017, wawekezaji wengi wa
sekta ya viwanda wanalalamikia mazingira magumu ya uwekezaji katika sekta hiyo
kutokana na kuzorota kwa uzalishaji na kukosekana soko la bidhaa za Zanzibar kwa
upande wa Tanzania Bara.
2. Kwa mujibu wa malengo ya Mkuza III mfumko wa bei Zanzibar unaonekana kuvuka
malengo ya mpango huo ambao umekadiria ifikapo mwaka 2020 kuwa na mfumko
wa bei wa asilimia 5%1.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kutokana na kupanda kwa kasi ya mfumko wa bei katika nchi washirika wa biashara
na Zanzibar kama China, UAE na India, Kamati inaishauri Serikali kupanua wigo wa
kibiashara kwa kufungua milango ya kibiashara kwa nchi nyengine, kwa lengo la
kupunguza athari za mfumko wa bei unaotokana na nchi washirika.
2. Kamati inaisisitiza Serikali kuendelea kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha za
umma katika miradi mikubwa ya kitaifa ambayo isiposimamiwa vyema itapelekea
kuzorota kwa uchumi wa nchi pamoja na kuongeza mzigo wa deni la taifa.
1 Zanzibar Strategy for Growth and Reduction of Poverty III, 2016-2020, pg. 79
10
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI ROBO YA PILI
(OKTOBA – DISEMBA 2018/2019).
Kamati ya Bajeti katika kutekeleza majukumu yake ilipokea taarifa ya utekelezaji wa bajeti
kwa robo ya pili (Oktoba-Disemba) 2018/19, iliyohusisha mwenendo wa hali ya uchumi,
utekelezaji wa mpango wa maendeleo na utekelezaji wa Bajeti.
Mapato
Kwa kipindi cha Oktoba - Disemba, 2018/19, Serikali ilipanga kukusanya jumla ya TZS
241.8 bilioni. Kati ya fedha hizo, TZS 198.7 bilioni mapato ya ndani na TZS 43.1 bilioni
mapato ya nje. Ukusanyaji halisi wa mapato ulifikia TZS 281.8 bilioni sawa na asilimia 117
ya matarajio ya makusanyo ambapo makusanyo ya ndani yalifikia TZS 190.1 bilioni na TZS
91.7 bilioni mapato ya nje.
Matumizi
Kwa kipindi cha Oktoba – Disemba, 2018 Serikali ilikadiria kufanya matumizi jumla ya TZS
188.7 bilioni kwa kazi za kawaida na TZS 82.6 bilioni kwa kazi za maendeleo. Matumizi
halisi yalifikia jumla ya TZS 290 bilioni ambapo jumla ya TZS 207.6 bilioni kutoka vianzio
vya ndani na TZS 82.4 bilioni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo
Kupitia Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/19, jumla ya programu 27 na miradi 55
ilitegemewa kutekelezwa. Kwa kipindi cha Oktoba – Disemba, 2018 jumla ya TZS 155.5
bilioni zilipangwa kugharamia programu na miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo TZS
39.5 bilioni zilipangwa kutoka Serikalini na TZS 116.02 bilioni zilipangwa kutoka kwa
washirika wa maendeleo. Hadi kufikia Disemba 2018, jumla ya TZS 97.6 bilioni sawa na
asilimia 63 zilipatikana kugharamia programu na miradi ya maendeleo.
Ukuaji wa Pato la Taifa
Kamati ilielezwa kuwa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa imara ambapo kwa mwaka
2017 ulifikia wastani wa asilimia 7.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.8 kwa mwaka
2016. Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani ya nchi wa bidhaa na
huduma. Sekta zilizochangia katika ukuaji huo ni Sekta ya Kilimo, Viwanda na Huduma.
11
Mfumko wa Bei
Kwa mwaka wa 2018, kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na huduma ulishuka na kufikia
wastani wa asilimia 3.9 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2017. Hali hii
ilitokana na kushuka kwa mfumko wa bei za bidhaa za chakula ambapo kwa mwaka 2018
ulifikia asilimia 1.4 ikinganishwa na asilimia 5.5 kwa mwaka 2017.
Kwa upande wa bidhaa zisizo za chakula nazo ziliendelea kushuka kidogo. Takwimu
zinaonesha kuwa, kwa mwaka 2018 mfumko wa bei zisizo za chakula zilifikia asilimia 5.7
ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2017.
Utalii
Katika kipindi cha Oktoba – Disemba 2018, Sekta ya Utalii iliendelea kufanya vizuri na
kupelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka watalii 130,945 katika
kipindi cha mwaka 2017 na kufikia watalii 142,337 kwa mwaka 2018. Kamati iliarifiwa
kuwa, miongoni mwa sababu zilizopelekea ongezeko hilo ni pamoja na kuwepo kwa vivutio
vya watalii kama vile matamasha ya sanaa na utamaduni na kuwepo kwa ndege za moja kwa
moja za kuwaleta watalii nchini.
Thamani ya Shilingi
Kwa kipindi cha mwaka 2018 Shilingi ya Tanzania ilibadilishwa na dola ya kimarekani kwa
wastani wa TZS 2,264 ikilinganishwa na wastani wa TZS 2,229 katika kipindi kama hicho
kwa mwaka 2017. Takwimu hizo zinaonesha kuwa Shilingi ya Tanzania ilishuka thamani
kidogo dhidi ya dola ya Kimarekani.
Mwenendo wa Sekta za Kibenki
Kamati ilielezwa kuwa, kwa kipindi cha Oktoba - Disemba 2018, sekta za kibenki
zimeendelea kufanya vizuri na kumekuwa na ongezeko la kuweka akiba kutoka kwa wateja
uliofikia TZS 847.8 bilioni ikilinganishwa na TZS 737.6 bilioni kwa kipindi kama hicho kwa
mwaka 2017, na pia ongezeko la mikopo kwenda kwa wateja wake binafsi na
wafanyabiashara. Kufanya vizuri kwa sekta za kibenki kumetokana na kuongezeka na
kukuwa kwa shughuli za kiuchumi.
Sekta za Nje
Katika kipindi cha Oktoba – Disemba 2018, Kamati iliarifiwa juu ya kuongezeka kwa
uagiziaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi na kupelekea nakisi kufikia jumla ya TZS 20.6
12
bilioni (Januari – Juni) 2018 ikilinganishwa na nakisi ya TZS 11 bilioni mwaka 2017.
Ongezeko la nakisi hiyo limetokana na usafirishaji mdogo wa karafuu ambapo ununuzi wa
zao hilo umepungua na kufikia tani 54.6 zenye thamani ya TZS 262.8 milioni mwaka 2018
kutoka tani 5790.7 zenye thamani ya TZS 80,697.6 milioni katika kipindi cha mwaka 2017.
Deni la Taifa
Kwa kipindi cha Oktoba – Disemba 2018/19, Deni la taifa limeripotiwa kufikia TZS 779.0
bilioni sawa na ongezeko la asilimia 99 ukilinganisha na deni la TZS 391.8 bilioni
lililoripotiwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2017/18.
TATHMINI YA KAMATI JUU YA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA
SERIKALI KWA ROBO YA PILI (OKTOBA – DISEMBA 2018/2019)
1. Kwa kipindi cha Januari – Juni, 2018 uchumi wa Zanzibar uliendelea kuimarika
ambapo sekta zilizochangia katika ukuaji huo ni pamoja sekta ya viwanda asilimia
(16.9), mawasiliano (10.4), fedha na bima (9.1), ujenzi (49.8) na sekta ya uchimbaji
mawe na mchanga (16.7).
2. Kamati imebaini kushuka kwa kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na huduma kwa
mwaka 2018 sambamba na kushuka kidogo kwa bidhaa zisizo za chakula.
3. Kamati imebaini kuongezeka kwa miradi mipya (14) kwa kipindi cha 2018/19 licha
ya kuwa na idadi kubwa ya miradi (41) ya zamani ambayo Serikali inatakiwa
kuendeleza utekelezaji wake.
4. Kamati imebaini ongezeko kubwa la Deni la Taifa ambapo limefikia TZS 779.0
bilioni sawa na ongezeko la asilimia 99 ikilinganishwa na deni la TZS 391.8 bilioni
liloripotiwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2017/18.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa takwimu zinaonesha uchumi wa Zanzibar uliendelea kuimarika ambapo
kwa mwaka 2017 ukauaji wa pato la taifa ulifikia wastani wa asilimia 7.7
ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.8 kwa mwaka 2016, katika kuhakikisha kuwa
ukuaji huu unamnufaisha mwananchi moja kwa moja , Kamati inaishauri Serikali,
pamoja na kutumia pato la taifa kuwa ni kipimo cha maendeleo, ihakikishe inapanga
sera za uchumi na kijamii zinazoweza kupima maendeleo na ustawi wa watu wengi
katika jamii kwa kuangalia mabadiliko yaliyopo katika jamii.
13
2. Kwa kipindi cha Januari - Juni 2018, Kamati imebaini mafanikio ya kiuchumi
yaliyochangiwa na sekta ya viwanda (16.9), mawasiliano (10.4), fedha na bima (9.1),
ujenzi (49.8) na sekta ya uchimbaji mawe na mchanga (16.7). Licha ya mafanikio ya
kiuchumi yaliyofikiwa kupitia sekta mbali mbali, Kamati inaishauri Serikali
kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi na kuwa na takwimu za mchango wao katika
uchumi kwani sekta binafsi ina mchango mkubwa na muhimu katika kuinua uchumi
wa nchi.
3. Kamati inaishauri Serikali kuandaa mikakati madhubuti katika kudhibiti bei za bidhaa
na huduma ambazo zitazingatia maslahi ya mfanyabiashara pamoja na mtumiaji bila
ya kumkandamiza yeyote.
