Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Embed Size (px)

DESCRIPTION

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Citation preview

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI, AGOSTI 06 2015KUNGATUKA WADHIFA WA MWENYEKITI WA TAIFA WA CUFKwa mara ya kwanza nilichaguliwa na Mkutano Mkuu wa CUF kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama, Novemba 1999. Nilichaguliwa tena kushika wadhifa huu 2004, 2009 na 2014.Nimejitahidi kujenga Chama chetu hasa Tanzania Bara. Ndani ya Chama na nje ya Chama nimejitahidi kujenga umoja kati ya Wazanzibari na wananchi wa Tanzania Bara. Januari 25 2001, nilikamatwa na Polisi, kupigwa na kuvunjwa mkono, kuporwa saa na kuwekwa jela kwa kudai Katiba Mpya, Tume huru ya Uchaguzi, Utawala Bora na uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2000 urejewe ili Wazanzibari watendewe haki na wachague viongozi wanaowataka. Januari 27 2015, Chama kiliandaa niongoze maandamano na mkutano wa hadhara kuomboleza mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola Zanzibar na hasa Pemba tarehe 27 Januari 2001. Polisi walizuia maandamano hayo na kutupa taarifa tarehe 26 Januari saa 12:30 jioni. Nilipoenda kuwapa taarifa wanachama na wananchi waliokusanyika kufanya maandamano, mimi na viongozi na wanachama wa CUF wa Tanzania Bara tulikamatwa, kupigwa na wengine kuumizwa vibaya. Hivi sasa tumembabikiziwa kesi na kushitakiwa kwa kula njama kufanya vitendo vya uhalifu na kufanya maandamano yasiyo halali. Kesi iliyoanza tarehe 29 Januari 2015 bado inaendelea mahakama za Kisutu.Si kuwa na nia ya kugombea Uenyekiti, mwaka 2014 lakini mchakato wa kupata Katiba Mpya itokanayo na Maoni ya Wananchi ilinisukuma niendelee na uongozi wa CUF.Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikuwa na mambo ya msingi ambayo kama tungefikia Muafaka wa Kitaifa kuhusu Katiba hiyo tungeweza kuanza kuifua Tanzania Mpya inayoenzi na kuzingatia Tunu za Taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji.Ndani ya Bunge Maalum la Katiba tulianzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa lengo la kutetea na kuyaheshimu maoni ya Wananchi yaliyoratibiwa na Tume ya Jaji Warioba na kuwekwa katika Rasimu ya Katiba. Tumeendeleza kushirikiana ndani ya UKAWA kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ili hatimaye tupate katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi na tuwe na serikali itakayoenzi na kuyatekeleza yaliyomo ndani ya katiba hiyo.Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi ni nyezo ya kufikia malengo mapana zaidi ya kuwa na taifa la wananchi walioelimika na kujitambua, wenye afya bora, linalojenga uchumi imara unaoongeza ajira kwa vijana wetu, kutokomeza umasikini, kutumia raslimali na maliasili za nchi kwa manufaa ya wananchi wote, kupambana na rushwa na ufisadi na kuwa taifa lenye utu, uzalendo, uadilifi, umoja, uwazi na uwajibikaji. Katiba mpya inayosimamiwa na wananchi itaiwajibisha serikali kutenda haki sawa kwa wote. Nimeshiriki katika vikao vingi vya UKAWA vilivyotufikisha hapa. Hata hivyo dhamira na nafsi yangu inanisuta kuwa katika maamuzi yetu ya UKAWA tumeshindwa kuenzi na kuzingatia Tunu za Taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji. Rasimu ya Katiba na maudhui yake tumeyaweka kando. Waliyoipinga Rasimu ya Katiba ya Wananchi ndani ya Bunge Maalum la Katiba ndiyo tunaamini wataturahisishia kushinda uchaguzi. Tumeshindwa kuongozwa na maadili.Tarehe 1 Agosti 2015 niliiarifu Kamati ya Utendaji ya Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu wa Chama chetu kuwa nitawajibika na kujiuzulu Uenyekiti wa Taifa baada ya wenzangu kukamilisha taratibu za ushirikiano ndani ya UKAWA.Makamu Mwenyekiti wa Chama chetu Juma Duni Hajj ambaye Baraza Kuu lilimpitisha kuwa Mgombea wa Uwakilishi jimbo la Bububu amehama Chama na kujiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.Leo hii nimeikabidhi ofisi ya Katibu Mkuu, barua yangu ya kungatuka nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, lakini naendelea kuwa mwanachama wa CUF na kadi yangu imelipiwa mpaka mwaka 2020.Katika kipindi cha kabla ya uchaguzi mkuu nitajishughulisha na kuandaa ushauri wa mambo yanayopaswa kufanywa na serikali ijayo ikiwa ni pamoja na Kujenga uchumi imara unaoongeza ajira kwa vijana wetu Kuhakikisha kina mama wajawazito na watoto wanapata lishe bora ili watoto wajenge ubongo na maungo yao na wawe ni kinga ya mwili. Tanzania inahitaji mapinduzi ya kilimo kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao mengine ya biashara. Mkakati madhubuti wa kuboresha elimu ili tuwe na taifa la wananchi walioelimika na wabunifu wanaoweza kuajirika na kujiajiri. Kuweka utaratibu wa uboreshaji wa huduma za kinga na tiba ya afya na kuanza kujenga mfumo wa huduma za afya uliokamilika toka zahanati hadi hospitali za rufaa. Kujenga mfumo madhubuti wa hifadhi ya jamii hasa kwa wazee ambao hutelekezwa na kutopata matunzo kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa sababu na wao ni masikini. Kusimamia ujenzi wa miundombinu mizuri kama vile barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, nguvu za umeme, mawasiliano na maji. Miundombinu inayounganisha nchi jirani ni muhimu kwa kukuza uchumi na ulinzi wa taifa. Kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali kufikia asilimia 20 ya pato la taifa na kuhakikisha matumizi ya serikali yana tija. Rushwa ni adui wa haki na ni adui maendeleo. Rushwa na ufisadi ni mfumo wa utendaji ndani ya serikali. Hata hivyo mkakati wa kupambana na rushwa unahitaji utashi wa kisiasa Kuweka mkakati wa kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals) nchini TanzaniaBaada ya Uchaguzi nitajikita katika kufanya utafiti na kutoa ushauri kuhusu maendeleo ya uchumi shirikishi wa taifa letu.Nawashukuru wanachama wa CUF na wananchi kwa ujumla kwa kuniunga mkono wakati nikiwa kiongozi wa Chama hiki. Nawaomba radhi sana wanachama na wananchi walioniamini na kuonesha mapenzi makubwa kwangu na katika uongozi wangu. Katika hali halisi iliyopo ndani ya uongozi wa Chama chetu mimi naonekana ni kikwazo na kwa hiyo siwezi kuwa na mchango wa maana kama Mwenyekiti katika mapambano ya kudai haki sawa kwa wote katika kipindi hiki.HAKI SAWA KWA WOTE Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, Mwenyekiti Mstaafu wa CUF, 06 Agosti 20152