4. Kwa kipindi cha Oktoba – Disemba, 2018, Kamati imebaini ongezeko la mapato,
matumizi na deni la taifa. Katika kuhakikisha kuwa ongezeko la mapato, matumizi na
deni la taifa vinakuwa na tija katika ustawi wa nchi, Kamati inaishauri Serikali
kuhakikisha kuwa, matumizi yanayofanywa yanakwenda sambamba na malengo ya
bajeti kama yalivyoidhinishwa na kuhakikisha kuwa fedha zinazotokana na mikopo
zinatumika vyema ili kuondokana na mzigo wa madeni kwa vizazi vya sasa na
vijavyo.
MAMLAKA YA KUENDELEZA VIWANDA VIDOGO VIDOGO NA VYA KATI
(SMALL AND MEDIUM INDUSTRIAL DEVELOPMENT AUTHORITY – SMIDA)
Kuwepo kwa viwanda vya aina mbali mbali katika nchi ni moja wapo ya njia muhimu za
kuchochea uchumi wa nchi. Uzoefu unaonesha kuwa nchi nyingi ambazo zimejiimarisha
katika viwanda zimepiga hatua kubwa za maendeleo. Umuhimu wa viwanda unadhihirika
kwa wananchi kutokana na faida zinazotokana na viwanda hivyo, ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa bei nafuu zaidi badala ya kuagiza bidhaa hizo kutoka
nchi za nje. Aidha, viwanda ni kichocheo muhimu katika upatikanaji wa ajira kwa wananchi.
Serikali katika kuhakikisha kuwa inaendeleza viwanda ikiwa ni moja wapo ya hatua ya
utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020 (vision 2020) ya
kuwawekea mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo na
wa kati (Micro, Small and Medium Enterprises – MSMEs) imeanzisha Mamlaka ya
Kuendeleza Viwanda Vidogo Vidogo na vya Kati (SMIDA).
14
Miradi midogo midogo ya wajasiriamali inachukuwa nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa
Zanzibar. Katika kufanikisha maendeleo ya miradi ya wajasiriamali wadogo wadogo, uzoefu
unaonesha kuwa, sekta ya viwanda inahitaji uratibu na usimamizi mzuri kwa ajili ya kusaidia
ukuajia endelevu wa sekta hiyo pamoja na kutoa nafasi za ajira ambazo zitachangia katika
ukuaji wa uchumi.
CHANGAMOTO ZA MAMLAKA YA KUENDELEZA VIWANDA VIDOGO
VIDOGO NA VYA KATI
1. Fedha ni changamoto kubwa ya Mamlaka katika kufikia malengo ya utekelezaji wa
majukumu yake kutokana na ukweli kwamba Sheria ya kuanzisha Mamlaka,
haikuweka vianzio vya mapato na hivyo kupelekea Mamlaka kuitegemea Serikali
moja kwa moja kama chanzo kikuu cha fedha.
2. Kamati imebaini Mamlaka ina upungufu wa wafanyakazi katika nyanja za ufundi,
utawala, masoko, fedha na biashara.
3. Miongoni mwa malengo ya Mamlaka ni kuwa na eneo lisilopungua hekta nne kwa
ajili ya shughuli za viwanda vidogo vidogo na vya kati katika kila Wilaya ya
Zanzibar, katika kulifikia lengo hilo, Mamlaka inahitaji kutafuta na kubainisha
maeneo kwa Wilaya zote, hata hivyo hadi Kamati ilipotembelea Mamlaka hiyo,
maeneo hayo bado hayajapatikana.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa lengo la kutekeleza
majukumu yake kama yalivyokusudiwa, Mamlaka Viwanda Vidogo vidogo inatakiwa
kubuni na kufikiria vianzio vyengine vya mapato ikiwa ni pamoja na kuanzisha
mahusiano na taasisi za nje ya nchi ambazo zitakuwa na majukumu yanayofanana na
Mamlaka, ambapo kupitia mahusiano hayo Mamlaka inaweza kupata fursa za ufadhili
pamoja na kupata uzowefu wa kazi.
2. Kamati inaisisitiza Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda juu
ya upatikanaji wa wafanya kazi katika nyaja mbali mbali ili ujuzi wa wafanyakazi hao
utumike katika kutekeleza kazi za Mamlaka.
3. Kwa kuwa hatua za awali zinasisitiza upatikaji wa ardhi kwa eneo lisilopungua hekta
nne kwa ajili ya shughuli za viwanda vidogo vidogo katika kila Wilaya za Zanzibar,
15
Kamati inaisisitiza, Mamlaka itatafute maeneo yenye uhakika na yasiyo na migogoro
ili shughuli za viwanda vidogo vidogo ziweze kufanyika kwa ufanisi.
MRADI WA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA ABEID AMAAN KARUME
(TERMINAL III)
Kamati katika utekelezaji wa majukumu yake, ilitembelea mradi wa ujenzi wa uwanja wa
ndege wa Abeid Amaan Karume (terminal III) ulioanza utekelezaji wake tokea Julai, 2010
ambapo Mkataba wa Ujenzi huo ulikuwa Baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji na Kampuni ya Beijing Construction
Engineering Group (BCEG) ya China uliotiwa saini mwaka 2009 ukigharimu jumla ya USD
70.4 milioni zilizotolewa na Benki ya Exim ya China kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo.
Mradi huo unakabiliwa na changamoto mbali mbali na lengo la Kamati kufanya ziara ya
mradi ni kuzifahamu changamoto hizo na kuishauri Serikali ipasavyo katika kuzitafutia
ufumbuzi.
CHANGAMOTO ZA MRADI WA UWANJA WA NDEGE WA ABEID AMAAN
KARUME (TERMINAL III)
1. Kutokusainiwa kwa mkataba wa fedha (Financing Agreement) kwa ajili ya fedha za
ziada USD 58 milioni. Licha ya kuwa rasimu ya mkataba huo tayari
imeshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango ya Tanzania lakini rasimu hiyo
haijasainiwa mpaka muda ambao Kamati ilikuwa inafanya kazi. Miongoni mwa
sababu zilizopelekea kutokusainiwa kwa rasimu hiyo ni Kamati ya Kitaifa ya
Uidhinishaji wa Mikopo kutokubali baadhi ya masharti, hali inayoweza kupelekea
kusimama tena kwa kazi za ujenzi.
2. Kamati inapata wasiwasi juu ya aina ya mikataba ambayo Serikali inaingia na
wakandarasi hasa panapotokea kasoro za utekelezaji wa mradi husika na kupelekea
kuongezeka kwa gharama au kukwama kwa mradi, kama ilivyotokea katika ujenzi wa
Terminal III ambapo Serikali iliamua kuendelea na kampuni hiyo hiyo bila ya
kufanya maamuzi ya kutoendelea na kampuni hiyo ambayo imesababisha kasoro
katika utekelezaji wa mradi huo.
16
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa mkataba wa fedha za ziada wa ujenzi wa Terminal III haujasainiwa na
kutosainiwa kwake kunaweza kuleta athari kubwa katika utekelezaji wa mradi,
Kamati inaishauri Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji wa Mikopo,
kuendelea kufuatilia na kuhakikisha kuwa mkataba huo unasainiwa kwa haraka ili
kazi za ujenzi ziendelee kama zilivyokusudiwa.
2. Kamati inaishauri Serikali kuwa na usimamizi madhubuti wa maeneo ya ardhi ikiwa
ni pamoja na kuyatambua mapema maeneo yanayotarajiwa kuekezwa miradi ili
kuepukana na gharama za kulipa fidia wananchi wanaojenga katika sehemu hizo.
3. Kamati inaishauri Serikali kuwa makini na mikataba wanayoingia na wakadarasi
pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia kuwa
fedha za miradi hiyo ni za mikopo na kutokufanikisha utekelezaji wake ni hasara kwa
nchi.
KIWANDA CHA SUKARI MAHONDA
Mnamo mwaka 1965, Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na mashirika, ilianzisha Shirika
la Sukari na Manukato kupitia Kiwanda cha Sukari - Mahonda kwa ajili ya uzalishaji wa
sukari, manukato na vinywaji vikali, kufuatia makubaliano ya kibiashara (The Trade
Agreement) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya watu wa
China. Ujenzi wa kiwanda hichi na utayarishaji wa mashamba yaliyokuwa na ukubwa wa
ekari 6529.23 katika maeneo ya Kitope - Mahonda, Chechele, Panga Tupu na Upenja ulianza
rasmin mnamo mwaka 1971 na kiwanda kilianza uzalishaji mwaka 1973 chini ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa mkopo kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Kamati ilipata fursa ya kutembelea Kiwanda cha Sukari - Mahonda na kuona marekebisho
makubwa yaliyofanywa ikiwa ni pamoja na kufungwa mashine mpya inayotumia teknolojia
ya kisasa kwa lengo la kuongeza uzalishaji kutoka kukamua tani 400 za miwa kwa siku hadi
kufikia tani 800 mpaka tani 1250 kwa siku. Marekebisho hayo yamefanya uwekezaji katika
kiwanda hicho kufika dola za kimarekani milioni 35. Kwa ujumla mpaka Kamati ilipofanya
ziara, kiwanda kilikuwa katika hali nzuri kimiundo mbinu na vifaa.
17
CHANGAMOTO ZA KIWANDA CHA SUKARI MAHONDA
1. Ardhi iliyopo ni finyu kwa ajili ya upandaji wa miwa, Kamati iliarifiwa kiwanda kina
ekari 3,900 tu ambazo zinatumika na kuvunwa miwa kati ya ekari 10,000 ambazo ni
mahitaji halisi ya kiwanda hicho. Changamoto hii ni ya muda mrefu na imewahi
kutolewa agizo na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
kuwa, kiwanda kipatiwe ekari 3,000 kama mkataba wa kiwanda hicho unavyoelekeza
na mahitaji kwa ujumla, lakini mpaka Kamati inafanya ziara katika kiwanda cha
Mahonda ni ekari 732 ndio zimekabidhiwa.
2. Kukosa kibali cha kuuza sukari inayozalishwa katika Kiwanda cha Sukari Mahonda
kwa upande wa Tanzania bara. Kutokana na ufinyu wa soko na bei ya sukari
inayozalishwa Mahonda, Kiwanda kinaendelea kuuza sukari Zanzibar pekee
kinakisababishia hasara ya shillingi 387,000 kwa kila tani moja ya sukari. Licha ya
jitihada mbali mbali bado kiwanda hakijafanikiwa kupata kibali cha kuingia katika
soko la Tanzania Bara ambako kuna bei nzuri itakayokiwezesha kiwanda kurudisha
gharama za uzalishaji.
3. Kuwepo kwa kodi kubwa ya ardhi ambapo kwa mwaka kiwanda cha sukari Mahonda
kinalipa TZS 670,000 (300 USD) kwa kila ekari moja, ambayo ni kubwa mno
ikilinganishwa na kodi ya ardhi kwa upande wa Tanzania bara ambayo ni TZS 5,000
tu kwa ekari kwa mwaka. Kimsingi kodi hii ya ardhi inaongeza gharama za uzalishaji
wa kiwanda.
4. Kutokuwepo kwa barabara zinazopitika wakati wote kuwafikia wakulima wengi zaidi
hasa wakati wa mavuno ya miwa hali inayopelekea gharama kubwa zaidi za
uendeshaji kuanzia uandaaji wa shamba mpaka uvunaji. Licha ya kiwanda kuwa na
mashamba yake, kimeanzisha mpango wa kuwatumia wakulima wa nje wa miwa
(out-growers scheme) kutoka maeneo mbali mbali kwa ajili ya kununua miwa kupitia
kilimo cha mkataba.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kamati inaishauri Serikali kuharakisha utaratibu wa upatikanaji wa eneo la ardhi
lenye ukubwa wa ekari 2268 kati ya ekari 3000 zilizoagizwa kupewa kiwanda na
Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kuwa
18
kutopatikana kwa eneo hilo la ardhi kunapelekea kiwanda kuzalisha chini ya uwezo
kutokana na kukosekana miwa ya kutosha.
2. Kamati inaishauri Wizara ya Biashara na Viwanda, kwa kushirikiana na Uongozi wa
Kiwanda cha Sukari Mahonda kuifuatilia kwa ukaribu na kuitafutia ufumbuzi
changamoto ya Kiwanda cha Sukari - Mahonda ya kukosa kibali cha kuuza sukari
Tanzania bara.
3. Kwa kuwa Kamati imeelezwa kuwa kiwanda cha sukari Mahonda hakina unafuu wa
kodi wala ruzuku ya aina yoyote kutoka Serikalini, inayokiwezesha kuzalisha kwa
gharama nafuu, Kamati inaishauri Serikali kuandaa utaratibu maalum wa kuweka
unafuu wa kodi au ruzuku kwa lengo la kukisaidia Kiwanda cha Sukari na
kuwahamasisha wawekezaji wengine wa viwanda kuwekeza Zanzibar.
MAMLAKA YA UDHIBITI WA UTAFUTAJI NA UCHIMBAJI WA MAFUTA NA
GESI ASILIA ZANZIBAR (ZPRA)
Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar
imeanzishwa chini ya Sheria namba ya 6 ya mwaka 2016 (Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji
Mafuta na Gesi Asilia) ikiwa na majukumu ya msingi ya kufuatilia na kudhibiti utafutaji na
uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, kuishauri Serikali juu ya mpango unaowasilishwa na
mkandarasi juu ya zoezi zima la uendelezaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu,
uzalishaji na ukomo wa shughuli za mafuta na gesi pamoja na kuhakikisha wadau wote
wanafuata Sheria za Zanzibar na mikataba ya mafuta na gesi asilia.
CHANGAMOTO ZA MAMLAKA YA UDHIBITI WA UTAFUTAJI NA UCHIMBAJI
WA MAFUTA NA GESI ASILIA ZANZIBAR (ZPRA)
1. Mamlaka inakabiliwa na uharibifu wa vifaa vya utafiti kwa ajili ya kupata taarifa za
mtetemo unaofanywa na baadhi ya wananchi na kuufanya utafiti huo kuwa wa
gharama zaidi.
2. Mamlaka inakabiliwa na ufinyu wa vifaa vya ofisini na vitendea kazi vyengine kama
gari kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli zake za nje ya ofisi, ambapo mpaka Kamati
inapokea taarifa hii, iliarifiwa kuwa Mamlaka ina gari moja tu ambayo haikidhi haja
kwa shughuli zake.
19
3. Uhaba wa wafanyakazi hususan wataalam waliobobea katika sekta ya utafutaji na
uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ambazo ni shughuli za msingi za Mamlaka.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa mkataba juu ya utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi umeshatiwa
saini, Kamati inaisisitiza Mamlaka kuongeza umakini katika kusimamia mkataba huo
ili kuhakikisha zoezi la utafutaji na uchimbaji wa mafuta linafanyika kwa ufanisi.
2. Kwa kuwa Kamati imearifiwa kuwa, Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na
Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar imeshaundwa na tayari imeshaanza
kazi, Kamati inaishauri Mamlaka iharakishe zoezi la uajiri wa wafanyakazi ili kukidhi
mahitaji ya Mamlaka.
MAHKAMA KUU - ZANZIBAR
Kamati ilifanya ziara katika ofisi za Mahkma Kuu ya Zanzibar - Vuga na kupokea taarifa ya
utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
CHANGAMOTO ZA MAHKAMA KUU
1. Kamati imebaini kukosekana kwa hati miliki za baadhi ya majengo ya Mahkma
Zanzibar ikiwa ni pamoja na jengo la Mahkama Kuu - Vuga na Mahkama ya
Mfenesini hali ambayo inaweza ikasababisha matatizo iwapo majengo hayo yatahitaji
kufidiwa au iwapo kutajitokeza migogoro katika umiliki.
2. Kuchakaa kwa majengo mengi ya mahkama kwa upande wa Unguja na Pemba,
ambapo Kamati imeelezwa kuwa, kwa upande wa Pemba Mahkama ya Wete na
Chake Chake zipo katika hali mbaya. Aidha, kwa upande wa Unguja, majengo ya
Mahkama ya Mfenesini na Mkokotoni nayo yapo katika hali mbaya na yanahitaji
kufanyiwa ukarabati wa haraka.
3. Ufinyu wa bajeti ya Mahkama isiyokwenda sambamba na wingi wa taasisi za
mahkama katika ngazi za wilaya na mkoa.
4. Kukosekana kwa Ofisi ya Tume ya Mahkama na ukumbi kwa ajili ya uendeshaji wa
shughuli zake.
20
5. Kamati imeleezwa kuwa, Tume ya Mahkama haina watendaji ambao wangesaidia
katika utekelezaji wa shughuli zake. Hali hii imesababishwa na Tume hiyo kutokuwa
na fungu la fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake.
6. Upungufu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na uchache wa vitabu vya kusomea na
kufanya rejea, vyombo vya usafiri na samani za ofisi kama viti na meza.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa majengo mengi ya Serikali hayana hati miliki, Kamati inaishauri Serikali
kuandaa mkakati maalum wa kuhakikisha majengo yote ya Serikali yanakuwa na hati
miliki kwa lengo la kuhakikisha majengo hayo yanaendelea kuwa chini ya umiliki wa
Serikali na kuepusha athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kukosekana kwa hati
miliki hizo.
2. Kamati inaishauri Mahkama katika kukabiliana na changamoto ya uchache wa vitabu,
kuanza kutumia mfumo wa maktaba za kielectroniki (e - library ) ambao ni mfumo wa
kisasa na unanufaisha watu wengi.
3. Kwa bajeti ya mwaka 2019/2020, Kamati inaishauri Mahkama kuongeza fedha
zinazotengwa kwa ajili ya Tume ya Mahkama ili kutatua changamoto ya upungufu wa
wafanyakazi na ofisi.
4. Kamati inaishauri Wizara ya Fedha na Mipango, kwa kushirikiana na Mahkama,
kuangalia namna ya kutatua changamoto ya ufinyu wa bajeti kwa Mahkama ili
kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa ufanisi zaidi.
MRADI WA MAHKAMA KUU - TUNGUU
Kamati ilitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa jengo jipya na la kisasa
la Mahkama Kuu Zanzibar unaotarajiwa kutekelezwa kupitia fedha za SMZ. Mradi huu
ulianza rasmini katika mwaka wa fedha 2016/17 chini ya Wizara ya Nchi, Afisi ya Raisi,
Katiba, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mnamo tarehe 19 Juni, 2017, Wizara hiyo
iliingia mkataba na Kampuni ya Landmark Consultant Ltd na kuanza kazi ya kushauri juu ya
ujenzi huo ambapo TZS 100 Milioni zilitengwa.
Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Mradi huo ulihamishiwa Mahkama Kuu ambapo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitenga TZS 900 Milioni na katika mwaka huo wa fedha
21
jumla ya TZS 500 milioni zilipatikana kwa ajili ya maandalizi ya kuanza utekelezaji wa
mradi huo.
CHANGAMOTO ZA MRADI WA MAHKAMA KUU TUNGUU
1. Kusuasua kwa ujenzi wa Mahkama Kuu - Tunguu ambao awali ulitarajiwa
kukamilika mwaka 2020. Ujenzi huu unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa
hati ya eneo la mradi na uhamishwaji wa usimamizi wa mradi kutoka taasisi tofauti.
Kamati iliarifiwa kwamba, awali mradi huo ulikuwa ukisimamiwa na Wizara ya Nchi,
Afisi ya Rais, Katiba, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na baadae ukahamishiwa
Mahkama Kuu, kwa mwaka wa fedha (2018/19) mradi huu fedha zake zimeingizwa
katika Wizara ya Fedha na Mipango kupitia fungu la Ujenzi wa Ofisi za Serikali.
2. Kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri baina Mahkama Kuu, Wizara ya Nchi, Afisi ya
Rais, Katiba, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati kulikopelekea mradi huo kukumbwa na changamoto ya kutopatikana
hati ya kiwanja kutokana na utanuzi wa barabara unaotarajiwa kufanywa na Idara ya
Barabara, hali iliyopelekea hati ya mwanzo kutofaa kwasababu ya kupungua eneo la
mradi kwa takribani mita 75.
3. Changamoto ya mkataba ambao awali ulifungwa baina ya Afisi ya Rais, Katiba,
Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mshauri elekezi, kwa sasa mradi huo
unasimamiwa na Mahkama Kuu, hivyo kunakosekana nguvu ya moja kwa moja kwa
Mahkama kumuwajibisha mshauri elekezi iwapo kutatokea kasoro katika utekelezaji
wa mradi huo.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kamati haijaridhishwa na mwenendo wa mradi wa Mahkama Kuu Tunguu pamoja na
utaratibu wa uidhinishaji wa fedha za mradi huo ambazo zimekuwa zikihamishwa
katika mafungu (vote) tofauti, iliyopelekea kutokuwepo kwa ufanisi wa mradi.
Kamati inashauri fedha zilizotengwa za mradi ziingizwe katika fungu la Mahkama
kwa kuwa ndio wasimamizi wa mradi huo.
2. Kutokana changamoto ya utanuzi wa barabara uliopelekea eneo la mradi wa
Mahkama Kuu kupunguwa, Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha kunakuwepo kwa
mawasiliano na mashirikiano wakati wa uandaaji na utekelezaji wa miradi, ili
22
kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kuepuka gharama zisizo na
msingi.
3. Kamati inaishauri Serikali kuifanyia kazi changamoto ya kimkataba inayopelekea
usimamizi usio na ufanisi wa mradi wa ujenzi wa Mahkama Kuu ili kuondoa
changamoto hiyo na hatimae kuukamilisha mradi huo kwa ufanisi.
ENEO LA KUHIFADHIA MAFUTA NA GESI NA UJENZI WA BANDARI
UKANDA WA MANGAPWANI - BUMBWINI
Kutokana na umuhimu wa Nishati ya Mafuta na Gesi, Kamati ilitembelea Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) yenye jukumu la kudhibiti huduma za maji
na nishati Zanzibar. Kamati ilipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka na
kufanya ziara katika eneo la kuhifadhia mafuta na gesi Mangapwani – Bumbwini.
Katika eneo hili lenye upana wa mita 400 kutoka ufukweni kuelekea nchi kavu limetengwa
kwa ajili ya kujengwa miundombinu itakayotumiwa na taasisi za Serikali zinazohusiana na
nishati ya mafuta na gesi na eneo jengine lenye upana wa mita 200 limepangwa kwa ajili
matumizi ya wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi.
CHANGAMOTO ZA ENEO LA KUHIFADHIA MAFUTA NA GESI
1. Kumekuwepo kwa baadhi ya wawekezaji wenye biashara za masuala ya mafuta na
gesi ambao wameonesha nia ya kutaka kupanua uwekezaji wao kwa kuanzisha
biashara nyengine katika eneo hilo ambazo hazina uhusiano na shughuli zilizopangwa
katika eneo hilo.
2. Kutokuwepo kwa udhibiti wa bei za gesi baina ya Zanzibar na Tanzania bara hali
inayopelekea wawekezaji wa Zanzibar kununua gesi Tanzania bara kwa bei ya juu
zaidi na kushindwa kuhimili ushindani wa kibiashara na kupanda kwa bei ya gesi
kwa wananchi.
3. Kusitishwa kwa zoezi la ulipaji fidia ya mazao (vipando) vya wananchi katika eneo la
mradi kutokana na viwango vidogo vya malipo ya fidia vilivyoelekezwa katika
Kanuni ya Mazao ya Mwaka 2013 ambayo inatokana na utekelezaji wa kifungu cha
100(1) (f) cha Sheria ya Usimamizi na Uhifadhi wa Rasilimali za Misitu Nam. 10 ya
mwaka 1996.
23
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa Serikali ina nia ya kuwahamisha wawekezaji katika eneo la Mangapwani,
Kamati inaishauri Serikali iharakishe kuwatafutia eneo jengine la kuendeleza
uwekezaji wao kwa lengo la kuunga mkono jitihada za wawekezaji wazalendo.
Aidha, kwa sasa Kamati inaishauri Serikali iwaruhusu wawekezaji hao kuendelea na
shughuli zao mpaka itakapokuwa tayari kulitumia eneo hilo.
2. Kamati inaishauri Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati ya Zanzibar
(ZURA) itafute namna ya kuwasaidia wafanya biashara wa gesi Zanzibar kwa
kufanya mashauriano na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati ya Tanzania bara
(EWURA) juu ya utaratibu mzuri zaidi wa kibiashara ambao utawadhibiti
wafanyabiashara hiyo katika upangaji wa bei kwa lengo la kuimarisha huduma ya
upatikanaji wa gesi baina ya Zanzibar na Tanzania bara na kuepusha upandaji wa bei
ya gesi kiholela.
3. Kamati inaishauri Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
kufanya marekebisho ya Kanuni ya Mazao ya Mwaka 2013 ambayo inatokana na
utekelezaji wa kifungu cha 100(1) (f) cha Sheria ya Usimamizi na Uhifadhi wa
Rasilimali za Misitu Nam. 10 ya 1996, ili iendane na thamani halisi ya mazao
(vipando) na kuiwezesha Serikali kutoa fidia ili wananchi waondoke katika sehemu
ya utekelezaji wa mradi.
MRADI WA UJENZI WA BANDARI YA MPIGA DURI
Mradi wa Bandari ya Mpigaduri unatarajiwa kujengwa katika eneo la Maruhubi Mjini
Zanzibar kwa mfumo wa ubia kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya
“China Harbor Engineering Company LTD (CHEC)”. Mradi huo unatarajiwa kugharimu
jumla ya Dola za Kimarekani 231,400,000 kati ya fedha hizo Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itatoa jumla ya USD 200,000,000 kupitia mkopo wa Benki ya China – Exim Bank
na Kampuni ya China Harbor Engineering Company Ltd itatoa jumla ya Dola za Kimarekani
31,400,000. Mkataba wa ujenzi huo ulitiwa saini mwaka 2014 kati ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na Kampuni ya CHEC.
24
CHANGAMOTO ZA MRADI WA UJENZI WA BANDARI YA MPIGA DURI
1. Changamoto kubwa ya mradi huu ni kutokufanyiwa kazi kwa rasimu ya Mkataba
wa fedha (Drafting Finance Agreement) ambayo inapaswa kupitiwa na kupatiwa
maoni na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili Mkataba
halisi uweze kusainiwa. Kamati ilifuatilia suala hili Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Kitaifa ya uidhinishaji wa Mikopo na
iliarifiwa kuwa, suala hilo bado halijafanyiwa kazi na badala yake Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetakiwa kupeleka tena upembuzi yakinifu
(Feasibility Study) ili mradi upitiwe kwa mara nyengine.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Ili kupata maelezo juu ya changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa fedha za Mradi
wa Bandari ya Mpiga Duri, Kamati ilifanya ziara maalum ya kufuatilia suala hili
Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano ambapo Kamati ilipata taarifa
tofauti na taarifa ambazo ilizipata Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na
Usafirishaji. Hivyo, Kamati inaamini kuwa hakuna uwazi katika kutoa taarifa za
baadhi ya miradi ya Serikali.
MRADI WA KIWANDA CHA KUZALISHA MAZIWA FUMBA
Kiwanda kilianza kuzalisha bidhaa ya maziwa mwaka 2014. Uwezo wa kiwanda ni kuzalisha
maziwa lita 180,000 kwa siku, lakini kutokana na changamoto ya soko kiwanda kinazalisha
maziwa wastani wa lita 22,000 mpaka 25,000 kwa siku. Uzalishaji wa kiwanda kwa kiasi
kikubwa unategemea soko la Tanzania Bara kwani kwa upande wa Zanzibar mahitaji ya
maziwa kwa siku kwa mujibu wa takwimu za kiwanda hicho ni chini ya lita 5000.
Kiwanda kina jumla ya wafanyakazi 70 ikijumuisha wataalamu na wafanyakazi wengine wa
kawaida. Kamati ilifanya ziara katika kiwanda hicho ili kujua changamoto zinazokikabili na
kwa lengo la kuishauri Serikali namna bora ya kukisaidia, ili kiweze kuzalisha kwa faida na
kusaidia katika kujenga uchumi wa nchi.
CHANGAMOTO ZA KIWANDA CHA MAZIWA - FUMBA
1. Malighafi ya kutengenezea maziwa inaagizwa kutoka nje ya nchi kutokana na kuwa
maziwa yanayozalishwa Zanzibar hayako katika kiwango na ubora unaohitajika.
25
2. Kiwanda kinategemea soko la Tanzania bara lakini kutokana na kupanda kwa kodi ya
mifugo kupitia “The Animal Disease Act (CAP 156)”, Kiwanda kinalazimika kulipia
kodi ya TZS 2000/= kwa kila kilo moja ya unga wa maziwa unaoingizwa nchini. Kwa
Sheria hiyo Zanzibar inahesabika kama nchi ya kigeni. Hivyo, kiwanda kimeshindwa
kumudu gharama hizo na kulazimika kutoendelea kuzalisha bidhaa tokea Julai, 2018.
3. Wafanyakazi wa kiwanda hawana uhakika na ajira zao kutokana na hali ya kiwanda
kusuwa suwa katika uendeshaji wake. Kiwanda kimesitisha baadhi ya wafanyakazi
wake kuhudhuria kazini tokea mwezi wa Juni 2018, kutokana na changamoto ya
kupanda kwa kodi ya maziwa kwa bidhaa zinazopelekwa Tanzania bara. Licha ya
kuwepo kwa tatizo hilo, kiwanda bado kinaendelea kuwalipa wafanyakazi wake
gharama za mshahara kwa wafanyakazi wote ambao unafikia wastani wa TZS 30
milioni mpaka TZS 40 milioni kwa mwezi.
4. Kutokana na kuwepo kwa kodi ya mifugo inayochangia kuzidisha gharama za
uendeshaji, Kiwanda kimepunguza stahiki za wafanyakazi ikiwemo posho la usafiri,
chakula na malazi.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa soko kubwa la maziwa ya kiwanda cha Fumba lipo Tanzania bara na kwa
sasa soko hilo limeanguka kutokana na kupanda kwa bei ya maziwa kulikochangiwa
na kupandishwa kodi, Kamati inaishauri Serikali kuchukua juhudi ya kuweka sera
ambazo zitalinda bidhaa zinazozalishwa Zanzibar ili kuhimili hali ya ushindani wa
soko.
2. Kutokana na kusita kwa uzalishaji wa kiwanda, Serikali itakosa mapato mengi
yanayotokana na kodi inayolipwa na kiwanda hicho ambayo ni zaidi ya milioni mia
tatu kwa mwaka. Kamati inaishauri Serikali kuleta mipango madhubuti ya kukinusuru
kiwanda ili kiweze kuendelea na uzalishaji.
3. Changamoto za soko kwa wawekezaji wa viwanda Zanzibar ambayo inaathiri
uwekezaji nchini na kuwavunja moyo wawekezaji wapya, kwa kuwa miongoni mwa
vivutio vikubwa vya uwekezaji ni pamoja na soko la uhakika na sheria rafiki kwa
wawekezaji.
26
ZIARA YA KAMATI YA BAJETI TANZANIA BARA
Kamati ilifanya ziara ya kikazi Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania tarehe 15/11/2018 hadi tarehe 16/11/2018. Katika ziara hiyo, Kamati ilionana na
Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo (National Debt Management Committee) pamoja
na kutembelea Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Kamati iliambatana na
baadhi ya Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Wizara ya Fedha na Mipango
Zanzibar, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar pamoja na Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Zanzibar.
Lengo la ziara ilikuwa ni kujifunza namna Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo
(National Debt Management Committee) inavyofanya kazi na kupata maelezo juu ya
changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa fedha za mikopo kwa ajili ya Miradi ya
Zanzibar ambayo fedha zake zina dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania .
Kamati pia ilijifunza mfumo wa uendeshaji na mgawanyo wa Mapato ya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) pamoja na kukagua Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa
Ndege “Terminal III”, kuona namna Mamlaka hiyo ilivyofanikiwa katika usimamizi na
uendeshaji wa Mradi huo, hasa ikizingatiwa kwamba Mradi kama huo unatekelezwa Zanzibar
na ambao unakabiliwa na changamoto za ujenzi na upatikanaji wa fedha.
KAMATI YA KITAIFA YA UIDHINISHAJI MIKOPO
Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo imeundwa kwa Mujibu wa Sheria ya Mikopo,
Dhamana na Ruzuku za Serikali ya mwaka 1974. Ambapo Wajumbe wake ni pamoja na:-
1. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango SMT Mwenyekiti
2. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango SMZ Mjumbe
3. Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu SMT Mjumbe
4. Katibu Mkuu Afisi ya Makamo wa Rais SMT Mjumbe
5. Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje SMT Mjumbe
6. Katibu Mtendaji Tume ya Mipango SMT Mjumbe
7. Katibu Mtendaji Tume ya Mipango SMZ Mjumbe
8. Mwanasheria Mkuu SMT Mjumbe
9. Mwanasheria Mkuu SMZ Mjumbe
27
10. Gavana Benki Kuu Tanzania Mjumbe
11. Mhasibu Mkuu SMT Mjumbe
12. Mhasibu Mkuu SMZ Mjumbe
13. Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo Tanzania Mjumbe
(TIB- Development Bank)
Mbali na Kamati hiyo pia kuna Watendaji “Secretariat” wa Kamati ya Wataalamu (Technical
Debt Managemenet Committee - TDMC) ambayo hufanya uchambuzi wa awali, kabla
kuwasilisha uchambuzi wao kwa Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo. Kamati ya
Wataalamu inaongozwa na Kamishna wa Sera na Madeni ambae ndie Mwenyekiti.
MAMBO YALIYOBAINIKA KATIKA KIKAO NA KAMATI YA KITAIFA YA
UIDHINISHAJI MIKOPO
1. Kamati iliarifiwa kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar
mara nyingi huwa hahudhurii vikao vya Kamati hiyo yeye mwenyewe na mara nyingi
huwakilishwa na watendaji wengine.
2. Kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo,
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano hawezi
kuwakilishwa na mtu mwengine, hivyo asipokuwepo kikao hakiwezi kufanyika.
3. Kamati hufanya vikao vinne vya kawaida kwa mwaka, hata hivyo kwa mwaka
2017/2018 imefanya zaidi ya vikao 14 vya dharura.
4. Jukumu la msingi la Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo ni kumshauri Waziri
wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuukubali au kuukataa
mkopo na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya mikopo iliyoidhinishwa.
5. Miongoni mwa sababu zinazochelewesha kupatikana kwa fedha za mikopo ya miradi
ni mchakato wa kina unaofanywa na Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo ili
kujiridhisha kwa kupata taarifa sahihi za wakopeshaji, masharti ya mkopo na ubora
wa mkopo husika.
6. Sababu zilizopelekea kuchelewa kwa fedha za Mkopo wa Mradi wa jengo la Abiria la
Uwanja wa Ndege Zanzibar ni Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo kutokubali
masharti ya kuchanganya mkataba wa mkopo na madai ya Kiwanda cha Urafiki
pamoja na kuwekwa dhamana ya mkopo kwa baadhi ya mali za Serikali. Hata hivyo,
28
Kamati ya Bajeti iliarifiwa kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ameshatowa maoni yake kuhusu kuondolewa kwa vipengele
hivyo na tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshawaandikia
wakopeshaji.
7. Kwa upande wa Mradi wa Barabara ya Wete-Chake Chake sababu za msingi
zilizokwamisha ni Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo kutokubaliana na
masharti ya Mkataba wa Mkopo huo ambayo yanahusiana na uwekaji dhamana wa
mali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Licha ya Serikali kutoridhika
na masharti,wakopeshaji hawajakubali kuyaondosha masharti hayo. Kwa sasa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inajaribu kutumia njia mbadala za kidiplomasia
(Diplomacy negotiations) ili kufikia muwafaka wa jambo hilo.
8. Kuhusu Mradi wa Bandari ya Mpiga Duri, licha ya kuwa Mradi huo ni wa siku
nyingi, bado upo katika hatua za awali, kwani Kamati ya Bajeti imearifiwa kuwa
Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo ndio kwanza imeomba kupatiwa nyaraka
za Upembuzi yakinifu (Feasibility study) wa Mradi huo ili upitiwe tena upya, hali
ambayo inaweza kupelekea mradi huo kuchukua muda mrefu zaidi.
MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA
Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria (TB III) ni mwendelezo wa upanuzi wa
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambacho kilianzishwa
mwaka 1956. Mradi wa upanuzi ulianza mwaka 2013 ambapo hadi sasa umefikia asilimia
85 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2019.
MAMBO YALIYOBAINIKA WAKATI WA ZIARA YA MAMLAKA YA VIWANJA
VYA NDEGE
1. Pamoja na ukweli kwamba Mradi wa uwanja wa ndege wa Tanzania Bara ni mkubwa
na umeanza mwisho ukilinganishwa na mradi kama huo kwa upande wa Zanzibar,
mradi huo uko katika hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
2. Sehemu ya Mapato ya Mamlaka ya Uwanja wa Ndege inayotokana na kodi ya Abiria
(Passengers Services Charge) inarejeshwa Mamlaka, tofauti na ilivyo kwa Mamlaka
ya Uwanja wa Ndege Zanzibar ambapo mapato hayo yote yanakwenda Serikalini.
29
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kamati ya Bajeti haikuridhishwa na Kitendo cha Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha na Mipango Zanzibar, kutohudhuria mara kwa mara vikao vya Kamati
ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo (National Debt Management Committee),
hasa kwa kuzingatia uzito wa vikao hivyo na nafasi yake katika Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
2. Kamati ya Bajeti imeshagazwa na taarifa kwamba wapo Wajumbe wa
Zanzibar wanaoshiriki vikao katika Kamati ya Kitaifa ya Uidhinishaji Mikopo,
ambao walipaswa kujua changamoto zinazokwamisha uidhinishwaji wa Fedha
za mikopo za miradi ya Zanzibar, ingawaje Kamati imekuwa inakosa taarifa
hizo kila mara wakati inapohoji sababu zinazopelekea kukwama kwa mikopo
ya Miradi hiyo.
3. Kamati ya Bajeti haijaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu ufuatiliaji wa fedha za Mradi wa Bandari ya
Mpiga Duri, kutokana na kuarifiwa kwamba, Kamati ya Kitaifa ya
Uidhinishaji Mikopo ipo katika hatua ya kupitia upya upembuzi yakinifu wa
Mradi huo, licha ya taarifa ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
Zanzibar kuonesha kuwa hatua za awali za mradi huo zimeshakamilika.
SHIRIKA LA BIMA LA ZANZIBAR
Shirika la Bima la Zanzibar ni miongoni mwa mashirika yanayomilikiwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia100. Shirika lilianzishwa mwaka 1969 na linafanya kazi
chini ya Sheria ya Mitaji ya Umma Namb. 4 ya 2002. Malengo Makuu ya Shirika la Bima la
Zanzibar ni pamoja na kutoa huduma zote kwa wananchi na kuwekeza katika miradi mbali
mbali.
Kamati katika kutekeleza majukumu yake ilifanya ziara Afisi za Shirika la Bima na kupokea
taarifa ya Shirika hilo kuhusu mafanikio na changamoto tokea kuanzishwa kwake pamoja na
mchango wake katika Bajeti ya Serikali. Aidha, Kamati ilitaka kujua mkakati unaotumiwa na
Shirika hilo katika kukabiliana na ushindani wa soko la Bima. Kamati iliarifiwa kuwa,
miongoni mwa mafanikio ya msingi ya Shirika hilo ni pamoja na kulipa gawio Serikalini kwa
mujibu wa viwango ambavyo Shirika linapangiwa, kuongeza mtandao wa Afisi zake
30
Zanzibar na Tanzania bara, kuekeza katika benki ambazo zina viwango vizuri vya riba,
kukodisha majengo yake, kulipa madai halali na kwa haraka na kujenga imani kwa wateja.
Huduma zinazotolewa na Shirika la Bima la Zanzibar
Miongoni mwa huduma zinazotolewa na Shirika la Bima la Zanzibar ni pamoja na bima ya
magari, bima ya moto, bima ya ajali, bima ya wizi, bima kwa ajili ya wataalamu
(Professional Indemnity), bima ya vyombo vya usafiri wa anga na majini (Marine and
Aviation) pamoja na kukinga madhara yanayosababishwa na matumizi ya bidhaa au
matumizi ya huduma (Public liability)
Uwekezaji wa Shirika la Bima
Shirika limeendelea kufanya uwekezaji katika maeneo mbali mbali ikiwemo uwekezaji wa
fedha katika mabenki (Fixed deposit) pamoja na uwekezaji katika ofisi zake ambazo
zimekodishwa kwa watu mbali mbali. Aidha, baadhi ya fedha za Shirika huwekezwa katika
huduma za hawala za Serikali (Treasury bill) za Benki Kuu kupitia minada ya kila wiki.
CHANGAMOTO ZA SHIRIKA LA BIMA
1. Kuongezeka kwa ushindani wa biashara ya bima ambapo makampuni binafsi
yanatumia mbinu mbali mbali katika kukuza biashara, ikiwemo mbinu za kurahisisha
kufanya malipo ya fidia kwa haraka zaidi ikilinganishwa na kampuni ya Serikali
ambazo hufanya malipo baada ya uchunguzi wa kina ambao huchukua muda.
2. Kuongezeka kwa ajali za magari kunakopelekea Shirika kulipa madai mengi na
makubwa
3. Ukosefu wa umiliki wa majengo ya ofisi zote yanayotumiwa na Shirika la Bima
Tanzania bara ambapo Shirika hulazimika kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kodi
ambazo zinaongezeka mwaka hadi mwaka.
4. Shirika linashindwa kuongeza maslahi ya wafanyakazi wake kutokana na kulazimika
kufuata muongozo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa viwango vya maslahi ya
watumishi. Licha ya kuwa Shirika linatoa huduma Tanzania nzima na pia lina ofisi
Tanzania bara, ambapo linakabiliwa na mazingira ya ushindani wa biashara kutoka
katika makampuni mengine, viwango vya mishahara ya Shirika hili ni vidogo
ikilinganishwa na mashirika mengine binafsi, jambo ambalo linapunguza ari kwa
watendaji na baadhi yao kufikiria kulihama Shirika.
31
5. Shirika linaongozwa na Sheria ya Utumishi wa Umma ya Zanzibar Sheria Nam. 2 ya
2011 ambapo kutokana na masharti yaliyomo kwenye sheria hiyo, kipaumbele cha
ajira kimewekwa kwa Wazanzibari. Hivyo inakuwa kikwazo kwa Shirika kufanya
uajiri wa kudumu wa wafanyakazi kwa upande wa Tanzania Bara ambapo Shirika
mara nyingi limekuwa likifanya uajiri wa muda.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kutokana na changamoto ya ushindani wa soko inayolikabili Shirika la Bima la
Zanzibar, Kamati inaishauri Serikali iweke mazingatio maalum katika muongozo
unaotolewa wa viwango vya mishahara kwa Taasisi za Serikali, kwa kuruhusu
kuongeza viwango vya maslahi ya wafanyakazi wa Shirika la Bima pamoja na
mashirika mengine ambayo yanatowa huduma kwa Tanzania nzima, ili mashirika
hayo yaweze kuhimili ushindani wa soko la ajira na kuhamasisha wafanyakazi wa
Shirika kufanya kazi kwa ari na ufanisi zaidi.
2. Kwa kuwa Sheria ya Utumishi wa Umma Nam. 2 ya 2011, imeweka kipaumbele
katika ajira kwa Wazanzibari, Kamati inaishauri Serikali kuifanyia mapitio na kuweka
mazingatio maalum ya uajiri kwa Mashirika ya Serikali yanayotoa huduma Tanzania
bara na kuyawezesha kuajiri wataalamu hususani kwa upande wa Tanzania bara
ambao watalisaidia Shirika katika kuendelea kutoa huduma bora.
3. Kamati imeridhishwa na mafanikio yaliyopatikana na Shirika la Bima la Zanzibar,
kutokana na Shirika hilo kujiendesha kwa faida na kuchangia vizuri gawio la Serikali
(dividend). Pamoja na mafanikio hayo, Kamati inalishauri Shirika kuendelea kuweka
mikakati imara zaidi itakayoliwezesha Shirika kukabiliana na ushindani wa soko
hususani upande wa Tanzania Bara ambako kuna kampuni nyingi zinazotoa huduma
za Bima.
4. Kamati inalishauri Shirika la Bima la Zanzibar kuendelea kutoa elimu kwa wananchi
juu ya taratibu na Sheria za Bima ili kuepusha migogoro na kukosa imani kwa
wananchi hao kutokana na kukosa elimu ya taratibu hizo, hususani pale mteja
anapokosa fidia ya madai yake kama alivyotarajia.
5. Kamati inaitaka Serikali ilitumie Shirika la Bima la Zanzibar, kwa kuhakikisha
inayakatia bima majengo ya Serikali pamoja na miradi yake yote. Aidha, katika
32
kutanua wigo wa soko, Kamati inalishauri Shirika kuzihamasisha Taasisi za Serikali
kutumia huduma za Shirika hilo.
6. Kamati inaishauri Serikali katika mikataba ya miradi ya ujenzi itakayoingia izingatie
kuweka kipengele cha Bima (Insurance Clause), ili kupata fidia endapo litatokea
tatizo katika utekezaji wa miradi hiyo.
SHIRIKA LA UMEME ZANZIBAR (ZECO)
Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) limeanzishwa kwa Sheria Nam. 3 ya mwaka 2006 na
linamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya usimamizi wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati. Shirika lina jumla ya wafanyakazi 758, kati ya wafanyakazi
hao, 582 kutoka Unguja na 176 kwa upande wa Pemba. Shirika katika utendaji wake wa kazi
linasimamiwa na Meneja Mkuu chini ya maelekezo ya Bodi ya Wakurugenzi.
Kazi kuu za Shirika ni kuzalisha na kusafirisha umeme, kusambaza na kuuza umeme katika
visiwa vya Unguja na Pemba. Katika kutekeleza kazi ya usambazaji umeme, Shirika
limeweza kusambaza huduma ya umeme vijiji 2,694 vya Unguja na Pemba sawa na asilimia
83 ya vijiji vya Zanzibar.
CHANGAMOTO ZA SHIRIKA LA UMEME LA ZANZIBAR (ZECO)
1. Ongezeko la madeni kwa Taasisi za Serikali ambapo Shirika linazidai Taasisi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jumla ya TZS 26.556 Bilioni na TZS 2.219 bilioni
kwa Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ongezeko la madeni
hayo, linaathiri sana mapato na gharama za uendeshaji wa Shirika.
2. Shirika linakabiliwa na deni linalodaiwa na TANESCO ambapo Shirika linaendelea
kufanya malipo ya deni hilo lililotokana na malimbikizo ya Ankara za ununuzi wa
umeme kutoka TANESCO.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kwa kuwa ongezeko la madeni kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) linaathiri
sana mapato na hata uendeshaji wa Shirika hilo, Kamati katika kukabiliana na hali hii
na kwa kuwa changamoto hii ni ya muda mrefu inalishauri Shirika kutoendelea
kuwapatia huduma ya umeme taasisi ambazo ni wadaiwa sugu.
2. Kutokana na Shirika kukabiliwa na deni la TANESCO, Kamati inalishauri Shirika
kuendelea na juhudi zake za kupunguza upotevu wa umeme na kuhakikisha kuwa
33
wateja wote wanaotumia umeme wanalipia huduma hiyo ili kukuza mapato ya
Shirika.
MFUKO WA HIFADHI YA JAMII ZANZIBAR -ZSSF
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) umeanzishwa chini ya Sheria Nam. 2 ya 1998
ambayo ilifanyiwa mapitio makubwa na kutungwa upya Sheria Nam. 2 ya 2005. Aidha,
Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho katika Sheria Nam. 10 ya 2016.
ZSSF imekuwa na mafanikio katika kuongeza wigo wa wanachama na uwekezaji wa vitega
uchumi kama vile Dhamana za Serikali (SMZ Stock), Hati fungani (Treasury Bond), Hati
fungani PBZ (Corporate Bond), Hisa (Shares), Mabenki (Fixed Deposits), Majengo
(Investment Properties) na Mikopo (Institutional Loans).
CHANGAMOTO ZA MFUKO WA HIFADHI YA JAMII ZANZIBAR - ZSSF
1. Kutofautiana kwa taarifa za wanachama wakati wa kujisajili katika Mfuko na zile
zinazokuwepo katika Idara za Utumishi za taasisi husika zilizowaajiri wanachama
hao. Hali hii huleta ugumu katika kupiga hesabu ya kiasi cha mafao kinachostahiki
kulipwa kwa mwanachama.
2. Kutojisajili wanachama wapya katika Mfuko kwa baadhi ya Taasisi zenye makao
makuu yake Tanzania bara. Taasisi zinazoajiri Zanzibar zinapaswa kuwasajili
wafanyakazi wake Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar.
3. Ugumu wa kuwasajili wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wengi wao wapo
katika sekta isiyo rasmi.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kamati inaishauri Mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar (ZSSF) ishirikiane na taasisi
ambazo ni waajiri wa wanachama wa Mfuko kwa ajili ya kuchunguza taarifa zao na
kuzifanyia marekebisho ili kuondoa mkanganyiko wakati mwanachama anapostaafu.
2. Kamati inaushauri Mfuko uzingatie uwekezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za
gharama nafuu kwa ajili ya wanachama wake, badala ya kuangalia uwekezaji wa
kibiashara pekee.
34
3. Kamati inaishauri Mfuko kutanua wigo wa uwekezaji kwa kujenga majengo na
miundombinu ambayo itatoa huduma za moja kwa moja kwa jamii kama vile vyoo
vya umma (public toilets), masoko ya samaki na mboga mboga
4. Kamati inaishauri Serikali kuitafutia ufumbuzi wa haraka changamoto ya
wafanyakazi wa Taasisi zenye Makao makuu yake Tanzania Bara zinazoajiri
Zanzibar ili wafanyakazi wote waliojariwa Zanzibar wasajiliwe katika Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii Zanzibar kama ilivyo kwa baadhi ya mashirika.
5. Kamati inaishauri Serikali kutengeneza kanzi data (data base) ya wafanyabiashara
wadogo wadogo ili kurahisisha upatikanaji wa mapato ya Serikali na kutanua wigo wa
wanachama wapya kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
KIKAO CHA PAMOJA BAINA YA KAMATI YA BAJETI NA
WAFANYABIASHARA
Kamati ya Bajeti kutokana na umuhimu wa sekta ya biashara ilifanya majadiliano na
walipa kodi wakubwa (Strategic Tax Payer) kwa upande wa Zanzibar kwa lengo la kuona
namna wawekezaji hao wanaweza kuimarishiwa mazingira ya kufanya shughuli zao na
kuongeza mapato ya Serikali. Kwa lengo la kuhakikisha Kamati inagusa biashara mbali
mbali, ilikutana na wawakilishi wa kamapuni ya ndege Ethiopian Airline, Oman Air,
kampuni ya ujenzi ya Salem Construction, kampuni ya mawasiliano ya Zantel na ZAT.
Katika kikao hicho, Kamati ilizialika baadhi ya taasisi za Serikali zinazohusika na
masuala ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi, ikiwemo Wizara ya Fedha na Mipango
Zanzibar, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
MAMBO YALIYOJITOKEZA KATIKA KIKAO
1. Imebainika kuwa baadhi ya wafanyabishara hususani wafanyabishara wa
kampuni za ujenzi, wanaathirika kutokana na changamoto ya usafirishaji na
ushushaji mizigo, ambapo inachukua takribani mwezi mmoja na nusu kutoa
mzigo kutoka Mombasa hadi kushushwa katika Bandari ya Malindi -
Zanzibar. Hali hii kwa kiasi kikubwa inachangiwa na uwezo mdogo wa
Bandari kutokana na miundombinu hafifu ikiwemo changamoto ya kuharibika
kwa winch (crane) iliyokuwa ikitumika kwa kushushia mizigo.
35
2. Wafanyabishara wa Zanzibar wameendelea kulalamikia changamoto ya kulipa
kodi ya Ongezeko la thamani (VAT) mara mbili, ambapo wengi wa
wafanyabiashara hao hawawezi kununua bidhaa viwandani, hali hiyo
inaendelea kuathiri mazingira ya biashara – Zanzibar.
3. Wafanyabishara wa Zanzibar wanalazimika kukata vibali vya Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi
Tanzania (TFDA) vinavyotolewa na Mamlaka za Tanzania licha ya kuwa
vibali kama hivyo wameshapatiwa Zanzibar kupitia Mamlaka kama hizo
zilizopo Zanzibar yaani ZBS na ZFDA. Kamati iliarifiwa kwamba Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ziliingia makubaliao
(MOU) kuhusu kuondosha vikwazo hivyo kwa kukubali vibali vinavyotolewa
na mamlaka za pande zote mbili, lakini utekelezaji wake umekuwa tofauti
kwani wafanyabiashara wa Zanzibar wanatakiwa kukata vibali hivyo tena
pindi wanapopeleka mizigo Tanzania bara.
4. Kwa upande wa wafanyabishara wa makampuni ya mashirika ya ndege,
Kamati iliarifiwa kuwa mashirika makubwa ya ndege yanalazimika kulipa
faini iwapo yatapindukia siku kumi na tano za mwezi kabla ya kulipa kodi
(safety and departure fee), jambo ambalo kwa mashirika ya kimataifa ambayo
kwa kawaida yanakuwa na vituo (destinations) vingi hulazimka kupitia hatua
nyingi mpaka kukamilika uidhinishaji malipo, hivyo muda uliowekwa wa siku
15 kutozwa faini iwapo malipo yatacheleweshwa ni mdogo sana hususani
kwa mashirika yanayotoa huduma Zanzibar ambapo makampuni hayo
yanalazimika kuripoti Afisi kuu ya Shirika - Dar es Salam na baadae makao
makuu ya Shirika .
5. Kamati imebaini kuna mvutano wa ukusanyaji kodi ya ongezeko la thamani
(VAT) baina ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwa makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano ya simu
Zanzibar na Tanzania bara, mvutano huo unatokana na maelekezo
yanayokinzana yanayotolewa na mamlaka hizo mbili juu ya mgawanyo halisi
wa kodi unaopaswa kulipwa na walipa kodi kwa Mamlaka hizo mbili, hali hii
inaathiri Makampuni ambayo ndio walipa kodi.
36
6. Kutokupewa kipaumbele kwa makampuni ya ndani wakati wa uendeshaji wa
zabuni za ujenzi za miradi ya Serikali, ambapo mara nyingi inaonekana ni
makampuni ya Kigeni yanayoshinda zabuni hizo na kuyaacha makampuni ya
wazawa yakiwa hayana kazi.
MAONI NA USHARI WA KAMATI
1. Kamati inaishauri Serikali kupitia Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kuongeza ushirikiano na wafanyabishara ikiwa ni pamoja na
kuandaa vikao vya mara kwa mara vya kusikiliza changamoto na maoni yao. Aidha,
kuwe na utaratibu wa kuwapatia elimu walipa kodi kuhusu mifumo ya kodi iliyopo
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
2. Kamati inaishauri Serikali kupitia Bodi ya Mapato (ZRB) kukaaa pamoja na
Makampuni ya Ndege, kusilikiliza malalamiko yao kuhusu muda wa kulipia kodi
(Safety fee na Depature fee) na kuangalia uwezekano wa kuwaongezea muda wa
kulipia kodi hiyo ndani ya siku 30 badala ya siku 15 kama ilivyo sasa. Hatua hiyo
itasaidia kujenga uhusiano mzuri baina ya walipa kodi na mamlaka zinazosimamia
kodi na pia itasaidia kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.
3. Ili kuvisaidia viwanda vya Zanzibar kutokana na changamoto ya mazingira magumu
ya soko na gharama kubwa za uzalishaji, Kamati inaishauri Serikali iweke sera ya
kuvilinda viwanda vya Zanzibar, kwani katika mfumo wa uchumi wa kiushindani
duniani, nchi nyingi zikiwemo nchi zilizoendelea zinatekeleza sera za kulinda
viwanda vyao vya ndani.
4. Ipo haja kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kukaa pamoja na kuzitatua changamoto zaa vikwazo vya kibiashara na
kodi ambavyo vinaathiri wafanyabiashara wa pande hizo mbili hususani
wafanyabiashara wa Zanzibar, ambako kuna soko dogo kutokana na idadi ndogo ya
watu wake. Hivyo, si busara kwa wafanyabiashara wa pande hizi mbili kuendelea
kulilia changamoto hizi ambazo zimekuwa za siku nyingi. Nchi nyingi duniani
zimekuwa zikianzisha mashirikiano ya kikanda (Regional Integration) ambayo
malengo yake makubwa ni kurahisisha biashara na uchumi wao. Hivyo ni vyema kwa
Serikali zetu mbili zikaondosha changamoto hizo na kuwa na Muungano imara
kiuchumi kama ambavyo Muungano huo umeimarika kisiasa.
37
5. Kamati inaishauri Serikali kuikarabati kwa haraka winch (crane) inayotumika
kupakua na kupakia makontena bandarini, ili winch (crane) hiyo ianze kufanya kazi
na kupunguza msongamano katika bandari ya Zanzibar.
6. Kamati inaishauri Serikali kuzipa kipaumbele kampuni za ndani hususani za wazawa
ambazo zinashiriki katika zabuni za miradi ya Serikali zenye uwezo unaofanana au
unaokaribiana na kampuni za nje kwa lengo la kuziendeleza kampuni hizo na
kuwahamasisha wawekezaji wa ndani.
KIKAO CHA PAMOJA BAINA YA KAMATI NA WAWEKEZAJI WA SEKTA YA
UTALII NA MAHOTELI
Kamati katika kuhakikisha inafanyia kazi maeneo yote yenye mchango mkubwa katika
uchumi wa Zanzibar ilifanya kikao cha pamoja na wawekezaji katika sekta ya utalii na
mahoteli kwa lengo la kujadili namna bora ya kuweka mazingira mazuri na kuhakikisha
makusanyo ya kodi za Serikali yanaongezeka. Miongoni mwa wawekezaji waliohudhuria
katika kikao ni pamoja na wawakilishi wa wawekezaji kutoka Hotel ya Park Hyatt,
Kiwengwa Strand Hotel, The Residence, Double Tree By Hilton, Nungwi Village na Nungwi
Royal Zanzibar pamoja na Taasisi mbali mbali za Serikali zinazohusiana na Sekta ya utalii.
Kwa upande wa Taasisi za Serikali zilizoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Biashara na
Viwanda na Wizara ya Fedha na Mipango.
MAMBO YALIYOJITOKEZA KATIKA KIKAO
1. Ukosefu wa barabara za lami zinazoelekea maeneo ya uwekezaji kwa baadhi ya
mahoteli yaliyopo kando kondo ya fukwe za bahari, hali inayopunguza hamasa ya
wageni kufika katika maeneo hayo.
2. Wingi wa kodi na tozo zinazotozwa na Serikali Kuu na Serikali za Wilaya hali
inayopelekea wawekezaji wa sekta ya utalii kupoteza muda mwingi katika kufuatilia
malipo ya kodi na tozo hizo.
3. Serikali kutowashirikisha kikamilifu wawekezaji katika uanzishwaji wa aina mpya ya
kodi na tozo mbali mbali zinazohusina na mahoteli na huduma nyengine zinazotolewa
na hoteli.
38
4. Ukusanyaji wa kodi na tozo nje ya muda wa saa za kazi hali ambayo inawafanya
wageni kukosa utulivu kutokana na mivutano baina ya walinzi wa mahoteli na
wasimamizi wa kodi.
5. Kuwepo kwa nyumba binafsi za makaazi zinazomilikiwa na wananchi kando kondo
ya mahoteli ambazo hukodishwa kwa wageni bila ya kufuata utaratibu na kutolipiwa
kodi yoyote, hali ambayo inaikosesha Serikali mapato na kuhatarisha usalama wa
wageni wanaokodishwa katika nyumba hizo.
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
1. Kamati inaishauri Serikali ihakikishe inazifanyia matengenezo barabara za ndani kwa
kuweka mazingatio maalum kwenye maeneo ya uwezekaji yenye hoteli na
yasiyofikiki kwa urahisi.
2. Kutokana na kuwepo kwa utitiri wa kodi na tozo katika sekta ya utalii na kwa lengo la
kuufanya mfumo wa kodi kuwa rafiki zaidi, Kamati inaishauri Serikali kuanzisha
mfumo wa kodi jumuishi (centralized) ambao utamuwezesha mlipa kodi kulipa kodi
mara moja kwa maeneo yote anayopaswa kulipia.
3. Kamati inaisisitiza Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kufuata utaratibu na maadili ya
kazi katika utekelezaji wa majukumu yake, kwa lengo la kutowakwaza wawekezaji
wa hoteli kwa kuwagongea wageni wkati wa usiku wanapokuwa wamepumzika, na
badala yake kutafuta utaratibu mbadala utakaowawezesha kujiridhisha juu ya idadi
halisi ya wageni.
4. Kamati inaishauri Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kuwachukulia hatua wananchi
wanaokodisha nyumba kwa wageni bila ya kufuata utaratibu, kwa lengo la kuwalinda
wawekezaji wa sekta ya utalii na kukusanya mapato ya Serikali yanayokosekana
katika eneo hilo.
KIKAO CHA PAMOJA BAINA YA KAMATI NA WAWEKEZAJI WA VIWANDA
VYA VINYWAJI VISIVYO NA KILEVI
Kamati ya Bajeti ilifanya kikao cha pamoja na wawekezaji wa viwanda vya vinywaji visivyo
na kilevi Zanzibar, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao ikiwemo ugumu wa utekelezaji
wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty).
39
Itakumbukwa kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bajeti ya
2012/2013 iliamua kuongeza mapato ya Ushuru wa Bidhaa zinazozalishwa nchini kwa
kuongeza Ushuru wa Bidhaa katika vinywaji visivyo na kilevi. Kwa upande mwengine,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Ushuru wa Bidhaa kama huo kwa vinywaji
visivyo na kilevi. Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016, kiwango cha Ushuru wa
Bidhaa (Excise Duty) ya “soft drinks” na maji ni TZS 58.0 kwa lita moja na kwa juisi ni TSH
9.5 kwa kila lita.
MAMBO YALIYOBAINIKA KATIKA KIKAO CHA PAMOJA BAINA YA KAMATI
NA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA VINYWAJI VISIVYO NA KILEVI
1. Iwapo kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kinachotajwa katika Sheria kitatekelezwa
kama kilivyo, gharama za uendeshaji wa viwanda Zanzibar zitaongezeka kwa
kiwango kikubwa. Aidha, kwa upande wa Zanzibar mzigo (burden) utakuwa mkubwa
zaidi ikilinganishwa na Tanzania bara ambako viwanda vyake vinanufaika na
uzalishaji mkubwa (Economies of Scale). Mfano kiwanda cha Coca cola, Pepsi, Azam
nk. Katika mazingira hayo, bidhaa zinazozalishwa Zanzibar hazitaweza kuhimili
ushindani katika masoko.
2. Viwanda vya Zanzibar ni vidogo na mali ghafi za bidhaa zinazozalishwa zinatoka nje
ya Zanzibar. Aidha, wataalamu katika sekta ya viwanda ni wachache, hali
inayopelekea viwanda vya Zanzibar kutopata faida kubwa ukilinganisha na viwanda
vikubwa vya Tanzania bara.
3. Kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 ambayo imeyataja Mambo ya Muungano, katika kifungu cha 10 (10th
item) jadweli la kwanza imeitaja TRA kuwa ndio taasisi pekee yenye mamlaka ya
kusimamia mapato yatokanayo na Ushuru wa Bidhaa Tanzania ikiwemo Zanzibar.
4. Kumekuwepo na uchereweshaji wa uingizaji wa bidhaa kutoka Zanzibar kwenda
Tanzania bara, kwa madai ya kukosa vibali vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
na Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Tanzania (TFDA), licha ya kwamba
wamepata vibali vya Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) na Wakala wa Chakula,
Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA).
40
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
Kwa lengo la kutekeleza Sera ya Viwanda kwa upande wa Zanzibar na kuvilinda viwanda
vya ndani, Kamati inaishauri Serikali kufanya mambo yafuatayo:
1. Kutoa msamaha maalum wa ushuru wa bidhaa kwa wazalishaji wa vinywaji visivyo
na kilevi au kutoza kiwango kidogo ambacho hakitaathiri uzalishaji wa bidhaa hizo
viwandani.
2. Kamati inaishauri Serikali, kuipa kipaumbele (upendeleo maalum) sekta ya viwanda
kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa Zanzibar. Endapo viwanda vitapunguza
au kusitisha uzalishaji kutapelekea kuathiri hali ya uchumi na fedha ikiwemo kupanda
kwa bei za bidhaa, kupungua kwa kiwango cha uzalishaji na mauzo, kukosekana kwa
ajira na hatimae kupungua pato la nchi.
3. Kamati inaishauri Serikali kuweka mipango madhubuti ya kuwasomesha vijana wetu
fani zinazohusiana na sekta ya viwanda ili Zanzibar iwe na wataalamu wa kutosha
katika sekta hiyo.
4. Kwa vile kuna makubaliano (MOU) baina ya ZBS na TBS na baina ya ZFDA na
TFDA wa kufanya kazi kwa pamoja. Kamati inaishauri Serikali kulifuatilia jambo hili
ili utekelezaji wa makubaliano hayo uanze mara moja. Hii itasaidia kuwapunguzia
gharama za ziada wafanyabiashara wa Zanzibar kuepuka faini za kuchelewesha kutoa
bidhaa zao bandarini Dar es Salaam kwa kuanza upya utaratibu wa kuomba vibali vya
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi
Tanzania (TFDA) wakati tayari wameshapata vibali vya Shirika la Viwango Zanzibar
(ZBS) na Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA).
41
SEHEMU YA TATU
HITIMISHO
Kamati inapenda kutoa shukurani za dhati kwa taasisi zote za Serikali na binafsi
zilizoshirikiana kwa muda wote wakati Kamati ikitekeleza majukumu yake. Aidha,
Kamati inawashukuru wadau wote walioalikwa na kufika mbele ya Kamati, kwani
michango na maoni yao imekuwa ni msaada muhimu katika kutekeleza majukumu ya
Kamati ya kuisimamia na kuishauri Serikali. Kamati inategemea Serikali itaifanyia kazi
taarifa hii na kuleta majibu muafaka juu ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati.